
Na Freddy Macha
Mwezi jana tulitoa sehemu ya kwanza ya mahojiano na mmoja wa wataalamu na wasomi wetu mkazi na mhadhiri anayeishi Uingereza Dk. Imani Silver Kyaruzi. Kitabu chake mkakata “Mbinu za Ujasiriamali” kitasaidia sana kuendeleza uchumi na akili za Mtanzania hasa yule anayependa kujiendeleza au kufanya biashara. Kilichapwa na “Mkuki Na Nyota” mjini Dar Es Salaam mwaka jana.
FM: Turudi katika uandishi Tanzania. Mkuki na Nyota ni wachapishaji pekee wanaowakilishwa kidogo nje, wenye tovuti na wanaojitahidi. Je kitabu kinauzwa vizuri? Ulichapisha nakala ngapi? Je, wasomaji wengi wako nje au ndani? Unayo njia ya kuyajua hayo?Unaridhishwaje na hali ya uandishi na usomaji wa vitabu nchini.
Dk. Imani Kyaruzi: Mkuki na Nyota wanao mpango wa kukiendeleza na kukisambaza kitabu hiki nchini kote. Kazi hii imeanza tayari na ninategemea mawasiliano hivi karibuni. Nakala zilizochapishwa ziko katika maelfu na ninaweza tu kuongelea wanunuzi wa bara la Ulaya. Wakati wa unzinduzi nilifanikiwa kusaini nakala nyingi sana na kitabu kilipokelewa vizuri na umati wa Watanzania waishio Uingereza. Baadhi ya nakala zilienda Ujerumani kwa wasomaji wa huko na marejesho yanaridhisha.
Nia ni kuwafikia wasomaji wa ndani na kazi hii itaanza baada ya majuma mawili. Ningependa kutoa mafunzo nyumbani wakati wa kukitangaza kitabu hiki.
Kuhusu uandishi na usomaji, inasikitisha sana kwani tumezoea kuona vitabu vya kina Michael Porter na kina Mr Smith na ninafikiri Watanzania tukianza kuandika italeta changamoto kwa waandishi walioko nyumbani ambao naamini wako wengi, tu. Kwa upande wa usomaji sina uhakika na hilo, ila tu ningependa kusisitiza kuwa vitabu vya mitaala hadi Chuo Kikuu viwakilishwe na vitabu vilivyoandikwa na wazalendo na vyenye kulenga katika hali halisi ya nchi. Hii ni muhimu kwani vitabu vyenye maudhui ya Kiulaya vinawatayarisha vijana wetu kutumikia nchi gani?
FM: Nini makusudi ya kuandika kitabu kuacha yale uliyoelezea mwanzoni (Utangulizi). Je, nini kilichokupa moyo au nia ya kuandika kitabu. Labda uliona hatusomi? Labda uliona wafanyabiashara Ulaya (kama bwana Richard Branson uliyemtaja) wanaandika vitabu? Tupe maoni zaidi.
Dk. Imani Kyaruzi: Wakati wa ziara ya utafiti barani Afrika (Tanzania, Uganda, Ghana, Swaziland na Botswana) niligundua baadhi ya vitu vilivyokuwa vikkikwamisha biashara za wazalendo. Watu walikuwa wema sana na walichangia mawazo nami nilihaidi kutumia mapungufu yao, si kwa kuwaonyesha kuwa hawawezi bali kuwarudishia kitu fulani ambacho wanaweza kukitumia kuendeleza biashara zao. Je, ujumbe ningeufikishaje wakati walio wengi hawaongei lugha za kigeni? Nilionelea ni vyema kuanzia nyumbani, hivyo nikajikuta ninaandika kwa Kiswahili. Nia haikuwa kutengeneza faida bali kurudisha kitu kidogo katika jamii iliyonilea kwa mapenzi makubwa. Pia kuna wale watu wenye nia njema ya kujenga uchumi wetu lakini hawakubahatika kwenda vyuoni na wana nia ya kujiendeleza – hawa wanahitaji msaada wetu mkubwa kwani kama wote tungefanikiwa kwenda vyuoni basi baadhi ya biashara zisingekuwepo! Mama Ntilie aliyenipikia nikiwa Tambaza na Mzee Sefu wa Chips nao pia wasingenipatia lishe bora iliyonisukuma hadi leo naweza kuitwa Bwana Daktari. Lakini jambo muhimu hapa ni kwamba si lazima uende chuo kikuu kujifunza namna ya kutathmini faida katika biashara, unaweza kusoma kitabu hiki na kufuata mifano…

FM: Sura ya Tatu muhimu sana; maana unaeleza “namna ya kupanga biashara.” Mantiki yako kwa maoni yangu mpitiaji ni kudokeza juu ya uholela na kutokuwa na nidhamu katika masuala yetu ya kikazi Bongo. Unafikiriaje kuhusu wafanyabiashara wetu. Je wana nidhamu, bidii na kujituma? Mbona Wakenya, Waganda na Wahindi wanatawala sana biashara zetu Tanzania?
