DR.REMMY ONGALA

Alipozaliwa wazazi wake walimuita Ramadhani Mtoro Ongala. Alizaliwa mwaka 1947 katika mkoa wa Kivu huko Democratic Republic of Congo ya leo ambayo hapo zamani kwanza iliitwa Belgian Congo kabla ya kuitwa Zaire. Familia yake iliishi katika eneo lililoitwa Kindu eneo ambalo halikuwa mbali sana kutoka mpakani na Tanzania. Baba yake alikuwa ni mwanamuziki mashuhuri pia akiwa mpiga ngoma kwa kutumia mkono na pia mbira. Pindi tu alipozaliwa familia yake ilihamia Kisangani.

Ipo habari kwamba kabla ya kuzaliwa kwake mama yake alipata ujauzito mara mbili lakini kwa bahati mbaya kila mara mtoto alifariki. Alipopata ujauzito mara ya tatu alienda kwa mganga wa kienyeji kumuomba ushauri afanye nini ili mtoto atakayezaliwa asiiage dunia pia. Bila kusita mganga wa kienyeji akampa ushauri wake. Akamwambia kwanza safari hii asiende kujifungulia hospitali bali akajifungulie maporini. Pia alipewa ushauri kwamba mtoto akishazaliwa asije akamkata nywele zake. Yote hayo yalitendeka na ndio kisa cha Remmy Ongala kutokata nywele zake kwa muda mrefu sana.

Mwenyewe anasema mwanzoni alikuwa anajisikia aibu sana kwa kuwa na manywele marefu namna ile mpaka hapo baadaye jina na taswira ya mfalme wa reggae ulimwenguni,hayati Bob Marley ilipopata umaarufu nchini Zaire, ndipo alipoipenda staili ile ya nywele kwani hata watu wengine pia walianza kuikubali na kuionea ufahari. Pia inasemekana Remmy alizaliwa akiwa tayari na meno mawili ya mbele kitu ambacho kilichukuliwa kama ishara ya baadaye kuja kuwa mganga wa kienyeji pia. Ingawa utabiri huo haukutimia, inasemekana huo ndio mwanzo wa yeye kujulikana hapo baadaye kama Doctor Remmy Ongalla.

Baba yake ndiye aliyeanza kumfunza mambo ya muziki tangia akiwa mdogo kabisa jambo lililomfanya aamini kabisa kwamba kama jinsi ambavyo watu wengine wamezaliwa kuwa; kwa mfano, madaktari, wanasheria,waalimu, wakulima nk, yeye alizaliwa ili awe mwanamuziki. Kwa bahati mbaya baba yake huyo alifariki dunia na kumuacha Remmy akiwa na miaka sita tu akiwa tayari ameshaanza shule. Lakini kutokana na ukosefu wa fedha na kwa sababu mama yake hakuweza kuendelea kumlipia shule, Remmy ilibidi aache shule.

Ilipofika miaka ya 60, Remmy tayari alikuwa ameshajifunza mwenyewe kupiga gitaa. Mwaka 1964 ulikuwa sio mwaka mzuri kwa Remmy kwani mama yake mzazi alifariki dunia jambo ambalo lilimuacha Remmy na mzigo wa kuwalea wadogo zake kwani yeye sasa ndio alikuwa mkuu wa familia. Bila elimu na ujuzi mwingine wowote,alilazimika kuanza rasmi kujitafutia riziki kupitia muziki. Ujuzi wake wa kupiga gitaa uliongezeka kwa kasi ya ajabu kitu ambacho kilimwezesha kuwa akitumbuiza kwa kupiga ngoma na gitaa katika hoteli mbalimbali katika sehemu mbalimbali nchini Zaire akiwa na bendi yake na vijana wenzake iliyoitwa Bantu Success.

Kwa miongo kadhaa iliyofuatia Dr.Remmy Ongala alizunguka katika sehemu mbalimbali za Zaire akiambatana na kupiga na bendi kadhaa maarufu za wakati huo nchini Zaire zikiwemo Succ s Muachana na ile ya Grand Mickey Jazz nchini Uganda.

