
Maggid Mjengwa sio jina geni.Bila shaka kabisa umewahi kumsikia,kumsoma na pengine hata kutembelea blog yake ambayo kimsingi ni kimbilio la yeyote yule anayependa kupata picha halisi ya maisha ya mtanzania wa kawaida hususani yule anayeishi kijijini kama ilivyo kwa babu na bibi yangu.Wasomaji,watembeleaji na wachangiaji wa blog yake wanapenda kumuita “Mwenyekiti”.
Yeye ni miongoni mwa waandishi wa makala zenye kuchoma kama sio kugusa hisia za wengi.Ukitaka kujua historia yake ya uandishi unaweza kuipata kwa kusoma mahojiano tuliyowahi kufanya naye siku za nyuma kwa kubonyeza hapa.
Maggid ni mpenzi wa michezo hususani wa soka.Ni mnazi wa Simba.Ni upenzi huo wa soka na michezo kwa ujumla ambao ulimfanya aanzishe gazeti lililoitwa “Gozi Spoti” ambalo lilidumu mitaani mpaka hivi karibuni alipoamua kulisitisha.
Jambo jema ni kwamba, kuondoka kwa “Gozi Spoti” kulifanyika kwa makusudi ili kulipisha gazeti jipya litakalojulikana kama Kwanza Jamii ambalo litaingia mitaani siku si nyingi chini ya usimamizi wa Ikolo Investment Ltd kampuni iliyo chini ya mwenyewe “Mwenyekiti”.Kwa hiyo tunaweza kabisa kuongeza cheo kimoja kwa “Mwenyekiti” na kumuita Mjasiriamali.
Kwanza Jamii ni jarida la uchambuzi wa masuala yanayohusu na kuigusa jamii.Haya ni pamoja na siasa,uchumi,elimu,michezo na utamaduni.Pia yatakuwemo masuala ya mazingira,jinsia na ukimwi . Ni jarida litakalokuwa linatoka kila siku ya Jumanne.
Tumepata nafasi ya kufanya mahojiano mafupi na ‘Mwenyekiti” kuhusiana na ujio wa jarida hili na pia kumdadisi kuhusu anachokiona kila atembeleapo vijiji na vijiji vya Tanzania.Anaona nini?Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo;

Hii ndio nembo (Logo rasmi) ya Kwanza Jamii.
BC: Natambua kwamba upo “bize” sana katika kipindi hiki ukijiandaa kumleta mwana mpya,Kwanza Jamii, hivi karibuni.Kwa hiyo shukrani sana kwa muda wako.Kwanza hebu tuambie,maandalizi yanakwendaje?
MM: Asante Jeff.Kwanza nikushukuru kwa kunipa fursa hii.Pili niwajulishe kupitia kwako,wasomaji wetu watarajiwa kuwa maandalizi ya “KJ” kwa maana ya “Kwanza Jamii” yanakwenda vyema kabisa.Ni kazi ya timu na timu iko imara.
BC: Kwanza Jamii linaingia katika ushindani wa habari na mawasiliano wakati ambapo dunia inazidi kushika muelekeo mpya kwenye masuala mazima ya habari. Waliokuwa wanaitwa “wasomaji” siku hizi ndio ‘wachangiaji” muhimu wa habari,mijadala nk.Watu wengi wanazidi kujikita mtandaoni ili kupata habari badala ya kusubiri magazeti yanayosambazwa mitaani.Kuna blogs,facebook,myspace,digg nk.Mmejiandaaje kukabiliana na ushindani huo au tuseme hali halisi ya ulimwengu wa habari na mawasiliano hivi sasa?
MM: Tunajua fika kuwa tunakwenda kwenye ushindani mgumu. Tulipokuwa tukiandaa “Gozi Spoti” tulikuwa wageni na wachanga hasa. Lakini sasa tumepata uzoefu wa kutusaidia katika mapambano yajayo.
Tunakwenda kushiriki ushindani na hatuogopi kushindwa. Ni kazi ngumu lakini tuna imani uwepo wetu utasaidia katika kupanua wigo wa kupata taarifa,maarifa na burudani.
