Habari ambazo zimetufikia hivi punde zinasema kwamba Rais Jakaya Mrisho Kikwete amechaguliwa kuwa Mwenyekiti Mpya wa Umoja wa Afrika (AU).
Rais Kikwete amechaguliwa katika kikao cha 10 cha Wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika kilichoanza leo huko Addis Ababa,Ethiopia na kinachotarajiwa kumalizika siku ya Jumamosi Februari 2,2008.Rais Kikwete anamrithi Rais wa Ghana,John Kofi Agyekum Kufuor ambaye amemaliza muda wake.
Kwa kawaida Mwenyekiti wa Umoja huo hupatikana kwa njia ya mzunguko wa kikanda (geographical rotation) ambapo kwa mujibu wa utaratibu huo, Mwenyekiti mpya alitakiwa kutoka miongoni mwa nchi wanachama zilizopo mashariki mwa Afrika eneo ambalo linazo nchi 14 ambazo ni Burundi, Comoro, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Madagascar, Mauritius, Rwanda, Seychelles, Somalia, Sudan, Tanzania na Uganda.
Raisi Kikwete anayaanza majukumu yake huku akikabiliwa na changamoto nzito kama hii ya mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini Kenya.BC inaungana na watanzania wote kumpongeza Rais Kikwete na kumtakia kila la kheri katika kazi zake yakiwemo majukumu mapya ya Uenyekiti wa AU.Wakati huo huo unaweza kuisoma hotuba ya Rais Kikwete ya kila mwezi,kwa mwezi huu wa Januari hapa
HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWA WANANCHI, 31 JANUARI, 2008
Ndugu Wananchi;
Ninayo furaha kwa mara nyingine tena kuzungumza nanyi kupitia utaratibu huu mzuri wa mawasiliano baina ya Rais na wananchi wa nchi yetu.
Jambo la kwanza ninalopenda kulizungumzia linahusu uzingatiaji wa sheria na taratibu za uhamiaji na kuishi nchini.
Ndugu Wananchi;
Tarehe 23 mwezi huu, nilimaliza ziara ya siku kumi Mkoani Kagera. Jambo moja nililoliona kwenye ziara hiyo ambalo sikufurahishwa nalo, ni ukiukwaji wa sheria na taratibu za uhamiaji na uingizaji mifugo nchini.
Kwa muda sasa, raia wa nchi jirani zinazopakana na Mkoa wa Kagera wamekuwa wakiingia na kuishi nchini mwetu kwa vibali vya viongozi na watendaji wa vijiji na kata. Baadhi ya watu hao pia wamekuwa wakiingiza mifugo kwa vibali vya viongozi hao hao.
Wageni hao wamekuwa wanaingia na kuishi nchini isivyo halali. Sheria na taratibu za uhamiaji zinatoa mamlaka hayo kwa Maafisa Uhamiaji tu na si vinginevyo. Viongozi na watendaji wa vijiji na kata hawana mamlaka hayo. Hivyo basi, vibali vyote walivyotoa viongozi hao si halali na havitambuliki. Napenda kurudia kauli yangu niliyoitoa Mkoani Kagera kwamba ni marufuku kwa kiongozi au mtendaji wa ngazi yoyote ile nchini kutoa kibali cha mgeni kuingia au kuishi nchini kama siyo Afisa wa Uhamiaji.
Ndugu wananchi;
Wageni wanaoishi nchini kwa kutumia vibali ambavyo havikutolewa na Idara ya Uhamiaji wanaishi isivyo halali. Wenzetu hawa wanatakiwa kufanya yafuatayo. Kwanza wajitokeze na kutoa taarifa kwa Maofisa Uhamiaji, Wilayani au katika vituo vya mpakani. Pili, iwapo watachagua kuishi nchini, wafuate taratibu zilizowekwa kuomba kibali cha kuishi nchini. Idara ya Uhamiaji ndiyo itakayoamua. Tunawapa siku sitini za kufanya hivyo. Baada ya hapo, hatua zipasazo za kisheria zitachukuliwa kwa wale ambao watakuwa hawakufanya hivyo.
Nilipokuwa Mkoani Kagera niliwaagiza Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya kufuatilia utoaji wa vibali unaofanywa na viongozi na watendaji wa vijiji na kata katika maeneo yao. Nimewataka wawachukulie hatua zipasazo za kinidhamu watumishi hao wa umma pamoja na kuwabana wahamiaji haramu kufuata sheria za uhamiaji za nchi yetu au warudi makwao. Napenda kusema kuwa maagizo hayo ni kwa Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya nchini kwani inawezekana matatizo haya yanaweza kuwepo katika mikoa mingine.
Najua kwamba kuna Watanzania wenzetu wanaohifadhi wahamiaji haramu kwa kuwa wananufaika kwa kuwafanya vibarua au wafanyakazi wao. Ukweli unabaki pale pale kwamba wanatakiwa waingie na kuishi nchini kwa kufuata taratibu zinazotambulika kisheria. Sheria za nchi, na sio manufaa ya mtu au watu binafsi, ni lazima zizingatiwe.
Ndugu Wananchi;
Jambo lingine baya linalofanyika katika mpaka wetu na nchi jirani Mkoani Kagera ni kuruhusu mifugo kuingia nchini holela. Hiki ni kitendo ambacho kinakiuka taratibu zinazotawala uingizaji wa mifugo kutoka nchi za nje. Pia ni kitendo cha hatari kwani kinaweza kupelekea mifugo yenye maradhi kuingia nchini bila kudhibitiwa na kusababisha maafa makubwa nchini. Kanuni na taratibu zimewekwa kisheria kutawala mifugo kuvuka mipaka na kuepusha hatari za namna hiyo zisitokee.
