ANA KWA ANA NA “MWENYEKITI” MAGGID MJENGWA.

Kama wewe ni msomaji mzuri wa magazeti na majarida mbalimbali kutoka Tanzania,basi sina shaka kabisa kwamba jina Maggid Mjengwa (pichani) litakuwa sio geni kwako! Makala zake za kusisimua,kuchokoza hisia na kujenga hoja za nguvu ni miongoni mwa vivutio muhimu vya wasomaji wa magazeti ndani na nje ya Tanzania. Leo hii tunaweza kabisa kuthubutu kusema kwamba Maggid ni miongoni mwa wanahabari bora tulionao kwani hana uoga wowote pale anapokuwa anaandika au kuongelea jambo ambalo analiamini kwa dhati.

Lakini Maggid,kama ambavyo pengine unafahamu tayari, haishii magazetini tu bali pia ni blogger maarufu hivi sasa. Blog yake ya picha ambayo mwenyewe anaiita “kijiji” na hivyo wasomaji wake na watembeleaji wake “wanakijiji”, imejipatia umaarufu sana kwa kuonyesha au kwenda kule ambapo ndiko kunahesabika kuwa kwenye hali halisi ya maisha ya mtanzania. Ukiitembelea na kuisoma blog yake vizuri kwa kutizama picha lukuki zinazoipamba blog yake,utaweza kuwa jaji mzuri kama “bongo ni tambarare” au bado zile ahadi za uchaguzi uliopita ni mbwembwe za kisiasa tu.Mwenyewe anasema blog yake ni kimbilio na sauti kwa wale ambao kila mara huwa wanasahauliwa!

Maggid pia ni mjasiriamali.Yeye ndiye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ijulikanayo kama Ikolo Investment Co ambao ndio wachapishaji wa Gozi Spoti; jarida la michezo, sanaa, maisha na burudani linalotoka kila Jumatano. Maggid pia ni mwanamichezo,mpenda michezo na shabiki mkubwa wa soka.

Hivi karibuni,baada ya kumsaka kwa muda mrefu kutokana na ratiba zake za kazi kumbana,tulifanikiwa kupata fursa ya kufanya naye mahojiano utakayoyasoma hivi punde.Kama ambavyo ungetegemea,Maggid anatoa “darasa” katika mahojiano haya.Mbali ya kukupa historia ya maisha yake kwa undani,Maggid anakumbusha vipengele fulani fulani vya historia ya nchi yetu ambavyo ni muhimu. Lakini kwa mapana, anaongelea kuhusu suala la uandishi na pia blog yake bila kusahau changamoto ambazo nchi yetu inakabiliwa nazo hivi leo katika nyanja mbalimbali. Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo;

BC: Maggid Mjengwa,karibu sana ndani ya BongoCelebrity

MJENGWA: Asante sana!

BC: Kwanza kabisa ningependa kupata kutoka kwako mwenyewe historia fupi ya maisha yako.Ulizaliwa wapi,lini,ukasomea wapi,unatoka kwenye familia ya watoto wangapi na mambo kama hayo.

MJENGWA: Awali ya yote, natanguliza shukran zangu za dhati kwako Jeff kwa heshima uliyonipa kwa kufanya mahojiano nami kupitia jukwaa hili la kijamii. Naitwa Maggid John Ramadhan Mjengwa. Nina bahati ya kuwa na asili zaidi ya moja. Nina asili ya pwani na bara. Nimezaliwa Kliniki ya Ocean Road, Dar Es Salaam. Mimi ni mmoja wa wale ambao huwaita wa kizazi cha Azimio la Arusha la mwaka 1967. Nimekulia Ilala, Mtaa wa Iringa nyumba namba 27. Baadae familia yangu ilihamia Kinondoni Biafra, mwaka 1977.