Ni kweli kuwa tekinolojia za kisasa imesaidia sana watu kuweza kupata habari kutoka vyanzo vingi. Hata hivyo,jamii pana ya watanzania wa kule Kilosa,Ikwiriri na kwingineko,bado hawajafikiwa na tekinojia hiyo.
BC: Mtu mwingine atasema; ah tayari kuna magazeti chungu mbovu nchini Tanzania, kwanini tuongeze tena lingine?Unamwambiaje mtu kama huyo au nini kinatarajiwa kuwa tofauti kabisa kati ya Kwanza Jamii na magazeti mengine ambayo tayari yapo katika soko nchini Tanzania?
MM: Sidhani kama tumefikia mahali tunaweza kusema kuwa tuna magazeti chungu mbovu hapa Tanzania. Kwa kuangalia idadi ya watanzania, bado tuna magazeti machache.
Na katika hili la magazeti suala si wingi wa magazeti yaliyopangwa mezani bali yaliyomo ndani ya kurasa za magazeti hayo.Wasomaji wa leo si wajinga.Katika meza iliyojaa magazeti,wanajua wanachokitaka.Kwanza Jamii litakuwa na tofauti.Si muda mrefu kutoka sasa litakuwa mitaani na tofauti hiyo itaonekana.
BC: Mara nyingi (kama sio mara zote),inasemekana kwamba gazeti linapoanzishwa huwa lina “walengwa” au wasomaji watarajiwa.Kwanza Jamii litakuwa linawalenga watu gani?
MM: Kama lilivyo jina la gazeti lenyewe,mlengwa wa kwanza wa “Kwanza Jamii” ni jamii kwa maana ya wananchi.Tutajikita katika kuandika habari zitakazomsaidia mwananchi wa kawaida.Tunataka mwananchi aweze kupata habari,maarifa na burudani.
Na maarifa haya ni yale yatakayomsaidia,kwa namna moja au nyingine, abadilishe maisha yake kutoka katika hali duni kwenda kwenye unafuu.Kwanza Jamii lina adhma pia ya kuwasaidia tuliowapa dhamana za uongozi kwamba na wao wasome fikra endelevu zitakazotolewa na wachangiaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.
Ni imani yetu kuwa mchango wa fikra unaweza kabisa kusaidia kuleta mabadiliko na hatimaye maendeleo katika jamii yetu iwapo tuliowapa dhamana za uongozi watakuwa makini kufuatilia michango hiyo.
BC: Kupitia blog yako, mtu anaweza kuona picha halisi ya Tanzania. Unapita kijiji mpaka kijiji ukishuhudia hali halisi ya mwananchi wa kawaida.Je ni ujumbe gani ambao pengine unaupata kila sehemu unayokwenda na kwa hali halisi unadhani matatizo yanayowakabili wananchi huko unapopitia yanatokana na nini?Uongozi?
MM: Hili ni swali zuri sana.Na sehemu moja ya swali hili inataka maelezo marefu ya uchambuzi.Ni pale unapouliza matatizo yanayowakabili wananchi huko yanatokana na nini? Umetaja “uongozi” na kuweka alama ya kuuliza.Swali lako ni jibu pia.Naam.Jibu ndio hilo.Matatizo mengi ya wananchi yanatokana na uongozi mbovu katika ngazi hizo hizo za chini.
Majuzi hapa nilipita shule moja ya kijiji Wilaya ya Kinondoni inaitwa Tondolo.Nilipiga picha mazingira ya shule ile.Yanasikitisha.Nikaandika katika blogu yangu; kuwa miaka 48 ya Uhuru bado tuna shule kama ile!
Shule ile ni mfano mzuri wa haja ya kuhimiza utawala bora kwa kuonyesha vielelezo.Shule ile ni kielelezo cha kushindwa kwa utawala bora katika eneo lile.Kabla hatujakimbilia kwa RC tujiulize; uongozi wa kijiji unafanya nini?DC? Mbunge na kadhalika wamelishughulikiaje suala la Shule ya Msingi Tondolo?

Shule ya Msingi Tondolo anayoiongelea Mjengwa.
BC: Mjengwa nakutakia kila la kheri katika gazeti lako jipya.Nakuahidi kwamba nitakuwa msomaji na pia mchangiaji.