Dk. Imani Kyaruzi: Hii imenifurahisha sana! Kuna biashara za aina nyingi Bongo lakini zinazotawala ni zile za kina bwana Kauzeni – hajui tofauti ya rafiki na mteja, msambazaji na mzalishaji n.k Wote hawa huwaweka kundi moja na hata mtaji hajui alianzia wapi na kuishia wapi. Mifumo mingi ni kama ya genge – nyaya zikija unanunua tenga – zote mbivu, mbichi na zilizooza ; siku zikiharibika mtu anasema ni kudra ya Mungu, zikiuzwa zote anasema ridhiki imeingia. Watanzania wanajituma sana, tatizo ni nidhamu katika kazi na huduma kwa wateja. Waganda, Wakenya na Wahindi wanaweza sana kutawala biashara zetu kwani utamaduni wao unatofautisha biashara na sindimba. Wakiwa katika biashara uhusiano wao hubadilika na hufuata kanuni za biashara na wakati wa sindimba kanuni zinazotumika ni zile za midundo. Lakini tumeanza kubadilika – tunaweza kujifunza kutoka kwa hawa wenzetu; ila tusijifunze kila kitu kwani tabia zingine za wageni si za kuiga.
FM: Je unaamini ubepari utaleta maendeleo Tanzania? Yaani ukilinganisha enzi za Ujamaa (1967-1986) na Mwalimu Nyerere?
Dk. Imani Kyaruzi: Duh! Tanzania sio nchi ya Kijamaa na wala sio nchi ya Kibepari bali iko tu katika hatua za kusahau nasaha za ujamaa na kuuelekea ubeparini – tumeacha tu kuvaa kaunda suti lo! Kutokuwa na msimamo kamili ndo’ kunaleta utata juu ya faida na hasara za mifumo hii katika kuleta maendeleo. Kuna vitu viwili hapa – siasa zinajenga uchumi au uchumi unajenga siasa. Bwana mwandishi enzi za Nyerere siasa za ujamaa zililenga katika kujenga uchumi ulio bora na wenye uwiano. Sasa baada ya kifo cha ujamaa hadi leo hii uchumi ndio unaamua siasa gani ufuate! Sasa tukirudi katika swali lako jibu ni hapana na ndio! Ubepari utaweza kuleta maendeleo kwa watu wachache tu wanaojua kucheza katika anga za ubepari, walio wengi hawajui na hawatajua nini kinaendelea na wanaweza kuuzwa kwa bei ya jumla. Ubepari nia yake ni kulimbikiza mali na si rahisi kujenga uwiano – hapa ni rahisi kujenga jamii mbili za wazalishaji na walaji na mara nyingi masikini ndio wanakuwa wazalishaji. Kwa upande wa pili, ubepari unaweza kuleta maendeleo kwa kuendeleza ushindani. Kama nilivyoeleza katika kitabu, ushindani ni wa muhimu sana katika kujenga jamii yenye ari ya kujituma na kuzalisha bidhaa na huduma bora. Tatizo labda la huu ushindani ni kuwa mara nyingi unakuta washindanaji wana nguvu zisizowiana – kwa mfano Steers na Mama Hassan wa Sinza wakiamua kutengeneza vitumbua Mama Hassan atashindwa kwani hajaendelezwa au kuwezeshwa japo kufikia nusu ya kiwango cha mshindani wake. Maana yangu ni kwamba kabla hujaruhusu ushindani nyumbani kwako lazima uhakikishe wapiganaji wako umewalisha vizuri la sivyo nyumba yako inaweza kutawaliwa na wageni.
