“UTANGAZAJI NI KIPAJI,LAKINI…”-DINA MARIOS

 

Wiki chache zilizopita tulipoweka picha ya mtangazaji Dina Marios wa Clouds FM, mvua ya maoni ilianza kumwagika. Wasomaji wengi wakaonyesha kutamani sana kusoma mahojiano kamili na Dina Marios.BC hatukuwa na jinsi bali kumsaka Dina ili kukidhi haja ya wasomaji na watembeleaji wetu ambao kimsingi ndio “wafalme na malikia” wa BC.

 

Kipindi maarufu anachoendesha Dina hivi leo kinaitwa Leo Tena kupitia Clouds FM kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa mida ya saa tatu asubuhi mpaka saba mchana. Umaarufu wa kipindi cha Leo Tena haujaanza leo.Ulianzishwa na marehemu Amina Chifupa.Haishangazi basi hivi leo kusikia watu wakimtaja Dina Marios kama “mrithi wa Amina Chifupa au anayekalia kiti alichowahi kukalia Amina Chifupa”.Lakini cha maana zaidi ni kwamba Dina anajitahidi kuendesha kipindi cha Leo Tena kwa kufuata yale yote mazuri aliyoyaanzisha AC na kuongeza mengi mengine.Ubunifu,kipaji na kiu ya kufanya vizuri zaidi kila siku ndivyo vinavyomsaidia.

 

Hivi karibuni,katika kuitikia hiyo “popular demand” ya wasomaji na watembeleaji wetu,tulifanya mahojiano ya Dina Marios.Tulipofanya hivyo tuliongelea mengi yakiwemo masuala kama anajisikiaje kuwa mrithi wa Amina Chifupa hivi leo hususani baada ya kufariki(Dina alimrithi Amina pale Clouds FM kabla hajafariki).Unajua Amina Chifupa alimuomba Dina ampigie wimbo gani ambao Dina anauona kama ndio ulikuwa wa kumuaga? Je ni kweli sauti yake inafanana na ya marehemu AC kama ambavyo wengi husema?Yeye mwenyewe anasemaje?Kwa hayo na mengine mengi fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo;

 

BC: Kuna nyakati tungependa kuanza bila kukuuliza juu ya historia yako.Lakini kwa sababu hii ni mara yetu ya kwanza kufanya nawe mahojiano basi hatuna jinsi.Hivyo kwa kifupi tu unaweza kutueleza juu ya historia ya maisha yako?Ulizaliwa wapi,ukakulia wapi,ukasomea wapi,unatoka kwenye familia ya watoto wangapi nk?

DM:Kwanza asante kwenu BongoCelebrity kwa kuniweka karibu na wasikilizaji wangu kupitia kipindi cha Leo Tena.Mimi ni wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto wanne nikiwa ni msichana pekee katika familia. Nimezaliwa mkoani Arusha tarehe 23 Novemba.Baadaye kidogo familia yetu ikahamia hapa Dar nikiwa na miaka 7.Nikaanza elimu ya msingi katika shule ya msingi Ushindi.Nilipofika la nne nikahamia boarding school huko Iringa katika shule ya Lyalamona na kuhitimu mwaka 1998. Nilianza kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Shauritanga mkoani Kilimanjaro na kuhitimu kidato cha nne mwaka 2002. Kidato cha tano na sita nikasoma Mkwawa mkoani Iringa nilipohitimu mwaka 2004.

 

Sikuendelea na chuo kipindi hicho kwani nilikuwa napenda sana kuwa mwanamitindo na pia mbunifu wa mitindo. Nilikuwa nachora na kutengeneza nguo zangu mwenyewe kwa hiyo nikawa nipo Nyumba ya Sanaa katika kujifunza masuala hayo ya ubunifu wa mitindo.

 

Ndoto yangu ilibadilika siku niliyokuja jingo la kitega uchumi mwaka 2005 nikakutana na jamaa mmoja tukaongea mengi na yeye akanishauri niwe mtangazaji kwa sababu aliona nina sauti nzuri inayoweza kufaa kwenye utangazaji.Nikavutiwa na wazo hilo na ndio nikajiunga na chuo pale Royal School of Journalism.

 

Wakati huo huo, huyo jamaa aliniombea Times FM niwe nafanya mazoezi enzi za Taji Liundi. Sikukaa sana nikasafiri nikaenda Arusha kwa babu yangu mzaa mama.Kule nikakuta radio moja inayoitwa Triple A nikaomba kujiunga nikakubaliwa. Napo sikukaa sana Clouds Fm wakanichukua kuja kufanya Leo Tena kipindi marehemu Amina amechaguliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalumu.Ndio safari yangu Clouds FM ilipoanzia.

 

Dina Marios akiwa kazini.

 

BC: Nini kilikuvutia kuingia kwenye fani ya utangazaji?Unakumbuka ulipokuwa mdogo ni watangazaji gani ambao ulikuwa ukipenda kuwasikiliza?

