“SIJATETEREKA KWA CHOCHOTE,NIPO”-MR.NICE

 

Yakitajwa majina ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya ambao, kwa kutumia au kupitia muziki, wamekuwa ni “mabalozi” wazuri wa Tanzania katika nchi mbalimbali duniani, basi jina la Nice Lucas Mkenda au maarufu kama Mr.Nice ni vigumu au itakuwa sio uungwana likikosekana.

Tangu alipoibuka katika anga za muziki mwanzoni mwa miaka hii ya karne mpya, wengi wamecheza nyimbo zake, wakubwa kwa wadogo. Kwa wakubwa nyingi ya nyimbo zake zimekuwa zikiwakumbusha enzi zileeee… wakati kwa wadogo amekuwa akiwapa ladha ya wakati huo katika mirindimo ya kisasa. Nyimbo kama Kidali Po, Kikulacho na ule wa Fagilia ambao kwa muda fulani uligeuka kuwa kama wimbo wa taifa ni baadhi tu ya nyimbo zilizomfanya Mr.Nice asikike kila kona.

Katika siku za hivi karibuni, yamekuwepo maneno mengi sana juu ya msanii huyu. Yuko wapi? Mbona haonekani? Ni kweli kachacha na kufilisika kimuziki? Hivi nini kimemtokea? Ilimradi kila mmoja amekuwa na maswali yake na majibu yake mwenyewe hata kama sio timilifu.

Hivi karibuni kabla hajaungana na wasanii wenzake katika tour ya FIESTA, BongoCelebrity tulipata muda wa kufanya naye mahojiano yafuatayo ambapo alijibu maswali mengi yakiwemo hayo hapo juu ambayo wapenzi wa muziki wamekuwa na hamu ya kupata majibu yake. Anatarajia kutoa albamu yake mpya hivi karibuni. Kazi kwenu

BC: Unaweza kutueleza kwa ufupi historia ya maisha yako. Ulizaliwa wapi, ukasomea wapi na vitu kama hivyo?

MR.NICE: Mimi nimezaliwa Rombo katika mkoa wa Kilimanjaro tarehe 8/8/1978. Shule ya msingi nilisomea Ilala Boma jijini Dar-es-salaam kabla sijaelekea tena Moshi kusoma katika seminari ya Maua.

BC: Umekuwepo katika muziki unaojulikana kama muziki wa kizazi kipya kwa muda mrefu sasa. Ulianza vipi mambo ya muziki?

MR.NICE: Muziki ulikuwepo kwenye damu yangu siku nyingi sana. Kwanza nilikuwa mwimbaji mzuri sana wa kwaya makanisani kuanzia zile za watoto mahali kama pale kanisa la Msimbazi. Automatically nikajikuta napenda mambo ya muziki mpaka nilipokuja kuanza rasmi mwaka 2000.

BC: Je ulipokuwa mdogo maisha ya uanamuziki ndiyo maisha uliyokuwa ukiyatarajia mbeleni au?

MR.NICE: Kwa kweli sikufikiria kitu kama hicho. Mwanzoni sikuuchukulia muziki kama ndio itakuwa career yangu. Nilikuwa naimba kama hobby. Lakini baada ya mwaka 2000 ndipo liliponijia wazo kwamba huenda naweza ingawa bado nilikuwa sijiamini sana. Nikajaribu kutoa single yangu ya mwanzo iliyokuwa inaitwa Friday Night. Ile ndio ilinipa mwongozo na msukumo wa kuweza kufanya kazi za muziki maana ilipendwa ghafla bila hata mimi mwenyewe kujua. Kipindi hicho nilikuwa naishi na mama yangu mzazi Zanzibar kwa hiyo nilikuja Dar-es-salaam nikairekodi kasha nikaicha studio nikarudi zangu Zanzibar. Nilirekodi Mawingu Studio kwa rafiki yangu wa siku nyingi sana anaitwa Bony Luv ambaye mmojawapo wa maproducer wa mwanzo kabisa hapa Tanzania. Yeye kumbe ile nyimbo aliijua kwamba ni nzuri.Yeye ndio aliipeleka redioni bila hata kuniambia mimi. Kilichotokea ni kwamba wimbo ukaanza kupendwa bila hata kujua mwimbaji wake ni nani. Kwa hiyo mimi niko Zanzibar bila kujua chochote kinachoendelea ghafla nikaanza kuitwa kwenye interviews mbalimbali na matamasha nk.Huo ndio ukawa mwanzo wa muziki kujiingiza rasmi katika muziki.

 

BC: Unaweza kuielezea vipi style ya muziki wako? Kwanini uliamua kuiita TAKEU?