Sasa nini kifanyike! Kwa mtazamo wangu ubepari si mbadala halisi wa ujamaa. Baada ya mfumo wa ujamaa kufumuka tulitakiwa kusuka mfumo wetu wa ubepari ambao hauna matobo mengi kama tulionao sasa. Huu mfumo wetu wa sasa wa Pseudo-capitalism au wengine wanaita a transition to a market-led economy misingi yake ni ile ya kula kuku, mayai, manyoya na hata mbolea kistaarabu huku wananchi wakizidi kuumia. Maendeleo ya ubepari utayaona Oysterbay na Masaki lakini huko Mwanalugali sahau kabisa – maendeleo yatakuwa ni barabara za kupitisha mchanga wa kujenga nyumba za mapumziko ya wikiendi. Tutataendelea kupita huku watoto wadogo wenye kamasi vifua wazi wakiendelea kupungia magari yetu makubwa kama nyumba. Hatutasikia kelele zao kwani vioo vitakuwa vimefungwa ili hewa iliyochujwa isichanganyike…
Feedback / Comments
8 Responses to “DR.IMANI KYARUZI NA MBINU ZA UJASIRIAMALI-PART II”
Leave a Reply


sending...
Hi guys kutoka Helsinki,
Hongera Dr. Kyaluzi, mimi ninakukumbuka enzi hizo, tulisoma wote pale Tambaza secondary Form six, mwaka 1995.Kama nimekufananisha tafadhali nijulishe kupia email yangu waweza kuipata hapa,http://blogs.helsinki.fi/kashaga/
Kwa kweli soma lako zuri na nimuhimu sana kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania, Mimi ninakupa big up sana, ila ninaomba unitumie email yako ili nikuelekeze njia rahisi ya kufikisha elimu hiyo kwa watanzania wengi kama sio waaAfrica wengi,
good luck
Frateline
Nimefurahishwa na mahojiano ya Freddy na Dr Kyaruzi,kabla ya kwenda mbele katika utaratibu gani utumike kuhitimu kiwango cha biashara ambacho kimetawaliwa na jirani zetu,turudi nyuma na kujiuliza lini tutapiga hatua ya kurudisha “usomaji wa vitabu” kama ilivyokuwa miaka mingi iliyopita, tumerudi nyuma saana katika kujisomea vitabu,kuna umuhimu saana wanahabari na waandishi kuanza “vita ya kupigana na upandishaji wa usomi wa vitabu”
Hatutoweza kufanya vizuri kibiashara kama bado hatujapiga hatua ya mbele ya usomaji wa vitabu mbali mabli,walatusiwashutumu wahindi kwa kufanya vizuri katika biashara,wamezingatia misingi iliyowekwa na marehemu baba wa Taifa ya usomaji wa vitabu vya hadithi na biasahara , watanzania tunaweza kufanya vizuri katika “biashara” kama jitihada zitafanyika kuanzia elimu ya msingi kurudisha usomaji wa vitabu, ndipo tulipoanzia katika makuzi yetu chini ya mawazo ya busara ya usomaji kwa baba wa Taifa mwl J.K.Nyerere.
mickey@mail-online.dk
Denmark
Dr. Kyaruzi,
Hongera zako nyingi na pole sana, kwa kazi ngumu uliyoifanya katika kuwafumbua macho Watanzania kibiashara!
Dr. Kyaruzi, nataka kukufahamisha kitu kimoja kuwa, Watanzania wengi, wanaupenda sana utumwa wa kimawazo. (Haya ni mawazo yangu mimi).
