
Kama kuna kitu ambacho kilitokea katika upande wa burudani nchini Tanzania hivi karibuni na kuteka hisia za watanzania wengi,bila shaka kitu hicho ni kundi lililokuwa linajulikana kama Ze Comedy.Tunasema lililokuwa linajulikana kama “Ze Comedy” kwa sababu mpaka sasa kuna utata au kesi kuhusiana na haki miliki ya jina hilo!Kesi iko kwa pilato.
Ilifikia kipindi ukimtafuta mtu siku ya Alhamisi jioni(wakati kipindi cha Ze Comedy kipo hewani) usipompata yawezekana kabisa yupo mbele ya luninga yake akiwacheki Ze Comedy huku simu yake akiwa ameiweka katika mtetemko(vibration) katika kumaanisha kwamba “hataki usumbufu”.
Wakati kundi hilo likizidi kujipatia umaarufu mara ghafla zikaja habari kwamba Ze Comedy wanakwenda “mapumzikoni”.Pamoja na kwamba tangazo hilo liliwasikitisha watu,ilieleweka kwamba mapumziko ni jambo muhimu kwa kila binadamu kwa hiyo watu wakaelewa!
Tatizo lilikuja pale mgogoro ulipofumka baina ya Ze Comedy na uongozi wa kituo cha EATV ambacho ndio kilikuwa kinarusha kipindi cha Ze Comedy kila siku ya Alhamisi saa moja jioni.Mapatano ya mezani yakashindikana.Kesi ikaenda mahakamani(bado ipo).Siasa nazo zikaingilia kati.Vigogo wa nchi wakaingilia lakini wapi.
Leo hii watu wengi wanajiuliza,je Ze Comedy watarudi? Na wakirudi watarudi kwa namna gani,kwa kutumia jina gani?Unadhani watakamata tena?Unadhani kilichotokea mpaka hivi sasa kinatoa mafunzo gani kwa vikundi vingine na washika dau wote wa fani ya burudani nchini Tanzania?
Kuna habari ambazo bado hazijaweza kuthibitishwa zinazosema kwamba vijana hao mahiri kwa kuvunja watu mbavu huku wakielimisha jamii wana mpango wa kufanya ziara kabambe nje ya Tanzania.Tunasubiri.
Page 1 of 3 | Next page