
Pichani ni Waziri Mkuu ambaye pia ndiye mgeni rasmi wa tamasha la siku tatu la utamaduni wa Mtanzania linalowakilishwa na jamii ya Washubi na Wahangaza kutoka wilaya ya Ngara Mkoani Kagera, akionyeshwa baadhi ya vyakula vya kiasili ya makabila hayo leo mchana ndani kijiji cha Makumbusho jijini Dar.
Tamasha hilo limezinduliwa rasmi leo mchana na Mh. Pinda ambalo litadumu kwa muda wa siku tatu kuanzia leo ndani ya kijiji cha Makumbusho,jijini Dar. Ukipata nafasi pitia mitaa ya makumbusho ukajionee utamaduni wa wahangaza na washubi.

Tanzania huwa ina “zali” la kutembelewa na watu mbalimbali wenye umaarufu ambao unavuka mipaka ya nchi zao na hivyo kuwa na umaarufu karibuni sehemu zote za ulimwengu.
Mfano mmojawapo ni mwanamuziki Michael Jackson (Mfalme wa Pop) alipozuru Tanzania.Pichani ni MJ akipiga stori na aliyekuwa Rais wa Tanzania kipindi hicho,Ally Hassan Mwinyi. Maswali: Je unakumbuka MJ alifanya ziara hiyo lini? Alitembelea miji gani?

Tarehe Juni 8 mwaka huu wapenzi wa filamu nchini Tanzania watakuwa na sababu nyingine ya kuketi mbele ya luninga kwa ajili ya burudani. Msanii Steve Kanumba akishirikiana na wasanii wengine kibao akiwemo Big Brother 2007,Richard Bezuidenhout watakuwa wanakuja na filamu mpya iitwayo “Fake Smile” au kwa kiswahili tunaweza kusema tabasamu la uongo.Itahusu nini? Bonyeza hapa ili upate fununu.


Naomba nikuulize swali; Kwenye muziki unapenda zaidi ujumbe uliomo au midundo kwa maana ya beats? Kwako wewe muziki ni nini? Usiharakishe kunijibu. Fikiri kwanza.
Wakati unafikiri ngoja nikupe jibu langu.Mara nyingi huwa napenda wimbo wenye ujumbe. Midundo ikiwa imetulia huwa nazama pia.Ndio maana nampenda sana Oliver Mutukudzi(mwanamuziki kutoka Zimbabwe) wakati mara nyingi sielewi anachokiongelea mpaka pale ninapopewa tafsiri. Napenda jinsi anavyocharaza gitaa lake na kutawala jukwaa. Napenda muziki kwa sababu naamini muziki ni universal language(lugha ya dunia).
Miongoni mwa nyimbo ambazo nimezisikia hivi karibuni na kupenda ujumbe na midundo ni kutoka kwa mwanamuziki wa muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania anayekwenda kwa jina Roma(pichani). Jina la wimbo wake ni Tanzania. Msikilize Roma kwa kubonyeza player hapo chini kisha uniambie kama ujumbe uliomo kwenye wimbo huu unakugusa au la.
Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.
Hapo jana Rais Jakaya Mrisho Kikwete amekuwa kiongozi wa kwanza kutoka Afrika kukutana na Rais wa Marekani,Barack H.Obama katika Ikulu ya Marekani. Hizi hapa ni baadhi ya picha za ziara hiyo. Picha zote na Freddy Maro wa Ikulu.

Rais Jakaya Kikwete akitia sahihi katika kitabu cha wageni punde tu alipowasili katika Ikulu ya Marekani maarufu kama White House.

Rais wa Marekani Barack Obama(kushoto) akimkaribisha Rais Jakaya Kikwete katika ofisi yake maarufu kama Oval Office.

Rais Kikwete akiwa katika mazungumzo na mwenyeji wake Rais Barack Obama ndani ya Oval Office. Marais hao waliongelea mambo mengi ikiwemo ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani katika masuala mbalimbali.

Rais Kikwete akiendelea na mazungumzo ndani ya Oval Office na wenyeji wake akiwemo Waziri anayeshughulikia masuala ya nje wa Marekani, Bi.Hillary Clinton(kulia)

Naam. Wikiendi tena. Wakati wa burudani. Wakati wa vikao vya kiti kirefu,familia,harusi,ubatizo,ubarikio,mwali kutolewa ndani nk.Ni muda mwingine wa kupumzisha akili.Hata kama unafanya kazi weekend hii bila shaka utakubaliana nami kwamba hata huko mabarabarani hali huwa shwari. Zile vurugu za foleni,msururu wa watu nk huwa hakuna.Ukiitazama Samora Avenue unaweza kuona kutokea Askari Monument mpaka Clock Tower.Unabisha? Hebu jaribu uone.
Kikubwa wiki hii ni kwamba tumetimiza miaka miwili. Kwa maana hiyo bado tupo kwenye mauzamauza ya kufurahi,kujipongeza na katika semina elekezi ili kuweka mstakabali wa nini kinachofuata. Kwa upande mwingine umemsikia mwenyewe mkuu wa nchi.Anasema habari za uraia wa nchi mbili hazina budi kusubiri. Anasema wasomi wamemshauri kwamba mpango wa kula huku na kule sio mzuri. Mwenyewe akasita kuleta habari za “wivu”. Wakati huo huo mkuu anasema mjenge na kuwekeza “nyumbani”. Nyumbani tena? Sijui wewe unasemaje lakini mimi naona kazi kubwa bado ipo. Washauri wasomi najua wamenielewa. Kama hawajaelewa basi tena.
Turudi kwenye burudani kwani kama ujuavyo leo ni Ijumaa. Ni mambo ya sakayonsa. Mambo ya zilipendwa. Enzi zile ambapo ugonjwa ulikuwa ni mafua tu! Wimbo unaitwa Binadamu Hatosheki kutoka kwao Orchestra Makassy. Bila shaka utakubaliana na kina Mzee Makassy.Binadamu sijui umpe nini aridhike. Hivi kwanini tupo hivyo tulivyo? Kama wanavyoimba; ukimpa jua anataka mvua. Ukimpa mvua anataka jua!Kha. Ukimpenda sana anataka kuchukiwa na ndio maana atakuletea madharau,visa,vituko na visasi.Enewei,wasikilize mwenyewe Orchestra Makassy. Pata burudani na furahia weekend yako.
Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.
Subiri kidogo. Kwa sababu wikiendi hii tunaweza kusema ni wikiendi ya BC kwa maana ya kutimiza miaka miwili sidhani kama kuna ubaya kama tukiweka kibao kingine kama zawadi….sikiliza hapo chini;
Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.


