KWA KINA NA FREDDY MACHA

 

Kwa miaka nenda rudi, tangu miaka ya sabini,jina la Freddy Macha (pichani) limekuwa sio geni miongoni mwa wasomaji mbalimbali wa magazeti, vitabu vya hadithi fupifupi,wapenzi wa muziki na pia sanaa ya ushairi nchini Tanzania. Iwe unamfahamu Freddy kupitia muziki wake,makala zake au mashairi yake, utakubaliana nasi kwamba Freddy ni mojawapo ya hazina tulizonazo linapokuja suala zima la usanii. Wengi miongoni mwa wasomaji wa makala zake katika magazeti ya The Guardian na Mwananchi nchini Tanzania, wanakiri kwamba makala za Freddy huwa ni mojawapo ya sababu zinazowafanya wakati mwingine wadamke asubuhi na mapema ili mradi tu wasikose nakala za magazeti hayo hususani siku zinazochapishwa makala zake.

Wapenzi wengi wa muziki,ushairi, tamthiliya na ngoma mtakuwa mnamkumbuka Freddy Macha tangu alipokuwa na kundi la Sayari. Kundi hilo ambalo lilitamba sana mwanzoni mwa miaka ya themanini, ni mojawapo ya vikundi vichache vya sanaa nchini Tanzania vilivyopata mafanikio sio tu nchini Tanzania bali pia katika medani za kimataifa. Sayari liliwahi kufanya ziara kadhaa za kimaonyesho katika nchi mbalimbali za nje hususani za Ulaya enzi hizo.

Kwa upande wa uandishi,Freddy Macha alianza kunoa kalamu katika magazeti ya Uhuru na Mzalendo na baadaye kuwa mwanasafu(columnist) wa gazeti la kila jumapili la Sunday News hadi mwaka 1984.Freddy amewahi kushinda tuzo kadhaa za uandishi ikiwemo ile ya Ushairi ya BBC mwaka 1981 na hadithi fupi fupi ya Jumuiya ya Madola( Commonwealth of Nations) ya mwaka 1996.

Hivi karibuni, baada ya kumsaka kwa muda mrefu, tulipata nafasi ya kufanya mahojiano ya kina na mwandishi/mwanamuziki/mwalimu huyu ambaye hivi sasa anaishi London nchini Uingereza. Sasa kutokana na ukweli kwamba Freddy ni mmojawapo miongoni mwa wale watu ambao tunaweza kuwaitwa “wenye vipaji vingi”,tumeamua kuyagawa mahojiano yetu naye katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza, ambayo ndiyo hii unayoisoma leo, tumeongea naye zaidi kuhusu kazi zake za uandishi.Sehemu ya pili ambayo itawajieni baadaye kidogo,tuliongea naye kuhusu muziki,jamii na mengineyo kadha wa kadha.

Unataka kujua Freddy ametokea wapi?Amepitia mambo gani mpaka kufikia hapo alipo? Anasemaje kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, uandishi wa leo akilinganisha na ule wa zamani? Kwanini kitabu chake cha hivi karibuni amekiita Mpe Maneno Yake? Unafahamu kwamba Freddy aliwahi “kuzamia meli”?Ilikuwaje? Anasemaje kuhusu dhana za mawasiliano kama blogs? Kwa hayo na mengineyo mengi, fuatana nasi katika sehemu hii ya kwanza ya mahojiano yetu naye;

BC: Karibu sana ndani ya BongoCelebrity

FM: Ahsanteni…mambo?

BC: Poa kabisa. Tunayo furaha kubwa kupata nafasi ya kuzungumza nawe hivi leo.Labda tuanze kwa kupata historia yako kwa kifupi.Ulizaliwa wapi,lini,ukasomea wapi nk

FM: Nilizaliwa Old Moshi, mwaka 1955; wazazi wangu walihama hama kutokana na kazi ya Baba ya udaktari na walipiga muziki, Mama akiwa mwimbaji. Tuliishi Moshi mgombani na Bumbuli kule Tanga. Nilisoma huko huko Mgombani (Wachagga tunaita shamba mgombani shauri ya migomba na kahawa na mifugo); hadi mwaka 1967. Nikiwa darasa la sita nilihamia Arusha, shule ya Kaloleni. Aliyekuwa sasa mlezi wangu ni Shangazi Sara Materu ambaye alikuwa Mwalimu Mkuu maarufu wa Shule ya sekondari ya Arusha …akiitwa Mama Materu enzi hizo. Alichanganya tabia na mwenendo (ambao hadi leo anao) wa elimu bora, nidhamu, mapenzi na alinishughulikia vizuri sana.

