ONE ON ONE WITH MIRIAM CHEMMOSS

Endapo kuchanganya utaifa,damu na tamaduni mbalimbali ni mojawapo ya chachu za mafanikio fulani hapa duniani, basi ushahidi wa dhana hiyo unaweza kuupata kwa kuangalia maisha ya mrembo Miriam Chemmoss(pichani).

Miriam ni muigizaji,mwimbaji,mtunzi wa nyimbo na pia mwanamitindo (model) ambaye mpaka hivi leo ana haki ya kusimama na kujivunia rekodi yake katika ulimwengu changamani wa sanaa na maonyesho.Mwenyewe anasema safari yake ndio kwanza inaanza kwani bado ana ndoto na malengo chungu mbovu ya kutimiza.Hivi leo kazi zake nyingi anazifanyia kutokea jijini New York nchini Marekani anapoishi.

Kama ilivyo kwa wasanii wengi,safari ya Miriam katika ulimwengu wa sanaa inaanzia tangu akiwa mwanafunzi mdogo.Lakini ni pale alipohamia jijini New York mwaka 2004 na kujiunga na kundi maarufu lililojulikana kama The Marvallettes Revue lililokuwa chini ya Pam Darden, ndipo nyota yake ilipoanza kung’ara ipasavyo. Baadaye alijiunga na kundi lingine maarufu la Soukouss Stars kama mwimbaji pekee wa kike na mnenguaji kabla ya kuamua kuimba peke yake(solo artist) mwaka 2006.

Kwa upande wa uigizaji,Miriam ameshaigiza katika show mbalimbali maarufu ikiwemo ile ya “District” katika kituo maarufu cha televisheni cha CBS.Pia ameshiriki katika “Bedford Diaries” ya Warner Bros.Sauti yake imetumika katika matangazo mbalimbali ya biashara kama vile Western Union(USA-African Market) nk.Kwa upande wa mavazi Miriam amewahi kuwa model wa jeans za Levi’s,Getty Images/Brazilian Salsa Club(Print),Bebe Noir Clothing Line,New York nk.Mwaka 2007 mtandao wa Jamati.com ulimtaja Miriam katika orodha yao ya Top 10 Sexiest African Women akiwa ni miongoni mwa wasichana wawili kutoka eneo la Afrika Mashariki.

Hivi karibuni BC ilipata fursa ya kufanya mahojiano rasmi na Miriam.Katika mahojiano haya,Miriam anaweka wazi kuhusu utaifa wake.Je Miriam ni Mtanzania au Mkenya?Nini maoni yake kuhusu sanaa ya filamu nchini Tanzania?Anatoa ushauri gani kwa wadau wa sanaa hiyo? Na je,kwa msiomfahamu, Miriam ni nani?Ana malengo gani?Kwa hayo na mengineyo mengi,fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo;

Thank you,God Bless You.

BC: Miriam, asante kwa kukubali kufanya nasi mahojiano haya. Mambo vipi?

MC: Ahsante sana kunipa nafasi hii kufanya mahojiano haya hapa BC. Mambo poa, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote. Amenibariki sana katika kazi zangu.

BC: Kabla hatujasonga mbele sana, tungependa kuweka jambo fulani wazi. Kumekuwepo na ubishi ubishi (wa mitaani zaidi) kuhusu Utanzania wako,Ukenya wako nk. Nani miongoni mwa wazazi wako ni mtanzania na nani ni mkenya?

MC: Naelewa kwamba watu wengi wangependa nichague uraia mmoja lakini tangu utotoni, huwa nasema mimi ni Mkenya na pia ni Mtanzania. Kuna wengine wanasema mara ninafanana kama Mu-ethiopia, Mjamaica au mara Msomali.

Bila kusema mengi, baba yangu, marehemu Brigadier Jack Chemmoss, anatokea Kenya. Ni Mmasai wa Mt. Elgon. Mama anatokea kijiji cha Tingeni-Muheza, Tanga. Marehemu bibi mzaa mama ni Mbondei na marehemu babu ni mwingereza ambaye anatokea Scotland. Nimekulia Tanzania na Kenya, Ulaya na hivi sasa, Marekani. Sidhani kama ni muhimu kuchagua nchi moja, bali najivunia sana kuzaliwa na kutokea Afrika Mashariki.