Natoka katika familia ya watoto tisa. Wawili hawako tena duniani, mmojawapo ni kaka yangu, Grey John Ramadhan Mjengwa. Alifariki katika ajali ya basi mkoani Tanga zaidi ya miaka kumi iliyopita. Grey ndiye aliyenitangulia kwa kuzaliwa. Na mimi nilikuwa wa pili kuzaliwa. Elimu ya msingi na Sekondari nimesomea Dar. Nilimaliza Tambaza Sekondari mwaka 1987, baadae nilisoma Kidato cha Tano na Sita mkoani Mbeya pale Sangu Sekondari. Baada ya Sangu nilijiunga na JKT kwa mwaka mmoja ( Operesheni Kambarage 1990-91). Kisha nikaamua kwenda kuishi na kufanya kazi za kujitolea wilayani Njombe, Iringa. Niliishi kijiji cha Igagala. Huko nilifundisha kwa kujitolea kwenye Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi, Ulembwe. Kilomita 15 kutoka Njombe mjini. Nilipewa pia eka moja ya kulima. Nililima mahindi, viazi na maharage. Vile vile nilipiga picha na kuandika habari za huko na kutuma kwenye magazeti, mojawapo ni Daily News. Baada ya mwaka mmoja na nusu kijijiji hapo nilikwenda nchini Sweden. Huko nilikaa kwa miaka 12. Nimesoma kozi kadhaa kwenye vyuo vya Sweden na hatimaye kuhitimu shahada ya ualimu kwenye Chuo Kikuu cha Linköping. Nimefanya kazi pia ya kufundisha kwenye baadhi ya vyuo vya maendeleo vya Maendeleo ya wananchi vya nchini Sweden.

Naam. Nimesema nina asili mbili; pwani na bara. Nitafafanua. Baba yangu alizaliwa kijiji cha Nyeregete, kwenye bonde la Usangu, Mbeya. Babu yangu, Chifu Mtenji Ramadhan Mjengwa alikuwa kiongozi wa kijadi mongoni mwa watu wa kabila la Wasangu. Babu yangu mzaa mama, Fundi Pazi alitokea kwenye kabila la Wahehe wa Iringa. Yeye alifanya kazi ya ujenzi wa barabara. Katika kazi yake akaja kukutana na bibi yangu mzaa mama, Amina Binti Muhando Mwaruka. Hivyo basi, babu mzaa mama akalowea pwani na hususan Uzaramoni. Bibi yangu, Amina binti Muhando Mwaruka ( alifariki mwaka jana akiwa na umri wa miaka zaidi ya 87) anatoka kwenye ukoo maarufu wa Mwaruka. Ni ukoo huu anaotoka mwanamuziki mahiri, Marehemu Mbaraka Mwinshehe Mwaruka. Mbaraka alimwita bibi yangu shangazi. Nyumba ya marehemu bibi yangu kijijini Mzenga inapakana na nyumba ya Marehemu Mwinshehe Mwaruka, baba mzazi wa marehemu Mbaraka Mwinshehe Mwaruka.

Labda mpaka kufikia hapo kuna watakaoanza kunielewa kwanini napenda sana maeneo ya pwani kama vile Bagamoyo. Hakika, ni kutokana na asili yangu hiyo ya pwani kwa upande wa mama yangu. Kutoka Bagamoyo mpaka kijijini kwa mama yangu, Mzenga, Kisarawe ni mwendo wa dakika 45 kwa gari ndogo kwa kupitia njia ya mkato ya Bagamoyo-Miembe saba hadi Mlandizi.

BC: Unakumbuka wakati ukiwa mdogo au ukiwa shule ya msingi ulitaka kuwa nani pindi ukimaliza shule? Na labda kuongezea tu,ni waandishi gani wa habari uliokuwa ukipenda zaidi kuwasoma enzi hizo?Kwanini?