Ingawa kwa ujumla alijifunza mwenyewe kupiga gitaa, mwenyewe anakiri kwamba muziki wa kutoka nchini Cuba ambao wakati huo ulikuwa unaanza kujipatia umaarufu barani Afrika, ulimsaidia katika kupata staili ya pekee katika upigaji gitaa. Kwa upande wa uimbaji anasema uimbaji wa Joseph Kabasele na wa Franco ulimsaidia kupata style yake ya uimbaji kama tulivyoizoea.

Mwaka 1978 Remmy aliingia jijini Dar-es-salaam baada ya kuitwa na mjomba wake ili aje ajiunge na bendi maarufu ya wakati huo,Orchestra Makassy, iliyokuwa chini ya uongozi wa mjomba wake huyo, Mzee Makassy. Huo ndio ukawa mwanzo wa maisha ya Remmy nchini Tanzania. Akiwa na bendi ya Orchestra Makassy, aliandika wimbo wake wa kwanza uliojulikana kama “Siku ya Kufa”, wimbo ambao aliuandika kumkumbuka rafiki yake aliyefariki. Wimbo huo ulianza kumpatia umaarufu.

Dr.Remmy Ongala alivyo hivi sasa.

Alidumu na bendi ya Ochestra Makassy kwa kama miaka mitatu hivi kabla ya mwaka 1981 kuhamia katika bendi ya Orchestre Super Matimila iliyokuwa ndio inaanza kuchipukia miaka hiyo. Hiyo ilifuatia Mzee Makassy kuhamishia bendi yake nchini Kenya. Jina la bendi hiyo, Matimila, lilitokana na jina la kijiji kimoja kilichoko kusini mwa Tanzania. Baada ya kujiunga kwa Remmy, bendi ya Matimila ilijiongezea umaarufu katika anga za muziki nchini Tanzania wakati huo. Bendi hiyo kwa wakati mmoja ilikuwa na wanamuziki kama 18 hivi ingawa kati yao wanamuziki 6 mpaka 8 tu ndio waliokuwa wanalikwaa jukwaa kufanya vitu vyao. Pamoja na hayo kila mmoja alikuwa anapata japo nafasi ya kupanda jukwaani kuimba au kupiga chombo/vyombo. Wakati huo ilikuwa imeshakuwa chini ya uongozi wa Remmy Ongala ambapo pia baadaye aliiunda upya na kuibadilisha jina na kuiita Super Matimila.

Miaka iliyofuatia ilishuhudia umaarufu wa Remmy ukiongezeka hususani kutokana na mashairi ya nyimbo zake ambayo yaliegemea katika kuzungumzia mambo halisi ya kijamii kama vile umasikini, siasa nk. Mkusanyiko wa mashairi yake ulijulikana kama Ubongo au akili.

Mafanikio ya Remmy na kundi lake zima la Matimila hayakuishia nchini Tanzania kwani katika miaka ya mwishoni ya 80 walianza kujipatia umaarufu nje ya Tanzania na Afrika. Mwenyewe Remmy anasema zali la kuanza kupata mialiko ya nje lilikuja kama mchezo tu. Anasema alimpa rafiki yake mmoja mzungu aliyekuwa anaondoka nchini Tanzania kurejea kwao Uingereza kaseti yenye nyimbo zao. Rafiki yake naye alipofika huko aliwapatia jamaa wa WOMAD (World of Music,Arts and Dance) shirika linalopandisha chati wanamuziki na wasanii mbalimbali kutoka katika nchi za dunia ya tatu. Jamaa walivutiwa na nyimbo zao na hivyo kuwapa mwaliko kushiriki katika maonyesho yao barani Ulaya ya mwaka 1988.