Jambo linalonishangaza ni kwa nini viongozi wetu hawa hawajifunzi kutoka kwa majirani zetu. Wakati wote tulipofanya zoezi la kurudisha makwao wakimbizi au wahamiaji wasiokuwa halali na mifugo yao wenzetu waliweka sharti la mifugo hiyo hiyo iliyotoka kwao ichanjwe kwanza kabla ya kuvuka mpaka hata kama mifugo hiyo ilitokea nchini kwao na kuja kwetu. Nilidhani hili lingekuwa fundisho kwa viongozi wetu hawa kuwa thabiti kuhakikisha kuwa mifugo kutoka nchi jirani inachanjwa kabla ya kuvuka mpaka kuja Tanzania. Lakini, hawajali kufanya hivyo. Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi Watendaji wa Wilaya na viongozi na watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha kuwa hakuna mifugo inayoingia nchini holela. Lazima sheria na kanuni husika zizingatiwe.
Aidha, nimeelezwa juu ya kufahamika kuwepo vivuko haramu kadhaa mpakani. Nimesema nilipokuwa Kagera na narudia tena leo kwamba, maadamu vivuko hivyo vimejulikana lazima tuvidhibiti. Kadhalika tuanzishe vituo mpakani vya kupokelea mifugo na kila anayeingia na mifugo lazima apitie hapo na kupata idhini husika. Nimetaka viongozi wenzetu hao wasimuonee haya mtu yeyote anayeingiza mifugo nchini kinyume cha sheria na taratibu zilizopo. Kadhalika viongozi na watendaji wanaozembea wachukuliwe hatua kali za kinidhamu mara inapobainika kuwa mifugo imeingia kinyume na taratibu katika maeneo yao.
Kama ilivyo kwa uhamiaji usio halali, tatizo la kuingiza mifugo kinyume na utaratibu linaweza kuwepo mikoa mingine nchini. Hivyo, maagizo haya ni kwa mikoa yote na wilaya zote nchini. Pia yanaihusu Wizara ya Maendeleo ya Mifugo. Lazima Wizara itoe uongozi katika jambo hili muhimu kwa usalama na maendeleo ya mifugo yetu nchini. Napenda kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa hakuna nchi yoyote duniani inayoruhusu mifugo kuingia holela. Si vizuri Tanzania kuwa ndiyo nchi pekee inayofanya hivyo. Wenzetu na hata hao majirani zetu wanatustaajabu.
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ninalopenda kulizungumzia ni matatizo yanayoukabili uchumi wa dunia hivi sasa. Bado bei ya mafuta iko juu sana na kuathiri uchumi wa nchi zote duniani tajiri na maskini ingawaje nchi maskini zinaathirika zaidi. Hili si jambo geni kwetu. Napenda kurudia kauli zangu za siku za nyuma kwamba, hatuna uwezo mkubwa wa kujikinga na athari za bei za mafuta. Hata hivyo, hatuna budi tuendelee kuwa waangalifu na hasa wabanifu katika matumizi ya mafuta. Tuepuke matumizi yasiyo ya lazima.
Wakati huo huo tunaendelea na juhudi za kuzalisha nishati mbadala kutokana na mimea hususan miwa, mawese na mbono-kaburi (jatropha). Juhudi hizo zikifanikiwa zitatusaidia kupunguza mzigo wa mafuta tunayoyaagiza kutoka nje. Nafurahi kwamba juhudi zetu zina muelekeo mzuri na katika miaka michache ijayo tutaanza kunufaika na matunda yake. Pamoja na hayo tunaendelea na juhudi za utafutaji wa mafuta na gesi asilia hapa nchini. Mpaka sasa leseni 22 za utafutaji mafuta na gesi asilia zimetolewa na kazi inaendelea katika hatua mbalimbali. Tuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu atujaalie rehema zake na sisi tujaaliwe kugundua mafuta mengi hapa nchini yatakayotosheleza mahitaji yetu na ziada ya kuuza nje.
Ndugu Wananchi,
Tatizo lingine kubwa linaloukabili uchumi wa dunia sasa linatokana na matatizo yanayoukabili uchumi wa Marekani. Uchumi wa taifa hilo ambao ndiyo mkubwa kuliko wowote duniani umekuwa unapita kwenye misukosuko kwa miezi kadhaa na katika wiki chache zilizopita hali ikawa ngumu zaidi. Kasi ya ukuaji wa uchumi imepungua na thamani ya dola imeshuka. Serikali ya nchi hiyo imeanza kuchukua hatua za kukabiliana na matatizo hayo. Lakini, kwa kuwa uchumi wa Marekani ndiyo uchumi mkubwa kuliko wowote duniani na uchumi wa nchi nyingi duniani una uhusiano nao, matatizo ya uchumi wa nchi hiyo huathiri nchi nyingi. Na sisi Tanzania hivyo hivyo.
Nimeelekeza wachumi wetu wafanye uchambuzi wa kina juu ya athari hizo na kushauri hatua za kuchukua kupunguza makali yake. Moja ya jambo ambalo liko wazi ni lile la kushuka kwa thamani ya dola ya Kimarekani. Sisi tunaweka sehemu kubwa ya akiba yetu ya fedha za kigeni katika dola za Kimarekani. Ni dhahiri kwamba kushuka kwa thamani ya dola za Kimarekani kunatupunguzia uwezo wetu wa kuagiza bidhaa nchi za nje.
Uchunguzi wa Akaunti ya EPA
Ndugu Wananchi;
Jambo la tatu ambalo nimepanga kuliongelea leo ni hili suala la ukaguzi wa Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje na hatua zinazoendelea kuchukuliwa baada ya taarifa ya ukaguzi kutolewa.
