DR.ASHA-ROSE MTENGETI MIGIRO.

Tarehe 1 Februari mwaka 2007 ni tarehe ambayo Dr.Asha-Rose Mtengeti Migiro hawezi kuisahau kirahisi. Hii ndiyo siku alipokabidhiwa rasmi ofisi na majukumu ya unaibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa cheo ambacho tangu kuanzishwa kwake mwaka 1997 kilikuwa hakijawahi kushikiliwa na sio tu na mwanamke yeyote mweusi bali pia mwafrika yeyote. Kwa maana hiyo Dr.Asha-Rose Migiro ndiye mwanamke wa kwanza mweusi kushikilia wadhifa huo na pia mwafrika wa kwanza. Mwanamke mwingine ambaye ndiye alikuwa wa kwanza kushikilia cheo hicho alikuwa ni mzungu raia wa Canada Louise Frechette ambaye alianza kukitumikia cheo hicho mapema mwaka 1998.

 

Dr.Migiro anayo historia nyingine ya kujivunia. Yeye ndio alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania tangu nchi yetu ilipopata uhuru mwaka 1961. Aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje mwaka 2006.

Hivi leo Dr.Asha Rose Migiro ambaye ni mke wa Professa Cleophas Migiro na pia mama wa watoto wawili wote wakiwa wakike, ni fahari ya Tanzania. Ndiye “balozi” wa Tanzania anayetambulika kirahisi zaidi kimataifa hivi sasa. Yeye mwenyewe, katika mahojiano mbalimbali aliyofanya na vyombo vya habari kufuatia uteuzi wake, anasema uteuzi ule ulimshangaza lakini pia aliuona uteuzi wake kama sifa kwa bara zima la Afrika. Waliowahi kufanya naye kazi wanasema hawakushangaa kusikia kwamba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Kin Moon amemchagua Dr.Migiro kwa sababu ni mchapakazi, mnyenyekevu na msomi aliyebobea katika masuala ya sheria. Unyenyekevu, utu na uungwana ni sifa zingine ambazo zinafanya majumlisho ya siri ya mafanikio yake.

Dr.Asha-Rose Migiro na mume wake Prof.Cleophas Migiro.

Lakini Dr.Asha- Rose Migiro ametokea wapi? Historia yake inaonyesha kwamba alizaliwa Songea, Kusini mwa Tanzania mnamo tarehe 9 Julai mwaka 1956. Wazazi wake ni wenyeji wa mkoani Kilimanjaro ambako ndipo ilipo asili yake. Kikabila ni mpare.

Alianzia elimu yake ya shule ya msingi katika shule ya msingi Mnazi Mmoja iliyopo jijini Dar-es-salaam mwaka 1963 mahali ambapo aliposoma mpaka mwaka 1966 alipohamia shule ya msingi Korogwe iliyopo Korogwe,Tanga kuanzia mwaka 1967 hadi 1969 alipomalizia elimu yake ya msingi. Kuanzia mwaka 1970 hadi 1973 hapo alijiunga na shule ya sekondari ya wasichana WeruWeru iliyopo Moshi,Kilimanjaro. Kwa elimu ya high school Dr.Migiro kuanzia mwaka 1974, alisomea katika shule ya Sekondari ya Korogwe iliyopo Korogwe,Tanga ambapo alihitimu mwaka 1975.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam mwaka 1977 kuchukua shahada ya kwanza ya sheria. Alihitimu mwaka 1980. Baada ya hapo alifanya kazi ya uwakili kwa muda mfupi. Kuanzia mwaka 1982 hadi 1984 Dr.Migiro alirejea tena katika Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam kwa ajili ya shahada ya pili ya Sheria (Masters).

Dr.Asha-Rose Migiro akiwajibika Umoja wa Mataifa.

Safari ya kimasomo ya Dr.Asha-Rose Migiro haikuishia hapo kwani mwaka 1988 alijiunga na Chuo Kikuu cha Konstanz kilichoko nchini Ujerumani kwa ajili ya masomo ya kutoka chuo hicho hicho kikuu cha Dar-es-salaam mnamo mwaka 1984. Baada ya hapo alikwenda nchini Ujerumani kusomea shahada ya udaktari wa falsafa (PhD) katika masuala hayo hayo ya sheria katika Chuo Kikuu cha Konstanz ambapo alihitimu masomo yake mwaka 1992.

Kabla ya kuelekea Ujerumani, kikazi tayari alikuwa ni mwajiriwa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwa mkufunzi msaidizi mwaka kuanzia mwaka 1981 na baadaye, baada ya kurejea toka masomoni Ujerumani, kupanda katika ngazi za mhadhiri msaidizi, mhadhiri hadi mhadhiri mwandamizi, cheo alichokuwa nacho mpaka mwaka 2000 alipoingia kwenye siasa. Aliingia kwenye siasa na moja kwa moja kugombea ubunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa upande wa taasisi za elimu ya juu.

Dr.Asha-Rose Migiro na Raisi Jakaya Kikwete.

Baada ya kumalizika kwa uchaguzi, aliteuliwa na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, nafasi aliyoishika hadi mwaka 2005. Huyo ndio Dr.Asha-Rose Migiro, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, umoja ulioanzishwa mnano mwaka 1945 na wenye makao yake makuu New York nchini Marekani.

Page 1 of 3 | Next page