MM: Nami nashukuru sana kwa ushirikiano wako.
Feedback / Comments
14 Responses to “KARIBU “KWANZA JAMII””
Leave a Reply


sending...
hmmm…now u r talking….lol
BC,
Mbona hamkumwuliza kama gazeti litakuwa kwenye mtandao na gazeti litakuwa linafadhiliwa na nani?Maana hali ilivyo kwa sasa mafisadi wanatumia watu mbalimbali kuanzisha vyombo vya habari wakati wahusika wenye waki pembeni.
Si mnaona jinsi Bagenda alivyobadilika na sasa ni kutetea ufisadi tu?
Hej,
Mjengwa, det är Black=Blackmannen. Najua hiyo lugha unaifahamu vizuri sana wewe mtani wangu Mjengwa, mimi nipo hapo Gävle.
Gazeti lako la “Kwanza Jamii”, nitakuwa msomaji wake mkubwa, kama nilivyokuwa nikikufatilia katika gazeti lako la “Spoti”.
Wewe ukiwa mpenzi wa simba (ssc) na mimi Yanga (YASC)tukiwa watani wa michezo na ukabila. Na leo utani wa majina ya SSC au YASC, majina kama hayo, kwa sasa hayapo mitaani.
Picha yako ya Kahama , katika picha yako ya Mjengwa, ilikuwa ni nzuri sana, maana nyuma ya ile picha yako ya Hoteli za Watu wa “Visenti” ni nyumbani kwangu kabisa Mjengwa.
Picha za vijiji na miji. Endelea kutuletea kila mara katika gazeti lako jipya la “Kwanza Jamii”, maana, tutalipenda sana kama tulivyoipenda “Blog” yako ya Mjengwa.
Kwa leo sina mengi. Lakini salaamu zangu nyingi kwa wanao na mama yao.
It’s Great To Be Black=Blackmannen
Kuanzisha gazeti kwa nyumbani tz ni kama uwe na mtaji wa dola laki 1(million 100)na hizi hela ni nyingi sana kw amtu asiye na uhusiano na mafisadi na kumbuka kuwa mwaka jana tu sisi washika dau tulimchangia huyu Mjengwa million 1 tu za kamera na alipata kamera
Mjengwa hana uwezo wa kifedha za kuanzisha gazeti na habari nilizo nazo ni kuwa Mjengwa kafadhiliwa na fisadi ili kuwasafisha kw atuhuma hizi za kifisadi na yeye Mjengwa kakubali!
Mjengwa tunajua nini kitafuatia,na umetudhalilisha sisi wasomi na sikutegemea kama utafanya hivi yaani kuwa kibaraka wa akina Rostam Azizi kwa kukufadhili ili uondoke kwenye gazeti la kweli la Jenerali Ulimwengu na kuanzisha lako kwa kutetea ufisadi
Kama tu mtunzi Shafi aliposema kwenye Kitabu chake cha KULI aliposema “yana mwisho haya”na ipo siku Mjengwa,na wenzako akina Lowassa,Bagenda na huyu Rweyemamu anayewapa pesa kunyamazisha wapinzani na kuwasafisha akina JK mtafifia!
Ni hatua nzuri ya kupongezwa na kuungwa mkono kwa hali na mali.
Maggid anayo historia,na bila shaka historia hiyo inaaambatana na hadhi fulani ktk jamii.
Tusubiri tulione Kwanza Jamii na tumuunge mkono sio kwa kwa kulinunua tu bali pia kumkosoa kwa nia njema anapokosea yeye na Waandishi wengine.
Nawatakia kila la kheri ktk team yao.
Longo longo tupu!!!!!!!!!!!
kwanza inabidi kila wakati watu tufanye uchunguzi ili tujue ukweli badala yakujaza ushabiki vichwani mwetu. kuanzisha gazeti hakuhitaji kuwa na milioni 100 kama wengine wanavyotaka tuamini, uzushi huu inawezekana ni kutokana na jamii yetu kupenda kufuata maneno ya mitaani bila ya kufanya uchunguzi. kila kitu siku hizi ni TEKNOHAMA!
Tutumie neema ya akili ipasavyo;Mjengwa alikuwa anamiliki gazeti kabla;je,hoja ya milioni 100(sijui kwa mchanganuo upi?)ilikuwa wapi?