Ndugu Watanzania wenzangu;
Kwa mara nyingine tena nawapongeza na kuwashukuru wakaguzi wa Kampuni ya Ernst and Young kwa kazi nzuri waliyoifanya na kutoa taarifa ya kina kuhusu matatizo yahusuyo matumizi ya fedha za Akaunti hiyo. Nawashukuru pia Watanzania wenzangu kwa kuunga mkono hatua tulizochukua na tunazoendelea kuchukua kuhusu suala la Benki Kuu. Hata hivyo, nasikitishwa na taarifa ninazozipata kuhusu kuwepo uvumi mwingi unaoenezwa na baadhi yetu kuhusu suala hili. Baadhi ya uvumi huo umekuwa unapotosha ukweli na kuwachanganya wananchi. Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba wanaoeneza uvumi na uongo kuacha kufanya hivyo. Aidha, nawasihi wananchi wawe watulivu na wavumilivu.
Napenda kuwahakikishia kuwa, Serikali inayo dhamira ya dhati ya kulifuatilia suala hili mpaka mwisho wake ujulikane. Mwisho ambao utakuwa na maslahi kwa taifa letu. Pamoja na yote yatakayofanywa, tunataka kuhakikisha kuwa fedha zilizolipwa kinyume cha utaratibu zinarudishwa. Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wenzake, yaani Mkuu wa Jeshi la Polisi na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU wameanza kuchukua hatua. Nimewataka watoe taarifa kwa wananchi mara kwa mara kadri inavyowezekana pamoja na haja ya kuwa waangalifu kutokutoa mengi yahusuyo uchunguzi wanaoufanya ili ushahidi usiharibike.
Nawaomba Watanzania wenzangu tuwe na subira. Naamini kazi hii itakamilika ndani ya kipindi cha miezi sita tuliyowapa. Napenda kurudia ombi la Serikali kwa wananchi wenye taarifa zitakazosaidia katika uchunguzi na hatua katika suala hili waisaidie kamati yetu hiyo.
Ujio wa Rais Bush
Ndugu Wananchi;
Natumai mmesoma na kusikia taarifa katika vyombo vya habari kuhusu ziara ya Rais George W. Bush wa Marekani katika nchi yetu kunako katikati ya mwezi Februari, 2008. Tunaendelea kukamilisha ratiba na itakapokuwa tayari tutawapeni taarifa. Hilo ndilo jambo langu la nne leo.
Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba Watanzania tumpokee mgeni wetu huyu kwa mujibu wa mazoea na desturi za ukarimu wa Kitanzania. Huu ni ugeni mkubwa na wa heshima kubwa kwa nchi yetu. Rais Gerorge Bush ameipa heshima kubwa nchi yetu kwa kuamua kutumia sehemu kubwa ya ziara yake ya Bara la Afrika hapa kwetu. Ameonyesha upendo mkubwa kwetu nasi tumuonyeshe hivyo hivyo. Nawaomba Watanzania tujitokeze kwa wingi siku hiyo kumpokea mgeni wetu huyo mashuhuri.
Ziara hii ni uthibitisho wa kuimarika kwa mahusiano kati ya Marekani na Tanzania. Mahusiano hayo mazuri yameinufaisha nchi yetu. Marekani sasa ni moja ya nchi zinazoongoza kwa kutoa misaada ya maendeleo kwa Tanzania. Tangu mwaka 2003 kwa mfano, imekuwa inatoa msaada mkubwa ambao umetusaidia sana katika mapambano yetu dhidi ya maradhi ya UKIMWI nchini Tanzania. Kadhalika, Marekani imetusaidia sana katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria nchini.
Ndugu Wananchi,
Wakati wa ziara yake hapa nchini, Serikali ya Marekani inatarajia kutiliana sahihi msaada mkubwa wa maendeleo unaoelekezwa katika kuboresha miundo mbinu ya barabara, umeme na maji. Kwa msaada huo utakaotolewa kupitia Programu ya Mfuko wa Changamoto ya Millenia utatusaidia kutatua baadhi ya matatizo yaliyoonekana sugu katika baadhi ya maeneo hapa nchini.
Pamoja na hayo, ziara ya Rais George Bush nchini mwetu itasaidia kuitangaza nchi yetu na kuinufaisha sana utalii na uwekezaji hasa kwa soko la Marekani na marafiki zake. Tayari katika miaka miwili hii tumeshuhudia ongezeko kubwa la watalii wa Kimarekani kutembelea nchi yetu. Hivi sasa Wamarekani ndiyo wanaoongoza kwa idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi za Ngorongoro na Serengeti. Naamini baada ya ziara ya Rais wao watalii wengi zaidi wa Kimarekani watakuja. Hali kadhalika, wawekezaji wengi wa kutoka Amerika watajenga imani ya kuja kuwekeza nchini.
Ndugu Wananchi,
Wapo watu miongoni mwetu na hata nje wanajaribu kueneza uvumi wa uongo na kuihusisha ziara hii na masuala ya Makao Makuu ya Kamandi ya Afrika ya Jeshi la Marekani. Ni uongo na uzushi mtupu. Ziara hii haihusu hayo. Masuala hayo si agenda na wala Marekani haijaiomba Tanzania kuwa mwenyeji wa Kamandi hiyo. Nawasihi Watanzania wenzangu tupunguze hii tabia ya kuzusha na kueneza uongo. Tunajitia hofu wenyewe na wenzetu bila sababu. Haina tija yoyote. Nawaomba tujitokeze kwa wingi kumpokea mgeni wetu huyu. Aondoke nchini salama na arejee kwao akiwa na kumbukumbu nzuri ya nchi yetu na watu wake.