BC: Kwa kuangalia tu kazi ambazo umeshawahi kuzifanya,ni wazi kwamba umejaliwa kuwa na vipaji mbalimbali kwa pamoja.Unawezaje kuvihudumia vipaji vyote ulivyonavyo? Unakumbana na changamoto gani unapojaribu kuhakikisha kwamba unabakia kuwa muigizaji, mwanamuziki, mwanamitindo nk kwa wakati mmoja?

MC: Nimesomea ‘Musical Theater’ na ‘Communications(Media)’ chuoni na nimegundua shughuli zangu zote zinahusiana. Ninaweza kuvihudumia vipaji vyangu kwa mkupuo bila shida lakini inihitaji nidhamu na utashi.

Ingawa changamoto zipo, hasa ukiwa msanii wa kike, faida zipo nyingi zaidi. Sanaa inahitaji kujibuni mara kwa mara. Teknologia imebadilisha jinsi biashara inavyofanyika duniani. Utandawazi umeongeza fursa. Nimeweza kufapata kazi za utangazaji (redio; Voice of America, English to Africa), kazi za TV, magazeti, Theater, Voice Overs nk.Zote zinahudumia waafrika kila sehemu duniani. Siwezi kukataa nafasi yoyote inayonijia, hasa kama inahusiana na kutumbuiza. Huwezi kujua itakopokuelekeza!

Miriam akiwa mbele ya kamera wakati wa photo-shoot ya jeans za Levi’s jijini New York mwaka 2005

BC: Ungeambiwa leo hii uchague kufanya kitu kimoja tu baina ya muziki, uigizaji au uanamitindo ungechagua kipi?

MC: Nilianza kutumbuiza tangu mdogo sana, lakini nilikuwa na haya (aibu) na niliogopa kuimba hadharani. Kuigiza kwangu ni rahisi zaidi na ninapenda kuigiza mno, ila kuimba na mambo ya muziki kunahitaji kujiamini na uvumulivu.

Miaka chache iliyopita, niliamua kuwa nilitaka kuwa mtumbuizaji. Ilinibidi kupunguza woga na haya ya zamani. Niligundua kwamba muziki unaniuunganisha na nafsi za wasikilizaji wangu kwa hiyo hamna la kuogopa. Leo ninatunga nyimbo tofauti na kuimbia maswala yanayotutatiza wote duniani; upendo, amani na haki. Ninafurahia sana uimbaji.

Uanamitindo, kwa kweli sikuutafuta. Nashukuru kwamba nimepata nafasi nyingi kutokana na watu kunishawishi nijiendeleze na mambo ya uanamitindo. Kazi ninazozipata zinatokana na shughuli za kuigiza kama ‘commercials’ kwenye televisheni na magazetini. Ninafurahia kufanya vyote kwa kweli, kwa hiyo kuchagua kufanya kimoja sio rahisi.

BC: Mojawapo ya mambo ambayo katika siku za hivi karibuni yamekuwa yakizungumziwa sana kwenye vyombo vya habari ni suala zima la warembo (kama wewe) kujikondesha au kujinyima chakula ili waendelee kuwa wembamba. Unaliongeleaje suala hili? Unadhani kuna yoyote ambaye anastahili kubebeshwa lawama kutokana na suala hili ambalo wengine wanaliona kama ni janga fulani la kidunia hususani kwa sanaa ya urembo na mavazi?

MC: Siwezi kuwazungumzia wanadada warembo wanaojinyima chakula ili wawe wembamba kwani hilo sio suala la urembo bali ni la saikolojia na afya. Tunajua kwamba afya bora inatokana na kula chakula bora, kufanya mazoezi na kupumzisha miili yetu. Naelewa kuwa vipimo vya urembo viliyopo vinaweza kuchanganya akili na kufanya wengi watafute kupunguza mwili haraka.

Mimi naamini kwamba kila mtu ana mwili tofauti na tabia za kula tofauti.Kwa hiyo, hakuna urembo wa aina moja tu. Sielewi kwanini mpaka leo hii tunaendelea kukukubali tafsiri ya urembo inayoaaminika na kutangazwa magazetini na kwenye vyombo vingine vya habari. Sanaa ya urembo na mavazi lazima inachangia mengi tunayoiga. Ni wajibu wetu kupinga tafsiri potofu na kujivunia tafsiri za urembo zinazokubaliana na mila na desturi zetu.

Beauty is in the eye of the beholder.

