mike-sikawa-1982bcTakribani mwezi mmoja uliopita Tanzania ilipata pigo la kuondokewa na mwandishi na mtangazaji mashuhuri,Mike Sikawa.Kama wewe ni msomaji magazeti na msikilizaji mzuri wa redio, bila shaka utakuwa uliwahi kulisikia jina la Mike Sikawa.

Kifo cha Mike ni pigo kwa taaluma nzima ya habari na mawasiliano.Mike ni miongoni mwa waandishi ambao mchango wao katika ulimwengu wa kupashana habari kamwe hauwezi kubezwa.

Ingawa ni wiki kadhaa zimeshapita tangu kuondokewa na Mike ipo makala ambayo iliandikwa na mtu aliyemfahamu Mike Sikawa kwa karibu,mwandishi mwingine Freddy Macha ambayo tumeona itakuwa ni ukosefu wa adabu isipopata nafasi hapa ndani ya BC kwa heshima na kumbukumbu ya Mike Sikawa.Mtatusamehe kwa kuchelewa kuiweka hapa.

Picha ya Mike kwa hisani ya Da Chemi.

MAISHA YA MWANDISHI WA HABARI MIKE SIKAWA: UMUHIMU WAKE NINI KWA KIZAZI CHA SASA?…

-Na Freddy Macha

Faida kubwa ya kuwasoma na kuwachunguza watu maarufu au wenye majina ni mafunzo, hamasa na imani. Kwa mfano sasa hivi kitabu kinachouza kama njugu duniani ni Dreams From My Father cha Barack Obama.Humo utaona alivyogeuza maisha yake ya shida (kutaniwa kuwa chotara, kutomwona babake ) kuwa mapigano ya kuwa Rais wa Marekani.

Habari za watu wanaojulikana ni somo kuu la maisha.Ukimchunguza Nelson Mandela, utaona namna yeye pia alivyogeuza karaha ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini (jela miaka 26, mathalan)kuwa tabasamu.Mandela na Obama wanazo tabasamu za Kiafrika hasa….Karibu Mandela atatimiza miaka 90; hata asipotimiza, kaula, keshaula kautafuna uhai…

Kuna wengi wengine duniani wanaofanya mengi (hata kuwazidi hawa jamaa), wanaojitahidi lakini, wakashindwa. Wapo pia Wabongo wengi wanaotutoka bila kufahamika. Wanajaribu wee ; wanaharakatika wee wanaghairi; wanaishia makaburini, hakuna anayewajua; wanaowalilia ni ndugu zao au marafiki wachache tu. Yarabi, yarabi

Karibuni tumetokwa na mmoja wa waandishi wa habari wakubwa Tanzania.

Mike Sikawa aliyefariki akiwa na umri wa miaka 55 alijenga jina miaka ya Sabini na Themanini. Miaka Ishirini ya mwisho ya maisha yake alifanya kazi idhaa ya kiswahili ya BBC, kwanza London, kisha Dar es Salaam hatimaye Afrika Kusini. Wengi hawamjui kwa kuwa aliandika kwa lugha ya Kiingereza; alikuwa na safu katika This Day iliyoelezea visa na mikasa ya Bondeni yaani kule Johannesburg.

Nilikuwa naongea na mhariri wa Bongo Celebrity, Jeff Msangi akasema matatizo ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo ni kutokuwa na habari nyingi kuhusu watu muhimu wa zamani. Baada ya Mike Sikawa kufariki haikuwa rahisi kupata picha au habari zake. Bahati nzuri hii leo kumezuka mtindo wa mablogu kuweka kumbukumbu. Lakini ni wangapi (hasa vijijini) wana uwezo wa kusoma makompyuta?

UMUHIMU WA WAALIMU WETU

Nilimjua Mike Sikawa ujanani; tukisoma wote shule za sekondari Ilboru, Arusha na Mzumbe, Morogoro; tukafanya kazi ya uandishi wa habari (yeye Daily News; miye Uhuru). Ingawa alikuwa mbele yangu kwa kidato kimoja; Ilboru tulifundishwa fasihi na mwalimu machachari, Mama Chitepo, mkimbizi toka Zimbabwe(aliyekuja baadaye kuwa Waziri wa Elimu). Mama Chitepo, mkali lakini mcheshi; alitupa mshawasha mzuri sana wa kupenda vitabu na kuandika.

Mwalimu anayekufundisha ana uwezo wa kukuharibia maisha yako au kuyatengeneza. Ingawa Mama Victoria Chitepo alitoka katika shida za ukimbizi wa Zimbabwe hakukata tamaa na alitupa sisi vijana mshawasha wa kusoma. Hilo lilimsaidia Mike Sikawa kuja kuwa mwandishi mzuri wa habari.