 

DM:Nikiwa mdogo huwezi amini nilikuwa najua kuimba nyimbo za wakati huo,matangazo yote ya wakati huo kupitia Radio Tanzania.Lakini kipindi nilichokuwa nasikiliza kwa wakati huo, tena kwa umakini, ni cha Mama na Mwana cha Bi Debora Mwenda…hasa simulizi zake za ua jekundu,binti chura nk.Nilikuwa nampenda vile alivyoweza kuteka akili zetu wakati ule.

 

BC: Umewahi kufanya kazi zingine mbali na utangazaji?Unaweza kututajia?

 

DM:Hapana, japo natamani nifanye pia kazi nyingine ila kwa sasa mawazo yangu yapo katika kuisaka elimu zaidi.

 

BC: Watu wengi siku hizi wamekuwa wakikutaja wewe kama “mrithi wa kiti cha Amina Chifupa” hapo Clouds FM.Sasa ingawa ulianza kuendesha kipindi hicho kabla hata Amina Chifupa hajafariki,wengi tungependa kujua ulikipokea vipi kifo chake na je unadhani kifo chake kimekuachia jukumu gani katika kuendesha kipindi kama “Leo Tena”?

 

DM:Si vibaya watu kuniita hivyo japo waliniita hivyo hata kabla Amina hajafariki.Ila nazungumza hivi japo sio vizuri kwa sababu ameshaenda na mungu aipumzishe roho yake mahala pema pepo. Mwanzoni sikuwahi kuwa karibu sana na marehemu Amina ingawa nyakati za mwisho alikuwa ananifuatilia sana jinsi ninavyoendelea na alikuwa ananiusia mengi,hususani kwenye mambo kama playlist nk.Alikuwa ananitumia message na kuniandikia nyimbo za kupiga.Ananitumia message na akawa ananiambia hakuna kitu kizuri kwa mtangazaji kama kuwa na good playlist ya miziki.

 

Unajua nini????mara ya mwisho nimechat nae aliniambia atakuwa mshauri wangu kwa kunifuatilia pale atakapokuwa na nafasi ili kipindi cha Leo Tena kiendelee kuwa kizuri. Nikamwambia sawa nitafurahi kwa sababu nilikuwa nataka mtu wakunifuatilia na kuniongoza ili kipindi kibambe zaidi. Akaniambia tutaongea zaidi maana siku hiyo hakuwa na furaha then akaniomba wimbo wa Show Me The Way wa Papa Wemba.Toka hapo naamini nina jukumu kubwa la kuendeleza yote aliyoyaanzisha katika Leo Tena na zaidi.

Mhariri:Unaweza kuusikiliza wimbo huo kwa kubonyeza hiyo player.

Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.

 

BC: Baadhi ya wapenzi wa kipindi chako wamekuwa wakifananisha hata sauti yako na ile ya marehemu Amina Chifupa.Wewe mwenyewe ukijisikiliza unadhani kuna ukweli wowote katika hilo?Je Amina alikuwa ni mtangazaji ambaye ulikuwa ukifuatilia nyendo zake ili siku moja uwe kama yeye?

 

DM:Ha ha ha ha ha ha jamani yaani sijui nisemeje sijui kwa nini watu hufananisha sauti zetu. Hata nikipiga picha watu husema sura yangu inafanana na ya marehemu Amina.Lakini mimi mara nyingi husikiliza kipindi changu sidhani kama sauti yangu inafanana na ya marehemu Amina japo sio vibaya ikifanana. Unajua kipindi Amina anafanya Leo Tena na Kwa Raha Zetu sikuwa napata nafasi ya kusikiliza radio.Mtu niliyekuwa namuhusudu wakati huo ni Phina Mango.

 

 

 

BC: Kila kazi ina mazuri yake na mabaya yake.Kwa upande wako,unadhani ni mambo gani matatu unayoyapenda sana kuhusu kazi yako na yepi matatu usiyoyapenda?

 

DM:Ninachofurahi ni kwamba nina nafasi kubwa katika kuielimisha jamii.Huwezi amini sauti yangu huwafanya wengi wapate faraja ya kuja kunieleza matatizo yao yanayowasibu kwani hupata nafuu. Nina umri mdogo lakini nashukuru Mungu mpaka nashangaa kumbe jamii inanichukulia kama niliyekula chumvi nyingi kiasi cha kuyajua ya ulimwengu huu.Nashukuru sana kwa hilo na mimi bila kusita huwa nawashauri kwa uwezo nilio nao.

 

Pili napenda kwamba nina nafasi ya kuonyesha ubunifu wangu kupitia jingles za Leo Tena ambazo huandika mwenyewe,segment za kipindi topics za kuzungumza.Napenda mengi sana lakini tatu na mwisho napata nafasi ya kukutana na watu wengi ambao najifunza mengi kupitia kwao.

 

Sina ambayo siyapendi.Maudhi madogo madogo ni sehemu ya kazi.

