JENNIFER MGENDI: NYOTA INAYONG’AA KATIKA MUZIKI WA INJILI

jenny6bc

Akiwa tayari na albamu zisizopungua tano kibindoni, Jennifer Mgendi(pichani) ni miongoni mwa wanamuziki wa muziki wa injili au kwa kiingereza Gospel nchini Tanzania ambao wamejijengea sifa na umaarufu mkubwa kutokana na kazi yake hiyo ya uimbaji na kumtukuza mola.

Lakini tofauti moja kubwa ya Jennifer na wanamuziki wengine wa muziki wa injili ni kwamba yeye pia ni mtunzi mzuri wa hadithi za filamu.Baadhi ya filamu alizowahi kutunga ni kama vile Pigo la Faraja, Joto la Roho na Teke la Mama.

Alianza rasmi kujishughulisha na kazi ya muziki wa injili mwaka 1995.Albam yake ya kwanza iliitwa ‘Nini?’. Baada ya hapo alitoka tena na albamu zake zilizokwenda kwa majina ‘Ukarimu wake’, ‘Yesu Nakupenda’,’Nikiona Fahari’ na ya hivi karibuni zaidi inayoitwa Mchimba Mashimo.

Hivi karibuni tulipata nafasi ya kufanya naye mahojiano ambayo utayasoma hivi punde. Katika mahojiano haya,Jennifer anakupa kwa undani kuhusu historia yake kimuziki na kibinafsi. Ni kweli kwamba muziki wa injili wa leo ni wa “kidunia” zaidi ya “kiroho”? Anasemaje kuhusiana na hoja hiyo? Je Jennifer anaongeleaje tofauti za muziki wa injili na ule wa Bongo Fleva?Unakubaliana naye?

Nini mipango yake kwa mwaka huu wa 2009 na ana ushauri gani kwa vijana?Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo;

BC: Karibu Jennifer ndani ya BC.Sijui nikuambie mambo vipi au bwana asifiwe?

JM:Asante sana ndugu yangu. Yote mema tu kwani mambo ni safi na Bwana anaendelea kusifiwa…

BC:Kwa kifupi tu unaweza kutueleza historia ya maisha yako?

JM:Nilizaliwa miaka karibu 37 iliyopita hapa hapa jijini Dar es Salaam katika familia ya watoto watatu nikiwa nimetanguliwa na kaka wawili. Nimepata elimu yangu katika mikoa ya Dar es salaam na Tanga. Nilianza uimbaji rasmi mwaka 1995 na hapo katikati nilifanya kazi kadhaa za kuajiriwa kama Ualimu na Ukutubi lakini tangu mwaka 2007 niliacha kazi za kuajiriwa na mpaka hivi leo ninafanya shughuli zangu binafsi.

BC:Mara nyingi wasanii huwa wanaanza kwa kufuata mfano wa mtu,watu au kitu fulani.Kwa upande wako nini kilikushawishi uingie kwenye muziki wa injili.Je kwenye muziki wa injili ndiko ulikoanzia au ulianzia kwingine halafu ndio ukahamia kwenye injili?

JM:Watu wengi walikuwa wakinivutia sana na kunihamasisha kwa habari ya uimbaji lakini miaka hiyo nilivutiwa zaidi na Jim Reeves na Yvonne Chakachaka ambao walikuwa wananivutia sana.

Nimeanza moja kwa moja kuimba muziki huu wa injili kwa sababu tayari injili (ambayo ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye) ilikuwa imebadilisha maisha yangu. Kwa hiyo sina mwingine wa kumwimbia zaidi ya huyo mwenye Injili yaani Yesu Kristo.

BC:Kwa faida ya wale ambao hawajafuatilia kwa ukaribu kazi zako,mpaka hivi sasa umeshatoa albamu ngapi,zinapatikana wapi na wewe kama msanii wa muziki wa injili unafanyia wapi kazi zako?

JM:Mpaka sasa nina albam tano za kusikiliza ambazo ni Nini?, Ukarimu Wake, Nikiona Fahari, Yesu Nakupenda na Mchimba Mashimo. Pia nina video za nyimbo ambazo ni Yesu Nakupenda na Mchimba Mashimo. Hali kadhalika nina matoleo ya filamu ambayo ni Joto la Roho, Pigo la Faraja na Teke la Mama. Sina sehemu maalum ninayofanyia shughuli zangu kwani shughuli zangu sio za kukaa sehemu moja.

