Wengi wetu tumetokea kumjua kama Fresh Jumbe ila kwa kirefu na kikamilifu jina lake ni Fresh Jumbe Mkuu Waziri Kungugu Kitandamilima.Kila mwaka ifikapo tarehe 19 mwezi wa kumi (Oktoba) husheherekea kumbukumbu ya kuzaliwa.Alizaliwa mwaka 1968 katika hospitali ya Ngamiani iliyopo katikati ya jiji la Tanga. Anatoka kwenye familia ya watoto nane, wanne wa kiume na wanne wa kike. Wazazi wake wote wawili wametokea wilaya ya Pangani mkoani Tanga.Mama
akitokea katika kijiji cha Bweni kinachoangalia mto Pangani na baba
kwenye tarafa ya Mkwaja kijiji cha Buyuni kitopeni kilichopo mpakani
kabisa kati ya wilaya ya Pangani na Bagamoyo.

Akiwa Tanga sehemu anayoiita nyumbani ni Makorora “Mti Mkavu” karibu kabisa na shule ya msingi Makorora ambayo ndipo alipoanzia elimu yake ya msingi kabla ya kuelekea Bakwata Sekondari kwa ajili ya elimu ya sekondari.
Hivi sasa Fresh ni mmojawapo wa “mabalozi” wetu nchi za nje kupitia muziki.Anafanyia shughuli zake za muziki nchini Japan.Lakini walio wengi bado wanamkumbuka Fresh akiwa na bendi maarufu nchini Tanzania kama vile Sikinde,Msondo,Bicco Stars,Safari Sound nk. Kwa hakika Fresh Jumbe ni mojawapo ya majina ambayo washika dau katika medani za muziki hawawezi kuyasahau.
Siku chache zilizopita,tulipofanya naye mahojiano Fresh Jumbe alitueleza mengi.Katika mengi hayo suala la muziki wa Tanzania, inaposimama bongo flava alilipa kipaumbele cha aina yake. Tunaweza kudiriki kusema kwamba Fresh ametoa changamoto ya aina yake kwa wanamuziki wenzake,yeye mwenyewe,mapromota wa muziki,wana habari na kwa ujumla washika dau wote wa muziki nchini Tanzania. Ni changamoto gani? Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo;
BC: Ulipokuwa mdogo kule Tanga unakumbuka ulikuwa ukisikiliza miziki ya kina nani? Je ilikuwa ni ndoto yako tangu utotoni kuwa mwanamuziki?
FRESH: Wakati wa utoto wangu nilikuwa nikisikiliza sana miziki ya wanamuziki wote kama vile kina Moshi Wiliam, Zahir Ally, Hassan Bitchuka, Shaaban Dede, Muhidin Mwalimu “Gurumo”, Cosmass Chidumule, Beno Villa, Shem Karenga, Msafiri Haroub, Hemedi Maneti, Salehe Kakere, Juma Mrisho “Ngulimba wa ngulimba”, Juma Ubao “King Makusa”, King Kikii na Ndala Kasheba. Pia nilikuwa nikisikiliza sana mabendi yote maarufu kama vile Msondo Ngoma, Sikinde, Bima Lee, Vijana Jazz, Urafiki Jazz, Safari Sound, JKT Kimulimuli, Mwenge Jazz, Polisi Jazz, Maquis, Mzee Makassy, Simba wa nyika, Tabora Jazz na nyinginezo. Pia nilikuwa nikisikiliza sana wanamuziki wa nje kama vile kina Franco, Tabu Ley, Verkys, Kanda Bongo Man, Pepe Kalle, Nyboma, Nzaya Nzayadio, Madilu System, Pepe Ndombe, Bob Marley, Michael Jackson, Lionel Richie, James Brown, Fela Kuti, Manu Dibango, Papa Wemba na wengineo. Nilimpenda sana pia Abeti Masikini kwa uimbaji wake. Pia nilizipenda sana bendi za Orchestre Kyam, Belabela, Fukafuka n.k.
Lakini zaidi ya wote hao, niliyekuwa nikimsikiliza zaidi, kuvutiwa naye na hata kutaka niwe kama yeye alikuwa ni hayati Marijani Rajabu “JABALI LA MUZIKI” Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi.
SIKIA SAUTI YA FRESH HAPA AKIWA DAR INTERNATIONAL NA JABALI LA MUZIKI KATIKA NYIMBO “BWANA MASHAKA” na “MASUDI”
Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.
Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.
Ndiyo, nilikuwa na ndoto ya kuwa muimbaji. Nakumbuka wakati fulani nikiwa bado katika shule ya msingi kule Tanga, niliwahi kuapa kuwa maisha yangu ya ukubwani, kama yatakuwa ni ya kimasikini au ni yakitajiri au vyovyote vile, basi yatakuwa yametokana na miziki. Niliapa kuwa uimbaji ndio utakaoongoza maisha yangu. Kwahiyo ndoto yangu hiyo nilianza kuifuatilia mapema tu nikiwa bado mdogo kabisa na matokeo yake ni kuwa, mpaka leo maisha yangu ni miziki na miziki ndiyo maisha yangu.
BC: Je jina la Fresh ni jina lako halisi au ni la kisanii tu? Kama ni la kisanii nani alikutunga jina hilo ?
FRESH: Fresh ni jina langu halisi. Jina langu kamili ni Fresh Jumbe Mkuu, au kwa urefu zaidi ni Fresh Jumbe Mkuu Waziri Kungugu Kitandamilima.
BC: Mbali na kuimba unaweza kutumia vifaa gani vingine vya muziki kama vile gitaa,ngoma nk?
FRESH: Pamoja na kuwa uimbaji ndiyo hasa shughuli yangu, pia nina uwezo wa kupiga kinanda (Keyboards), gitaa la besi na pia napiga ngoma zote tu ikiwa ni pamoja na konga na drums. Pia nina ujuzi wa kurekodi muziki na kuchanganya sounds.
BC: Ni wanamuziki gani ambao unadhani walisaidia kwenye uamuzi wako wa kujiingiza kwenye kazi ya uanamuziki?.
FRESH: Marijani Rajabu kutokana na utungaji wake, uimbaji wake na ufanyaji wake wa kazi akiwa jukwaani alinifanya nitake kuwa kama yeye. Mwingine ni kaka binamu yangu “Marika Mwakichui” ambaye alikuwa muimbaji wa bendi ya Tanga International ya Tanga. Yeye pia alikuwa muimbaji mzuri na ndiye aliyenipandisha kwenye jukwaa kwa mara ya kwanza ili niimbe baada ya kugundua uwezo wangu wa kuimba nikiwa bado niko darasa la sita. Alinipa moyo sana na kuniambia kuwa mimi naweza kabisa kuimba kuliko hata baadhi ya waimbaji wakubwa wa wakati ule. Kwahiyo namshukuru sana huyu brother kwa msukumo na msaada alionipa na kunifanya nijiamini na niingie kikamili kwenye miziki mpaka kufikia nilipofikia leo hii.
BC: Mojawapo ya nyimbo zako zilizotamba sana ni ule wa Tuhifadhi Mazingira. Ilikuwaje ukautunga wimbo ule wakati ule ambapo masuala ya mazingira hayakuwa yakiongelewa sana kama ilivyo hivi sasa?.
Page 1 of 8 | Next page