Hali ya Kenya
Ndugu Wananchi;
Jambo la tano ninalotaka kulizungumzia ni hali ya kisiasa na kiusalama ya nchi jirani na rafiki ya Kenya. Kwa kweli inatusikitisha na kutuletea simanzi kubwa. Mioyo yetu inauma kuona na kusikia yanayotokea nchini humo. Jitihada yangu ya kuzungumza na pande zote zinazohasimiana pamoja na zile zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na wenzetu wengine bado hazijazaa matunda. Sisi hatutachoka na wala hatutaacha kuzungumza na pande zinazohusika kuhusu kuacha uhasama, kuacha na mapigano na kutafuta maridhiano kwa njia ya mazungumzo.
Tunaahidi kuendelea kuiunga mkono Kamati ya Mhe. Kofi Annan (Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa), Rais Mstaafu, Mhe. Benjamin Mkapa na Mama Graca Machel. Viongozi wetu hao wanaifanya kazi hiyo kwa niaba ya Umoja wa Afrika wanastahili msaada wetu na kuungwa mkono nasi. Aidha, tutaendelea kushirikiana na viongozi wenzetu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kusaidia juhudi za upatanishi. Napenda kutumia nafasi kurudia tena yale maombi yangu kwa viongozi wa PNU na ODM na wananchi wote wa Kenya kuyapa mazungumzo nafasi ya kumaliza tofauti zao. Mapanga, marungu na hata bunduki zisipewe nafasi, kamwe hazitasaidia.
Tutenganishe Uongozi na Biashara
Ndugu Wananchi;
Jambo la mwisho ninalotaka kulizungumzia linahusu maadili ya uongozi nchini. Hususan napenda kulizungumzia suala la viongozi wa siasa Mawaziri na Wabunge kuwa pia watu wanaojihusisha na shughuli za biashara moja kwa moja. Upo ushahidi wa kuwepo migongano ya maslahi kwa baadhi. Lakini, pia, hata pale ambapo hakuna dalili za wazi, hisia za kupata manufaa yanayotokana na nafasi zao hutawala. Matokeo ya yote hayo ni watu kupoteza imani na kutilia shaka uadilifu wa viongozi wetu.
Ndugu Wananchi;
Nchi za wenzetu hasa zile za kibepari zinazo taratibu nzuri za kushughulikia hali hizo. Wenzetu wanao utaratibu unaomtaka mtu mwenye shughuli za kibiashara anapokuwa Mbunge au Waziri kuacha kujishughulisha na biashara zake. Unakuwepo utaratibu rasmi unaotambuliwa kisheria wa wadhamini wanaoendesha hizo shughuli bila ya yeye kujihusisha nazo. Anapoacha uongozi wa siasa kama atapenda atachukua tena mali yake na kuendelea na shughuli zake.
Ni makusudio yangu kuwa utaratibu huu tuuanzishe hapa nchini. Viongozi wetu wachague kufanya jambo moja kwa wakati mmoja ama biashara au Ubunge na Uwaziri. Kwa ajili hiyo ni makusudio yangu kuanzisha mchakato wa kufanya marekebisho ya Sheria ya Maadili ya Uongozi ili tuingize utaratibu huo.
Ndugu wananchi;
Ni jambo lenye maslahi kwa nchi yetu na litasaidia sana kujenga heshima ya viongozi wa umma mbele ya macho ya wananchi. Nafurahi kwamba suala hili tumelizungumza katika kikao maalum cha Kamati Kuu ya CCM tulichofanya Dodoma juzi tarehe 29 Januari, 2008 na tumeelewana. Ni matumaini yangu kuwa sote tutaunga mkono.
Mwisho, nawatakia kila la heri kwenye shughuli zenu. Tuendelee kushirikiana kuijenga na kuiendeleza nchi yetu.
Asanteni sana kwa kunisikiliza!
Feedback / Comments
26 Responses to “KIKWETE MWENYEKITI MPYA AU”
Leave a Reply


Hongera sana Mkuu.
Hii inaonyesha kuwa kuwa unakubalika. Kinachofuatia ni kutimiza wajibu na kujenga imani zaidi hasa nyumbani.
Kwa hili tuko pamoja katika kukupongeza
Hongera
Hongera sana Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuchaguliwa kwako kuwa Mwenyekiti wa African Union (AU).
Mimi pamoja na familia yangu ninaungana na watanzania wote kumpongeza Rais Kikwete na kumtakia kila la kheri katika kazi zake yakiwemo majukumu mapya ya Uenyekiti wa AU.
Mungu Mwenyezi akulinde, akupe afya na akuongezee Hekima ya kuongoza AU. Amen.
Hongera Sana Mh. JK
Kweli sasa ninaamini kuwa Watanzania nasi tumo.
Umechaguliwa kati ya Marais 14; Hongera sana Baba na Mungu akulinde na akuwezeshe ufanya kazi aliyoifanya Nabii Musa ya kuwaondoa wana wa Israel kutoka Misri.
mheshimiwa Rais na wana BC napenda kutumia firsa hii ya demokrasia kukupongeza kuwa uteuzi huo.Napenda kukupongeza kwa hatua ulizochukua za KUJARIBU kutatua sakata zima la ufisadi wa BOT.