Katika watu wanaopenda Maendeleo kama Wa Nigerian, ukurasa huu na ule uliopita (Ujasiriamali – Part I), ungejaa maoni kibao na maswali yahusuyo Biashara. Lakini kwa kuwa Watanzania ni wavivu sana, na wapenda utumwa, sio tu kibiashara hata kimichezo, tazama Taifa Stars na Riadha. Lakini kwa kuchonga kisiasa, utadhani wote walisoma Kivukoni, na hasa kulaumu ni nambari wani.
Dr. Kyaruzi, wewe ni mwokozi halisi wa wawatanzania kiuchumi. Lakini utashangaa, tangu uletwe hapa BC (Ujasiriamali Part I na II), maoni yanayoletwa kwako yaangalie mwenyewe,Je, yanaridhisha?.
Lakini, angalia “Wema Sepetu” au “Ray C” anapowekwa hapa BC. Maoni ya watu ni kwa lugha za kiingereza na kiswahili, hata wengine hudiriki hadi kukufuru kwa kusema eti, hawajui kuandika kiswahili, ila kiingereza tu. Makubwa haya. Blogi ni ya Kiswahili na kichwa cha Habari kwa Kiswahili, lakini wanasema eti, hawajui kuandika kiswahili.
Dr. Kyaruzi, nakupongeza sana kwa kutuvumilia sisi Watanzania, na kutumia muda wako mwingi, kutuandikia kitabu chako hicho cha “Wajasiriamali”. Kwa kukitafsiri kwa lugha yetu ya Kiswahili, ahsante sana.
Mimi mwenyewe nitakinunua, nitakupigia simu kwa namba yako hiyo hapo nyuma (Ujasiriamali Part I).
Watanzania wengi walioko nchi za nje ni wale wasiokuwa na Elimu za juu. Ndiyo sababu inayotufanya Watanzania tulio nje tuonekane vituko nyumbani Tanzania. Maana wengi wetu wametoka Jolly Club.
Dr. Kyaruzi, Watanzania wenzetu wanapokutana na habari za Kisomi kama zako, “Wanagwaya”, hawajui waseme nini. Maana wanaogopa mambo ya Diferential Equations, Intergrals na Summations. Lakini wenye Elimu zao, umeona wameomba hadi simu yako ili waongee na wewe na kubadilishana mawazo yao na wewe. Hapa sio moja na moja ni mbili. Kuna mambo ya probabilities na mengine hapa.
Naandika habari hizi na uchungu mwingi, kwa sababu, wewe Dr. Kyaruzi, hapa BC, ulikuwa ni kitu muhimu sana kwa Watanzania wengi, kama sio wote. Sababu ilikuwa ni kupata mawazo ya kujiokoa katika utumwa wao wa kubeba maboksi na kuosha masufuria ya wazungu hapa Ulaya. Warudi nyumbani Tanzania na mawazo ya kimaendeleo, kibiasha na maisha yao wenyewe.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida. Kuna Diwani mmoja hapo Kinondoni Dar es salaam, aliwahi kuishauri serikali iwaruhusu machangudoa kuwekewa sehemu yao maalumu ya kuuza miili yao, ili serikali iwadhibiti kwa kulipa kodi wanapofanya biashara zao za miili, na kupimwa afya zao kila mara ili kuepusha maambukizi ya magonjwa Kwa Watanzania wengine. Lakini wazo hili lilitupiliwa mbali eti maadili ya Kitanzania, hayaendani na kitu hicho.
Watanzania tunajiua wenyewe kutokana na tabia zetu wenyewe. Dr. Kyaruzi yupo hapa kutusaidia kila Mtanzania kufanya biashara, lakini hakuna anayemtembelea hapa, na kuomba ushauri wake, lakini hebu angalia maoni yaliyopo sasa hivi hapa BC kwa “Nakaaya”. Heeee, Mungu Ibariki Tanzania!