MJENGWA: Nilipenda masuala ya siasa, picha na michezo tangu utotoni. Mazingira nayo yanachangia kumfanya mtu awe kama alivyo. Pale Ilala tulikaa karibu kabisa na uwanja wa Karume. Nakumbuka niliingia uwanjani Karume kwa mara ya kwanza nikiwa na miaka sita nikiongozana na kaka yangu Grey. Ilikuwa ni mechi kati ya Simba na Cosmo Politans. Tuliingia uwanjani kwa kuruka ukuta kwenye moja ya kona za uwanja huo. Grey alinipandisha na kunishusha uwanjani. Nilishangaa mgambo hawakunifuata bali waliwafuata wengine. Leo naelewa kuwa mgambo wale walikuwa ni watu wema sana. Wangefanya nini na mtoto wa miaka sita anayetamani kuona pambano la soka? Baadae ilikuwa rahisi zaidi kuingia uwanjani Karume na hata National Stadium. Ilikuwa ni kwenda getini, unamtafuta mtu mzima mmoja, unamuamkia kisha unamwomba akushike mkono muingie wote uwanjani kama mtoto wake. Mkishavuka geti hakuoni tena, wakati mwingine, kwa shauku ya mpira tulisahau hata kusema ‘asante’ kwa waungwana wale waliotusaidia kuingia bure uwanjani.

Mapenzi yangu kwa klabu ya Simba yalianzia katika mechi ile ya kwanza niliyoiona maishani mwangu kati ya Simba na Cosmo. Simba walivaa jezi nyekundu na nyeupe. Cosmo walivaa bluu. Basi, cha kwanza kwangu ilikuwa kuchagua rangi. Nilichagua nyekundu na nyeupe. Lakini si rangi tu, Simba siku ile walicheza vizuri na kushinda pambano hivyo basi kutonifanya nibadili uamuzi wangu.

Hakika, tangu utotoni nilikuwa na mwelekeo wa kupenda masuala ya kisiasa na kijamii. Kupenda michezo na picha. Kwa namna moja au nyingine, wazazi wangu walinisaidia sana kukuza vipaji vyangu. Nilianza kusikiliza redio nikiwa na miaka minne au mitano hivi, wazazi waliniruhusu kuchezea redio. Mwanzoni nilidhani kuna watu wanaongea na kuimba ndani ya redio! ( Nadhani baadhi yenu mlifikiri kama mimi). Mapema sana nilianza kusikiliza vipindi vyenye kuelimisha. Miaka hiyo kabla hata sijatimiza miaka saba nakumbuka kuanza kusikiliza vipindi kama; mbiu ya mikoa, ujumbe wa leo na mazungumzo baada ya habari. Hicho cha mwisho ndicho ambacho Mzee Paul Sozigwa alikuwa akikiandaa. Nakumbuka pia kila Jumapili Mkurugenzi wa RTD, Mzee David Wakati alikuwa na kipindi chake chenye kujadili masuala mbali mbali. Halafu nakumbuka kufuatilia kipindi cha ‘ Umoja wa Mataifa Wiki Hii’ ambapp ‘Born Again Pagan’ maarufu kama BAP na Abdalah Mbamba walikuwa wakikiendesha kwa nyakati tofauti.

Nilikuwa na kiu kubwa ya kusoma maandishi na kuangalia picha kwenye vitabu, majarida na magazeti. Nilifungua karibu kila kurasa ya kitabu kilichokuwa nyumbani. ( Hatukuwa na vitabu vingi sana). Nakumbuka kitabu cha Patrick Lumumba wa Kongo, sikuweza kusoma ( kiliandikwa kwa Kiingereza) lakini nilifuatilia picha za kitabuni na kumwuliza baba yangu. Nikafahamu kilihusu nini. Nakumbuka pia kitabu cha John Okello( Zanzibar Revolution) Hiki nacho kilikuwa ni kwa Kiingereza, niliangalia picha na kumdadisi baba yangu, alinieleza kilihusu nini. Nilipofika Sekondari niliweza kuvisoma vitabu vyote hivyo. Hicho cha mwisho kilinifanya nifatute kila namna ili nifike Zanzibar kuona kwa macho yangu mazingira ya kisiwa yalikofanyika mapinduzi aliyoyaelezea Okello kwenye kitabu chake. Nilifika Zanzibar mara baada ya kumaliza kidato cha nne. Na nilikuwapo kwenye sherehe za mapinduzi Januari 12, 1989. Yote hii inaonyesha kwa namna moja au nyingine jinsi vitabu vinavyoweza kutujenga kama wanadamu.

Page 1 of 6 | Next page