BC: Jambo moja ambalo mtu yeyote atagundua akijaribu kutafuta habari zako kupitia mtandao wa Internet ni kwamba unaelewa suala zima la kujitangaza na mambo kama hayo. Unadhani kwa wakati tulionao, kuna umuhimu wa kiasi gani katika kujitangaza? Ungetoa ushauri gani kwa wasanii mbalimbali wanaochipukia nchini Tanzania au Afrika Mashariki kuhusu kujitangaza na kuzitangaza kazi zao?

MC: Tekinolojia inatupa sisi wasanii uwezo wa kujitangaza na kuwafikia watu wengi zaidi. Tunaweza kujitegemea kwa kubuni njia tofauti za kujitangaza ili kujiendeleza. Kila kinachoandikwa kwenye mtandao kinaenea haraka bila gharama.Hii ni tofauti na zamani ambapo wasanii ilibidi wajitangaze kwa njia moja au mbili.

Ningewashauri wasanii walio Afrika Mashariki washirikiane na wajifunze zaidi kuhusu masuala ya tekinolojia jinsi inavyoiendesha biashara ya utumbuizaji siku hizi. Ni muhimu kujitangaza nyumbani lakini wajue kuwa kuna waafrika kila sehemu duniani kwa hivyo soko halina mipaka siku hizi. Kama jinsi unavyoweza siku hizi kujinunulia tiketi ya ndege kwenye mtandao ndio hivyo hivyo inawezekana kuuza au kununua kazi za sanaa mtandaoni.Kwa hiyo ni vizuri kutumia njia zote zilizopo, mpya na za zamani.

BC: Ingawa uko mbali na Tanzania, tunatumaini huwa unafuatilia maendeleo ya sanaa ya urembo,mavazi na hata filamu. Unayaongeleaje unayoyaona? Tunapiga hatua au tunarudi nyuma? Ni waigizaji gani wa filamu ambao unavutiwa na utendaji wao, wanaume kwa wanawake?

MC: Ndio, ninafuatilia sana yote yanayoendelea katika sanaa ya urembo, mavazi na filamu Tanzania na Afrika nzima. Naamini kwamba tunapiga hatua nyingi sana lakini ningependa kuona mengi zaidi nitakapokwenda nyumbani mwaka huu. Ninafuatilia sana wasanii wa kike na wa kiume wa Tanzania.Wengi wao nawajua binafsi.

Miaka 10 iliyopita, nilikuwa Dar es Salaam na wasanii wengi ambao wanavuma sasa hivi, walianza kazi zao wakati huo na wanaendelea kufanya vizuri sana. Nimepata kuona kazi za Stephen Kanumba, Sultan Tamba, Blandina Changula na wengineo. Wote ni wasanii hodari kweli na wanaendelea kutupa moyo sisi ambao tuko mbali na nyumbani. Ningependa kuona waafrika wakiwaridhia wasanii hawa ili wajiendeleze zaidi. Inabidi tujivunie sanaa na mitindo yetu ili kuwapa wasanii moyo ili watimize malengo yao.

BC: Sasa hebu tuongelee muziki wako. Nini kilikuvutia kuingia kwenye fani ya muziki? Ulianza lini rasmi shughuli za muziki? Na je unakumbuka ni lini ilikuwa mara yako ya kwanza kupanda jukwaani na kutumbuiza kama mwanamuziki?

MC: Kama nilivyosema hapo awali, nilianza kutumbuiza tangu mdogo sana. Ninafurahia kutumia fani ya muziki kuburudisha, kuelimisha na kuhamasisha yeyote anayependezwa na mtindo wa muziki wangu.

Nilianza shughuli za muziki nilipokuwa nikisoma nchini Kenya. Niliimba katika mashindano ya kuimba shuleni na kusomea muziki hadi chuoni. Kusomea muziki shuleni kumenisadia sana kutunga nyimbo za aina mbalimbali. Nilipokuwa nyumbani niliombwa mara nyingi kuimba jukwaani katika shughuli tofauti.

Kama ninakumbuka vizuri, mara ya kwanza kupanda jukwaani na kutumbuiza nilikuwa na umri wa miaka 10, nilipoimba shairi moja mbele ya wanafunzi na walimu wa shule ya Msingi ya St. Nicholas, Nairobi.

Miriam akifanya vitu vyake jukwaani wakati alipokuwa na Soukouss Star.

BC: Nini mchango wa wazazi wako katika vipaji na shughuli unazozifanya hivi leo? Je walikuunga mkono tokea mwanzo au kidogo ulikwaruzana nao hususani tukizingatia kwamba wazazi wengi wa kiafrika zamani waliyaona masuala ya burudani ndivyo sivyo?