Hiki ni kizazi kipya cha waandishi ambacho kitawarithi wakongwe.Tuwape moyo badala ya kuanza kuwakatisha tamaa.Tusubiri tulione Kwanza Jamii na tutasema wakati ukifika.
Majjid na team yako-Keep it up.
Kama aliweza kuanzisha gazeti la michezo la Gozi spoti, na likachapishwa na kuwepo mitaani na watu wakalisoma, kuna tofauti gani katika gharama za kuchapisha gazeti la michezo na la kuelimisha jamii? Huyo anayesema inahitajika kama milioni 100 atuletee ushahidi hapa ama sivyo yeye ndiye FISADI wa mawazo. Na hili tatizo la uzushi pale mtu anapothubutu kufanya jambo ndilo linalotufanya hadi leo tuwe nyuma kimaendeleo na hasa katika suala zima la ujasiriamali.
Kuna watu waliothubutu kwa mtaji wa milioni moja, na wengine milioni tano tu sasa hivi wananunua maghorofa Kariakoo baada ya kufanya kazi kwa bidii na mitaji yao kukua. Tanzania kuna opportunities kibao na watu wenye kuziona na kufanya bila woga wako mbali ila wale walio na ufisadi wa mawazo bado wanasubiri mitaji ya milioni 100, na ndio hao hao wanaoua Ma albino ili wapate utajiri kwa kuona kwamba haiwezekani jambo fulani kufanyika bila hivi au vile.
Bi Mkora bora ulivyomjibu huyo Mbassa yaani mtanzania akianzisha kitu lazima watataka wamkatishe tamaa hivi kwani mpaka hapa alipofikia wanadhani kafikaje?Acheni mambo ya kijibaroho bana keep it up Mjengwa kazi nzuri unaweza kufanya chochote alimradi umeamua and no one can tell u can’t cause they are not u.Keep up the good work.
Naungana na Mbassa, Magged nilidhani ni mwanamapinduzi wa kweli, nilipenda makala zake lakini mafisadi wamemnunua. umasikini mbayaya jamani.Kuna magazeti mengi ambayo Maggid na wengine wangeendelea kuandika na kutoa makala zao kama Raia Mwema na Mwanahalisi.
Lakini kwa vile Kina Johnson Mbwambo na Jenerali Hawanunuliki, mafisadi wameona Maggid kuwa ni boya linanunulika kirahisi.Hili ni gazeti la kusafisha mafisadi.Rudi kundini Maggid.Tamaa Mbaya kaka
I need the news of raia mwema of 2 or 3 june 2009
MJENGWA CLARIFY DOUBT KWANZA , HALAFU NA NYINYI WATANZANIA ACHENI WIMBO WA UFISADI FANYENI KAZI NA TOENI MAWAZO YA KIMAENDELEO! MSIJIFICHE NYUMA YA KUKEMEA UFISADI KUMBE NANYI NI MAFISADI WAKUBWA WA FAMILIA ZENU TUKIWAPA NAFASI MTATUFIKISHA WAPI? KWANZA ZUNGUMZIENI ISSUES ZENYE ATHARI ZITAKAZOENDELEA KUTUUMIZA NA SIYO ZILIZOTUUMIZA!KAMA NI EPA,RCHMOND ZILIITUUMIZA SANA LAKINI ZIMEPITA WHERE WE GO? MSILETE UBISHI WA SLAA BADALA YA KUTUAMBIA NJIA YA KUELEKEA ANATUAMBIA KUHUSU UFISADI NA KUTUACHA HEWANI NA HOJA ZA KUFIKIRIKA ZA CEMENT YA 5000!
Ndugu mhariri wa gazetihili KERO yangumimi ni kwa shirika la maji mkoa wa Iringa IRUWASA halitutendei haki sisi kama wateja wake,kwani ni mwezi sasa na wiki ya2 maji hayatoki taarifa nimetoa lakini fundi haji kutengeneza kilatukienda wanasema tusubiri fundi atakuja lakini hatokei.2Naomba msaada wako.MWAKIRISHI WANANCHI WA FRELIMO MAJENGO MAPYA MUUNGANO.