Mkasa wa maisha yake sio wa kipekee. Ni mambo ambayo yameshatokea na yangali yakitokea kwenye jamii zetu na pia ulimwenguni kote. Kinachoufanya mkasa wake uwe wa aina yake ni uwazi alioupa na pia uwezo wake wa kuusimulia kupitia sanaa kama ya muziki. Sauti yake ni kitu kingine ambacho kinasadia sio tu kusisimua wasikilizaji wa muziki wake bali pia kufikisha ujumbe anaotaka na anapotaka kuufikisha.

Hivi leo haimbi tena kusimulia kisa cha kusikitisha cha yeye kutelekezwa na baba yake mzazi tangu akiwa kichanga (baada ya mama yake mzazi kufariki) kwani anasema hayo yamepita. Leo anasimama kama mmojawapo kati ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya anayekubalika na kupendwa na mashabiki kibao.Bado mashairi yake yamesheheni visa vya ukweli hususani kwenye mambo ya mapenzi na mahusiano. Jina lake ni Abubakari Shaaban Katwila ambaye wengi hii leo tunamjua kama Q-Chilla ingawa bado jina la Q-Chief halijamuacha aende.
Albamu yake mpya ameiita “Tajiri wa Sauti”.Ipo sokoni hivi sasa. Lakini anasemaje kuhusu alipo hivi sasa kisanii na kimaisha? Uhusiano wake na baba yake mzazi ukoje hivi sasa? Q-Chilla pia ana habari za bendi yake anayotarajia kuizindua rasmi hivi karibuni ili aweze kuwapa burudani wapenzi wa muziki “live”.Unajua ameipa jina gani na kwanini? Kwa hayo na mengine mengi, soma mahojiano haya tuliyofanya naye hivi karibuni;
BC: Kwa faida ya wale ambao hawafahamu historia ya maisha yako,unaweza kutuambia ulizaliwa lini,wapi na ukasomea wapi?
Q-CHILLA: Jina langu kamili ni Abubakar Shaaban Katwila, nimezaliwa tarehe 18 Mei mwaka 1984 huko wilayani Muheza mkoani Tanga. Kwa maana hiyo nimezaliwa mwaka 1984. Kwa upande wa shule nilikuwa nahama hama sana kwa hiyo nitakutajia mbili tatu ambazo nilikaa muda mrefu zaidi. Nilianzia Muheza shule ya msingi kuanzia darasa la kwanza mpaka la tatu.Baada ya hapo nikahamia Dar-es-salaam ambayo ndio yakawa makazi yangu ya kudumu. Sikukaa sana ikabidi niende kusoma kwa mama yangu mkubwa nchini Botswana katika jiji la Gaborone. Pale nikasoma mpaka darasa la sita ambapo kwa bahati mbaya mama yangu huyo akafariki dunia. Baada ya hapo ndio ikabidi nirejee nchini Tanzania nikisindikizana na mwili wa marehemu. Baada ya kurudi nikajiunga na shule ya msingi Olympio kwa darasa la sita hadi la saba. Sekondari sikusoma sana kwani nilishindwa kuendelea na masomo kwa ukosefu wa ada.
BC: Unakumbuka nini kuhusu harakati zako za mwanzo kuwa mwanamuziki?
Q-CHILLA: Kwa uhakika kabisa mimi nashukuru mungu kwamba kwenye muziki sikupata sana tabu kuingia. Nadhani naweza kusema hii ni kutokana na kipaji nilichokuwa nacho na ujumbe uliokuwemo kwenye nyimbo zangu.Wimbo wangu wa kwanza ulihit na ndio ukawa mwanzo. Kwa hiyo matatizo ambayo wasanii wengi huwa wanayapitia kama vile kukaa nje huku mvua inanyesha au jua kali kumsubiri producer nk mimi mambo hayo hayakunipata sana.
BC: Mwanzoni ulijiita Q-Chief na hivi sasa unajiita Q-Chilla. Nini chanzo cha majina haya na kwanini ulibadilisha kutoka Q-Chief kwenda Q-Chilla?
