UKIAMBIWA MICHUZI NI MVIVU UTAKUBALI?

Ukimuita Issa atakuitikia,ukimuita Muhidini hatoshangaa, ukimuita Michuzi atakuitikia kisha mtaketi chini na kuzungumza mengi. Hivyo ndivyo ilivyo kuwa hivi karibuni BongoCelebrity ilipopata nafasi adimu ya kufanya naye mahojiano.

Safari yake katika ulimwengu wa picha aliianza loooong time.Wanaomjua tangu siku hizo watakuambia hajabadilika, umaarufu haujamfanya asahau alikotoka.Bado utamkuta katikakati ya gumzo.Liwe ni kuhusu soka,bongo flava,siasa kidogo,utanzania nk,Michuzi hutomkosa.

Hivi sasa anajulikana zaidi kwa mambo mawili, ni mmiliki wa blogu yenye watembeleaji wengi kuliko sio tu blogu zingine zote za kitanzania/watanzania bali hata tovuti nyingine yoyote ile ya Tanzania. Jambo la pili ni kwamba yeye ni shabiki wa kutupwa wa klabu ya Liverpool ya kule nchini Uingereza. Fuatilia mahojiano yafuatayo;

BC: Unaweza kutuambia ulianza vipi masuala ya upigaji picha? Nini kilikuvuta katika ulimwengu wa sanaa hii ya upigaji picha? Je ulichukua mafunzo yoyote maalumu ya upigaji picha?

MICHUZI:Nakumbuka nilianza mwaka 1980 kwa kutumia kakamera ka shemeji yangu ambapo mdogo wake na mimi tulikaiba na kwenda kupigia picha zetu (mie na mdogo wa shemeji yangu) sehemu mbalimbali. Matokeo yakanivutia na kunifanya niwe na kiu ya kuwa mpiga picha.Miaka mitano baadaye rafiki yangu mmoja alinizawadia Pentax Spotmatic ambayo nilikuwa sijui hata namna ya kuitumia. Bahati wakati huo kulikuwa na masomo ya jioni ya photogrtaphy pale Goethe Institute (jengo la IPS) na mwalimu wangu wa kwanza alikuwa Tom Mwewuka wa us info. services. Masomo ya vitendo yalinifanya niwe napiga picha mitaani kama mazoezi hatimaye nikajikuta ukumbi wa YMCA ambako disko la ma DJ Kalikali, Neagre J na wengineo lililokuwa juu sana enzi hizo. Wengi hawajui siri hii kwamba picha nilizokuwa napiga zilikuwa ni kwa ajili ya pesa za kusafishia (sio faida) ili kupata mazoezi.Nilifanikiwa sana kwa hilo kwani nilifaulu vizuri masomo yangu. Baada ya masomo niliendelea pale YMCA na kisha mitaani ambako kila mtu alitaka kupigwa picha na mimi kutokana nadhani na uzuri wa picha zangu. Nakumbuka picha za ajali ya jumba lililobomoka na kuua watu wawili mtaa wa Msimbazi ambapo gazeti la Mfanyakazi walitumia nne hivi. Hizo picha zangu za kwanza gazetini.