Kuna jamaa mmoja wa gazeti huru hapo bongo kaongea point moja kali sana ambayo kama wengi wangeiona hii point then wangekubaliana nami kuwa RAIS WETU INABIDI UPUNGUZE KUTUPIGA NA MICHANGA YA MACHO.kama ushapewa ripoti ya akina E&YOUNG kuna haja kweli ya kuanza kuchunguza ufisadi wakati ushapewa nondo kamili na hao jamaa.I mean kwa nini usiamuru tu kuwa kila mtu katika listi adakwe halafu ndo ufungue ukurasa mpya wa kuchunguza kwa kina wakati hao mafisadi wanakula KCK hapo segerea.
jamani ee mimi nimeshachoka na hii mijitu da sina la ziada coz it makin me insane just to think about it! am sad !laana tupu zimemwagwa bongo!
please check this article
http://www.raiamwema.co.tz/08/01/30/lula.php
Me naungana na no 4 sioni sababu ya kumpongeza rais kwa kuchaguliwa kutokana na sababu zifuatazo:
1.Mimi sielewi kama nchi tutanufaika vp na huo uenyekiti wa AU
2.Sidhani kama Kikwete anastahili katika hiyo nafasi kwani si mtu wa kufanya maamuzi magumu. Nitoe mifano hapa.Kwanza, alishasema anawajua wala rushwa anawapa muda wajirekibishe,wezi unawapa muda wajirekibishe muda gani huo,why dont fire them right away? Pili ni hii audit ya EPA juzi iliyofanywa na E&Y, kapata report badala ya kuchukua hatua ameunda tume nyingine kuchunguza uchunguzi-what is this. Badala ya kuchukua hatua ikiwemo kufukuza kazi na kutaifisha mali ameunda tume nyingine tena
3.Rias wetu ni mtu wa safari wote tunalijuwa hilo. Unenyekiti wa AU unainvolve safari sasa ukijumlisha na zile safari zake za kawaida nahisi rais atakuwa na muda mdogo sana wa kulitumikia Taifa unless amezipunguza.I’m afraid itatokea wakati atasafiri mwezi mzima,kwani ameshawahi US wiki tatu nzima.
Mtakoma sasa Vasco Da gama na hizo safari za Addis.
Nafikiri atanunua nyumba kabisa huko!
Congratulations JK,
This time I hope you will use AU Presidency to bring Real Madrid to Tanzania….hahahahahaha!
Hongera
sana mheshimiwa kwani inaonyesha kuwa watanzania tunae kiongozi anaekubalika kimataifa na kitaifa.
Haya ni majukumu mazito mmno kwani kuongoza umoja wa nchi za afrika ambao ndani yake kila nchi inamtazamo wake si jambo la mchezo.mfano wenzetu wakenya wanaamini machafuko ndio njia sahihi ya kuleta mabadioliko kufuatia matokeo ya uchaguzi walioufanya mwishoni mwa mwezi wa 12 kwa hiyo hili ni jukumu mmojawapo ambalo mheshimiwa unatakiwa kuwa muangalifu sana kwa kipindi chako.
Kwa mtazamo wangu mh JK amepewa majukumu haya ili aungane na wasuluhishaji wengine wanaosuluhisha suala la vurugu wa kisiasa au kikabila kama unavyoelekea huko Kenya. Hili nalo ni nje ya uwezo wako kwni wasuluhishi wa kuu ni Wakenya wenyewe hasa viongozi wanaosababisha vurugu hizo kama wasipowasikiliza wananchi wao je watawasikiliza viongozi wasuluhishi?
Mh JK majukumu haya yasikufanye utusahau nyumbani bwana kwani hata sisi tunakuhitaji sana.
Kabla hujatimiza ahadi zako kwa watanzania umepewa jukumu kubwa la Kiafrica jamani mheshimiwa je waweza kutumikia mabwana wawili kitu ambacho hata msaafu na biblia vinakataza.
Usibase sana na ya Kiafrika timiza yako ya ndani kitu ambacho umesema taratibu mabadiliko yatatolea.
Congraturation Prezidaaa! umeonyesha unakubalika miongoni mwa marais wengine.
Mungu akupe nguvu ya kweli katika kutatua migogoro ya nchi zinazolumbana, Mungu anamakusudi yake na ndo maana umechaguliwa wewe yote hayo ni sababu yeye ni mwema.
What difference does make? I don’t see any kind of advantage to majority of Tanzanian. What i see is the big levarage that Tanzanian have to carry for couple of years.
We need to focus more on our own problems, lather than engage in African mess. We need to find altenatives on healthcare, education, economy and infrastracture. African Union is a 0 marks organization, it is a group of dictators from each corner of Africa who gathered to gather to talk non sense.
Tell me what movement did this organization archived in recently years. How about Sudan turmoil? Congo crisis? Kenya tribalism civil war? You name any crisis that had been resolved by this nappy organization.
We need JK to focus on our business, which he promised during campaign. We need him to worry about 36 million people reside in Tanzani, and not billion of people reside in each corner of Africa.
No time to waste, we need him to engage in 24/7 Tanzanian business.
I will post my reflection toward that speech. It is the time that our president need to focus more on Tanzania economy, and stop throw excuses about world economy which majority of his economist doesn’t know anything about it.
Mr president elaborated about slowing in US economy vs Tanzania economy. I want to know first what correlation did Mr president team used to elaborate that point? Majority of Tanzanian doesn’t understand when they heard US economy mighty get into recession, first let me explain what is recession. It is a point when the country economy shrink due to certain reasons that affiliated with economy. The slow down of GDP can cause the country to get into recession. So, when president economy analyst get some points from CNN or SKY news about USA economy is in bad shape they jump and type so president can come out and scare people.
Come back on the point, US economy is facing challenge from sub-prime lenders mess, this has caused many banks to rewrite their assets, which cause some losses in financial sectors. When you hear all this story about US economy is in bad shape and other non sense, just ask them what is the return on S&P 500 index, what is return on emerging market, what is the return in Nikkei index, and many other world index? Then they will pause because they know that you know what your talking about. Only problem in US economy is Financial institutions which loan people money careless, same as Mr President tries so hard to convice banks to loan money to people. Financial institution doesn’t make even 19% of US economy.
I am gland that Mr Bush will be in Tanzania, i will personal request USA to stop provides funds to Tanzania government, until JK cabinet provides check and balance, prosecutes all mafisadi who stole billions of dollar, and last until he promise to help those who need the funds most.
