Bila kusita tunaweza kuanza kwa kusema Lady Jaydee(pichani) ni miongoni mwa wanamuziki wa Tanzania ambao hawahitaji utambulisho mrefu sana miongoni mwa wapenzi wa muziki wa kizazi kipya popote walipo nchini Tanzania na duniani kote. Leo hii ukipenda waweza kumuita Jide au Lady Jaydee. Aliwahi pia kuwa na majina mengine lukuki.Unayakumbuka?

Pamoja na hayo jina lake rasmi ni Judith Daines Wambura Mbibo.Ukipenda unaweza kumuita Mrs.Gardner G.Habash jina ambalo ana haki zote za kulitumia kwani ameolewa na Gardner,mtangazaji maarufu wa Clouds FM. Judith Wambura alizaliwa mkoani Shinyanga tarehe 15 Juni,1979 kwa Martha na Lameck Isambua Mbibo ambao ndio wazazi wake.Inasemekana alianza kuimba akiwa na umri wa miaka saba.Alianzia kuimba kanisani kama ilivyo kwa wasanii wengi.Baada ya kumaliza shule,Lady Jaydee aliwahi kufanya kazi Clouds FM kabla ya kuamua kujikita kwenye uanamuziki moja kwa moja mwaka 2000.
Baada ya kudumu kwa muda mrefu kama solo artist,mwaka huu Lady Jaydee amefanikiwa kufanya mambo mawili muhimu.Kwanza alianzisha rasmi bendi yake iitwayo Machozi Band na pili kutoa albamu yake ya nne aliyoipa jina Shukrani. Kabla ya hapo alishatoa albamu tatu ambazo ni Machozi(2000),Binti(2003) na Moto(2005).
Leo hii ukitaka kumuona Lady Jaydee kifanya vitu vyake akiwa na bendi yake,Machozi Band, unachotakiwa ni kujongea kila Ijumaa usiku ndani ya ZHONG HUA GARDEN, Regent Estat- Ally Hassan Mwinyi Road jijini Dar-es-salaam. Hutojutia uamuzi wako.
Hivi karibuni tulifanya mahojiano na Lady Jaydee ambapo tuliongelea mambo kadha wa kadha yakiwemo yake binafsi kama mwanandoa,binti maarufu,kazi zake za kimuziki,matarajio yake ya baadaye na mengine mengi.
Ingawa albamu yake ya Shukrani imetoka miezi kadhaa iliyopita,hatukuona haja ya kutoongelea machache juu ya albamu hiyo ambayo kama zilivyo albamu zake zilizopita,hii nayo inasambazwa na GMC Wasanii Promotors ya jijini Dar-es-salaam.Hii ndio albamu yenye wimbo uliotamba sana mwaka huu wa Siku Hazigandi. Bado inapatikana mitaani na madukani kwa wale ambao wangependa kuinunua.Yafuatayo ni mahojiano kamili;
BC: Unaweza kutueleza wewe ni mtu wa aina gani kwa kutumia maneno yasiyozidi matano?
JIDE: Mwanamke mwenye kipaji, uwezo na fikra.
BC: Unakumbuka nini kuhusu maisha yako ulipokuwa binti wa miaka 18? Unadhani umebadilika kwa kiasi gani tangu wakati huo mpaka hivi leo?
JIDE: Kipindi hicho ndio nilikuwa namalizia form four pale Zanaki Girls, nilikuwa natokea katika matamasha ya wanafunzi nikiigiza nyimbo za kina Mc Lyte, Da Brat na wengineo.Nakumbuka nlikuwa rapper zaidi, msela zaidi na mgomvi kwa wastani wangu. Leo hii naangalia nyuma naona nimebadilika sana. Nimekuwa muimbaji zaidi, hata rap siwezi tena, nimeacha usela nimekuwa mwanamke zaidi, nina majukumu ya maisha, nimeacha ugomvi lakini usiingie katika reli yangu. Kwa kweli nimekuwa mkubwa/mtu mzima.
BC: Unakumbuka ilikuwa lini na wapi ambapo ulipanda jukwaani kwa mara ya kwanza kama msanii. Ilikuwaje?
JIDE: Jukwaani nimenza kupanda tangu nikiwa sekondari lakini nakumbuka jukwaa la professional nilipanda kufungua shows ya Chaka Chaka na pia ya Brenda Fassie,wanamuziki kutoka Afrika Kusini ambao walikuja nchini Tanzania katika nyakati tofauti tofauti. Ilikuwa na msisimko tofauti. Nilikuwa muoga sana lakini nakumbuka nilipokelewa vizuri, hadithi za wakubwa zangu kina Bonie Love, Mr C, Ruge, OJ nk wanasema watu walipenda “sauti ya haka katoto”.

