NERVOUS CONDITIONS KUTOKA KWA NAKAAYA

 

Kila kukicha vipaji vipya vya wasanii au wanamuziki nchini Tanzania vinazidi kujitokeza.Mojawapo ya vipaji hivyo ni kutoka kwa binti aitwaye Nakaaya(pichani). Ingawa sio muda mrefu sana tangu alipojitokeza rasmi kwenye anga za muziki nchini Tanzania,tayari ameanza kujitengenezea jina na nafasi maalumu katika fani.

Isitoshe anaelekea kuwa mwanamuziki anayeelewa jinsi gani,yeye kama msanii,anapaswa kuhakikisha kwamba jasho lake halipotei bure.Kwake yeye,muziki sio tu burudani bali pia biashara ambayo inahitaji kila aina ya jitihada za kibiashara.

Hivi karibuni amefyatua albamu yake ya kwanza inayokwenda kwa jina la Nervous Conditions.Ipo mitaani hivi sasa ikiwa imesheheni nyimbo kali ikiwemo hit single yake Mr.Politician inayotamba hivi sasa kupitia vituo mbalimbali vya televisheni na radio.

Kwanini ameeiita albamu yake Nervous Conditions?Tuna maana gani tunaposema Nakaaya ni msanii ambaye amedhamiria kuhakikisha jasho lake halipotei bure?Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo;

BC: Nakaaya,karibu ndani ya BC,hongera kwa kufanikiwa kumaliza albamu yako ya kwanza. Labda kwa kifupi tu na kwa faida ya wasomaji wetu ambao hawajapata fursa ya kutembelea tovuti yako na kujua mengi kuhusu wewe,unaweza kutuambia juu ya historia ya maisha yako kwa ufupi tu?

NAKAAYA: Mimi ni msanii wa kiafrica, nilikulia Kenya na muziki nimeufanya tangia utotoni, nimeuchukulia kwa makini kuanzia mwaka 2006 na mpaka sasa unazidi kunifurahisha.Nimemaliza album yangu ya kwanza baada ya mwaka mzima studio na ninaamini ni muziki wa tofauti na tulichokizoea.

BC: Nini kilikusukuma hasa kuingia kwenye fani ya muziki?Je unao ndugu au jamaa zako wa karibu ambao ni wanamuziki pia?

NAKAAYA: Ndio, mama na baba ni wanamuziki wazuri tu, na kilichonisukuma ni maisha. Muziki kwangu mimi ni kama tiba, na sehemu yangu ya kujieleza na ya kufurahisha nafsi yangu…

BC: Mbali na kutengeneza pesa na kufanya kazi aipendayo na kutumia kipaji chake,mwanamuziki huwa anaweza kuwa na malengo mengine kabla ya kufyatua albamu. Nini hasa malengo yako katika albamu hii ya kwanza? Na kwa upande wa maudhui au ujumbe katika albamu nzima,ni upi?

NAKAAYA: Malengo kwa kweli ni mengi, hasa hasa ni kuibadilisha sura ya muziki wa bongo, ili ulimwengu ujue kwamba Tanzania au Africa inaweza, pia ninalenga kuwa ‘the next Miriam Makeba’!!!! ujumbe sio mmoja kwenye album. kama maisha yalivyo, album yangu ina message tofauti tofauti… Nawashauri wapenzi wa muziki wainunue kwani nina uhakika watapata vitu tofauti ;-)

 

BC: Kumekuwepo na hisia kwamba muziki wa siku hizi hauna ujumbe kama ilivyokuwa katika miziki ya hapo zamani kidogo.Unasemaje kuhusu hilo?

NAKAAYA: Ni kweli kwa kiasi fulani, lakini ninaamini kwamba wa kwangu una ujumbe na mimi ni mwanamuziki wa sasa hivi, it’s a musical revolution!

BC: Kwanini umeiita albamu yako Nervous Conditions?Ina nyimbo ngapi?

NAKAAYA: Ina nyimbo 11.Nimeiita Nervous Conditions kwa sababu, mimi nikiwa msichana wa kiafrika, ni vitu vingi sana ninategemewa nifanye, tangia kuzaliwa, kwa mfano, jinsi ya kuongea, nini cha kusema, nini nivae, kwa kifupi, jamii ina tupresha sana wanawake hivyo muda wote tuna ‘nervous conditions’.

BC: Umewashirikisha wasanii gani katika albamu yako na imetengenezwa katika studio gani?

NAKAAYA: Nimewashirikisha wasanii wawili tu, M1 of Dead Prez, na Lufu. Album ilirekodiwa 41 records, Dar–es- salaam.

BC: Wakati tunaanda mahojiano haya umetudokeza kwamba wewe mwenyewe ndio unasimamia shughuli nzima ya usambazaji wa albamu hii.Kwanini umeamua kufanya hivyo?Pia unaweza kutuambia mpaka hivi sasa,wapenzi wa muziki wanaweza kuipata wapi albamu hii?

NAKAAYA: Nimeamua kufanya hivyo kwa sababu nime invest muda na pesa kwenye project hii, na haina maana kwangu mimi kumtumia distributor, ambaye ni mmoja tu hapa Tanzania na ambaye kila msanii anamlalamika, sio maendeleo mazuri. Kama tunataka muziki wa bongo uendelee na ulipe, sisi kama wasanii lazima tun’gate msumari na tufanye wenyewe hadi siku tutakapompata distributor mwenye haki na faida kwetu sisi.

Wanaweza kuipata au kuinunua kupitia Shear Illusions- Millennium Towers na Mlimani City, Rose Garden na pale Nakiete Pharmacy. Pia wanaweza kuinunua online kupitia www.cdbaby.com.Wakiingia pale wanaweza kusearch tu jina ‘Nakaaya” wataipata.

 

Cover la Nervous Conditions

Page 1 of 4 | Next page