MZEE FRANK HUMPLINK HATUNAYE TENA!

Wakati wa harakati za kugombea uhuru wa Tanganyika kati ya mwaka 1954 mpaka 1961, jina moja lilitamba sana katika fani ya muziki. Jina hilo ni la Frank Humplink. Humplink alikuwa mwimbaji na mpiga gitaa maarufu sana wakati ule. Alikuwa akipiga muziki wake akishirikiana na dada zake wawili Maria Regina na Tecla Humplink.

Habari za kusikitisha ni kwamba Frank Humplink hatunaye tena. Mzee Humplink amefariki dunia jana tarehe 25 August 2007 huko nyumbani kwake Lushoto,mkoani Tanga. Alizaliwa tarehe 3 Aprili mwaka 1927. Amefariki akiwa na umri wa miaka 80.

Marehemu atakumbukwa sana kwa wimbo wake uliokuwa na mashairi yafuatayo, ‘Uganda nayo iende, Tanganyika ikichangamka, Kenya na Nyasa zitaumana’. Wimbo huo ambao ulikuwa ukiwasisimua sana wananchi, ulikuwa umesheheni ujumbe mkali wa kisiasa jambo ambalo lilikifanya chama cha TANU kuufanya kama vile wimbo wake rasmi kwani ulikuwa ukipigwa katika mikutano yake yote. Mikutano ya TANU ya siku za mwanzo ilikuwa ikifanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja mbele ya Princess Hotel. Sahani ya santuri ilikuwa ikipigwa katika gramafoni kupitia kipaaza sauti.

Pamoja na kutamba sana kwa wimbo huo haikupita muda serikali ya kikoloni ikaelewa ujumbe mzito uliokuwemo katika wimbo huo ambao kimsingi ulikuwa unasema Tanganyika itakapoamka, kutakuwa vilevile na mapambano nchini Uganda, Kenya na Nyasaland.

Kilichofuata ni kupigwa marufuku kwa wimbo huo jambo ambalo inasemekana kuufanya pengine kuwa wimbo wa kwanza kupigwa marufuku katika historia ya utangazaji Tanganyika.

Enzi hizo Frank Humplink alijulikana zaidi kama “kijana wa kichaga kutoka Moshi” kwa sababu mama yake aliyejulikana kwa jina la Odilia Shayo alikuwa anatokea Kilema, Moshi mkoani Kilimanjaro. Baba yake alikuwa mzungu.

Ukiachilia mbali wimbo huo nyimbo zingine za marehemu na dada zake zilizotamba sana na zingali inapigwa mpaka leo katika sehemu mbalimbali zinapopigwa “oldies” ni pamoja na Chaupele Mpenzi, Mwalimu Shekinuru, Sisi kwa sisi, Hodi mimi mgeni, Kichupukizi, Bibi Maria Salome,Shida,Masuti Njiani, Nyoka Kabatini na kibao maarufu cha Harusi ambacho baadaye kilikarabatiwa na bendi ya Afro 70 na kuwa moja ya vibao vinavyopigwa hadi leo kwenye sherehe za harusi.

Katika ulimwengu wa muziki Marehemu Frank Humplink anasimama kwenye safu moja na Mzee Gabriel Omolo, Marehemu Fadhili William, Marehemu Fundi Konde, Marehemu Ahmed Kipande, Marehemu salum Abdallah na wengine wengi waliovuma katika miaka ya sitini. Ni hoja isiyo na ubishi kwamba majina kama hayo hapo juu ndiyo yanaweza kusemwa kuwa ni msingi wa muziki wa dansi Afrika Mashariki.

Marehemu ameacha mjane, watoto sita (watatu wa kiume na watatu wa kike),wajukuu kadhaa na kilembwe mmoja. Anatarajiwa kuzikwa jumamosi ijayo huko nyumbani kwake Lushoto mkoani Tanga alipohamia tangu miaka ya 60. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.

Page 1 of 3 | Next page