KARAHA ZA SHULE YA MZUMBE ZILIMPA MWAMKO WA KUIPENDA JAMII YAKE YA TANZANIA

Kwangu, Mzumbe ilikuwa karaha, baada ya mazingira niliyozoea kaskazini ya Tanzania. Morogoro ilinizoga: vumbi, upupu, nyoka, ugenini. Na Sikawa aliyenitangulia kidato kimoja tayari sasa mwimbaji kiongozi wa bendi ya shule Earthquakes (Tetemeko la Ardhi) ; akisaidiana na mpiga gitaa mkimbizi toka Afrika Kusini, Tabiso Leshoai, wakanikaribisha.

Kwa kuwa nilishaanza kutwanga gitaa nikajiunga nao…Enzi hizo gwiji mashuhuri Morogoro, Mbaraka Mwinshehe alipenda kuja kutumbuiza pale shuleni, dansi lililohudhuriwa na wasichana wapenzi wetu toka Kilakala. Sikawa aliyekuwa na kipaji cha kuongea vizuri na watu alifanyiana masihara na Kaka Mwinshehe, akamlainisha gwiji kimaneno sukari. Wakati wa mapumziko tukapewa vyombo vyake tupige. Nakumbuka Earthquakes tukipigiwa makofi tulipoingia jukwaani, miye na gitaa la pili la ridhimu, nataka kujionyesha kwa wasichana; nikawaharibia wenzangu. Baadaye wakanifuata. Mike kafura: “Umepiga utumbo mtupu!”

Tabiso naye: “Hatuendi jukwaani kujionyesha bali kufanya kazi.”

Hawa jamaa hawakuendelea na muziki lakini miye kazi nimeishika hadi leo kinidhamu kutokana na somo la tukio lile dogo.

Miaka ya mwanzo ya Sabini ilikuwa ya mapambano makali duniani. Rais Richard Nixon wa Marekani kalazimishwa kujiuzulu, vita vya Vietnam vinawaka, mapambano ya Wamarekani weusi chini ya Black Panther dhidi ya ubaguzi wa rangi, mauaji ya Rais Mkuu wa Chile, Salvador Allende wa Chile aliyetolewa madarakani na majasusi wa CIA; huku Afrika harakati dhidi ya ubaguzi na ukoloni. Wakimbizi (Msumbiji, Zimbabwe, Angola, Afrika Kusini) wakiranda randa Bongo wakipanga njama za kujikomboa. Ilikuwa pia enzi ya waandishi walioandika safu zilizonguruma: Philip Ochieng na Jenerali Ulimwengu; huku kitabu kilichochangia elimu ya historia ya Mwafrika duniani How Europe Underdeveloped Africa cha Walter Rodney mzawa wa Guyana mhadhiri wa historia chuo cha Dar. Vile vile majaribio ya kupindua nchi baada ya majeshi yakiongozwa na akina Chipaka na Bibi Titi Mohamed kushindwa kuangusha serikali. Visiwani, Rais Sheikh Amani Karume akapigwa risasi mwaka 1972. Bongo haikuwa mchezo…

Kama hali ya migomo ilivyo leo Tanzania; wanafunzi hususan, hatukutulia.

Mzumbe ikajiunga na vurumai. Matatizo hayakuwa madogo: waalimu hawafundishi ( mishahara midogo); chakula kibovu, mabweni yamejaa vumbi, usiku tunaliwa na mbu; ufirauni; punde tukaandamana kwenda mjini, tumechoka; katikati ya safari tukarudishwa mkuku na Askari wa FFU. Wale tuliokataa kwenda darasani, hesabu yetu 150 tukafukuzwa nyumbani miezi mitatu. Viongozi wa msafara hawakurudi kabisa. Kati yao alikuwa mkimbizi, Tabiso Leshoai na Mike Sikawa.

Mike alikuwa mmoja wa viongozi wa mgomo na maandamano yale; alikuwa tayari kutoendelea na masomo ili mradi maisha ya pale yawe mazuri. Hii leo Mzumbe ni moja ya shule zinazosifiwa kwa elimu bora nchini.

KUFUKUZWA SHULE AU KAZINI HAINA MAINA MWISHO WA MAMBO

Baada ya kufukuzwa shule Mike alijawa na hamasa zaidi. Angekuwa mtu mwingine labda angeishia kuvuta bangi, kuwa mlevi na mgomvi. Ila alijitumbukiza katika kusoma vitabu, kujiendeleza kwa kuongea na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar (akina Professa Walter Rodney).Miaka hiyo Bongo haina Uhuru wa kusema: magazeti muhimu mawili tu : Uhuru na Daily News. Hakuna mtandao, mablogu wala runinga. Punde Mike akajiunga na Daily News, mwandishi chipukizi, chini ya Mhariri aliyekuja kuwa Rais wa Nchi, Benjamin Mkapa.