BC:Kumekuwepo na ukosoaji kwamba ninyi waimbaji wa muziki wa injili wa kizazi hiki mnapoteza kabisa uhalisia wa muziki huo.Wanaosema hivyo wanasema kwamba muziki wenu hauna vionjo vya “kiroho” bali umejaa vionjo vya “kidunia” kutokea kwenye midundo yake na wakati mwingine hata kwenye mashairi au ujumbe uliomo.Unasemaje kuhusu ukosoaji huo?

JM:Unajua ndugu yangu siwezi kukanusha wala kukubaliana na hoja yao hiyo. Inawezekana ni kweli wanavyosema na hii inatokea zaidi pale waimbaji tunapokosa kiasi. Hata hivyo “kiroho” kwa mtu mmoja kwa mwingine chaweza kuwa ni “kidunia”.

Kuna watu wengine hata kupiga makofi tu wakati unaimba kwao ni “kidunia”. La muhimu ni kwamba mradi mashairi na ujumbe unampa Mungu sifa na utukufu, binafsi sioni ubaya wowote wa nyimbo za injili kuwa na “midundo” na wala sijawahi kusoma kwenye biblia sehemu inayokataza kupiga midundo sanasana nimesoma Zaburi ikisema “….pigeni kwa ustadi…”.

Kuhusu ujumbe wa kidunia kwa kweli mimi sijasikia mwimbaji wa nyimbo za injili akiimba nyimbo za kidunia maneno yote tunayoimba yamo kwenye biblia au angalau hayapingani na mafundisho ya msingi ya biblia.

BC: Mara kwa mara kumekuwepo watu ambao aidha wanajaribu kukufananisha na waimbaji wengine wa muziki wa injili kama Rose Mhando,Bahati Bukuku na wengineo.Wengine wamethubutu hata kuwapambanisha.Je uhusiano wako na wanamuziki wengine wa injili ukoje?Mnajiona kama washindani au washirika katika Bwana?

JM:Ni kweli mara zingine wanafanya hivyo lakini nadhani kimsingi tunatofautiana na kila mmoja ana uimbaji wake kwa kadiri ya kipawa au kipaji alichopewa na Bwana. Ila la kufurahisha ni kwamba hatuna tabia ya kushindana kwani kila mmoja kapewa karama kivyake na kubwa zaidi ni kwamba tunatambua kuwa wote lengo letu ni moja, yaani kuujenga ufalme wa Mungu hapa duniani. Kwa hiyo huwa tunashirikiana sio jukwaani tu bali mara nyingine hata katika mambo ya kawaida ya maisha.

BC: Kwa muda sasa umekuwa mwanamuziki.Unadhani ni mambo gani matatu ya msingi ambayo umejifunza kutokana na kazi yako ya muziki na ambayo unadhani usingeyajua kama usingekuwa mwanamuziki?

JM:1. Nimejifunza nchi yangu na kuifahamu zaidi kwani nimesafiri sana katika mikoa na wilaya nyingi ambazo nisingefika kama sio muziki.

2. Nimejifunza mambo mengi sana yaliyonijenga kiroho kutokana na kualikwa kuhudhuria mikutano, semina na makongamano ya kiroho.

3.Nimejifunza kuishi aina fulani ya maisha yenye kiasi fulani cha nidhamu kutokana na nafasi yangu katika jamii, maisha ambayo pengine nisingekuwa maarufu nisingeishi hivyo.

jennifer-mgendibc

BC: Ni changamoto zipi unazokabiliana nazo ukiwa kama mwanamuziki wa injili nchini Tanzania?

JM:Kwa kweli changamoto ni nyingi lakini baadhi ni wizi wa kazi zangu jambo ambalo linanirudisha nyuma kimaendeleo kwa kunikosesha mapato. Changamoto nyingine ni umaarufu ambao mara zingine unaninyima uhuru binafsi na pia mara zingine ninaposhindwa kufikia matarajio fulani ya wanajamii basi wao hutafsiri wanavyopenda mfano kuona naringa au siwathamini.

Changamoto nyingine ni muda kila mara naona hautoshi kutokana na shughuli nilizonazo hasa safari za mikoani ambazo zinanitenga na familia yangu.

BC: Kama mkristo na mwimbaji inawezekana ikatokea ukawa na wimbo mmoja ambao ukiuimba huwa unapata hisia za kipekee.Je kwa upande wako kuna wimbo kama huo?Ni wimbo gani na kwanini hisia zinakuwa tofauti?

