
“Jina langu limevuma, Kwenye mitaa.Jina langu lina hadhi ya ki-superstar.Jina langu…..” Hayo ni maneno kutoka kwenye wimbo Jina Langu wa msanii mahiri wa Bongo Flava, PROFESSOR JAY au Prof Jiizeh. Hakuna ubishi, jina lake limevuma na ni kweli ana hadhi ya ki-superstar.
Alizaliwa jijini Dar-es-salaam tarehe 29 December 1975. Ni mtoto wa sita kati ya watoto tisa wa Mzee Leonard Steven Haule na Mama Rose Majanjara. Baadaye akasoma Ukonga Primary School kabla hajaelekea mji kasoro bahari(Morogoro) kusoma Kigurunyembe Secondary na baadaye Mbeya Lutengano High School.
Ana tuzo za muziki zisizopungua 25 ambazo amezikusanya ndani ya miaka 15 ambayo amekuwa kwenye game. Hivi karibuni BongoCelebrity iliketi chini na msanii huyu ambapo alifungua milango ambayo hajawahi kuifungua kabla. Katika mahojiano haya nadra, Professor Jay anazungumzia kwa undani shughuli zake za muziki, siasa za nchi,ushauri kwa vijana, role models, vilio vya wasanii kuhusu kazi zao na mzunguko mzima wa muziki. Pia anatoa ushauri makini kwa Raisi Kikwete, anabainisha mtizamo wake wa kisiasa na mengi mengineyo. Yafuatayo ni mahojiano kamili;
BC: Karibu sana katika BongoCelebrity na shukrani nyingi kwa kukubali kufanya mahojiano nasi.
PROF.JAY: Asante Sana na najisikia faraja sana kupata fursa hii ya kufanya mahojiano nanyi kwani itakuwa ni nafasi nzuri ya kuwajulisha mashabiki wangu kuhusu mustakabali wa shughuli zangu za kimuziki
BC: Unaweza kukukumbuka ni lini ilikuwa ndio mara yako ya kwanza kupanda jukwaani kama mwanamuziki huku umati wa watu ukisubiri uwape burudani. Ilikuwa wapi?
PROF.JAY: Yeah nakumbuka ilikuwa ni mwanzoni mwa mwaka 1992 nikiwa pamoja na mshkaji wangu KILLA B pale Chuo Kikuu cha Dar es salaam ukumbi wa UDASA. Nakumbuka watu walikuwa kibao nanilikonga sana nyoyo za mashabiki wa muziki huu kwa style yangu ya enzi hizo ya TONGUE TWIST.
BC: Mara nyingi wanamuziki wengi huwa wameanza muziki kutokana na kupata ushawishi (influence) fulani hivi. Unaweza kutuambia nini au nani alikushawishi kuingia katika masuala ya muziki?
PROF.JAY: Nilikuwa napenda sana kusikiliza nyimbo za akina RUN DMC na PUBLIC ENEMY kwa kuwa walikuwa wanaimba nyimbo za kupigania na kutetea haki za mtu mweusi. Kwa hiyo nikawa nazikariri na kuziimba shuleni na pia nikawa najaribu kuongeza maneno yangu na mwisho nikawa taratibu na mimi natunga mashairi yenye ujumbe tofauti tofauti kwenye jamii yangu iliyonizunguka.
BC: Ulipojitokeza rasmi katika ulimwengu wa muziki ulijulikana kama Nigga Jay, kisha yakafuata majina kama Jay wa Mtulinga, Mti Mkavu nk.Baada ya hapo majina kama HeavyWeight MC, Professa Jay na hivi sasa Daddy yakaibuka.Nini chanzo cha majina yote haya?
PROF.JAY: Ha hah hah mbona umeyaacha mengine mengi kama vile mchawi wa Rhymes ,Mr President,Mc Shupavu,Jay Tunakuzimia, Jay Arosto, Heavy Weight Mc,Prof Jiizeeh,Jiizeh for President, Madini mtoto wa mjini, na sasa hivi wananiita SAUTI YA HELA. Hayo yote ni majina ambayo napewa na mashabiki wangu kila mmoja wao ananitunga jina lake kutokana na anavyotafsiri muziki wangu na kwa kweli na mimi huwa nayapokea kwa moyo mkunjufu kwani naamini ni hao mashabiki wanaonifanya nikubalike kote.Siwezi kuwa PROFESSOR JAY bila wao.
BC: Baadhi ya ndugu zako kama vile Mr.Teacher (anayeishi na kufanya kazi zake nchini Marekani), Simple X, Black Rhino na Kolihombi nao ni wanamuziki. Je wazazi wenu nao walikuwa wanamuziki au hivi vipaji vinatoka wapi?