Baada ya kurudi kutoka Ulaya bendi ya Matimila ilitoa mkusanyiko wa nyimbo zao waliouita Nalilia Mwana ambamo zilikuwemo nyimbo zilizopendwa sana kama vile Ndumila Kuwili na Mnyonge Hana Haki. Mwaka 1989 Remmy na Matimila walirudi tena Ulaya kufuatia mwaliko mwingine wa WOMAD. Ni wakati huo huo ambapo walipata nafasi ya kurekodi kwenye studio ya kisasa zaidi ambayo ilikuwa inamilikiwa na mwanamuziki maarufu aitwaye Peter Gabriel. Studio hiyo ilikuwa inaitwa Real World Studios. Matokeo yake ni nyimbo maarufu kama Kipenda Roho nyimbo ambayo inasemekana aliuimba mahsusi kwa ajili ya mkewe mzungu muingereza ambaye wakati huo tayari walikuwa wameshazaa naye watoto watatu.

Mwaka 1990, Remmy na bendi yake ya Super Matimila walirejea tena katika studio za Real World ambapo walirekodi mkusanyiko wa nyimbo ulioitwa Mambo ambao ulikuwa na nyimbo kama hiyo ya Mambo (aliimba nyimbo hii kwa kiingereza pia ili kukidhi kiu ya wapenzi wake wasiojua Kiswahili) na nyinginezo kama ule wa “No Money, No Life” na “One World”.

Umaarufu wake ulizidi mwaka 1990 alipotoa wimbo wa Mambo Kwa Socks ingawa baadhi ya watu waliupinga kwa kusema kwamba “hauna maadili” ingawa kimsingi alikuwa anawaasa watu hususani vijana kutumia kondomu ili kuepukana na maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi.

Pamoja na yote hayo, miaka michache iliyopita Dr.Remmy Ongala aliamua kuachana na muziki wa dansi kwa madai ya kwamba umejaa mambo mengi ya kishetani. Remmy akaokoka, akatubudu dhambi zake na hivi sasa anamuimbia bwana. Mpaka hivi sasa ameshatoa albamu yake ya injili aliyooiita Kwa Yesu Kuna Furaha. Mapema mwaka huu alikuwa mbioni kukamilisha albamu yake ya pili. Bado anaishi Sinza (Kwa Remmy) mahali ambapo panaitwa hivyo kwa heshima yake.

Dr.Remmy Ongala(mwenye rasta) siku alipobatizwa.Pichani yuko na waumini wenzake.

Imeandikwa kwa msaada wa vyombo mbalimbali vya habari mtandaoni.

 1. Dinah, 20 October, 2007

  Kila la kheri ktk kutangaza Injili kupitia sanaa ya Muziki. Ni mtu muhimu sana katka hostoria ya sanaa ya Muziki.

  Kazi musuri!

 2. NDAKI GOMBERA, 20 October, 2007

  Kila la kheri Dr.Remmy umeitangaza sana nchi ya Tanzania,achilia mbali kuna kipindi serikali ilitaka kukugeuzia kibao eti sio raia kisa kumsifikia kipindi kile Mrema alipokuwa serious na kazi.

  Tupo pamoja.Alleluyah …..Ameni

  Naomba kuwasilisha.

 3. Kimori, 20 October, 2007

  You have turned 60 and you look capable still…It is never too late to serve the Lord after all you don’t loose anything!

  Preach the Word….all of it!

 4. maya65, 22 October, 2007

  ndaki unasema eti serikali ilitaka kukugeuzia kibao..je huyo remmy ni mtanzania?
  umeshasoma historia yake kuwa anatoka congo…harafu bado hujui kuwa ni mkongo!!!!
  au kwa kuwa amekaa sana hapo bongo?
  huyo jamaa ni mkongo na ataendelea kuwa mkongo!!!!

 5. hombiz, 22 October, 2007

  maya65 hebu acha ubwege wewe. Inabidi uende ofisi za uhamiaji ukapate dondoo juu ya sheria za uhamiaji. Dr Remi ni raia wa Tanzania hivi sasa ingawa ni kweli alizaliwa DRC. Kafuata sheria zote za uhamiaji na kutunukiwa uraia wa Tanzania baada ya kukidhi matakwa ya sheria za nchi ktk swala zima la uhamiaji. Hongela Dr Remi kwa kuitangaza tanzania na kuwa Mtanzania ingawa si wa kuzaliwa.

