TUNAMUITA “MZEE WA MACHARANGA”!

Kunako miaka ya 80 mpaka 90 ushindani wa soka nchini Tanzania ulikuwa ni wa aina yake. Ilikuwa ni kama kosa la jinai kusema wewe huna timu unayoishabikia baina ya mafahari wawili wa soka enzi hizo ; Simba na Yanga. Ilikuwa ni lazima uwe Simba au Yanga ! Kipindi cha michezo radio Tanzania cha saa mbili kasorobo usiku kilikuwa ni almasi.Hakuna anayetaka kukikosa !

Ni wakati huo huo ambapo kama ulikuwa huna fedha au muda wa kwenda uwanjani, hususani Uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam, bado ulikuwa na nafasi ya kupata uhondo wa kinachoendelea taifa. Watangazaji wa Radio Tanzania walikuwa wanakupeleka « live » japo kimawazo tu uwanja wa taifa. Ulikuwa unapata msisimko wa kinachoendelea uwanjani kutokana na umahiri wa watangazaji wa mpira. Msisimko ulikuwa unazidi kutokana na vionjo na madoido ya watangazaji wenyewe. Kila kona ya nchi wapenzi wa soka ambao hawakuweza kufika Uwanja wa Taifa walikuwa wameketi chini, wameizunguka radio wakisikiliza mpira kwa makini kabisa.Ole wako upige kelele bila sababu.

Charles Hilary akiwa kazini

Mmojawapo kati ya watangazaji waliokuwa wakiturushia uhondo ule kiasi kwamba bila hata kutaja jina lake, kila mmoja aliweza kumtambua kwa sauti yake tu ni CHARLES MARTIN BARNABAS HILARY NKWANGA (pichani) ambaye wengi tunamjua tu kama Charles Hillary au « Mzee wa Macharanga ». Hivi karibuni tulifanya naye mahojiano motomoto kabisa. Hapa utapata historia nzuri ya maisha yake binafsi na yale ya utangazaji, mtizamo na ushauri wake kuhusu soka la Tanzania hivi sasa nk. Lakini pia utapata kujua ni kwanini mpaka hii leo bado tunamuita « Mzee wa Macharanga » ? Angepewa fursa ya kuwaalika wageni wanne kwa chakula cha jioni angewaalika kina nani ?Anakumbuka kitu gani kuhusu enzi zake za kutangaza soka Uwanja wa Taifa na mengineyo mengi.

Hivi sasa Charles Hilary anafanya kazi BBC London ambapo pamoja na shughuli zingine za utangazaji wapenzi wa ligi ya soka ya Uingereza (Premier League) na wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC London bado wanapata fursa ya kuendelea kufaidi umahiri wake katika fani ya utangazaji hususani wa soka. Unaweza pia kusikiliza Idhaa ya Kiswahili BBC mtandaoni kwa kubonyeza hapa. Mahojiano kamili haya hapa ;

BC : Ulianza lini rasmi kazi ya utangazaji? Nini kilikuvutia kuingia kwenye kazi ya utangazaji? Uliwahi kufanya kazi nyingine mbali na utangazaji?

CH : Nilianza rasmi kazi ya utangazaji mwaka 1981 ingawa nilijiunga na Radio Tanzania mwaka mmoja kabla yaani mwaka 1980.Ilibidi kwa utaratibu wa wakati ule uzoee mazingira ya kazi kwa kipindi fulani,ukiwa unapanga kadi za salamu na mambo kama hayo na baadae unasoma masomo ya utangazaji ambayo yanahusisha mambo mengi ikiwemo namna ya kutumia mikrofone,utayarishaji wa vipindi,namna na kufanya mahojiano,vipindi vya muziki na siasa ya utangazaji,si unajua tena Radio ya serikali ni lazima upigwe msasa nk.Kwa hiyo baada ya mwaka mmoja nikaanza kazi ya utangazaji rasmi hiyo ni mwaka 1981 nikiwa kijana kabisa pale Radio Tanzania,ukumbuke kuwa wakati huo radio ilikuwa ni hiyo moja tu.

Nilivutiwa na kazi ya utangazaji tangu ningali mdogo tu. Nilipokuwa shule ya sekondari wenzangu wengi walikuwa wakipenda niliwakilishe darasa letu katika debate mbalimbali kwa maelezo kuwa nilikuwa naweza kujieleza kwa ufasaha. Hiyo ikanipa changamoto ya kuweza kusimama mbele za watu na kuzungumza bila soni. Hiyo hasa ndio ilinivutia kuingia kazi ya utangazaji wa Radio.Kwa umri wangu sasa wa miaka 48 sijawahi kufanya kazi nyingine zaidi ya hii ya utangazaji wa RADIO.