Lady Jaydee(katikati) ametoka mbali.Pichani ni enzi hizooo akiwa katika pozi na msanii mwenzake wa muziki wa kizazi kipya, Ray C(kushoto) pamoja na mtangazaji,mchota katuni,mbunifu wa mitindo,Masoud Kipanya (kulia)
BC: Hivi karibuni umetoa albamu uliyoipa jina Shukrani jambo ambalo limepelekea watu waanze kujiuliza kama ndio unasema kwaheri katika mambo ya muziki au? Kwanini umeiita albamu yako Shukrani?
JIDE: Nina mapenzi ya kweli na muziki, pia muziki ndio ajira yangu, sina nia ya kuacha. NDIO KWANZA NIMEANZA. Albamu ya Shukrani ni namna ya mimi kucheki nyuma na kusema asante kwa Mola, Wazazi, Wadau wa muziki,wapenzi wa muziki wangu na Watanzania kwa ujumla. Wamepokea kipaji changu na kunikuza katika hatua hii ya kwanza muhimu.
BC: Inakuchukua muda gani kutengeneza albamu kama hii ya “Shukrani”?
JIDE: Muda wa kutengeza albam unatokana na malengo ya msanii. Shukrani nimeitengeza polepole kama kwa miezi kama 11 hivi.
BC: Umewashirikisha wasanii gani katika albamu hii? Ina nyimbo ngapi?
JIDE: Ina nyimbo 12, nimewashirikisha Mad Ice, Nako 2 Nako na Chamilion.
BC: Unaweza kutuambia kidogo kuhusu mlolongo mzima wa kutunga wimbo,kuupa beats na kisha kuuweka kwenye video? Wewe kama msanii unashiriki vipi katika zoezi hilo zima?
JIDE: Nikipata hisia ya wimbo kwanza inakuja melody, halafu naandika tungo kutokana na hisia zangu au stori fulani, kisha nawekesha muda wa studio na mtengenezaji ninayeamini atamudu wimbo nilionao. Tukiwa studio mara nyingi huwa mimi naimba kibwagizo halafu producer anapiga kufuatana na ninavyoimba. Kitu kinatoka.

Lady Jaydee akiwa nyumbani kwake.
BC: Mwaka huu umeanzisha bendi ijulikanayo kama Machozi Band na hivyo kuanza kuperform nyimbo zako “live”. Nini kilikusukuma katika kuanzisha bendi hiyo? Unatoa ushauri gani kwa wasanii ambao bado wanatumia ‘playback” katika maonyesho yao?
JIDE: Niliwahi kukutana na Oliver Mutukuzi(mwanamuziki kutoka Zimbabwe anayeheshimika sana barani Afrika na duniani)huko Sauzi mwaka 2002 nadhani. Akanishauri niwe naweka milio ya vyombo live wakati wa kurekodi, nikaanza kufanya hivyo katika albamu ya ‘Binti’ nikaona inapendeza na inadumu zaidi. Basi nikafikiria si vibaya hata onyesho liwe live pia. Basi tangu hapo nliendelea kupiga live japo kwa band za zing zong. Muda ulipofika nikaona niwe na kundi langu mwenyewe. Nashukuru ngoma imekubali na sasa tunapiga gig kila Ijumaa.
Nashauri artists watumie live pale inapobidi, si lazima kila mtu awe na band, lahasha, maana ni gharama sana lakini ni muhimu kwao kujua kutumia band.

Page 1 of 5 | Next page