Ukishakuwa mtu maarufu na mwenye mafanikio fulani, ni jambo jema sana kujitolea,kwa njia moja ama nyingine,kuihudumia jamii yako. Wenzetu wa magharibi hupenda kusema (kwa kutumia lugha yao) “Giving back to your community”.Stara Thomas(pichani),mwanamuziki maarufu wa miondoko ya zouk nchini Tanzania,anatambua hilo.
Stara amekuwa mstari wa mbele katika kuelimisha na kuunga mkono juhudi za kuhakikisha vifo vya watoto na kina mama wakati wa kujifungua vinapungua kwa asilimia kubwa kama sio kutokomea kabisa.Kwa kifupi Stara ni “balozi” wa uzazi salama.Anafanya hivyo kwa kutumia kipaji chake,kupitia muziki wake. Mfano mzuri ni wimbo wa “Play Your Part” wimbo ambao umekuwa ukitumiwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa kama UNFPA.
Sauti yake ni mojawapo ya sauti ambazo zinatambulika kirahisi.Ukiusikia wimbo wake,ni rahisi kutambua kwamba huyo ni fulani. Mwaka 2003 alipata tuzo ya Mwimbaji Bora wa Kike nchini Tanzania. Mwaka huu wapenzi wa muziki wake watarajie albamu ya tatu kutoka kwake. Nini kinamsukuma katika kujitolea katika jamii? Nini mtazamo wake kuhusiana na muziki wa kizazi kipya?Ana ushauri gani kwa wadada wengine wanaotaka kujiingiza kwenye muziki?Je, ana mpango wa kuingia kwenye siasa? Ili kupata majibu ya maswali hayo na mengineyo,fuatana nasi katika mahojiano yetu na “mama wa zouk” nchini Tanzania
BC: Stara karibu sana ndani ya BongoCelebrity.Kwa kuanzia,unaweza kutueleza kwa kifupi tu historia ya maisha yako?Ulizaliwa wapi,ukasomea wapi na vitu kama hivyo?
ST: Mimi nimezaliwa Mwanza, ni mtoto wa tatu kwenye familia ya watoto wanne,mmoja akiwa ni mvulana na waliobakia ni wasichana.Mimi ni wa tatu kuzaliwa. Shule ya msingi nimesomea kwanza Lake Primary School huko Mwanza mpaka darasa la tatu nilipohamia Dar-es-salaam na kumalizia Upanga Primary School.Sekondari nimesomea Mzizima Secondary School.Baada ya Mzizima nilichukua Diploma ya mambo ya Tourism and Airlines.Baada ya hapo nikasomea mambo ya kompyuta nk ili kujiandaa na kazi ambapo nimefanya kazi mbalimbali kama vile Public Relations, kwenye tour and airlines mbalimbali kabla sijafanya kazi ya utangazaji wa radio East Africa Radio.
BC: Nini hasa kilikuvutia mpaka ukaamua kujiingiza kwenye masuala ya muziki?Na je unaweza kukumbuka baadhi ya majina ya wanamuziki ambao pengine uliwaona kama “role models” wako kiasi kwamba wakachangia uamuzi wako wa kuingia kwenye muziki?
ST: Kwa ujumla ni mapenzi binafsi tu katika muziki ndio yaliyochangia.Yes,majina kama Lionel Richie,Whitney Houston, Mariah Carey(huyu nilikuwa naimba sana nyimbo zake wakati nikiwa shule). Pia wanamuziki kama Papa Wemba, Tabu Ley,Mbilia Bel,Tshala Mwana, Yvonne Chakachaka walikuwa wananivutia.Wengi wa wanamuziki hawa nilikuwa nazisikia nyimbo zao nyumbani kwani baba alikuwa anawapenda pia na hivyo mara nyingi yeye ndio alikuwa akileta miziki yao nyumbani.
Kwa upande wa Tanzania, kwa ujumla bendi zote za wakati huo(bahati mbaya nyingi zimeshakufa) zilikuwa zinanivutia sana…hii ni pamoja na waimbaji wake.Ingawa hivi leo sikumbuki majina halisi ya wanamuziki wengi wa enzi zile,nyimbo zao nyingi bado zikipigwa hata hivi leo nazikumbuka vizuri.