MC: Wazazi wangu wamechangia mno katika vipaji na shughuli zangu. Tangu utotoni, walinihimiza kufuatilia chochote nilichopenda. Marehemu baba alipenda niwe wakili lakini alijua kwamba nilipenda masuala ya kutumbuiza zaidi.

Nilipokuwa Kenya na Tanzania, wazazi wangu na familia yangu walikuja kunipa moyo nilipokuwa nikiigiza au kuimba jukwaani. Mama yangu, kama mama yoyote, anaendelea kuniongoza kwa kunikumbusha kwamba, ‘ukitaka cha mvunguni, sharti uiname’ na kwamba lazima nikumbuke ninapotoka mara zote. Hata kama niko mbali na nyumbani, ninajitahidi kukumbuka utamaduni, dini, elimu na ushauri wa wazazi wangu. Wamenifunza mengi kwa kweli na ninamshukuru mungu sana kunipa wazazi ambao wamenipa mengi ya kujivunia na ya kunielekeza maishani mwangu.

Miriam(wa pili kutoka kulia kwenda kushoto) akiwa jukwaani wakati alipokuwa na kundi la Marvelettes Revue.

BC: Kila mwanamuziki huwa ana tafsiri yake kuhusu muziki au dira yake kimuziki. Kwako wewe, muziki ni nini? Au kwa maneno mengine kwanini unafanya muziki?

MC: Kweli, kila mwanamuziki ana tafsiri yake kuhusu muziki. Muziki kwangu ni kama lugha ambayo inanisaidia kujieleza na kuponya yote yanayokera moyoni. Lugha ya muziki inaeleweka na kila mtu duniani. Nimeweza kutumia muziki kujihusisha na maswala muhimu kama mapenzi, dhuluma, upatanishi nk. Natarajia kuwa nitaweza kuchangia mengi muhimu katika jumuiya kwa kutumia kipaji cha muziki.


BC: Ni wanamuziki gani kutoka Afrika Mashariki ambao wanakuvutia kutokana na kazi zao? Na kutoka nje ya Afrika Mashariki je? Wepi ungependa kushirikiana nao kisanii?

MC: Ninavutiwa na wanamuziki wengi sana ingawa wote wana mitindo tofauti na ya kwangu. Ninavutiwa sana na wasanii kutoka Afrika Mashariki kama T.I.D, Nameless, Ragga Dee, Ray C, Nakaaya, Kaz, Jay D, Eric Wainaina, Atemi, Bamboo na Chameleon nk. Nje ya Afrika Mashariki, ninavutiwa na Fally Ipupa, Angelique Kidjo, Khadja Nin, 2 Face, Busi Mhlongo na wengineo. Ningependa kushirikiana na yeyote kwa kweli, hasa nitakaporudi nyumbani mwaka huu.

You need to a flashplayer enabled browser to view this YouTube video

Wimbo “Rudi” ni single ya kwanza ya Miriam kutoka katika albamu ya Love in Reverse anayotarajia kuifyatua mwaka huu.

BC: Tulipowasiliana nawe kwa mara ya kwanza siku chache zilizopita ulitueleza kwamba uko mbioni kukamilisha albamu. Unaweza kutuambia kidogo kuhusu albamu hiyo? Umeipa jina gani, unatarajia kuitoa lini na mambo kama hayo?

MC: Albamu karibu kukamilika (Summer mwaka huu) na ninapanga kwenda kutembelea Tanzania na sehemu nyingine za Afrika hivi karibuni. Albamu hii imenichukua muda mrefu lakini nimetambua umuhimu wa subira na uvumilivu katika sanaa.

Ninaamini kwamba kila mtu atakayechukua muda kuisikiliza, atapata kitu kimoja au viwili ambavyo vitamfurahisha. Albamu inaitwa, “Love In Reverse”, inasisitiza umuhimu wa kusameheana, kuungana na kufuta chuki kibinafsi na katika jamii. Sana sana, albamu hii inazungumzia mifano ya changamoto nilizozikabili maishani mwangu. Nimejiunga na wanamuziki mbalimbali kutoka kila sehemu duniani, kwa hiyo natumai muziki wangu utawafikia watu wa kila aina. Sitaki kusema mengi sana, mnaweza kupata habari zangu katika mtandao, 🙂 www.myspace.com/miriamchemmoss

Miriam akifanya vitu vyake jukwaani huko Boston,Massachusetts mapema mwaka huu wakati wa tamasha lililojulikana kama VUMA ambalo lilikuwa maalumu kwa ajili ya watu waliokuwa wameathiriwa na vurugu zilizofuatia uchaguzi mkuu wa Kenya.