Nilifaulu na kuingia Sekondari Ilboru, hadi mwaka 1972, baadaye nikaendelea sekondari Mzumbe, Morogoro kidato cha tano na sita hadi 1974.

Enzi hizo tulitakiwa kisheria kujiunga na jeshi la kujenga taifa (JKT) baada ya masomo. Niliingia kambi ya Mafinga mkoani Iringa na kisha kuanza kazi kwenye gazeti la Uhuru mwaka 1976. Kazi yenyewe sikuiomba, niliitiwa kutokana na makala na barua nilizokuwa nikiandika tangu nikiwa shuleni.

 

Freddy Macha(wa pili toka kushoto) enzi akiwa kidato cha nne pale Lutheran Secondary School, Ilboru,Arusha mwaka 1972.Wengine kwenye picha kutoka kushoto ni Mohamed Miro, Tony Sarwatt(marehemu), Barnabas “Bandindo”Sengati(marehemu) na John Meciri(marehemu). Picha na Emmanuel Yuda.

BC: Ingawa una vipaji vingi mbalimbali,kama ambavyo tutaviongelea vyote katika mahojiano haya,wengi tunakufahamu zaidi kama mwandishi.Nini kilikuvutia kuingia katika fani ya uandishi?

FM: Najulikana kama mwandishi nyumbani Bongo, lakini nchi za nje kazi yangu kuu ni mwanamuziki. Vitu hivi viko katika damu.

Nikiwa mdogo sikuwa mzungumzaji sana…nilipenda kusoma, kusikiliza, kutazama watu, kuchanganyikana nao lakini kuwasoma…Katika familia kulijaa waandishi, wataalamu na wanamuziki. Babu yangu (Mchungaji Anaeli Macha ) alikuwa mchungaji maarufu na mwandishi ,akachapisha vitabu kadhaa vya tabia, dini, familia na jamii. Pia shangazi zangu wengi walinipa moyo toka utotoni. Nakumbuka mmoja wao,Shangazi Eva, alikuwa akisifia barua zangu akisema “Freddy akiandika barua ni kama kitabu.”

Uandishi rasmi wa kijumuiya ulianza nikiwa kidato cha pili. Ilikuwa hivi. Nilipokuwa Ilboru nilikuwa nikisaidia baadhi ya wenzangu kuandika barua zao za mapenzi kwa akina dada (“girlfriends”) nikaanza kudai pesa. Wakati huo nilikuwa mwanachama wa kikundi cha vijana tukijiita “The Gringos.” Kuna wakati tulipigwa na wahuni na wanajeshi baada ya kuwaandikia wasichana fulani waliogombana na mmoja wetu barua. Zile barua nyingi niliziandika kutokana na ushauri wa kikundi hicho chetu.Zilikuwa si mchezo. Tuliishia kupigwa kishenzi na pia chapwa viboko vya faru na kulazwa hospitali.

Nilipokuwa nikisoma Mzumbe tulikuwa na bendi mbili. Ya walioimba Kiingereza, “Earthquakes” (niliyokuwepo) ikiongozwa na mkimbizi na mpigania Uhuru wa Afrika Kusini, Tabiso Leshoai na Mike Sikawa (aliyekuja kuwa mwandishi Daily News siku hizi yuko BBC anaandikia This Day)…ya pili ilikuwa ya muziki wa Kiswahili. Zote zilipewa moyo na marehemu Mbaraka Mwinshehe aliyekuwa akija pale Mzumbe kupiga piga dansi letu na dada zetu, wapenzi wetu wa shule ya Kilakala.

Page 1 of 8 | Next page