BC: Wazazi wengi nchini Tanzania wamekuwa hawapendelei kuona watoto wao wakiingia kwenye masuala ya muziki kutokana na dhana (potofu) kwamba muziki ni uhuni.Kwa upande wako wazazi wako walichukulia vipi uamuzi wako wa kuingia kwenye muziki?
ST: Kwanza kabisa ningependa kukuambia kwamba wazazi wangu,wote wawili,walikuwa ni waalimu. Kwa hiyo ilikuwa ni ngumu kwa kiasi fulani.Lakini kama unavyojua tena,ukiwa mbishi unakuwa mbishi tu.Kwa hiyo tulikwenda hivyo hivyo,mara wanakubali mara wanakataa.Kwa bahati nzuri mimi nilikuwa sifanyi muziki katika namna ambayo wao walikuwa wanaifikiria.Kwa hiyo nilikuwa natoka kisha narudi.Hata kama walikuwa wanafoka mimi mwenyewe nilikuwa najua kwamba nikitoka siendi kufanya kitu chochote kibaya. Nadhani hili ni kawaida katika mahusiano ya mtoto na mzazi.Mara nyingi mzazi anakuwa anakazania zaidi kukusomesha.
Isitoshe,kipindi kile muziki ulikuwa haulipi ukilinganisha na ilivyo hivi leo.Maisha ya wanamuziki wengi wa wakati ule yalikuwa yanakatisha tama.Kwa hiyo wazazi walikuwa wakiona mtoto wao naye anataka kujiingiza kwenye muziki,lazima iwe ngumu.Lakini baadaye walipoona tofauti na pia nikawa nimeshakua,walikuwa hawana jinsi bali kukubali.Kwa hiyo mwanzoni ilikuwa ngumu.
BC: Wengi leo hii tunakufahamu kama “Mama wa Zouk” kwani miziki yako ipo zaidi katika staili hiyo ya muziki.Kwanini uliamua kupiga zaidi muziki wa aina hiyo na sio aina zingine kama chacha,rhumba nk?
ST: Unajua kusema ukweli siku za nyuma nilikuwa nikiimba pia aina zingine zote za muziki ikiwemo hiyo uliyoitaja. Nyingi wakati huo zilikuwa ni kukopi kutoka kwa wanamuziki wengine. Sasa wakati naingia rasmi kwenye muziki wa kitanzania(pindi ilipoonekana wazi kwamba muziki wa kitanzania/Kiswahili) sasa unakubalika zaidi na unalipa) nilikuwa nishakuwa mama.Kwa hiyo kabla sijaingia nikajiangalia mimi mwenyewe,umbo langu nk.
Hapo nikagundua kwamba miziki hii ya kibongo flava,sio yangu tena.Kwa hiyo nilikaa nikasema nataka nipige aina ya miziki ambayo hata nikisimama mbele za watu,wataukubali kutokana na mimi mwenyewe nilivyo na pia maudhui ya ule muziki ambayo yananiwezesha hata mimi nikisimama kwenye steji nicheze.
Hii ni tofauti na miziki kama bongo flava ambayo ukifika pale stejini inabidi urushe miguu,mikono n.k kitu ambacho kinakuwa tofauti ukizingatia muonekano wangu na mambo mengine.Kwa hiyo hizo ndizo sababu zilizonisukuma mimi kuamua kufanya muziki wa zouk kwani nilitambua kwamba nitakuwa comfortable zaidi na muziki huu.

BC: Stara,kitu kingine ambacho kinakutambulisha wewe zaidi ni sauti yako.Mara nyingi mtu anayefuatilia muziki wa Tanzania akisikia tu sauti yako anatambua kwamba huyo ni Stara Thomas.Nini siri ya sauti yako na unafanya nini ili kuhakikisha inabakia namna hiyo?
ST: Mimi nafikiri siri anayo Mungu mwenyewe.Nasema hivyo kwa sababu mimi mpaka naanza kuimba sikuwa najua kitu chochote kuhusiana na sauti.Nilikuwa naona ni sauti ya kawaida tu.Kwa hiyo nadhani ni Mungu tu ndio amenibariki na hiki kipaji na hivyo sauti pia amenipa yeye.
Page 1 of 6 | Next page