 6. maya65, 23 October, 2007

  “kukidhi matakwa ya sheria za nchi katika suala zima la uhamiaji” hayo matakwa aliyekidhi mbona hutuambii?
  ina maana hata wewe huyajui ila unashabikia tu… na wewe ni bwege tu?
  haahaahaaaa…..

 7. Colin, 23 October, 2007

  Dr remmy ni shujaa na mfano wa kuigwa kwa kizazi hiki na kijacho ni msanii wa kweli sio mwanamziki,Nyimbo za remmy zinafundisha,burudisha na zingine chache baadhi ya jamii haikizikubali kwa kile walichokiita maadili.Remmy huwezi kusema mziki wa dansi umejaa uhuni na shetani,hayo ni mawazo yako binafsi ,uhuni ulikuwa unaufanya wewe sio mziki wa dansi,Bangi na Umalaya vilikuwa ni vitu vyako binafsi na sio mziki wa dansi.Ulivyoona umezidiwa na rahaa na magojwa kanisa ndo likawa kimbilio ,bado tunaufeel mziki wa dansi .

 8. Mwl. Ngimbudzi Fredy, 24 November, 2007

  Mpendwa Remmy,
  Binafsi ninakupongeza kwa kumrudia Mungu na kuamua kumtumikia yeye siku za maisha yako kwa njia ya uimbaji.
  Nakutakia baraka zake Mungu na namwomba yeye akujalie afya na nguvu ili kupitia uinjilisti wako watu wengi wamrudie. Ikimpendeza yeye upite sehemu mbalimbali nchini ili utoe ushuhuda wako kwa wengine. Pita mikoani na vijijini kaseme Mungu anakusudi nao. Imba mpaka waisikie sauti yake Mungu.
  Bwana anakupenda sana Remmy.
  Ubarikiwe sana.

 9. Mie, 27 December, 2007

  Mwl. Ngumbudzi Freddy unapenda kufahamu waimbaji wa injili Tanzania? karibu http://www.strictlygospel.wordpress.com
  Ubarikiwe sana

 10. hombiz, 03 May, 2008

  Wewe maya65 hii ni kwa ajili yako

  Uraia wa kuandikishwa, raia wa nje atapata uraia wa Tanzania wa kuandikishwa kwa kuomba kwa Waziri mwenye dhamana ya uraia na pia ombi lake liwe limekidhi masharti yote ya kisheria ambayo ni:-

  – Awe amekaa nchini mfululizo kwa kipindi kisichopungua miaka 10;

  – Awe ni mwenye manufaa kwa Taifa kiuchumi, kisayansi, kiteknolojia, maendeleo ya jamii au utamaduni;

  – Awe na uwezo wa kuongea kwa ufasaha lugha ya Kiswahili au ya Kingereza au lugha zote mbili;

  – Awe ni mwenye tabia njema na alipojitangaza kwenye gazeti hakutolewa pingamizi na mtu yoyote; na

  – Baada ya kupata uraia aonyeshe utii kwa nchi na nia ya kuishi nchini muda wote.
  Hayo ndio matakwa ambayo Dr.Remmy Ongala ameyatimiza na kufanikiwa kupata uraia wa Tanzania.

 11. Joji, 06 May, 2008

  Namwunga mkono Colin (N 7).

  Hasa zile nyimbo za zamani zitafanya Dr Remmy atakumkukwa kwa miaka mingi, au niseme daima na milele. Yeye mwenyewe aliimba : ‘Muziki sio uhuni’. Muziki wake – hasa zile nyimbo za kabla ya kuokoka kwake – ni zawadi kutoka kwa Mungu!

  Dr Remmy Ongala alikuwa nabii. Lakini kama manabii wa kweli aliimba jangwani… Nasikitika sana wimbo wake bora zaidi ‘Mambo kwa soksi’ ulipigwa marufuku na mpaka sasa haupatikani kwenye CD.

 12. Gandu, 09 September, 2008

  Mbona Remmy ! unatoa historia ya Uhongo?
  wakati wewe unasema umeokoka! na huku unaongopa?

