“UREMBO SIO UZURI”-HASHIM LUNDENGA

Ni vigumu sana kuzungumzia mashindano ya urembo nchini Tanzania hususani yale ya Miss Tanzania bila kumtaja Hashim Lundenga au Uncle Hashim kama ambavyo wengi hupenda kumuita. Sio tu kwamba Hashim Lundenga ndio aliyafufua tena mashindano ya urembo mwaka 1994 bali kampuni yake ya Lino International Agency Limited ndio haswa mratibu wa mashindano hayo ambayo kila mwaka yanazidi kuwa maarufu na hivyo kuwa tukio linalosubiriwa kila mwaka kwa hamu.

Kwa mwaka huu wa 2007,mashindano ya Miss Tanzania huenda yakawa yameandika historia mpya kabisa nchini Tanzania. Mshindi wa mwaka huu,Richa Adhia, ni mtanzania wa kwanza mwenye asili ya Asia (India) kutwaa taji hilo.Isitoshe ushindi wake umepokelewa kwa hisia tofauti miongoni mwa watanzania jambo ambalo limebakia kuwa gumzo mpaka hivi leo.

 

Sasa ili kujua kwa undani kuhusu mashindano haya ya urembo huna budi kumuuliza Hashim Lundenga.Hivyo ndivyo tulivyofanya hivi karibuni katika mahojiano naye ambapo aliweka wazi nini kilimsukuma kufufua mashindano haya, anasemaje kuhusu ushindi wa Richa Adhia na nini watanzania tutegemee kutoka katika mashindano ya dunia (Miss World) mwaka huu? Pia Hashim anajibu swali ambalo limekuwa likiulizwa sana na wananchi;Je mashindano ya urembo ni kwa watoto wa “vizito’ peke yao?Haya hapa mahojiano kamili;

BC: Ulianza lini rasmi kujishughulisha na mashindano ya urembo? Ilikuwaje?

HL: Baada ya serikali kuamuru kufutwa kwa mashindano ya urembo mwishoni mwa miaka ya 1968 / 69 hapakuwepo na shughuli zozote za urembo hadi mwaka 1994.

Wazo la kurudisha upya mashindano ya urembo lilinijia baada ya mrembo wa kitanzania aitwaye Miriam Ikoa kushinda taji la urembo nchini Kenya. Kwangu niliona ni changamoto kwa vile niliona ni fedheha msichana wa kitanzania kufanya vizuri ugenini.

Nikaamua kuanzisha upya mashindano ya urembo nchini baada ya kufuata taratibu zote ambazo zilikuwa zinatolewa na serikali kupitia Wizara ya Elimu na Utamaduni [wakati huo] na chini ya Baraza la Sanaa la Taifa [BASATA] nikasajiliwa rasmi mwaka 1994 nikishirikiana na bwana Prashant Patel mfanya biashara ambaye alikuwa anamiliki hotel ya White Sands iliyopo Kunduchi jijini D’salaam. Toka mwaka huo mashindano yamekuwa yanakua mwaka hadi mwaka.

 

BC: Kumekuwepo na tafsiri mbalimbali kuhusiana na dhana “urembo”.Kwa mtazamo wako nini maana hasa ya urembo?

HL: Urembo ni sanaa. Urembo ni umaridadi, urembo ni hali ya mtu kujiremba kuwa msafi na kujiweka katika hali ya kupendeza.“Urembo sio uzuri” kuna wazuri na pia kuna warembo.

BC: Majuzi tulipoandika kidogo kuhusiana na mashindano ya mwaka huu ya Miss Tanzania mmoja wa wasomaji wetu aliacha swali akiuliza Tanzania imepata faida au hasara gani kutokana na mashindano ya urembo tangu mwaka 1994 mpaka leo?

