“NIPO TAYARI KUIKABILI CHANGAMOTO HII”-MICHUZI

Kama utani, miaka miwili iliyopita, mpiga picha maarufu nchini Tanzania, Muhidini Issa Michuzi, alianzisha kitu ambacho tunaweza kusema kimekuwa ‘a national phenomena kama sio international phenomena”. Alichokianzisha ni blog ambayo hivi leo ndio imetimiza miaka miwili tangu kuanzishwa kwake rasmi.

Kwa mara ya tatu Michuzi ametupa nafasi adimu ya kufanya naye mahojiano.Wakati huu tumeongea naye kuhusiana na siku hii ya kusheherekea miaka miwili ya blog yake, kutafakari pamoja muelekeo wa blog yake katika siku za mbeleni, ushauri wake kwa vyombo vya habari kuhusiana na tekinolojia n.k. Unajua Michuzi anaogopa mambo gani maishani? Nini siri ya mafanikio yake? Kwa majibu ya maswali hayo na mengine mengi haya hapa mahojiano kamili yanayoambatana na picha kibao;

BC: Kwanza hongera sana kwa kutimiza miaka miwili tangu uanzishe rasmi blog yako kule Helsinki, Finland. Karibu tena ndani ya BongoCelebrity.

MM: Ahsante sana kwa heshima hii ya kutinga tena katika BongoCelebrity kwa mara ya tatu. Kwa kweli nimehemewa kwa hilo na pia kubaini kwamba kweli siku hazigandi kwani ile kufumba na kufumbua miaka miwili imekatika toka niianzishe www.issamichuzi.blogspot.com kama mchezo vile kama ulivyosema kule Helsinki Finland siku kama hii. Nakumbuka muda ulikuwa saa saba na robo wakati tumetoka kwa mapumziko ya mchana ya mkutano wa Helsinki nami nikalekea chumba cha mawasiliano ambako nilimkuta kaka Ndesanjo Macha ambaye hakufanya hiyana nilipomuomba anielekeze namna ya kuanzisha blog. Baada ya hapo, na kama wanavyosema, mengine ni historia

BC: Hivi kwa nini unasherehekea leo na sio Septemba 8 siku ambayo Ndesanjo alikualika rasmi na hivyo tunaweza kusema ulianza rasmi ku-blogu?

MM: Swali zuri sana. Ukienda kwenye link ya huo mwezi September 2005 http://issamichuzi.blogspot.com/2005_09_01_archive.html) utakuta kwamba ukurusa wa mwezi huo wa kwanza kuanza kublogu unaishia Septemba 25, 2005 siku ambayo niliweka picha ya kuku anayelea bata. Maoni mawili yaliyotumwa siku hiyo ndiyo yaliyonifanya niamue kufanya kweli na sio utani kama nilipoanza hiyo Septemba 8. Hivyo kaa ukielewa mimi nahisi kwamba kama ni mimba iliingia Septemba 8 na blogu ikazaliwa Septemba 25.

Michuzi at 10 Downing Street,makazi ya waziri mkuu wa Uingereza.

BC:Muasisi wa blog za Kiswahili Ndesanjo Macha alipokuwa nchini Afrika Kusini hivi karibuni katika mkutano wa Digital Citizen Indaba alikaririwa akitoa mfano wa blog yako kama mojawapo ya mafanikio makubwa ya blogs za Kiswahili. Nini siri ya mafanikio yako?

MM: Siri ya mafanikio ni kuweka maslahi ya wadau mbele na yangu binafsi nyuma.Huwa sina raha kuwaacha wadau wangu wanaotegemea mambo mapya ama jambo jipya kila siku watoke patupu, labda iwe nina dharura nzito ama niko eneo ambalo halina mtandao.

Michuzi akiwa na wadau wake.

BC: Ni mambo yepi matatu uliyoyategemea na pia matatu ambayo hukuyategemea kutokea ulipoanzisha blog yako miaka miwili iliyopita?

MM: Duh! Hili ni bonge la swali. Haya, nitajaribu. Matatu makubwa ambayo nilitegemea ni (1) Kubobea katika fani ya mawasiliano ya kisasa na kujulikana dunia nzima (2) Kupata shida katika kuchuja pumba na mchele kwenye maoni (Ndesanjo alinikanya mapema kwamba endapo naamua kuruhusu anonymous na wakati huo huo kuchuja, nijiandae kwa kazi nzito; na kweli. Huwa kuna wakati nakuta maoni yanayohitaji kusomwa na kuchujwa zaidi ya 600, hasa hasa kama nitazembea kupitia blog mara tatu kwa siku), na (3) Kuona kwamba wadau wengi wana hamu ya kujua mengi, kucheka na kutaniana na kutambua watu ama sehemu mbali mbali duniani.

Matatu ambayo sikuategemea ni (1) Blog yangu kuwa maarufu na kujulikana na karibu kila mtanzania aliye nje ya nchi na pia hata watu wasio watanzania bali wazungumzaji wa Kiswahili. Siku hizi napata barua pepe toka vyuo vikuu mbalimbali duniani kuniuliza hili na lile na kuna mialiko kama mitatu hivi ya kwenda kutoa somo juu ya kuwa bloga wa Kiswahili (2) Kupata wadhamini (3) Kufanya watu wengine wahamasike na kujikuta wana hamu ya kuwa na blogs zao. Nami huwa napenda sana kusaidia watu kama hawa kwani peke yangu ama wachache tulio na blogu, hasa za picha, si wengi wa kutosheleza mahitaji kwani mambo ni mengi na Tanzania ni kubwa sana.

Michuzi na Hasheem Thabeet walipokutana huko Boston,Marekani mwaka jana.

BC: Kadiri siku zinavyozidi kwenda ni wazi kwamba watanzania wengi wanazidi kukutegemea wewe kupitia blog yako katika kuwaletea ” breaking news”,picha na matukio zaidi. Unajiandaa vipi kuendelea kukabiliana na changamoto hiyo?

Page 1 of 5 | Next page