JM:Wimbo ambao nikiuimba hata mimi unanigusa ni Moyo Tulia ulio kwenye album ya Mchimba Mashimo huwa unanifariji sana.

BC:Je ishawahi kukutokea ukashangaa au kujiuliza kwamba kwanini Mungu amekuchagua wewe kufanya kazi unayoifanya?

JM:Huwa sishangai sana yeye kunipa kipaji cha kuimba kwa sababu wapo watu wanaosomea uimbaji na wapo waimbaji wengi wazuri sana kuliko mimi japo hawajulikani.

Lakini huwa nashangaa sana jinsi Mungu alivyoweza kunifanya mimi niamini neno lake na kuweza kuokoka kwani kuna watu wengi sana wema na wana tabia nzuri kuliko mimi lakini hawajampokea Yesu kama mwokozi wao kwa hiyo mimi kunipa hiyo neema huwa nashangaa sana.

BC: Kuna tofauti ngapi za kimsingi kati ya muziki wa injili(kama huu unaofanya wewe na wengine) ukilinganisha na huu wa Bongo Fleva?

JM:Tofauti kubwa ninazoona mimi zipo kama tatu. Kwanza, ujumbe wa muziki wa Injili unaelekea katika kuijenga roho ya mtu wakati muziki wa Bongo fleva asilimia kubwa unalenga katika mambo yahusuyo mwili tena mara zingine unapotosha roho ya mtu (mfano nyimbo za kuhamasisha ngono, kuutukuza mwili, kujisifia’kusifia wanawake,nk. Tazama hata video za Bongo fleva nyingi zina vitendo ambavyo havifai hasa kwa watoto tofauti na nyimbo za Injili.

Pili, miziki hiyo inatofautiana upande wa midundo yake na hata uimbaji wake. Watu wa Bongo flavour wanatumia zaidi style za RnB, uimbaji ya kufokafoka na aina nyingine zinazofanana na hizo wakati muziki wa injili style zake utakuta reggae,rhumba na miziki mingine.

Tatu, wanamuziki wenyewe wanatofautiana kwani wanamuziki wengi wa Injili wanakuwa na mipaka kutokana na imani waliyonayo tofauti na wale wa Bongo fleva wengi wana ile hali ya “full kujiachia” kwa hiyo sio ajabu kwao kuvaa jukwaani tuseme chupi na sidiria, kupigana, kutumia vileo na mambo mengine jambo ambalo huwezi kuliona kwa wanamuziki wa Injili.

BC:Ni wanamuziki gani wa muziki wa injili ndani na nje ya Tanzania wanaokuvutia zaidi?Kwanini?

JM:Ndani wengi wananivutia zaidi Rose Muhando kwa mashairi yake na anavyosukuma sauti yake na Upendo Kilahiro kwa jinsi anavyoweza kucheza na sauti yake.Nje navutiwa na Yvonne Chakachaka na Rebecca Malope.

BC: Nini mipango yako katika mwaka huu tuliouanza?Nini ujumbe wako kwa vijana wa leo kuhusiana na suala zima la imani,kazi na uwajibikaji katika jamii?

JM: Mwaka huu nina mpango wa kutoa sehemu ya 2 ya filamu ya TEKE LA MAMA,Kutoa albam mpya ya nyimbo na video yake, pamoja na kutengeneza Remix ya nyimbo zangu za zamani zilizopendwa na video yake.

Pia nina malengo ya kutembelea mikoa ya Tabora, Singida,Mbeya, Kigoma , Bukoba , Mtwara na mji wa Songea.

Vijana nawashauri wamrudie Mungu kwa faida ya maisha yao ya sasa na ya milele.Pia vijana waache tabia za kukaa vijiweni kupika majungu na kuangalia wanawake wanaopita huku wakiwachambua kwa kisingizio cha kukosa kazi ya kufanya.

BC: Asante kwa muda wako Jennifer.Tunakutakia kila la kheri katika kazi zako

JM:Asante sana kaka nakutakia kazi njema.