MR.NICE: Unajua mimi nilitoka tofauti kidogo na wasanii wengine.Kama unavyojua wasanii wengi wa Tanzania wanarap na kufanya style za hip hop. Sasa mimi nikawa naimba sio kwa R& B bali kufuatisha uasili na ndio maana ukitazama nyimbo zangu utakuta kuna mambo ya uasili hususani katika beats ambazo zipo kwenye uasili zaidi na sio commercial kama wanavyofanya wasanii wengi wa hip hop.. Kwa hiyo nikaamua kuuita TAKEU ambapo TA inasimama badala ya Tanzania na KE kwa Kenya na U kwa Uganda. Kwa hiyo ni nimejaribu kukusanya tamaduni za nchi hizi tatu za Afrika Mashariki na kuziweka pamoja. Na utaweza kuona kwamba baada ya hapo wasanii wengi pia wamekuja kuhamasika na kuanza kuimba wakitumia style hiyo. Kwa hiyo naweza kusema mimi ndio mwasisi wa TAKEU style. Kwa sababu mtu anajaribu kuimba na kusema ngoja niimbe kama Mr.Nice na kweli anakuwa. Kwa hiyo imekuwa ni style yenye mafanikio.Unaweza ukasimama mbele ya wadau wa muziki na kusema unaimba style ya TAKEU na ukaeleweka kwamba unaimba style ya Afrika tofauti na styles zingine kama hip hop ambazo kila mtu anajua kwamba ni ya kimarekani. Hiyo imenisaidia sana hata katika kujimarket na ndio maana unaniona imekuwa rahisi kwangu kupata show za nje. Hiyo inatokana na historia yangu, uimbaji wangu na hata uchezaji wangu.

BC: Maneno au tungo unazotumia katika nyimbo zako ni maneno ambayo yamezoeleka miongoni mwa watanzania tangu enzi na enzi. Nyimbo kama Kidali Po, Kikulacho nk. Unaweza kutueleza hatua kwa hatua katika jinsi unavyotunga nyimbo zako? Huwa unaanza na nini kwanza?

MR.NICE: Kwa kifupi naweza kusema mimi nina bahati ya kupendwa sana na watoto wadogo.Halafu nina bahati ya kupendwa pia na watu wazima wenye heshima zao. Sasa hapo kuna mambo mawili, ni lazima nijitahidi kukidhi haja za makundi hayo mawili ya watu kwa wakati mmoja. Kwa hiyo ninapokaa kutunga mashairi yangu nahakikisha kwamba kama baba, mama na mtoto wamekaa sebuleni wanaweza wakasikiliza au wakaangalia. Kwa sababu ukianza kuweka yale maneno mazito mzazi hawezi kukubali mtoto wake akasilikiza au mtoto hawezi kuyasikiliza mbele ya wazazi wake au akaangalia mbele ya wazazi . Kwa maneno mengine unakuwa umewatenga watu katika makundi fulani fulani.Lakini mimi nakuwa nipo kote kote. Ukichukulia nyimbo kama kidali po kwa mfano..wewe uliimba mimi niliimba, babu zetu waliimba, baba mama na hata watoto zetu wanaozaliwa sasa hivi bado wanauimba huo. Kwa maana hiyo hata usipoupenda wewe mwanao anaweza akakushawishi ukaupenda.Ukisikiliza utakumbuka jambo fulani au enzi fulani. Ninachojaribu ni kuepuka kurekodi wimbo ambao watu watashindwa kuangalia au kusikiliza mbele za watu kwa sababu ya kuona aibu jambo ambalo linamfanya mtu asiwe na jinsi bali kuzima TV au redio.

Pia nyimbo hizi zinanisaidia kujenga urafiki wa kudumu na watoto kuanzia wakiwa wadogo.Kwa maana hiyo jina langu litaendelea kuwepo vichwani kwao kwa miaka mingi sana ijayo. Pia kwa sababu napiga miziki ya kuburudisha zaidi inakuwa inanipa heshima kwani ndio maana napata mialiko mingi. Wanaonialika wanakuwa wanajua kwamba tukimleta Mr.Nice hapa tutapata show nzuri na ya heshima isiyo ya kihuni. Huwezi kumfukuza mtoto kwa sababu wimbo wa Mr.Nice umeanza kupigwa.

 

Mr.Nice akiburudika na watoto.

BC: Kuna wakati ulikuwa ndio msanii anayelipwa au ghali zaidi (kwa kila tamasha) kuliko msanii yeyote Afrika Mashariki. Ni kitu au vitu gani ulivyovifanya au kununua kutokana na kipato “kinene” kama msanii?

Page 1 of 6 | Next page