Energy matter and Tanzania economy. Mr President elaborate that rising of oil price in world market has direct impact in Tanzania economy. I want you my fellow Tanzania to oppose those opinions. It is not true Tanzania economy slow because of rises of gas price in world market. This is why, Tanzania economy relied on agricalture for more than 45%, and most of the farmers use pilau hoe or Jembe la mkono. So, increases in oil and gas has no impact on that sector. Second, Tanzania is not an industrial economy, it is few industry that uses oil in their daily basis, however those industry are not contribute even 10% of our economy. Rise in gas price in the world market has effect on consumers who own cars, who doesn’t make even 25% of whole Tanzania economy.
Fallen of dollar, since mid last year to this monent, the US dollar falls for about 13%. What effect does it have to foreigners? First, most of the investors from other countries had get an oppurtunity to invest in USA (world giant economy), countries like UAE bought more than 2% of Citi group, Kuwait bought some shares in Merrill Lynch and China pour some money in US. So, falling of dollar has advantage for other countries and not disadvantage as Mr JK elaborated. However, falling of dollar have impact to countries that depends US as their big market, countries like China, Japan and Mexico, because their products will be more expensive. For country like Tanzani, fallen of dollar value has nothing to do with our economy, because we don’t produce anything. You maight argue about, how about tourism industry? My answer will be what percent does tourism industry contribute to Tanzania income? Very little, so currency fluctuion has no bi effects. others may said, how about Barrick products? My answer will be Tanzania collect 3% of the total profit, and i guess at this moment still Barrick enjoy tax subsidy, so it doesnt make any difference if the dollar falls or stays up.
Last, Mr President need to put Enerst & Young report public. So, we can see if E. Massawe perform a good job, or if it is bad job then we will ask if he knows anything about US bribes act? Then we want those who stole out money to face the justice system and pays the price. We want investigations in other alligations especial Kiwira mining, Richmond, MB bank, BOT twin towers and many others. We want you Mr president to kept your promise of “Maisha bora kwa kila Mtanzani”.
Mungu ibariki Tanzania, asanteni kwa kusoma
We BC sasa mbona umeni-block, mi nimekukosea nini?
Hapo Kikwete umeongezewa majukumu usisahau tu Tz mana’ke mpaka sasa miaka 2 na miezi kadhaa bado maisha ya Mtanzania halisi hayaeleweki.
Labda Uenyekiti utasidia ku-save kodi zetu zinazotumiwa kukusafirisha kama raisi na watendaji wako pale mnaposafiri-safiri “inji za inje” ili tujenge barabara, tuboreshe huduma za hospitali, ufuatilaiaji mzuri wa kesi na kupunguza wafungwa kwenye magereza ambao wanalishwa vyakula vibovu lakini amofisa wanadai wanatumia mamilioni kuwalisha n.k, vilevile kuzitumia pesa hizo kama malipo pale utakapo amua ku-create jobs za kima cha chini na kuzifanya ziwe valuable.
How? Nitafute nikupe mbinu….
hebu chekini example ya mchanga wa macho
“Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wenzake, yaani Mkuu wa Jeshi la Polisi na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU wameanza kuchukua hatua. Nimewataka watoe taarifa kwa wananchi mara kwa mara kadri inavyowezekana pamoja na haja ya kuwa waangalifu kutokutoa mengi yahusuyo uchunguzi wanaoufanya ili ushahidi usiharibike.”
hivi kweli ushahidi si umeshaharibika kama umekaa nao ofisini halafu unawapa presha akina mwanyika na mwema?
huyu jamaa kaanza kuwa mafia sasa.
halafu katika topic zote jamaa anasema ndugu wananchi alipofika katika suala za BOT akawachombeza wananchi kwa kutoa “ndugu watanzania wenzangu” LOL
ila big up mr president unajua kuwaliwaza watu ila haifai kwa sasa ishakuwa soo!
Hii ni Made in Tanzania tu!
Home – Kipima Utu
Januari 23, 2008
JOHN Nolan, yule raia wa Ireland aliyejaribu kuighilibu Serikali ya Tanzania imruhusu aanzishe mashamba ya kamba (prawns) ambayo yangeiharibu kabisa Delta ya Rufiji, alipata kuliambia gazeti moja la Uingereza kwamba kati ya nchi za “ajabu” alizopata kuishi ni Tanzania. Nolan aliliambia gazeti hilo ya kwamba Tanzania ndiyo nchi pekee duniani ambayo Mzungu anaweza kuingia akiwa na dola tano tu mfukoni na akaondoka miaka mitano baadaye akiwa milionea! Alitoa mfano wa yeye mwenyewe kwamba aliingia Tanzania akiwa hana kitu, lakini ‘akatengeneza pesa’ akiwa katika chumba chake cha hoteli kutokana na dili walizochonga na viongozi ambao walimwamini kwa kuwa tu ni Mzungu!
Lakini Nolan si mgeni pekee aliyepata kuikejeli Tanzania. Mwaka jana gazeti la Mtanzania lilipata kumnukuu mwekezaji mmoja kutoka China, anayefanya biashara ya kuuza kamba na kambakochi Mashariki ya Mbali, akiikejeli Tanzania kwamba rushwa yake ni “poa”.
Kwa mujibu wa Mchina huyo, ni katika Tanzania tu ambapo unaweza kumwita hakimu nyumbani kwako na kumpa rushwa ya Sh. 100,000 tu, na kisha kumpa maelekezo ya namna ya kutoa hukumu ya kesi ya mamilioni ya pesa inayokuhusu!
Lakini kama utashangaa na kutoziamini kauli hizo za Nolan na za Mchina huyo, utasemaje kuhusu hii ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kuanzisha kampuni yake ya biashara (ANBEM) yeye na mkewe, mwaka 1999, akiwa bado Ikulu?. Kwa kufanya hivyo, Mkapa akawa Rais wa kwanza katika historia ya Tanzania kufanya biashara akiwa Ikulu. Historia bwana, nani hapendi kuweka historia ya ujasiriamali?