 1. Ommy, 08 March, 2009

  Hi dada Jennifer,
  Praise The Lord,
  Well napenda sana nyimbo zako zote na nasema ubarikiwe sana na endelea hivyohivyo dada yetu. L akini umenichekesha kusema wewe sio DEMU umri wako sio kitu sana hata vile kuwa mama wa watoi wawili sio shida maana hata demu mwenye miaka 26 anaweza kuwa hata na watoi watatu. Ingawa kama ulivonena kiswahili cha Bongo neno DEMU ni kama la kihuni fulani lakini wewe usijali sana maana kila mtu ataandika anachoona yeye ama akili yake inavyomtuma but for sure never mind or even taking trouble of yourself for such minor things let them say what they think is right to say or rather to comment but I applaud the way you are, you real represent the culture of our country and we are proud of you in that way. In life you can’t avoid challenges just part and parcel of the life long.But also the government should be strict on the copyright for the other people use your products for their own benefit without your knowledge thats very bad ever and should be stoped immediately coz discouraging though.Anyay what I want to say as a point of summingup just keep it up for the sake of the Lord. I have listened Nalia at the Youtube very interesting and you made up my day.For I miss home too much being in Australia for so long struggling with love to make difference back home . Anyway you can make a tour to Perth Australia and we can listen to your Gosple songs live for we are many Tanzanians and Kenyans , Rwandes, Burundians, DRCs, so hope we can organise you to come over just think of it.
  Praise the Lord
  Dr. Ommy Sima Hillary, PhD

 2. Ommy, 08 March, 2009

  OK my sister Jennifer, I meant life not “love” as it appeared in the previous message for just a typing error for I don’t want you to missinterpret me coz having my PhD I should behave the way am supposed to in order to be a point of reference for the good manner.
  Otherwise I say again congratulation on the way you behave and the way you do your gosple. Good Bless you and stay blessed dada.
  Dr. Ommy SIMA HILLARY

 3. kissa george, 26 March, 2009

  hongera sana j mngendi mimi siko nyuma na wenzangu nami nakupongeza sana,shika sana kalama yako hiyo ya uimbaji asije mtu au mwozu akakunyang’anya,pole kwa huduma nakuombea udumu sana katika kazi hiyo na mungu akubariki

 4. kissa george, 28 March, 2009

  barikiwa sana mama

 5. leah, 31 March, 2009

  Bwana YESU asifiwe sana,dada jeny nakupa pongezi sana kwa kazi zako nzuri na filamu zako ingawa nimefanikiwa kuitizama moja tu joto la roho hope hizo zingine ntazitafuta.MUNGU akubariki

 6. leah, 31 March, 2009

  dada jeny katu usikubali kuitwa hilo jina na napenda kukuambia kuwa unaufahamu mkubwa sana kwani kwa sie wanawake wa kibongo huwa hatushituki kabisa pindi tuitwapo kwa hilo jina la demu,kama mchangiaji mmoja alivyolidadavua hili neno ni la ufaransa likimaanisha si tu mwanamke bali mwanamke anayejiuza.
  na hii iliweza kuelezwa vizuru pale ambapo Dr.Asha rose Migiro naibu katibu mkuu wa umoja wa mataifa alipotakiwa na Ambwene yesaya(Ay)japo aonekana tu katika video yake ya “mademu watafutaji”kwamba aonekane kielelezo cha kuwa demu mtafutaji lakini alikataa na kuwaelewesha kwa nini kakataa
  Dr.Rose Migiro hakukataa kwa kuwa siku hizi amekuwa na maringo ila alikataa kwa sababu ya matumizi ya neno demu,kuwa yeye anaangaliwa dunia nzima ndo akaitwe demu yaani mwanamke malaya wa kifaransa yamkini ule wimbo ungekuwa na ujumbe wa wanawake watafutaji angekubali kuonekana katika video so huyo ni kiongozi wa dunia tu je itakuwaje kwa mtumishi anayemuwakilisha MUNGU duniani kuitwa demu,

 7. Mjololo Ng,ughuya, 02 May, 2009

  Mwanangu Jennifer,nyimbo unazoimba zina uzima utokao mbinguni,usijiinue acha Mungu akuweke juu kuliko mambo yote,wewe umebarikiwa.

  Naitwa Mjololo Ng,ughuya
  Arusha

 8. Rebecca, 14 May, 2009

  Dada J mungu akubariki sana napenda sana kuona jinsi mungu anavyokutumia zidikumtegemea mungu kila wakati na usifutishe namna ya dunia na bwana hatazidi kukuinua barikiwa sana.