Leo ni siku ya furaha. Ni siku ya kufurahi na kutafakari. BC imetimiza miaka miwili hivi leo tangu ianzishwe! Ni vigumu kuamini kwamba siku na miaka zinakwenda kwa kasi ya namna hii.
Hatuna mengi ya kusema hivi leo zaidi ya kukushukuru wewe mtembeleaji na mchangiaji wa BC. Mtandaoni zipo blogs nyingi sana na katika lugha mbalimbali ikiwemo hii yetu ya Kiswahili. Lakini kwa sababu umechagua kila mara kututembelea na kuchangia mawazo na mtizamo wako hapa, hatuna budi kukushukuru sana sana.Tunaamini kwamba hiyo ni kwa sababu unaipenda BC na unathamini mchango wake katika ulimwengu wa habari na mawasiliano. Asante sana. Shukrani nyingi pia ziwaendee ninyi nyote ambao mara kwa mara mmekuwa aidha vyanzo vya habari zetu,burudani zetu. Pia shukrani kwa wale ambao wamekuwa wakitukosoa pale tunapoteleza. Tungependa kukuhakikishia kwamba tunathamini sana michango hiyo ikiwemo kukosolewa.
Pamoja na hilo, BC kama mojawapo ya vyanzo vya habari au kisima cha kusambaza habari, si kitu bila ushirikiano wa vyombo vingine vya habari na mawasiliano. Kwa hali hiyo ni lazima na sharti tuseme shukrani nyingi sana kwa vyombo vyote vya habari nchini Tanzania zikiwemo radio,magazeti na hata luninga.
Juu ya yote shukrani sana kwa bloggers wenzetu.Bila ninyi kazi ingekuwa ngumu maradufu.Asante sana.
Tunauanza mwaka mwingine. Kama ambavyo umeshuhudia katika kipindi kilichopita, kikubwa ambacho tunajaribu kujitahidi nacho ni kuboresha kazi zetu. Ni kazi kubwa na yenye gharama zake lakini tumedhamiria kuifanya kwa sababu tunathamini na kuamini katika ulimwengu huru wa habari na mawasiliano. Asanteni.
Anaitwa Hussein Rashid ingawa umaarufu wake unakuja na jina la Hussein Machozi (pichani) ambalo ndilo jina lake la kisanii. Alizaliwa mwaka 1986 katika wilaya ya Manyoni mkoani Singida. Hivi sasa Hussein Machozi ni miongoni mwa majina mapya katika anga za muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Kama uliwahi kuusikia wimbo unaoitwa Kafia Ghetto unaozungumzia story ya jamaa mmoja ambaye alimfukuzia au kumtaka urafiki wa mapenzi binti mmoja kwa muda mrefu sana. Baada ya muda huo mrefu, siku moja binti huyo akaamua kwenda “ghetto” kwa ajili ya huyo jamaa ili kumpa taarifa kwamba amekubali ombi lake. Kijana akafurahi sana na kisha kumuacha binti ghetto na kuelekea dukani kumnunulia soda. Aliporejea alitahamaki kukuta binti amejilaza kitandani kwake. Alipojaribu kumgusa akagundua kwamba binti amekata roho. Jamaa akachanganyikiwa asijue la kufanya. Kwa ufupi hiyo ndiyo story iliyomo ndani ya wimbo Kafia Ghetto. Mwisho wa wimbo Hussein anauliza ungekuwa ni wewe hali hiyo imekutokea ungefanya nini? Je walimwengu watakuelewa kwamba hukumuua binti? Je ungemtoa vipi humo ndani mwako?
Hussein Machozi hakuishia hapo. Aliendelea kudhihirisha ukali wake kwa kutoa wimbo mwingine uliokwenda kwa jina Full Shangwe akimshirikisha AY. Nyimbo hizo pamoja na zingine kama vile Maji Yakimwagika, Niambie zinapatikana katika albamu yake ya kwanza inayoitwa PROMISE aliyoitoa mwaka jana 2008.
Kwa sasa Hussein Machozi anakamilisha albamu yake ya pili ambayo ameipa jina KWA AJILI YAKO katika studio za Tetemesha zilizopo jijini Mwanza. Mapema mwezi uliopita aliachia single ya kwanza kutoka katika albamu hiyo inayokwenda na kubeba jina la albamu Kwa Ajili Yako. Usikilize wimbo huo hapa.
Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.

