Leo hii dunia inaadhimisha miaka 28 tangu Mfalme wa Reggae ulimwenguni,Hayati Bob Marley, alipoiaga dunia kwa ugonjwa wa saratani huko Miami Beach,Florida nchini Marekani.
Wakati tunamkumbuka Robert Nesta Marley ambaye kwa wengi bado anabakia kuwa gwiji na mtazamo halisi wa muziki wa Reggae, hatukuhitaji kuvuka bahari,misitu,mito na mabonde kumtafuta mtu ambaye bila shaka sio tu mfuasi halisia wa muziki wa reggae bali ndio picha halisi ya muziki wa reggae nchini Tanzania hivi sasa. Huyu si mwingine bali msanii,mwanamuziki wa reggae anayetamba vilivyo ndani na nje ya Tanzania, Jhikoman(pichani)
Katika mahojiano haya utaweza kujua historia kamili ya Jhikoman. Aliianza vipi safari ya muziki?Kwanini akaishia kwenye muziki wa reggae? Je anasemaje kuhusu siku ya leo ambapo ulimwengu unamkumbuka Bob Marley? Nini mtazamo wake kuhusu muziki wa reggae,siasa na muelekeo wa Tanzania hivi leo? Kwa hayo na mengine mengi,fuatana nami katika mahojiano haya na Jhikoman.
BC: Jhikoman, karibu sana ndani ya BC. Mambo yanakwendaje?
JHIKOMAN: Nashukuru ndugu yangu, tunaendelea kutoa mchango wetu kwa jamii kama ilivyo ada!
BC: Kwa sababu hii ni mara yako ya kwanza hapa BC,mashabiki na wapenzi mbalimbali wa muziki bila shaka wangependa kwanza kujua historia ya maisha yako kwa ufupi tu. Ulizaliwa wapi,ukakulia wapi,ukasomea wapi na mambo kama hayo?
JHIKOMAN: Asante. Mimi nimezaliwa hapa hapa jijini Dar-es-salaam katika hospitali ya Ocean Road. Nimekulia Dar-es-salaam na Morogoro kutokana na kwamba Mzee wangu alikuwa mtumishi wa serikali kitu ambacho kilitulazimu kuwa tunahamia mikoani katika vipindi tofauti tofauti. Kwa mfano tuliwahi kuhamia Arusha, Songea,Mtwara nk. Morogoro niliishi na mjomba wangu kaka wa mama yangu. Sehemu zote tulizokuwa tukihamia nilikuwa nalazimika kuhama shule pia! Muda mwingi wa shule nimeutumia mkoani Morogoro.

Jhikoman
BC: Wasanii wengi wa muziki ambao nimeshafanya nao mahojiano huwa wananiambia kwamba walianza muziki baada ya kuvutiwa au kushawishiwa na mtu au watu fulani fulani. Kwa upande wako ilikuwaje ukaamua kuwa mwanamuziki na zaidi kwanini muziki wa Reggae?
JHIKOMAN: Nyumbani kwetu tuliishi na wajomba zetu wadogo wa mama yetu. Mama na wadogo zake walikuwa wakiimba kwaya. Pia binamu yetu mpwa wa baba yetu naye aliimba kwaya. Kaka yangu ninayemfuata kuzaliwa ndiye hasa alinivutia kuwa mwanamuziki kwani yeye alikuwa akipiga gitaa. Nilipenda sana nyimbo za Balisidya, Mzee Makasi, King Kiki, Dr.Remmy Ongala, Marijan Rajab. Nilipomtembelea mjomba mjini Morogoro nilivutiwa sana na santuri za Mbaraka Mwinshehe. Kipindi hicho nilikuwa sijaanza hata shule ya msingi.
Shule ndiyo ilikuja kunifanya nielewe kilichokuwa kinaongelewa katika muziki wa reggae. Reggae ni sauti ya kweli na haki yenye nguvu ya kuvunja minyororo ya fikra. Hiyo ndiyo sababu iliyonifanya nikazama zaidi katika muziki wa reggae.
BC: Jina “Jhikoman” linamaanisha nini na je ni jina ulilojipa mwenyewe au kuna mtu alikupa?
JHIKOMAN: Jina langu ni Jhikolabwino Manyika. JHIKOMAN ni muunganiko wa herufi tano(5) za jina langu la kwanza na tatu(3) za jina la pili.
BC: Muziki wa Reggae na wasanii wa muziki huo kama vile wewe, huenda sambamba na imani ya ki-rastafari. Je kwa upande wako hiyo imekaa vipi? Unaamini na kuabudu kufuatana na imani gani? Labda unipe pia darasa kidogo kuhusu uhusiano uliopo kati ya imani ya kirastafari na muziki wa reggae.
JHIKOMAN: Reggae ni muziki ulioanzia kwenye nyumba ya Rasta. Asili yake ni Afrika japo kuwa hivi sasa watu wanaofuata njia mbalimbali za maisha wanapiga muziki huo kwa mfano makanisani, watu wasio na asili ya Afrika kuanzia Ulaya,Asia, Marekani nk.
Jhikoman ni Rasta;mtu wa kiroho na si mtu wa dini!
BC: Pamoja na kwamba muziki wa reggae ni miongoni mwa mitindo ya muziki iliyo maarufu sana duniani, nchini Tanzania bado wasanii wa muziki huo mpo wachache ukilinganisha na aina zingine za muziki kama vile bongo fleva nk. Unadhani hiyo inatokana na nini?
JHIKOMAN: Wachache? Wasanii wa Reggae tupo wengi. Mazingira yaliyopo hayatoi fursa kwa wasanii wa Reggae kusikika kirahisi. Hiyo ndio labda inayosababisha ionekane kana kwamba wasanii wa reggae tupo wachache nchini Tanzania.
BC: Leo hii dunia inaadhimisha miaka 28 tangu Mfalme wa Reggae, Hayati Bob Marley afariki dunia. Unajisikiaje unapoadhimisha siku hii?
JHIKOMAN: Inadhihirisha nguvu ya roho na uwepo wake Bob Marley kwani ujumbe wake upo pale pale. Na jamii ya wanadamu wanaendelea kuelimika na kuona mwanga katika giza nene lililoigubika dunia hii ya leo kupitia muziki wake. Ni heshima kubwa na najisikia amani kuwepo hai hivi leo ili kuadhimisha siku kama hii.