  (a) umezaliwa katika kijiji cha Kindu kule Bukavu?
  upande moja wa wazaziwako ni Mmanyema na upande wa
  pili ni Mmayoke!
  Ulipozaliwa unasema ulipewa jina la Ramadhani Mtoro
  yaani mtoto alezaliwa na meno
  Kutokana na maelezo yako ya majarida mbali mbali ya siku za nyuma!
  (b) Ulipokuja Tanzania kwa mara ya kwanza kutoka kwenu
  ulikuwa (bitoz) mzuri mwenye nywele fupi katika miaka 19975
  hata picha zako za siku za nyuma zinaonyesha hivyo!

  Sasa hapa ukisema kuwa ulikuwa na nywele ndefu kwa sababu ya ushauri alipoewa mama yako kutoka kwa mganga wa kienyeji! kidigo unadanganya!

  Kuanzia miaka ya 1980s ndipo ulipoanza kuweka Rasta… na kabla yako kuna yule mpiga gitaa wakowa mwanzo Kassongo mliyekuwa naye makassy ndiye aliyeweka rasta

  Jaribu kuwa mkweli wewe sasa unamwimbia bwana…ALELUYA
  bwana Ramadhani Mtoro Ongara Karimagonga ukifika
  Kindu,Uvila na Kalemi tusalimie

 13. noel, 20 May, 2009

  BWANA ASIFIWE SANA,SONGA MBELE NA YESU, ILA ONGEZA BIDII KTK KUTOA INJILI KWA NJIA YA UIMBAJI KAMA MWENZAKO CHIDUMULE, DUNIANI HUKU HAKUNA DEAL USIKAE MBALI NA COSMAS AKUPAGE USHAURI ILI USONGE MBELE

 14. salum, 29 August, 2009

  KWNZA WALA SIO MBONGO HUYO.

 15. momo, 02 November, 2009

  Well, Wa bongo mna nuka roho mbaya mtu akiomba uraiya na akipewa yeye ni raia. Kiufupi ongala ni mbongo kama amepewa uraiya yeye ni mbongo, Asilimiya ya watu ulimwenguni ni wahamiaji so what? nini midomo ya chachu inaleta malumbano. Huyu mbomgo ametutangaza katika kipindi chake na sote tuli mkubali. kwa kipindi hichi muacheni awaburudishe walio okoka kwani maisha ni mafupi hatujuwi lini na siku yake. well mr ongala I Im still having your tapes and I miss new songs from you. labda unaweza kutowa albamu moja na wana muziki wakizazi kipya kabla ya kifo chako. kanisa?

 16. SALUM, 13 December, 2009

  SASA MOMO WEWE NDIO UMEMPA HUO URAIA AU ULIKUWEPO ALIPOPEWA HUO URAIA.MBONA WENGI WANAO URAIA WA TANZANIA LAKINI SIO WABONGO. AU UNATAKA MFANO? NELSSON MANDELA. SASA SEMA MBONGO YULE?AU HUJUI TAFAUTI YA MBONGO NA MTANZANIA? MTANZANIA YEYOTE ANAWEZA KUWA AKIFUATA UTARATIBU WA WIZARA YA MAMBO YA NDANI. LAKINI MBONGO MPAKE UZALIWE HAPO.SASA HUKO NDIO KUNUKA ROHO MBAYA? AU NDUGU YAKO?.

 17. Daniyli Gubula, 16 December, 2009

  Nyimbo “Siku ya kufa” ni nyimbo namba wan! Lakini nyimbo “Sukuma” ni nyimbo nzuri wilewile. Nakumbuka sana Remmy alikaa nyumbani yangu kule Mbugani, Chuo Kikuu cha DSM.
  Danyeli

 18. alfred, 13 December, 2010

  mungu amlaze pema peponi amin
  bwana ametoa bwana ametwaa

 19. Mpenda Mkude, 13 December, 2010

  acheni kulumbana juu ya uraia wa mtu. Mwalimu aliwahi sema ukichunguza sana hutampata huyo anayejiita Mtanganyika!!!

