Ingawa vyombo vya habari mbalimbali,katika nyakati tofauti tofauti,vimekuwa vikiandika habari zake na yeye kualikwa katika mihadhara mbalimbali kuzungumzia masuala ya kujitolea, umasikini,maradhi na mambo mbalimbali yahusuyo ubinaadamu,yawezekana kabisa ukawa hujawahi kulisikia jina lake wala kuiona sura yake.
Anaitwa John Mashaka (pichani),kijana mdogo wa miaka 30 ambaye kama walivyo watanzania wengine wengi, anakerwa na hali za umasikini,ujinga na maradhi zinazowakabili mamilioni ya watanzania hivi leo.Tofauti yake na watanzania wengine wengi ni kwamba yeye ameamua kujitoa mhanga kusema na pia kusaidia kwa hali na mali anapoweza.Kwa maana nyingine,John Mashaka ni kijana ambaye anajaribu kuamsha upya hali ya kujitolea bila kujali sana hali ya utajiri aliyo nayo.Anasisitiza kile ambacho tumekuwa tukiambiwa tangu enzi na enzi;Kutoa ni moyo na wala sio utajiri.
Pamoja na hayo,hivi karibuni, habari zake zilipotolewa kwenye blog maarufu ya Issa Michuzi, mjadala mkubwa ulizuka kuhusu anachojaribu au alichowahi kukifanya.Kama kawaida ya binadamu,wapo waliomuunga mkono na wapo waliompinga kwa nguvu huku wakidai kwamba huenda anajitafutia tu “umaarufu” au kujifagilia njia ya kisiasa.Wengi wakawa wamemhukumu bila kumpa nafasi ya kumsikiliza.
Baada ya kusoma ule mjadala na kutafakari mambo kadhaa,BC tuliamua kumtafuta bwana Mashaka ili kufanya naye mahojiano utakayoyasoma hivi punde.John Mashaka ni nani?Je,Mashaka anajiandalia tu njia ya kuukwaa “ubunge” siku za mbeleni?Je ni kweli anakerwa kwa dhati na matatizo yanayomkabili mtanzania wa kawaida hivi leo?Vipi,inawezekana na wewe ukamuunga mkono katika anachojaribu kukifanya?You will be the Judge!Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo;
BC: Mashaka,Shukrani sana kwa kukubali kufanya nasi mahojiano haya.Kwanza kabisa watu wengi wangependa kufahamu kidogo kuhusu historia ya maisha yako.Unaweza kutuambia ulizaliwa lini,wapi na kisha ukasomea wapi mpaka kufikia hapo ulipo hivi sasa?
JM: Nimezaliwa na kukulia huko Tanzania miaka 30 iliyopita, na hatimaye kusoma shule ya msingi na sekondari nchini Kenya kabla ya kujiunga na elimu ya juu nchini Marekani kwa shahada za kwanza na zingine za juu.
BC: Hivi sasa hapo nchini Marekani unajishughulisha na nini haswa? Unafanya kazi gani?
JM: Nafanya kazi kama Investment Banker. Ila, sitapendelea elimu yangu, au nafasi yangu katika jamii, ihusishwe na kazi zangu au wito kwa binadamu wenzangu. Sipendelei kuyazungumzia kwa sababu haya yote ni batili tunapolizungumzia suala la ubinadamu.
Let my character and deeds decide on who I am. Elimu isiyotumika katika njia sahihi ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya kijamii inakuwa ni mzigo mkubwa, nafasi au cheo isiyo na manufaa kwa binadamu wenzetu inakuwa kero.
Wapo vijana wengi wenye elimu, na kazi nzuri kuliko mimi ambao wanahitaji msukumo au changamoto ili nao pia wasaidie nyumbani. Ila nikiingia ndani sana kuhusu kazi ninazozifanya nahisi kwamba nitakuwa nakiuka imani zangu na baraka za Mwenyezi Mungu, na kuikaribisha jeuri.
BC: Mara nyingi waafrika tumekuwa tukitupiwa lawama kwamba hatuna moyo wa kujitolea(volunteerism) ikilinganishwa na wenzetu wa nchi za magharibi. Je unakubaliana na lawama hizi na kama ndio unadhani ni kwanini waafrika hatupendi au hatuko mstari wa mbele katika kujitolea? Nini kinaweza kufanyika ili kubadili hali hiyo?
JM: Waafrika tumsilaumu shetani.Shetani ni sisi wenyewe. Kumsaidia mwenzio inakuwa shida kwa kuhofia atakushinda bila kufahamu ya kwamba shida inayomkabili mwenzio hivi leo usiposaidia kuitatua itakuja kukuathiri hata wewe mwenyewe kesho.Siyo lazima uwe na hela au tajiri ndio uweze kusaidia.Yeyote anaweza kusaidia. Kuna watoto wengi wanaoharibikiwa maishani kwa kukosa muongozo mzuri ili wawe raia wema, na hii inaweza kutekelezwa na mtu yeyote mwenye moyo wa kujitolea siyo lazima uwe na hela nyingi kama ambavyo wengi tunadhania.
Sioni kitu cha ajabu kwa mtu kujitolea kwani ni jambo la kawaida huku katika nchi za magharibi au Ulaya kama ilivyozoelekwa miongoni mwa wengi.Ajabu ni kwamba tunaporudi kusaidia nyumbani kila mtu wazo lake ni ubunge au siasa. Nadhani hii kasumba inatokana na mazingira mtu anayoishi ambayo yanatawaliwa na wanasiasa.
Maendeleo katika jamii hayaletwi na mwanasiasa, yanaletwa na watu kama mimi na wewe.Kujitolea hali na mali ndio dawa pekee ya kukomesha ujambazi, uzururaji na pia wimbi la watoto yatima wanaojitokeza kila kona,kila kukicha.
Hii ndio dawa pekee dhidi ya umasikini siyo kuwatazama macho viongozi tukidhania kwamba watatuletea miujiza. Uongozi lazima uanzie kwenye nafsi zetu. Sikuzaliwa na chochote, maishani nimesaidiwa, sikusaidiwa na mwanasiasa hata mmoja nilisaidiwa na raia wa kawaida.
BC: Tangu habari zako zianze kusambaa kupitia vyombo vya habari na blogs mbalimbali za watanzania, kumekuwepo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakidai kwamba wewe unasaidia yatima ili kujiwekea mazingira ya kugombea nafasi za kisiasa baadaye(kama ubunge) au kujipatia tu umaarufu na mambo kama hayo.Unasemaje kuhusu shutuma au habari kama hizo?
JM: Kuna umaarufu wa aina mbili.Umaarufu unaotokana na wema (vipaji maalum) na ule unaotokana na uovu. Sitapenda umaarufu wa aina yoyote, kwa maana nikiwa maarufu kutokana na wema, nitakuwa natekeleza jukumu langu kama binadamu.Wote tumeumbwa ili tupendane na kutenda wema. Namuomba Mungu anipe moyo wa unyenyekevu ili niepukane na tabia mbovu kama kiburi ambayo ni matunda ya umaarufu.
Nakumbuka mwandishi wa habari Tanzania aliniuliza swali kama hilo, lakini kwa kifupi ni kwamba mabadiliko katika jamii siyo lazima yaletwe na mbunge au mwanasiasa.
Wote tuna majukumu ya kuibadilisha sura za jamii zetu, nchi yetu, bara letu na pia dunia kwa ujumla. Raia wa kawaida anayeguswa na matatizo yanayoikabili nchi lazima atatafuta namna ya kusaidia.
Page 1 of 6 | Next page