PROF.JAY: Wengi sana wanajiuliza hilo swali, maana hata dada yetu anayeitwa VIOLAH HAULE naye alikuwa ni kiongozi wa waimbaji wa kwaya ya shule tulipokuwa tunasoma sekondari kiasi kwamba watu walikuwa wanamuita Equalizer. Ukweli ni kwamba baba yetu alikuwa anapiga gitaa kwa kujifurahisha tu alipokuwa kwenye mapumziko yake na mama hakuwahi kuwa mwanamuziki, mimi naamini hizi ni karama tu za mungu katika familia yetu kwa kutujaaalia vipaji visivyochuja tangu enzi na enzi.
BC: Prof. kumekuwepo na malalamiko kadhaa kutoka kwa wasanii wanaojaribu chipukizi (underground artists) kwamba ni vigumu sana kwa wao kuchanua.Wanalalamika kwamba Djs wanawabania, studio ni gharama sana nk.Nini maoni na ushauri wako katika hilo?
PROF.JAY:Sio kwa wasanii chipukizi peke yao bali hata kwetu sisi wakongwe. Hilo tatizo lipo na linatukera sana , kwani wenye studio bongo hawapo serious na kazi zao wanaifanya biashara ya muziki kama biashara ya kuuza mapera.Wanafanya wakitakacho tofauti na mlichokubaliana na kwa wakati wanaotaka wenyewe sio unaotaka wewe na radio djz wamehalalisha hongo kwamba ukirelease wimbo lazima uambatanishe na takrima ili waweze kujikimu, kitu ambacho sio sawa na kinadumaza vipaji vya wasaniii bora na kuwapa nafasi wenye senti wasio kuwa na vipaji timilifu.
BC: Kwa upande wenu ninyi wasanii wenye majina makubwa tayari, malalamiko mengi yamekuwa kwamba ‘wadosi” hawako fair katika malipo mkilinganisha na jasho mnalolitoa katika kuandaa albamu nk. Ninyi kama wasanii mmefanya nini mpaka hivi sasa kukabiliana na hali hiyo?
PROF.JAY: Kitu cha msingi hapa ni kuwashawishi watu wenye uwezo na wenye nia nzuri na sanaa hii wawekeze katika muziki huu na sio kulalamika tu wakati hakuna dalili zozote za kupata tiba mbadala. Ni kweli wengi hatufurahishwi na mpangilio wa mauzo ya kazi zetu, je dawa ni kutopeleka kazi kwa wahindi? Hapana, wakijitokeza watu wakawekeza kwenye distribution naamini kabisa kwamba kutakuwa na challenge wao kwa wao so huyu usiporidhika nae unakwenda kwa huyu tofauti na sasa wapo wachache na ni marafiki.Ukimzunguka huyu anampigia simu mwenzake kisha inakuwa 4*4-16 = 0 .Hii sanaa ni kama kivuli chetu hatuwezi kuikimbia na dawa ya tatizo ni kulikabili sio kulikwepa.
BC: Sifa yako kuu sio tu kwamba unajua kurap bali pia ni mtunzi mzuri sana wa mashairi (lyrics) kwa ajili ya nyimbo zako. Unaweza kutuambia jinsi unavyoanza kuandika mashairi yako mpaka kufikia kuyaweka kama muziki?
PROF.JAY: Swali zuri, huwa naanza kwanza kufanya research na kujua nini ambacho jamii inahitaji na ni kwa muda gani, kisha natafuta topic ambayo watu wa rika zote wataielewa ipasavyo. Baada ya hapo naanza kunote down mwongozo wa mambo ya msingi ninayotaka kuyazungumzia mwisho nakuja kuoanisha pamoja na kufanya mtiririko unaoeleweka vema kwa HADHIRA.
BC: Tukiwa bado kwenye suala la uzuri wa mashairi, katika baadhi ya nyimbo zako zilizotamba sana kama vile Ndio Mzee na Siyo Mzee na collaboration kama uliyofanya na Juma Nature katika wimbo CCM na CUF, umezungumzia zaidi masuala ya siasa. Je una mpango wowote wa kuwa mwanasiasa siku za mbeleni? Na je nini maoni yako kuhusu utawala wa raisi Jakaya Kikwete hivi sasa?
PROF.JAY: Bado ni mapema mno kuongelea kama nitakuja kuwa mwanasiasa au lah. Nasema hivyo kwa sababu naamini siasa ni wito na unatakiwa uwe umejiaandaa kuwa mwanasiasa kabla ya kuingia ndani ya siasa.
Page 1 of 5 | Next page