MIKE SIKAWA HAKUWA MWOGA

Silaha kuu ya mwandishi wa habari ni kalamu. Lakini ukiichezea unaweza kufungwa, kuuawa. Mike Sikawa hakuwa mwoga. Akapewa safu maalum (Roving Reporter). Alipita mitaani na mpiga picha akifichua habari za walioharibu maendeleo, akifichua uzorotaji wa maofisi na viwanda.

Kiuchumi mambo yakaanza kuwa magumu (kama ilivyo leo) hasa baada ya vita vya kumng’oa Idi Amin wa Uganda (1979) ; vijana wengi akiwepo Mike tunafurukuta; wengine tunatamani ubaharia na kwenda Ulaya.

Nakumbuka mwaka 1983-84 tuko Hoteli ya Kilimanjaro, Mike akawa anakosolewa na Mmoja wa Mawaziri wakubwa nchini. Mike alikuwa akimtazama yule Waziri akiongea, hakusema kitu. Siri ya mwandishi mzuri ni kusikiliza. Mike alikuwa mzungumzaji na alipenda sana kubishana, lakini mara nyingi alisikiliza. Ukitaka kuandika au kusema la maana sikiliza.Hakumsemesha huyo Waziri. Alimsikiliza tu.

ULEVI NA KISUKARI CHA MIKE SIKAWA

Matatizo ya uchumi ya mwaka 1978-88 (hadi alipoingia Mzee Rukhsa) yaliwafanya vijana wengi watake kuhama Bongo; wapo waliokuwa majambazi, wapo waliofariki mapema kutokana na umaskini; kuna waliojiua, au waliohama nchi (kama mimi); Mike aligeuza pombe kuwa chai. Alikuwa mlevi kiasi ambacho kila ukikutana naye (hasa usiku) anapepesuka; kauchapa.Lakini aliendelea kuandika.

Huenda ugonjwa wa kisukari(uliomuua) ulitokana na pombe zile. Ugonjwa huu unatumaliza baadhi ya Watanzania leo. Moja ya asilia zake ni unene (kutofanya mazoezi ya viungo) ulevi au kurithi. Sina hakika ulimpataje marehemu Sikawa. Ninavyojua tuliwahi kuongea sana juu ya suala la kufanya mazoezi na namna kitendo hicho kinavyoweza kuihami afya ya mwanadamu. Kuna wanaopata Kisukari kutokana na unene. Kuna wanaokipata kutokana na urithi. Siri wataijua zaidi waganga waliomtibu…

ALIPENDA SANA WATU

Mike alipenda sana watu. Nakumbuka alivyopenda kulalamika juu ya wanaume walioonea au kuwapiga wanawake:

Si vizuri wakati ukiongea na mwanamke; badala ya kumwangalia usoni; uko bize tu kumkodolea maziwa yake au miguu, ni kama unadharau kile anachosema unamwona kama kitu tu.”

Alikumbusha shairi maarufu la gwiji wa fasihi Shaaban Robert kuwa Mwanamke Si Kiatu.

Kikazi alijenga jina kama mmoja wa waandishi wakongwe wa Daily News. Alitumia lugha rahisi kusoma kwa mtu wa rika na tabaka lolote; hakubadili mtindo wa kuandika. Moja ya vipaji vyake ilikuwa uwezo wa kubishana na kujadiliana na mtu yeyoye awe maskini, tajiri, mzee, kijana, kigogo au yatima. Miaka ya mwanzo ya 1980 tulishtushwa alipotoka na mahojiano na aliyekuwa Rais wa Zambia, Kenneth Kaunda. Kila mtu mitaani alisimama dede….

ALICHAPA KAZI HADI MWISHO…

Mara ya mwisho kumwona Mike ilikuwa 1992, mjini London. Alikuwa Idhaa ya Kiswahili ya BBC. Kaanzwa na kisukari, mlokole, hanywi pombe, akili zake pevu bado hachoki kujadiliana; anasoma chuo cha habari, mjini Cardiff.

Katika mazishi yake mmoja wahariri wa BBC alisema hawakujua Mike alikuwa mgonjwa vile maana hakuwa mtu wa kulalamika au kudeka kuwa mgonjwa. Alikuwa mchapa kazi.

Tunaweza kufaidika sana kama makala zake (gazeti la This Day) zitachapwa kitabu maana uhodari wake wa kujieleza katika lugha nyepesi inayoeleweka hauna mfano. Ni hazina katika historia ya uandishi na fasihi ya Mtanzania.

Mungu Aiweke Roho Yake Pema Peponi.