Q-CHILLA: Jina la Q-Chief mwanzo wake ni mama yangu.Nilipokuwa mdogo alikuwa anapenda sana kuniambia kwa kunitania “you are so cute”. Sasa nilipoanza muziki nilitaka kuadopt ile “cute” lakini ikawa ngumu kidogo. Kwa hiyo kiusanii ndio nikaiweka Q badala ya C. Na Chief ilitokana na kwamba babu yangu alikuwa ni Chifu enzi hizo kwenye kabila la wabondei
Q- Chilla ni jina ambalo nilipewa na msanii mwenzangu Papii Kocha “Mwana wa Mfalme” wakati huo ilikuwa ni kabla hajafungwa jela.Hivi sasa yuko jela ambako anatumikia kifungo cha maisha. Kabla ya hapo tulikuwa tunaimba wote na tulifanya tour ya albamu zetu za mwanzo pamoja.Kwa kweli alikuwa ni msanii mwenye kipaji sana. Kwa hiyo yeye alikuwa anapenda kuniita Q-Chilla badala ya Q-Chief. Alipofungwa maisha nikaamua kulichukua jina hilo kama njia mojawapo ya kuendelea kumkumbuka.
BC: Naomba nikuulize swali ambalo hatujawahi kumuuliza mtu mwingine yeyote tuliyewahi kufanya naye mahojiano. Unadhani kwanini wewe hivi leo ni mwanamuziki na sio labda kwa mfano polisi,daktari,mwanasheria nk.Kwa maneno mengine kwanini uliamua kuwa mwanamuziki?
Q-CHILLA: Mambo mawili ya msingi nadhani ni kwamba kwanza nina kipaji na pili ni mapenzi ya mungu. Isitoshe bila elimu ni wazi kwamba ingekuwa ngumu sana kwangu mimi kufanya kazi labda za kiofisi au kwa mtu mwingine yeyote. Kwa hiyo nadhani mwenyezi mungu alishanipangia kwamba riziki yangu itatokana na muziki. Namshukuru mungu kwa hilo.
BC: Mojawapo ya mambo yaliyofanya muziki wako ukakubalika kwa haraka sana ni sauti yako.Pamoja na hayo kisa cha kweli cha kuzaliwa kwako na jinsi baba yako mzazi alivyokutelekeza kilivuta hisia za wengi sana. Uhusiano wako na baba yako ukoje hivi sasa?
Q-CHILLA: Mimi na baba yangu hivi sasa tuko okay. Ningali najifunza kusamehe, kusahau na kusema asante. Kwa hiyo mimi nimemsamehe na yeye pia amegundua kosa lake lilikuwa wapi. Pia nadhani ni vigumu sana kwangu kujua nini kilitokea wakati huo. Kwa hiyo cha muhimu ni kusameheana na kuendelea mbele.
BC: Sasa kwa sababu wewe mwenyewe ni baba pia, unadhani hiyo imekusaidia kidogo kumuelewa baba yako zaidi?
Q-CHILLA: Kweli kabisa. Hiyo pia imenisaidia na inaendelea kunisaidia. Naelewa zaidi nini mzazi anaweza kufanya na nini hawezi kufanya wakati mwingine.

Q-Chilla na msanii mwingine maarufu wa muziki wa kizazi kipya,TID.
BC : Tukirudi kwenye suala la sauti yako. Unafanya nini ili kuhakikisha kwamba sauti yako inabakia kuwa hivyo ilivyo?
Q-CHILLA : Kusema ukweli hakuna cha ziada ninachokifanya kuhusiana na kuhakikisha sauti yangu inabakia hivyo. Kama nilivyosema hapo mwanzo, naamini sauti na uimbaji ni kipaji kutoka kwa mwenyezi mungu kwa hiyo namuachia yeye zaidi katika kunilindia vipaji hivi.
BC : Msanii siku zote anategemewa au inasemekana ni kioo cha jamii. Kwa sababu hizo yapo mengi ambayo hayategemewi kutoka kwake au kumtokea. Mojawapo ni kupelekwa mahakamani au kutuhumiwa kwa vitu kama wizi nk. Wewe umewahi kutuhumiwa na pia kufikishwa mahakamani. Nini kilitokea? Una ujumbe gani kwa jamii kuhusiana na shutuma hizo? Kesi imeisha?
Page 1 of 5 | Next page