Lakini hakuishia hapo. Mwaka mmoja kabla ya kuondoka madarakani; yaani Desemba 29, 2004, Mkapa huyo huyo akashirikiana na aliyekuwa Waziri wake wa Fedha na baadaye Nishati na Madini, Daniel Yona, kusajili kampuni nyingine binafsi iitwayo Tanpower Resources Company, na akaisimamia kununua asilimia 85 ya uliokuwa mradi wa umma wa makaa ya mawe wa Kiwira mkoani Mbeya.Lakini pia hakuishia hapo. Akautumia wadhifa wake wa urais kuhakikisha kampuni yake hiyo mpya – wakurugenzi wakiwa ni pamoja na mkewe na mtoto wake, kuingia mkataba wa kuiuzia Tanesco megawati 200 za umeme katika gridi ya taifa.
Raia wema waliohoji iwapo hakuna mgongano wa maslahi kwa Rais kufanya biashara akiwa bado Ikulu; huku akinunua kampuni ya umma (Kiwira) na kuingia mkataba wa kibiashara na kampuni nyingine ya umma (Tanesco), walinyamazishwa haraka kwa kuambiwa Mkapa ni “mjasiriamali”, na kwamba anaonyesha “ujasiriamali” kwa vitendo akiwa Ikulu! Upo hapo? Kama hiyo haitoshi kukuthibitishia vioja vya Tanzania, utaielezeaje hii ya Jeetu Patel kufanikiwa kughushi na kuchota Sh. bilioni 90 kutoka Benki Kuu kwa kutumia makampuni manane tofauti aliyoyasajili?
Ilikuja ya kwanza ikachota, ikaja ya pili ikachota, ikaja ya tatu ikachota, na vivyo hivyo mpaka kampuni ya nane! Na bado Watanzania tunatakiwa tuamini kwamba hakuna aliyejua kuwa hati zilizotumiwa na makampuni hayo ni za kughushi, hadi majuzi ripoti ya ukaguzi ya Ernest & Young ilipotua mezani kwa Rais Kikwete!
Lakini kama hilo halikushangazi au kukushtua, hebu tafakari na hili jingine: Watanzania masikini wanapandishiwa umeme kwa asilimia 21 kwa sababu Tanesco iko hoi kifedha. Kwa nini iko hoi? Kwa sababu vigogo serikalini wameiingiza katika mikataba mibovu ya Richmond, IPTL na Songas.
Kwa sababu ya mikataba hiyo mibovu, Tanesco inailipa IPTL Sh. bilioni 3.3 kila mwezi, Songas Sh. bilioni 5.8 na Richmond Sh. bilioni 4.7. Kwa viwango hivvyo vya malipo, unahitaji kuwa na kampuni yenye utajiri
wa Microsoft ya Bill Gates, kutotetereka kifedha. Na hivyo Tanesco ilitetereka. Ili isife, ikaamua kuongeza umeme kwa asilimia 21! Hiyo maana yake ni nini? Hiyo maana yake ni kwamba Watanzania masikini na walalahoi wa nchi hii ndiyo “wanaobebeshwa” zigo hilo la Tanesco la kufidia gharama zilizosababishwa na vigogo serikalini za mikataba ya IPTL, Richmond na Songas. Cha kushangaza zaidi, vigogo hao waliotubebesha zigo hilo kwa kuingia mikataba hiyo mibovu, bado wanadunda mpaka leo serikalini!
Na bado wameona hiyo haitoshi. Sasa Serikali inajiandaa kuwasilisha bungeni muswada wa sheria kuziruhusu kampuni binafsi kufanya biashara ya kuuza umeme nchini. Yaani; Serikali inakuwa mstari wa mbele kulitafutia shirika lake (Tanesco) wapinzani wa kuliua kibiashara, tena inafanya hivyo ikiwa yenyewe tayari imeshalikamua hadi kuwa hoi bin taaban!
Na Tanesco ikifa na biashara hiyo ikashikwa na makampuni binafsi ya nje, (ambayo bila shaka baadhi ya vigogo nchini watakuwa na hisa), nani atayazuia yasipange bei ya pamoja ya kuuzia umeme (cartel) ili yanufaike zaidi kwa kuwakamua zaidi Watanzania? Na bado tunaambiwa kuna vita inayoendelea nchini ya kuwakomboa masikini.
Biashara ya chakula ipo mikononi mwa watu binafsi, nishati nayo sasa inawekwa mikononi mwa watu binafsi, maji nayo yataelekea huko huko …mwishowe sekta zote nyeti zinazohusu usalama wa taifa zitakuwa mikononi mwa watu binafsi hususan wageni. Tusisahau Nyerere alitabiri: “Mtabinafsisha hata Magereza.”
Lakini yawezekanaje mambo yote haya yatokee nchini na umma wa Watanzania ukae kimya tu? Jibu ni kwamba ni kwa sababu Tanzania ni nchi ‘poa’, nchi ya amani. Watanzania ni watu wasiotaka makuu, na ndiyo maana kina Nolan wanaamini kwamba duniani hakuna nchi kama Tanzania. Hayo aliyoyaona Nolan akiwa Tanzania ni Made in Tanzania tu. Huwezi kuyakuta kwingineko duniani!
Dear Ed,
If you venture to express yourself in English, please do that and not otherwise!
we kimori mbona unamaind vitu vidogo waache ma soldier wa express wanachotaka wanavyotaka mbona unataka kujifanya BC?
Kimori, did u understand the arguments? if you have other points please create arguments and not otherwise. My intation was to use as simple english as posible. I guess i pursue the goal.
Let us focus on our economy, and don’t be a political monga. Does Tanzania people buy the concept of JK and economy? You have arguments concern my elaborations, bring on son.