Feedback / Comments

10 Responses to “MIKE SIKAWA: 1953-2008”

  1. Comment by rasto on December 15th, 2008 5:40 pm

    ahsante sana kwa historia ya mike.ni moja kati ya watangazaji mashuhuri kutokea eneo letu la afrika mashariki.mwenyezi mungu ailaze roho yake pema peponi.je mikidadi mahmoud,christina chekunegela,halima kihemba wamo?

  2. Comment by hombiz on December 15th, 2008 6:20 pm

    MOLA amrehemu apumzike kwa amani, AMEN

  3. Comment by BLACKMANNEN on December 15th, 2008 7:25 pm

    Ukweli ni kwamba, Watanzania wengi, tunaipenda sana lugha yetu ya Kiswahili. Gazeti lolote linaloandikwa kwa kiswahili linasomwa na Watanzania wengi wenye viwango vyote vya Elimu. Hili linathibitika katika “Blog” zote zinazoandika na kutumia lugha ya kiswahili, zinatembelewa na Watanzania wengi.

    Mwandishi Mahiri “Mike Sikawa” (R.I.P), hakuwa anajulikana na Watanzania wengi, kutokana na lugha (Kiingereza), aliyokuwa akiitumia katika uandishi wake habari. Pia sehemu, (Afrika Kusini) aliyokuwa akifanyia kazi yake, ni Watanzania wachache, wanaotaka kupata habari za nchi hiyo.

    Idadi ya Watanzania kulisoma gazeti alilokuwa akiandika Mike Sikawa, ingeongezeka kama angekuwa akiandika kwa lugha ya kiswahili, kitu ambacho pengine ilikuwa haiwezekani. Kazi yake pia, haikuwa ya kuandika, ili ajulikane na Watanzania, bali ilikuwa kupasha habari, umma wa dunia yote, kwa lugha inayoeleweka na nchi zingine duniani.

    Na kutokana na hali halisi ya kazi yake hiyo, ndiyo imetukosesha kumfahamu Mtanzania mwenzetu Mike Sikawa, aliyekuwa na uwezo wa hali juu katika kupasha habari kwa watu wote.

    Shukrani zetu ziwaendee Freddy Macha na Bongocelebrity, kwa kutuwekea habari za “Mwandishi” huyo hapa, na mmetufungua macho sisi wote ambao tulikuwa hatumfahamu. Ahsanteni sana. Mwenyezi Mungu Aiweke Roho ya Marehemu “Mike Sikawa” Peponi – Amen!

    This Is Black=Blackmannen

  4. Comment by Mattylda on December 16th, 2008 2:32 am

    ohhh jamani,apumzike kwa amani AMINA.

    Asante BC,sijawahi kumsikia kabisa labda kwa kuwa sio msomaji mzuri wa magazeti!

  5. Comment by any on December 16th, 2008 10:08 am

    blackmannen, too late, the guy is gone, may be other journalists may use your advise in the future.
    POLENI familia ya Mike. Mimi mwenyewe ndio nimemfahamia apa BC! RIP.

  6. Comment by Bob Sambeke on December 16th, 2008 5:08 pm

    Dah Poleni familia yake na wapenzi wa habari kutoka kwake!

    R.I.P Mike Sikawa!
    R.I.P Amina Chifupa
    R.I.P Aaliyah
    R.I.P CJ Massive “Mtoto wa Dandu”

  7. Comment by Rodrick on December 17th, 2008 2:27 am

    Si tu fani ya uandishi na utangazaji wa habari ulipata pigo, bali ni Tanzania nzima.
    Mike alikuwa mtu wa watu, mwanaharakati, mchapakazi na sifa nyingine kem kem unazoweza kumpa.
    Yaani basi tu, kwa kuwa ni amri ya MUNGU, vinginevyo tungeweza kugoma na kuandamana ili kushinikiza asiende huko aliko enda.
    Lakini hata hivyo, tunamshukuru MUNGU kwa kuwa alitupatia Mike wa jinsi alivyokuwa; Jina lake lihimidiwe.
    Rodrick

  8. Comment by Simon Kitururu on December 17th, 2008 5:00 am

    Mungu Aiweke Roho Yake Pema Peponi!

  9. Comment by Dunda Golden on December 19th, 2008 2:02 pm

    ULALE PEMA PEPONI

  10. Comment by Edward Ismail on January 1st, 2009 3:08 pm

    Thank you Freddy for this most compelling and accurate article on Mike. Freddy, Mike Sikawa lived with me here in Washington, for six months, before BBC and South Africa. Freddy, your article was so powerful, I became very emotional. I visited Mike in London when he was at BBC. That was the last time I ever saw Mike alive. We had the most wonderful political and social conversations in his small London abode. I miss my Meru brother Mike Sikawa.
    .

Leave a Reply