HL: Tanzania inapata faida kubwa sana kupitia sanaa hii ya urembo kwa mfano:-

(1) Ajira: Mashindano haya yanasaidia sana kutoa ajira kwa washiriki na hivyo kuipunguzia mzigo serikali kwa kuwa na watu wengi wasio na ajira. Mchakato wa kumtafuta Miss Tanzania hufanyika nchi nzima. Kwa mkoa wa Dar-es-salaam kuna Vitongoji zaidi ya 15, Wilaya 16 kwa nchi nzima, na mikoa yote 20 Tanzania bara. Kuna Kanda 9 kwa nchi nzima na hatimaye washindi wa ngazi hiyo hushiriki katika fainali za taifa kila mwaka.

(2) Mashindano yote hayo hutoa ajira hata kama ni ya muda kwa makundi mengi ya jamii, kama mafundi cherehani, [kwa kushona mavazi mbalimbali ya warembo] mafundi seremala, [kwa kutengeza majukwaa [stage] n.k wapambaji, Washereheshaji, [MC] Wana muziki, wasanii wa kuchora, Matangazo, katika vyombo vya habari, na kadhalika, na kadhalika.

BC: Kwa muda sasa kumekuwepo na malalamiko kwamba mashindano ya urembo yanamdhalilisha mwanamke. Vazi la kuogelea ndio limekuwa likizungumziwa zaidi. Kwa mtizamo wako, kuna uhusiano gani kati ya udhalilishaji wa wanawake na mashindano ya urembo? Kama haupo unadhani malalamiko haya yanatoka wapi na yanatokana na nini?

HL: Ni lazima kwanza ufahamu kuwa mashindano yetu yanafuata taratibu na kanuni za mashindano ya urembo ya dunia, [Miss World] vazi la kuogelea likiwa ni sharti mojawapo, lakini ni vazi ambalo halitakiwi kumdhalilisha mtazamaji wala mvaaji mwenyewe. Miaka ya mwanzoni tulipata tabu sana na wanaharakati, lakini tuliwaachia wananchi wenyewe waamue, na walio wengi waliunga mkono vazi hilo liwepo. Katika vazi la ufukweni ndipo tunapo muangalia mshiriki / mrembo kwa vizuri zaidi umbo lake, kwani moja ya sifa ya ushindi ni lazima mshiriki / mrembo awe na umbo zuri. Sasa iwapo mshiriki / mrembo akivaa suruali au ushungi, utamuonaje umbo lake zuri?!??!Malalamiko zaidi yanatoka kwa wanaharakati nadhani unanielewa nikisema hivyo.

BC: Kumekuwepo shutuma kwamba mashindano ya urembo yanawabagua watu masikini kwani ili kuingia mashindanoni ni lazima ukawa na pesa kiasi fulani kwa ajili ya kununua mavazi,viatu nk. Unasemaje kuhusu hilo? Na je kama kuna ukweli ndani ya shutuma hizo ninyi kama kamati ya Miss Tanzania mnalishughulikiaje suala hili ili kuhakikisha hamkosi mrembo halisi kutokana na masuala ya kiuchumi?

HL: Mashindano yetu hayana ubaguzi kati ya watu masikini na matajiri, wote wanakaribishwa. Ni lazima ufahamu kwamba sanaa hii ya urembo inahitaji gharama kidogo, kwa mavazi, pamoja na kuhudumia mwili au ngozi ya mshiriki / mrembo. Ni lazima mshiriki / mrembo ajigharamie ili aweze kuonekana mrembo. Hatujawahi kupata malalamiko yoyote kutoka kwa mshiriki kwamba eti ameshindwa kwa sababu amekosa pesa za kujiremba na kuonekana mrembo, yapo mashirika hata watu binafsi ambao wapo tayari kumgharamia mshiriki kwa maana ya kumpa ufadhili / udhamini ili ndoto yake iweze kutimia.

 

Hashim Lundenga (katikati) akiwa na mbunge wa Kinondoni Idd Azan(kushoto) na katibu wa Baraza La Sanaa la Taifa Chief Shogholo Chali(kulia)

BC: Je ni kweli kwamba mojawapo ya vigezo mnavyovitumia katika kumtafuta mrembo wa ni wembamba? Kama ndio unadhani hii inapeleka ujumbe gani kwa watoto wadogo au watu wanene?

Page 1 of 4 | Next page