Bob Marley
BC: Watu mbalimbali wanasema kwamba kusikiliza CD yako ni bab kubwa lakini kukuona kwenye stage wakati wa live performance ni bab kubwa zaidi. Sasa ninavyojua mimi live performances huweza kuwa na vimbwanga vyake. Vyombo vinaweza kuwa havitoi sauti vizuri, unaweza kuwa husikiki nk. Je hali kama hiyo imeshawahi kukutokea? Kama bado ikitokea unadhani utafanya nini?
JHIKOMAN: Kwanza nashukuru kusikia kwamba watu wanafurahia live shows ninazozifanya. Unajua sasa hivi tumepiga hatua sana kwani tuna vyombo vizuri hapa nchini na mafundi wazuri. Mimi nawatumia mafundi ambao wamezoea sound yangu na sina hofu ya sound. Siku za nyuma yaani miaka kadhaa nyuma tumepitia kwenye hali ngumu ya vyombo hafifu na kusema kweli bila uvumilivu hali ile ilikuwa inavunja moyo.
Kwa hiyo kujibu swali lako,hali hiyo haijawahi kunitokea ila nina imani kwamba kutokana na maendeleo ya tekinolojia tuliyonayo,haitokaa itokee.

Jhikoman akiwa jukwaani huko Mji Mkongwe,Zanzibar wakati wa Tamasha la nchi za Jahazi. Picha na Eirik Folkedal.
BC: Wasanii wa reggae mnatambulika zaidi kama conscious artists kwa maana ya kwamba mnaangalia kwa mapana na marefu masuala ya jamii. Unapoiangalia Tanzania, unadhani tunapiga hatua kwenda mbele au kwenda nyuma? Kwanini? Ungeshauri nini kifanyike?
JHIKOMAN: Inategemea katika nyanja gani. Lakini kwa mfano kitaaluma vijana wengi wanajitahidi kusoma kwa bidii na hii ni ishara nzuri kwani minyororo ya kiakili inaendelea kuvunjwa. Ushauri wangu ni kwamba elimu itolewe bure. Mwisho wa siku tutagundua kuwa hatujatoa elimu bure kwani watatayarishwa wataalamu ambao watasukuma gurudumu la maendeleo mbele. Mpaka leo hii bado katika nyanja mbalimbali muhimu tunaagiza wataalam kutoka nje. Tusingekuwa tunafanya hivyo endapo tungewekeza zaidi katika elimu.
BC: Una mpango wowote wa tour ya kimataifa mwaka huu?
JHIKOMAN: Natarajia kwenda nchini Uingereza mwezi wa saba mara tu baada ya Tamasha la nchi za Jahazi. Baadaye pia nategemea kuzitembelea nchi za Scandinavia.
BC: Asante kwa muda wako Jhikoman. Kila la kheri katika kazi zako.
JHIKOMAN: Nashukuru sana. Nawe pia nakutakia kila la kheri katika kazi zako.Rastafari.

Note: Albamu ya Jhikoman iitwayo Yapo ipo sokoni hivi sasa na unaweza kujipatia nakala yako kwa kubonyeza hapa
Feedback / Comments
6 Responses to ““ELIMU ITOLEWE BURE”-JHIKOMAN”
Leave a Reply


sending...
SAFI SANA HAKIKA NYIMBO ZAKO MKUU JHIKO MAN ZINAZIDI KUPASUA ANGA KULA KUKICHA.UJUMBE MZITO MIDUNDO YA UHAKIKA BONGO MPAKA
DARWIN AUSTRALIA NA WANALIA NA MIZIKI YA NYUMBANI
Asante kwa hii BC! Asante Jhikoman na moto uleule tutafika!
Asanteni sana BC! Heshima kwenu, tupo pamoja!
Kwa wapenzi wa Jhikoman. Nyimbo zake pia zinapatikana kwenye itune na Amazon mp3 stores!
Toka nimenunua CD ya Jhikoman from cdbaby sijaona muziki mwingine wa kusikiliza
U ar doing great brother
Na unao uwezo mkubwa sana wa kujibu maswali kwenye interviews
Kipaji brother-Hubahatishi
Hakika Jhikoman anafanya kazi nzuri,muziki una ujumbe mzuri na midundo pia.Kila la kheri katika kazi yako na kuzidi kuuza muziki katika mchi mbalimbali ulimwenguni kote.
Bless I ‘n I