BC: Unaweza kututajia sehemu mbalimbali ambazo umewahi kufanya kazi kama mtangazaji?

CH: Nimefanya kazi ya utangazaji kuanzia mwaka 1980 hadi mwaka 1993 Radio Tanzania Dar es Salaam. Mwaka 1994 nilijiunga na Radio One ikiwa ni radio ya kwanza binafsi kuanzishwa nchini Tanzania.Wakati huo nikiwa mmoja wa waanzilishi wake pamoja na kina Mikidadi Mahmoud na Julius Nyaisangah.

Mwaka 2003 niliamua kuacha kazi Radio One na kujiunga na Radio DW Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani ambapo nilifanya kazi mjini Koln na baadae Bonn hadi mwaka 2006 nilipokatiza mkataba wangu baada ya kupata ajira Idhaa ya Kiswahili ya BBC London,ambako nilijiunga mwaka 2006 tarehe 14 mwezi wa august na nipo hapo hadi sasa.

BC: Wengi tunafahamu kwamba ulizaliwa Zanzibar mnamo mwaka 1959. Unaweza kukumbuka mambo gani ya visiwani Zanzibar wakati wa utoto wako?

CH: Kwa bahati pamoja na kuzaliwa Zanzibar lakini sikukaa sana kwani mwaka 1968 nilikwenda Dar es Salaam na kusoma huko ambako niliingia darasa la pili katika shule ya Mchikichini,Ilala Dar-es-salaam.Kwa hiyo siifahamu zaidi Zanzibar kuliko ninavyoifahamu Dar es Salaam. Hata hivyo jambo moja ninalokumbuka wakati wa utoto wangu ni lile la mwaka 1964 siku moja baada ya mapinduzi ya Zanzibar,ambako nikiwa na umri wa miaka mitano nilikoswakoswa risasi na mtu mmoja namkumbuka akiitwa Herman kwa vile alikuwa ni rafiki wa marehemu baba yangu nilikuwa napenda kumuita Baba rafiki,yeye pamoja na mzee wangu walikuwa ni askari polisi na walikuja nyumbani kwetu kule Jang’ombe na wakiwa na bunduki zao alianza kuiangalia kama ilikuwa na risasi au la na hapo wakati akiwa anafanya hivyo marehemu mama yangu akawa anamsihi aache kuchokonyoa hiyo bunduki kwani ni hatari. Basi Baba Rafiki akawa anaendelea tu na mikakati yake huku akitoa uhakikisho kuwa ile bunduki haikuwa na risasi na ghafla ulisikika mlio mkubwa kuashiria risasi ilitoka.Mimi wakati huo nilikuwa nimekaa mkekani nakunywa chai na ile risasi ikapiga hatua chache kutoka nilipokaa,kama ingenipata basi hapana shaka ingeuvuruga mguu wangu wa shoto.Kulikuwa na shimo kubwa nyumbani kwetu kutokana na hiyo risasi.Pamoja na kuwa na umri mdogo tukio lile halinitoki mawazoni.Hofu yangu kubwa ni kuwa utaalamu wakati ule wa mtu kuingiwa na risasi sijui kama ulikuwepo wa kuweza kuitoa au pengine mguu ungekatwa sijui lakini namshukuru Mungu.

Tukio jingine ni kuondoka Zanzibar na kwenda kuishi Dar es Salaam.Nakumbuka ilikuwa tarehe 11 Machi mwaka 1968. Pamoja na kwamba wakati ule Dar kama tulivyokuwa tukiita tulikuwa tunaiona kama ulaya lakini nilihuzunika kuwaacha ndugu na hasa marafiki zangu nikiwa na umri mdogo kwenda kuanza maisha mapya ugenini.Nashukuru nilizoea haraka maisha ya Dar na sasa inaniwia vigumu kuishi Zanzibar kwa zaidi ya mwezi mmoja jinsi nilivyoizoea na kuipenda Dar.

BC: Ingawa wapo baadhi ya watanzania ambao wanaweza kusema waliufahamu muziki kutoka nchi za Latino au “macharanga” hata kabla hujautambulisha rasmi, wengi wameusikia na kujenga mapenzi na aina hiyo ya muziki kupitia kwako. Nini kilikuvutia katika aina hiyo ya muziki? Nani aliutambulisha kwako na kwanini ukauita “macharanga”?

Page 1 of 6 | Next page