 9. Neema Morris, 17 December, 2009

  Hi
  Jennipher
  Napenda kukupongeza sana kwa uimbaji wako na moves unazo zitoa kuelimisha jamii ningependa kupata mawasiliano yako ili uni elekeze na mimi kwani na mimi ni mwimbaji napenda sana sauti yako pamoja na ya Bahati Bukuku natamani niongee na wewe uso kwa uso Je umejiandaaje na krismas mimi na kutakia maisha marefu katika uimbaji wako Mungu awe pamoja nawe AME!!! NAMBA YANGU NI 0688581004

 10. Chriss, 16 June, 2010

  Shaloom Dada,
  Kazi yako ni njema sana, Mungu akuinue zaidi.
  Natamani tuonane uso kwa uso maana kila ninapoenda nafananishwa sana na wewe….
  some times bichwa linakuwa kubwa kufananishwa na super star kama wewe.
  Karibu sana Moshi, Kanisa la Victorious…
  TUNAKUPENDA SANA…..

 11. John JK Prophet musa, 26 August, 2010

  Shaloom!!
  mpendwa mtumishi wa mungu nakusalimu kwa salam zote za rohoni bwana yesu apewe sifa!!Dada nakupongeza sana kwa juhudi zako ktk kuitangaza safari ya wokovu,nakupa moyo kuwa usife moyo ktk kupigana vita na ibilisi kwani nimeona kuna baadhi ya comment ambazo zmetoka kwa wasio na upeo wa kiroho.Jipe moyo mkuu,kazi zako ni nzuri na mungu azidi kukuinua ktk huduma aliyokuitia.
  Amennnnnnnn.

 12. Rose, 10 November, 2010

  Bwana apewe sifa,4 sure csta umzur na umependeza,cfa na utukufu apewe bwana

 13. malema, 15 December, 2010

  Dada majibu yako ni mazuri umeongea ktk mahojiano hayo bila kumkwaza mtu yeyote.Mungu akubariki sana kwani neno la Mungu linasema ya kwamba tusiionee haya Injili ili na Baba yetu wa Mbinguni asije akatuonea haya mbele ya Baba yake itangaze ipasavyo mtu wangu.

 14. jemima mbutu, 19 February, 2011

  Nakupongeza sana ongeza bidii kumsifu MUNGU nae atakuzidishia maradufu.

 15. Idd, 18 March, 2011

  Hi,Nakupa pongezi kwani mimi ni muumini wa kiislam,napenda kusikiliza baadhi ya single zako.upo juu

 16. tula tweve, 27 June, 2011

  MUNGU AKUBARIKI DADA JANE KAZI ZKO NI NZURI NA NINAFATA UNYAYO WAKO TUKUMMBUKANE KATIKA MAOMBI, NA MUNGU KAMWE HAMTUPI MJA WAKE.

 17. Minasema, 29 July, 2011

  Dada Djen, nakupongeza.

  Wewe mrembo, tena mnyeyekevu. Ila usifurahie hayo. Watu wanakutazama. Kuna wale wanaofurahia urembo wako nakusahau unayoyaimba.
  Kuwa mrembo ni jaribu moja, kuwa na sura “mbaya” ni jaribu lingine.
  Umkumbatie Kristo ili wanaotafuta demu wakimkuta Yesu, wagonge mwamba, la sivyo watakunyemelea, hata wengine watatafuta namba yako ya simu, watajifanya marafiki wako, watatoa misaada kwa kazi “ya Mungu”. Kumbe mgongoni wamebeba!
  Uwe mwangalifu Dadangu.

  Niko nchini CHAD.

 18. LUCY, 03 December, 2012

  Mimi ni dogo tu kwako siwezi kusema chochote ila MUNGU moja BABA moja na ROHO moja.

  Tuko pamoja tunasonga mbele.

 19. SETH MWANDUNGA, 01 April, 2013

  POLE MISS MGENDI OR MRS MGENDI I DO KNOW BALI FURAHIA KUISHI KATIKA UWEPO WA MUNGU KAZI ZAKO ZITAIMALIKA SONGA MBELE MAMA.

 20. Shukuru msangi, 18 July, 2016

  Mimi ni shukuru msangi,niko arusha. Mtumishi, Mimi Nina swali moja tu kwako_mahojiano Hays yangerudiwa Leo majibu yako yangekuwa haya haya au yangekuwa tofauti kidogo?na kwa mini?

 21. Jeff Msangi, 18 July, 2016

  Hello Shukuru, Asante. Tunajiandaa kufanya mahojiano mengine na Jennifer.Bila shaka atakusikia

Copyright © Bongo Celebrity