BC: Kwa mapana na marefu, wewe ni binti ambaye watu wengi hawasiti kukuita “mrembo”. Sasa kila mrembo inasemekana ana siri ya urembo wake. Nini siri ya urembo wako?

MC: Ahsante kwa maoni yako, ninashukuru kwamba watu wananiona hivyo. Siri sina kwa kweli, sidhani kuna siri moja ya urembo zaidi ya kwamba siogopi kujaribu njia mpya bora za kula. Inahitaji nidhamu kali kula upya lakini ninajivunia kuwa Vegetarian muda wa miaka 7 sasa. Sili nyama (ya kuku, ng’ombe, mbuzi, nk), nakula samaki tu na nimeongeza vyakula muhimu kama mboga, matunda, na vyakula vingine vya faida nyingi zaidi. Nimekuwa mvivu kwenye mazoezi(huwa nakimbia na kuogelea kila nikipata muda), kupumzika mara kwa mara, kunywa maji…. Sio rahisi kupata muda wa kufanya yote kama inavyotakiwa lakini ninajitahidi.

BC: Nini malengo yako katika miaka mitano ijayo?

MC: Nitaendelea kuimba, kuigiza na kutumbuiza, haswa Afrika Mashariki na kusaidia katika jitihada za kusambaza ujumbe wa amani, upendo, ukweli na haki. Ningependa kusaidia katika jitihada za kueneza elimu na katika projects za maana.

BC: Miriam umeshaolewa?

MC: Nikiwa tayari kupanga harusi, kualika familia yangu na marafiki zangu………., nitawataarifu :-).

BC: Asante kwa muda wako Miriam. Tunakutakia kila la kheri katika kazi zako.

MC: Ahsante pia kwa muda wako na fursa hii. Nitaendelea kuwajulisha habari zangu. Nawatakia kila la kheri na baraka maishani na katika kazi zenu.

Kwa habari zaidi kumhusu Miriam Chemmoss tafadhali bonyeza hapa, hapa na hapa

 1. www.cbs.com, 18 May, 2008

  […] UnionUSA-African Market nk.Kwa upande wa mavazi Miriam amewahi kuwa model wa jeans za Levi??s,Gettyhttp://bongocelebrity.com/2008/05/18/one-on-one-with-miriam-chemmoss/Cbs LEtting you download full Ep. of ThresholdYou can now download full episodes of threshold tv […]

 2. link:www.cbs.com | Inmars, 18 May, 2008

  […] ONE ON ONE WITH MIRIAM CHEMMOSS1 hour ago by bongocelebrity Endapo kuchanganya utaifa,damu na tamaduni mbalimbali ni mojawapo ya chachu za mafanikio fulani hapa duniani, basi ushahidi wa dhana hiyo unaweza kuupata kwa kuangalia maisha ya mrembo Miriam Chemmoss(pichani). …BONGO CELEBRITY – http://bongocelebrity.com […]

 3. noela, 19 May, 2008

  so good mamae,endelea zaidi na zaidi mungu akusaidie

 4. Pearl, 19 May, 2008

  acha niseme ukweli jamani, mtoto wa watu mzuri huyu kwanza amekolea mpaka rangi sijui anaogea maji gani!!!!

 5. Ali kunik, 19 May, 2008

  Safi bint endelea kama mpenda maendeleo nakutakia kila kheri
  usivunjike moyo pale unapota mtetereko kwani ndio njia pekee na siri ya maendeleo

 6. Dinah, 19 May, 2008

  What a mix Masai na Mtanga ndio maana kazuri! BC shukurani kwa mahojiano haya, Miriam Hongera na kila la kheri ktk shughuli zako.

 7. binti-mzuri, 19 May, 2008

  kumbe half castI!mzuri kwa kweli

 8. baker, 19 May, 2008

  Duhh Ebwana weeeeeee! uko hot binti wa watu! jitahidi hakuna mafanikio yanayokuja kiulaini siku zote, lazima utoke jasho ili ulie kivulini, kweli life ya mtoni hai danganyi.
  Big up all the best dada etu.