 

Dina (wa pili kutoka kushoto) akiwa na watangazaji wenzake na mpenzi wa Clouds FM.Kushoto ni Gardner G.Habash,mpenzi wa Clouds(samahani jina hatuna) na Sakina Lyoka.Hii ilikuwa ndani ya Mkwakwani Stadium,Tanga wakati wa tamasha la Fiesta 2007.

 

BC: Kwa maoni yako,utangazaji ni kipaji cha kuzaliwa nacho au ni kitu ambacho yoyote anaweza akajifunza na kisha kumudu kuwa mtangazaji mahiri?

 

DM: Kwa maoni yangu utangazaji ni kipaji ndugu yangu na pia ukiendeleze na shule ili uweze kuwa wa ukweli ukweli. Ndio maana kila binaadamu ana ujuzi wa kufanya kazi fulani ambavyo naamini ni vipawa kutoka kwa mungu.

 

A usual charming face of Dina Marios.

 

BC:Lipo suala la jinsia kwenye kazi mbalimbali ikiwemo ya utangazaji au u-DJ.Jamii ya kitanzania bado haijazoea au haina DJs wengi wanawake.Unadhani ni changamoto gani ambazo DJ au mtangazaji mwanamke anakabiliana nazo ikilinganishwa na zile wanazokabiliana wanaume katika fani hiyo hiyo?

 

DM:Sipendi kuwashawishi wanawake wenzangu kufanya kazi isiyo na manufaa kwao kwa maana ya kipato,maisha magumu nk.Lakini kazi ya udj sio mbaya kwa mwanadada na si lazima iwe katika radio hata kwa kupiga katika kumbi mbalimbali za burudani na kwa jinsi ilivyozoeleka ni kazi ya wanaume iwapo wasichana watajifunza na kujitokeza belive me watazoa ajira tu. Hivyo cha msingi ni kukomaa tu kwani hakuna anayeweza kukuyang’anya maarifa yako.

 

BC: Mbali na utangazaji unapenda kujishughulisha na nini? Na ni mambo gani ya kijamii (mfano haki za wanawake,watoto,yatima nk) ambayo unapenda kujishughulisha nayo.Kwanini?

 

DM: Hivi karibuni nilipata na nafasi ya kuwa mwanachama wa kijiji cha watoto yatima cha SOS cha pale ubungo na nimepewa jukumu la kupeleka mtoto mmoja yatima kila mwaka kwa ajili ya kupata malezi yote muhimu ikiwemo malazi na elimu. Ni kijiji kizuri sana ambacho kinashughulikia ustawi wa watoto yatima.Wakifika hapo wanalelewa mpaka watakapoweza kujitegemiea wenyewe.Watoto hukuwa kwa heshima,usalama na upendo.Wanawake wengi hunijia na matatizo mengi ni vile sina uwezo natamani ningeweza kutatua tatizo la kila mmoja lakini sina uwezo ila ipo siku.

 

Sipendi niwe kama uwa lililokosa harufu kwa maana ya kuzungumza pasipo matendo ila mungu akinijaalia nitafanya mengi kwa wanawake wa jamii yangu.Hayo ndio mambo ambayo napenda kujishughulisha nayo zaidi ya kazi yangu ya utangazaji.

 

BC: Kabla ya kumaliza mahojiano haya tungependa kukuuliza kidogo swali binafsi.Je umeolewa au una mchumba?

 

DM:Jamani mhh..sijaolewa japo nina boyfriend.

 

Dina katika pozi tulivu.Anaelekea kusema “Pole,I am taken”

 

BC: Mwisho unatoa ushauri gani kwa vijana wanaotaka kuingia kwenye fani ya utangazaji hivi leo? Ujumbe wowote kwa wapenzi wa kipindi chako?

 

DM: Wanakaribishwa ila sio kazi ya kujaribu na ulelemama ni kazi ya kujitolea maana wengi hufanya wakidhani ni point ya mtu kupata umaarufu,kama una kipaji follow your dreams na kusoma pia ni muhimu.

 

Mwisho nawaambia wasikilizaji wangu tuwe pamoja kama kuna mengineyo wanapenda wanifahamishe kupitia dina@cloudsfm.co.tz

 

BC: Asante sana Dina kwa muda wako.Tunakutakia kila la kheri.

Picha zote kwa hisani kubwa ya MichuziJR.

  1. Samweli Ndunguru, 11 November, 2011

    UKWELI NI KWAMBA MIMI SIJAWAHI KUMSIKILIZA AKITANGAZA ILA TUU KUPITIA MANDIKO HAYA NAAMINI HUYU ANAKIPAJI HICHO NA ANAHITAJI MSAADA WA UIMIRISHAJI WA KAZI YAKE .

  2. fina mosses, 17 June, 2012

    Yani nlikuwa natamani sana kumuona dina, nimefurahi sn kwa sababu huwa nasikiliza leo tena. hongera,

Copyright © Bongo Celebrity