It’s Great To Be Black=Blackmannen
Dr. Kyaruzi,
Kazi nzuri na tafadhali usichoke. Kusema tu Watanzania wavivu haitoshi ni lazima tuanze sasa. Suala la ujasiriamali kwa watanzania ni msamiati mpya.Wengi tumezaliwa na kukulia katika mfumo wa ujamaa. Ujamaa kama ulivyochukuliwa na watanzania enzi hizo ni siasa za kula kwa msaaada.Tulijua elimu “BURE”, AFYA Bure, n.k. Watanzania tumeanza kujua kuwa elimu na afya havikuwa bure vilikuwa vinagharamiwa na serikali na pengine sehemu kubwa na wafadhili tukalemaa. Sasa wakati tunaamka usingizini wenzetu walikwisha safiri wako mbali. Sasa michango wa akina Dr. Kyaruzi itasaidia kuendeleza changamoto kwa watanzania ili wabadilike na kuanza kuwa wenye kuona mbele. Kitu cha msingi cha kuangalia ni kuendelea kuwahimiza watawala wetu kuhakikisha utaalam na wataalam ndio wanasaidiwa kutoa dira ya maendeleo ya nchi. Wanasiasa wawe wahamasishaji wa mipango iliyoandaliwa na wataalam. Pia rasilimali za nchi zisizamishwe tu kwenye siasa. Mfano kama kweli nchi imedhamiria kufanya mapinduzi ya kilimo na kwa kuwa rasilimali ni adimu, nchi ikaamua kwa nia nzuri kwamba sasa kwa miaka kumi kipaumbele ni kuwekeza katika kilimo na kuelekeza kila rasilimali kuendeleza kilimo. Inawezekana tukakubaliana kuwa fedha zote za kufanya uchaguzi zitumike kwenye kubadilisha kilimo na baada ya miaka 10 tutafanya tathmini kuangalia kama malengo yalifikiwa na mambo mengine ya siasa yanaendelea.
Tanzania tunathamini sana kuomba kuliko kufanya kazi. Hatuoni aibu kuomba ila tunaona aibu kufanya kazi. Hili ni suala la kufanya mabadiliko ya fikra na namna ya kuishi.
Dr. Kyaruzi, mchango wako wa chapisho ni mkubwa ingawa bado tunakudai zaidi ya hapo kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania. Pale Tambaza ulisomeshwa na fedha za walipa kodi wa Tanzania . Wewe pamoja na wengine mliopo huko mlete changamoto ya maendeleo ya nchi yenu hii nzuri sana duniani. Msijisahau mkajichukulia kama sehemu ya maendeleo ya dunia hii ya kwanza.
Asante kwa mchango wako mkubwa na tunategemea utabuni kitu kingine cha kutuletea changamoto watanzania kwani kuna msemo usemao UKITAKA KUMSAIDIA NDUGU YAKO MFUNDISHE KUVUA BADALA YA KUMPA SAMAKI.
Mgusii
Hongera.
Umeandika na kuelezea mambo mengi na mazuri sana, mimi sina imani kama jina lako lilivyo Dr., kwamba ujumbe wako utawafikia wengi kwa kuwa Watanzania wengi hawana utamaduni wa kusoma, na baadhi ya wachache watembeleao tovuti(ktk vijana) hujikita kuyakinia picha za ngono na kutuma barua pepe.Waweza nisaidia kwa nini Watanzania hatuna utamaduni wa kujisomea?
Nimesoma makala yako vizuri na imenihamasisha katika biashara sana tu, sasa tatizo langu ni hivi jinsi ya kustahimili katika ushindani wakati mimi nina mtaji kidogo, naomba nisaidie zaidi kwa hilo
Habari kaka Kyaruzi
Nimesoma makala yako, imenipa moyo kumbe nami naweza kutoka kama nitafuata ushauri wako. Kakangu nahitaji kufanya biashara ila sina mtaji wa kutosha ila unaweza kunisaidia nitumie njia zipi ili niweze kutoka kwa hicho kidogo nilichonacho.
mimi nataka kuanzisha biashara ya kuuza wadudu nje ya Tanzania lakini nimeshindwa kupata soko kwa sasa nipo chuo nasoma lakini nimeshindwa maisha inahitaji pesa nyingi nisaidie