SIPONGEZI CHOCHOTE ILA NADHANI NDO UMASKINI UTAZIDI KUONGEZEKA KWA WA TANZANIA
hongera Baba kikwete!!!!
Yani hapo unazidi kuitangaza Tanzania yetu.
griet Tanzaniaaaaaaaaaaaaaa!
Ilikuwa lazima achgaguliwe yeye siyo kwa sababu anafaa ila kulinganisha na nchi ambazo alitakiwa atoke mwenyekiti, yeye ndo pekee yupo madarakani kwa hali iliyo angalau na uhalali kwa mbali. so viongozi hakuwa na choice ila yeye.
Ref.No.7 Kimori:Aise babangu……… kwa kweli umenifu…..funja mbavu zangu kweli! Ifi mbona una Big ideas hivyo kweli? Ni aja……… ajabu na kweli!
Nakupongeza Rais Kikwete kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa sasa wa Au!LAKINI, utambue unakabiliwa na Kibarua kigumu.Kuwa M/Kiti wa AU ujue ni kuwa M/KITI wa kusuluhisha migogoro isiyokwisha barani Afrika.Ili uepukane na ile dhana ya ‘Kesi ya Nyani kupelekewa Ngedere’,itakulazimu ufanye jitihada za ziada kusafisha uchafu wote uliokithiri katika safu ya uongozi katika ngazi zote hapa nchini ili uwe na timu adilifu ya kukusaidia katika majukumu hayo pamoja na mengine!Ukihitajika ukasuluhishe mgogoro wa kisiasa uliotokana na kutokuwepo kwa utawala bora na wa Demokrasia,basi Tanzania itatakiwa iwe mfano bora na kielelezo makini cha usuluhishi katika hilo;ukihitajika ukasuluhishe mgogoro wa kisiasa uliosababishwa na kutokuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi, basi Tanzania itatakiwa iwe mfano bora na kielelezo halisi katika hilo;Ukitakiwa ukakemee ukabila na ubaguzi wa aina yoyote katika sehemu nyingine ya bara la Afrika, basi Tanzania iwe mfano bora katika hilo;ukitakiwa ukasuluhishe mgogoro wa kisiasa uliosababishwa na Katiba iliyopitwa na wakati au Katiba inayolinda maslahi ya wachache wenye nacho na kupuuzia misingi yote muhimu ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa,basi Tanzania iwe mfano bora katika hilo!Na mengine mengi.Utakapo lazimika kuwanyooshea kidole wenzetu wenye migogoro katika nchi zingine barani Afrika, watanzania tuwe tayari kukosolewa kwa mapungufu tuliyonayo.Huo ndiyo ugumu wa majukumu yatakayo kukabili Rais Kikwete katika kutekeleza wajibu wako kama Mwenyekiti wa AU mwaka huu.Hakuna lisilo wezekana.Tanzania ilijiwekea rekodi safi sana katika kusaidia ukombozi wa bara la Afrika.Iwapo nia na dhamira ya kuleta mabadiliko na mageuzi ya kweli ipo, basi Rais Kikwete utakuwa na nafasi nyingine pekee ya kuweka rekodi nyingine mpya barani Afrika ya kuleta mageuzi ya kweli katika mifumo ya utawala bora itakayozingatia misingi ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa kama inavyokubalika kimataifa.Mwenyezi Mungu akuzidishie hekima na busara ya kutenda yaliyo mema kwa jamii unayoiongoza!
2faced
Mh. Raisi Hongera sana kwa kuwa kiongozi wa Taifa kwa muhula huu na huenda ukapata muhula ujao pia. Mheshimiwa, mimi nimekuwa nikifuatilia sana yale uyasemayo na kuyatenda, na kwa kiasi fulani nimeridhishwa sana na utendaji wako au serikali uiongozayo. Lakini hata hivyo kitu ambacho sikifurahii ni kutokamilisha miradi muhimu ya taifa inayotuama katika miundo mbinu. Ningependa kuona kuwa kila muhula panakuwepo miradi maalumu inayokamilishwa kutokana na kiasi kidogo cha fedha zinazokusanywa kama ni kodi ya mapato ya taifa. Badala ya kuendelea kutengemea misaada wakati ambapo tunatambua fika kuwa baadhi ya nyakati nchi rafiki zinazotusaidia kuwa hazifanikishi utekelezaji wa ahadi zao. Kwa hivyo basi, kwa nini tusijitegemee? Mheshimiwa raisi natambua fika kuwa ukumbi huu ni wa wataz na huwenda ukawa hautazamwi mara kwa mara. Lakini ukipata nafasi ya kuuchungulia basi tafadhali, chonde chonde, fanya ufanyavyo, lakini hakikisha kuwa malengo machache yanayotekelezeka kwa mwaka kwa mfano, ni bora kuliko malengo makubwa ya miradi mikubwa isiyotekelezeka au kutokamilika. Kumbuka kuwa hatua moja mbele ni utekelezaji wa mradi wowote wa taifa kiukamilifu, na kurejea nyuma ni kutokamilisha mradi wowote wa taifa. Kwa kuwa mradi usiokamilishwa, utakuja kumea tu sehemu ya bajeti ya mwaka mwingine mpya wa fedha. Mh Rais, nakutakia kila la kheri. Mungu Ibariki Tz na wananchi wake. Mungu ibariki Africa.
Narekebisha makosa katika comment iliyopita. sehemu ya mwisho inayohusu mradi usiokamilika. ni kuwa:- mradi usiokamilishwa utakuja kumega tu sehemu ya bajeti ya mwaka mwingine mpya wa fedha. Mh Rais, nakutakia kila la kheri. Mungu Ibariki Tz na wananchi wake. Mungu ibariki Africa.