BIBI TITI,WIKIPEDIA

Ukiachilia mbali blogs au tovuti mbalimbali zinazojitahidi kuhifadhi historia au kumbukumbu za watu wetu mashuhuri mtandaoni,mradi kama Wikipedia ndio pengine unaongoza hivi sasa katika kuhifadhi historia mbalimbali,kuelimishana,kupashana habari nk.Uzuri ni kwamba Wikipedia inaandikwa katika lugha mbalimbali ikiwemo yetu ya Kiswahili. Burudani zaidi inakuja pale ambapo wote,mimi na wewe,tunaweza kuchangia katika kuziandika historia za watu wetu mashuhuri.Hapo hakuna mjuzi zaidi ya mwingine.Kila mtu anajua kitu fulani kwa hivyo anachangia. Kama nitaandika kwamba Tanganyika ilipata uhuru mwaka 1962,nitakuwa nimekosea.Bila kutoana ngeu,unaingia unanirekebisha tunapata ukweli.Huo ni mfano tu,Wikipedia ina maarifa mengi zaidi.

Kwa mfano; Hayati Bibi Titi Mohamed,pichani kushoto akiwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ni mtu mashuhuri na muhimu sana katika historia ya nchi yetu achilia mbali juhudi za ukombozi wa mwanamke.Pamoja na hayo,ukienda kwenye ukurasa wa Wikipedia wa Kiswahili,utakuta kwamba habari za Bibi Titi zimeandikwa kwa kifupi sana. Ni kama vile hakuna anayejua mengi kuhusiana na Bibi Titi,si watu wa enzi zake wala wa enzi hizi.Mbali na uchache wa habari za Bibi Titi kwenye Wikipedia,kwa ujumla mtandaoni habari zake zipo kwa uchache sana.Tunaishi katika nyakati mpya,za habari na mawasiliano ya hali ya juu.Ni muhimu tukazitumia katika kuhifadhi historia pia.Sio za Bibi Titi tu bali wengineo wengi waliowahi kutokea,waliopo na watakaoendelea kutokea nchini mwetu.

“Bibi Titi Mohammed ni mmoja wa wanawake wa kwanza kushika nafasi za ubunge na uwaziri nchini Tanzania na pia ni kati ya wanawake wa kwanza kujiunga na harakati za kugombea uhuru wa Tanganyika.

Mwaka 1969 Bibi Titi Mohammed alikamatwa na mwaka uliofuata alifikishwa mahakamani kwa kosa la kula njama ya kutaka kupindua serikali. Katika kesi hiyo, Bibi Titi alikuwa ni mwanamke pekee katika washtakiwa 7. Baada ya kesi hiyo kusikilizwa alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha. Hata hivyo, mwaka 1972 alisamehewa na rais Julius Nyerere

Ukienda kwenye ule ukurasa wa Wikipedia wa Kiingereza kumhusu Bibi Titi,utagundua kwamba pameandikwa mambo mengi kidogo kumhusu Bibi Titi. Kwanini? Mara nyingi tumekuwa tukiacha historia yetu,ya watu wetu,iandikwe na watu wengine.Wakiandika wanavyotaka wao,kwa kuipotosha, tunalalamika.Ajabu huwa hatuna muda wa kuirekebisha. Zamani tulikuwa na sababu,hatuna tena.

Kupitia kurasa kama Wikipedia,tunaweza rekebisha historia zetu.Kwanini leo usijiandikishe katika Wikipedia na kuanza kuchangia chochote unachokijua kuhusu historia,siasa,jamii zetu? Unaonaje kama tukianza na kupanua zaidi historia ya Bibi Titi Mohamed? Kumbuka unapohifadhi historia huhifadhi kwa ajili yako tu bali vizazi na vizazi vijavyo.Binadamu asiyejua historia yake ni….

Picha kwa msaada wa Issa Michuzi.

Page 1 of 3 | Next page