 20. Noname, 13 December, 2010

  Bukavi ni mji mkuu wa Kivu. Remmy kazaliwa Kindu, Manyema.

 21. rogers msokelo, 14 December, 2010

  Do!!!! kila nafsi itaonja umauti , tutakukumbuka milele Dr Remmy kwa mchango wako kwenye tasnia hii ya music, tungo zako zitaendelea kusikika kwenye masikio ya wengi kwani ujumbe wake hauchoshi daima. BWANA AMETOA NA BWANA AMETWAA JINA LAKE LIHIMIDIWE MILELE aaaaaamen!!!!!

 22. samwel ringo, 14 December, 2010

  mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi jina la bwana lihimidiwe

 23. daniel wainaina, 14 December, 2010

  poleni sana jamaa na marafiki wa huyu msanii.
  mimi ni shabiki wake ambapo napenda nyimbo zake sana nikiwa huku kenya.nitamkosa sana
  kheri njema.

 24. Kashinje Graphix, 14 December, 2010

  Kazi ya Mora haina makona, twamshukuru Mwenyezi kwa kutuletea Dr. Remmy dunia naye akatimiza kazi yake ya kuielimisha, kuiburudisha na kuionya jamii katika mambo ya ulimwenguni hapa, alijua ipo siku atatoweka na kuwaacha wengine duniani. Sasa tujiuli tuliobaki tuliletwa tufanye nini duniani. Dr. Remmy apumzike kwa amani

 25. Sir Obeid (Mwana wa Mungu), 14 December, 2010

  Haleluyah,

  hakuna ki2 kizuri kama kufa katika Bwana, maana kuna maisha ya furaha tena ya milele baada ya haya ya duniani. NINA MBARIKI YESU KWA KUMWAHI REMMY NA KUMUOKOA KABLA YA KIFO CHAKE. Otherwise, hajafa huyo bali amepumzika tu ikiwa aliendelea vizuri na wokovu.

  Nawaasa wote kumrudia Bwana na kuyaacha yote ya dunia yaliyo chukizo kwa Bwana kama vile uasherati, pombe, sigara, nk ili muwe salama baada ya kufa kama REMMY. MUNGU AKUBARIKI Remmy.

 26. Pedro Macintosh, 14 December, 2010

  May his soul RIP sisi tulimpenda lakini mungu amempenda zaidi apumzike kwa amani.

 27. sawe, 14 December, 2010

  Jamani nawapa pole wote waliofikwa na msiba japo ni wa Taifa lakini nawapa pole sana ndg zangu.ila ninawasihi ya kwamba msifanye mashindano ya kuwa mnajua jinsi ya kumwelezea Dr Remmy la hasha, cha muhimu tutafakari sisi tutaondokaje. je tutakapokufa kama Remy tunakwendaje na wapi. ila mko vizuri katika kutambua historia ya mastaa wetu. Nawapa BIG UP SANA.!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!

 28. Kaunda Mbaka, 14 December, 2010

  Asante sana kwa maarifa yako ndani ya musiki. Mbinguni pia waimbaji wanatakikana. Karibu nyumbani. Sisi sote tukojiani.Kifo hakina huruma. RIP

 29. Atley, 16 December, 2010

  Amemaliza kazi yake kwa amani, tulimpenda ila mola wetu kampenda zaidi. Lala kwa Amani Mzee wetu

 30. isdory, 06 February, 2011

  nilimpenda sana doc.remy,hakika mungu ni mwema.ona anavyowaangaza hata wale ambao shetani alijaribu kujiapiza kuwa ni wake rasimi.mungu akuangaze kipenzi ongala.

 31. dj cool, 19 November, 2011

  Dr Remmy ni msanii ambaye hatosahaulika sio Tanzaniatu bali hata hapa kwetu BURUNDI nyimbo zake zitakumbukwa daima na hususani ile ya KIFOOOO kweli kifo hakina huruma. BWNANA AMETOA NA BWANA AMETWAA JINA LAKE LIBARIKIWEE

Copyright © Bongo Celebrity