 9. hombiz, 19 May, 2008

  good luck qute chick!.

 10. Kamkaka, 19 May, 2008

  Miriam,
  U-mzuri na kazi zako ni nzuri.Please keep doing what you are doing.

 11. GEORGE MWANGOSI, 19 May, 2008

  Miriam,

  Hongera na Kila la kheri. Keep up the good work.
  All the best to you.

 12. mariam kabula, 20 May, 2008

  Kina mirium siku zote tunakuwaga wazuri na wenye akili.

 13. Amina, 20 May, 2008

  we miriam hovyo….hapa siyo pakujifagilia

 14. lil, 20 May, 2008

  Ummm how come on the link provided (sexiest african women) it says she is a Kenyan? We should be cheering for Flaviana instead beause she is on that list as well and poudly TANZANIAN! 🙂

 15. binti-mzuri, 20 May, 2008

  lakini jamani baba yake mkenya,na siku zote tunafataga kabila la baba,kwahiyo tusilalamike sana wakisema mkenya… flaviana matata is one hot babe

  mariam kabula wewe binafsi sikujui,ila kuna mariam ninaowajua na sura zao ni mmmh…miguno!!

 16. Tatu, 20 May, 2008

  I don’t think kama walimuuliza anatoka wapi kwenye Top sexiest african women. Waliwachagua hawa wasichana na kuwaandika based on their own knowledge. I am cheering for all ambao wanatokea East Africa. Bravo Miriam na Flavian.

 17. maryciana, 20 May, 2008

  yupo okay,not the pretiest gal i have eva seen

 18. michelle, 20 May, 2008

  Lil i support you 100% she considers her self as Kenyan even though she has Tanzanian blood, then why should we keep on fagilialing a kenyan model, lets fagilia our top model Flaviana Matata who is pure african no white or any mixture in her, wake up Tanzania, be proud of your nature.

 19. trii, 21 May, 2008

  hiii plz we are all one east africa,so its ok kumfagila,flavia is also in the list plzz ckeck.

 20. trii, 21 May, 2008

  check

 21. trii, 21 May, 2008

  mariam kabula—is ok jifagilie usipojifagilia wewe nani atakufagilia????mbona watu kibao hapa huwa wanajifagilia ooooh mara nipo uk,usa and so on and we dont mind,gooo on girl.jiamini

 22. Amina, 21 May, 2008

  mhhh hovyo kujifagilia ushamba,kama mzuri si alete ppicha yake hapa..mnajazana ujinga

 23. binti-mzuri, 21 May, 2008

  MH JAMANI JAMANI!!!

 24. trii, 22 May, 2008

  usilete lugha chafu hapa watu wote sawa mbele ya haki+ tumeumbwa kwa mfano wake.kuna watu wengine wameumbwa na roho za kwa nini,litakae mgusa ndo huyo huyo mmmmmmmmmm

 25. Jennas, 22 May, 2008

  Maisha Brrrrr vibration kwa kwenda mbele nipeni address ya huyo mkei sitiroku mtanzania niangalie kama naweza bonga nae sikuweza kusoma historia yake kwa kweli nina haraka na net yenyewe yakulipia mia tano kwa saa basi tabu tupu

 26. ser, 22 May, 2008

  Sexy Mariam, alisha wahi kuwa demu wa Mike Tyson huyu zamani.

 27. Amina, 29 May, 2008

  kama we unajiamini taja jina,unafumba nini?alichoki anakwambia unarusha jiwe kizani atakaekae lia nyweee ndo limempata,sasa nawewe kikikuuma ndo wewe wewe, dongo lako hilo bishosti

 28. Upendo, 24 July, 2008

  Miriam is beautiful both inside and out, she is humble and a joy to be around so stop hating players….damn!!!! Ndiyo maana wengine hatuendelei

 29. Crystal, 24 July, 2008

  I totally agree she doesn’t have an ounce of bad blood…I was with her in college in Iowa and she was bright, beautiful and hard working….hongera Miriam Mpenzi…keep it up girl!!! Hold it down sweetie!!!

 30. Abdullah Said, 18 February, 2009

  Mtoto wa mama yangu mdogo umejaliwa na mungu kwa yote unyoyafanya ila nakusihi usisahau mizizi yako Tanga ndio nyumbani sisi ndio ndugu zako na tunakupenda sana

 31. Nyido, 13 March, 2011

  Siyo half cast , quarter cast

Copyright © Bongo Celebrity