Lakini kujikita katika fani ilitokea kwamba siku moja, nakumbuka mwaka 1989, Jah Kimbute na kundi lake la Roots and Culture walifanya onyesho pale YMCA na waliniomba niwapigie picha za kumbukumbu. Mmoja ya wageni waalikwa alikuwa Attilio Tagalile wa Daily News ambaye hakuja na mpiga picha. Akaniomba nimpatie picha moja na nilipompa nakumbuka kwa mara ya kwanza Daily News walitumia picha ya msanii ukurasa wa mbele. Nahisi walivutiwa jinsi nilivyomtoa Jah Kimbute huku rasta zake zikiwa zimeruka juu na uso kaukunja kwa hisia kali za kuimba. Kuanzia hapo Tagalile akanitia moyo wa kuwa mie ni mtu wa magazeti. Pia mpiga picha mkuu wa Daily News wakati huo hayati Vincent Urio aliyekuwa na studio binafsi pale YMCA iliyoitwa Studio Laura akavutiwa nami na kunichukua. Kuanzia hapo nikawa naendelea na mafunzo ya vitendo na gwiji ambaye alinifundisha sio sanaa pekee ya picha bali pia mbinu za dark room za kusafisha mikanda (black&white) na kuprint. Nilijiunga rasmi na Daily News Januari 1, 1990 na kupelekwa Berlin nchini Ujerumani mwaka 1992 kwa mafunzo zaidi. Baada ya kumaliza tu TSJ (nilisoma 1994-96) nikapelekwa Cardiff, Wales kwa mafunzo ya juu ya upigaji picha za habari za kisiasa. Sisi ndio tulikuwa wa kwanza kufundishwa Digital Photography wakati huo. Nakumbuka Canon na Kodak walishirikiana kuunda kamera ya digital ambayo walituletea chuoni nasi tukawa kama wahusika kwa uchunguzi wao wa kuendeleza digital photography.

BC: Kwa wapiga picha wengi kitendo cha kumfuata mtu(watu) usiyemjua na kumuomba kumpiga picha sio jambo rahisi. Wewe kama mpiga picha huwa unavuka vipi kizingiti hicho ?

MICHUZI: Ni sawa na kuniuliza ukiwa mwindaji unapokuwa porini nawezaje kumpiga risasi mnyama. hapo ni akili kichwani kutegemea na situation ilivyo. kuna wakati unaiba ama unavizia ama unatabasamu na kuomba. inategemea. hakuna situation ya kufanana. ila naona raha sana kupata picha kwa kutumia akili na maarifa bila mwenyewe kujua.

BC: Je unakumbuka lini ilikuwa ni mara yako ya kwanza kulipwa kama mpiga picha?

MICHUZI: Siwezi kukumbuka vizuri. Labda mwaka 1987 nilipoanza kupiga picha disko la YMCA. Pesa ya maana nadhani ilikuwa mwaka 1989 ambapo kampuni ya Inter Consult walinipa tenda kubwa ya kupiga majengo wanayojenga nchi nzima. Nililipwa milioni moja na ushee hivi.Nusura nipate uchizi kwani enzi hiyo pesa hiyo ilikuwa nyingi sana. Nakumbuka nusu nilinunua kiwanja na kiasi kingine kamera mpya na flashi.

BC: Ni lini hasa ulipogundua kwamba sasa wewe ni mpiga picha weledi (professional photographer)?

 

MICHUZI: Baada ya kazi ya Inter Consult

BC: Ni aina gani ya vifaa unavyotumia katika kazi zako za kila siku za upigaji picha? Nina maana unatumia kamera ya aina gani na vitu kama hivyo.

 

MICHUZI: Ninatumia kamera nyingi , ila kamera kubwa natumia aina ya Canon d5 na eos d30 na lens zote toka fish eye (17mm), ya kati (35-185mm) hadi long lens (100- 1000mm) pia natumia skylight (light pibk) filter ama Ultra Violet clear filter muda wote na ninazo filter zote kuanzia polarising filter hadi neutral density (ND-L & ND8-L). Pia natumia flash nne za speedlite 580EX, tripod ya canon, memory card za 2gb kama sita hivi, light meter na photo-torch moja. Kila niendapo huwa mkobani nina Sony Cybershot 7.2megapixel DSC P200.

BC: Ni maeneo gani ambayo wewe hupendelea zaidi kupiga picha? Majengo, watu, milima, bahari nk?

 

MICHUZI: Chochote cha kuvutia hisia zangu na za watu.

BC: Unaweza kutueleza ni eneo gani la kustajaabisha (spectacular) ulilowahi kutembelea?

 

MICHUZI: Robben Island alikofungwa Nelson Mandela

BC: Nini unakipenda zaidi katika maisha yako kama mpiga picha?

 

MICHUZI: Tabasamu la furaha na kuridhika mtu niliyempiga picha ama anayeangalia picha niliyopiga

BC: Nini usichokipenda katika maisha yako kama mpiga picha?

Page 1 of 5 | Next page