TAMKO LA MUUNGANO WA ASASI ZA KIRAIA (FemAct) NA MITANDAO YA WAFUGAJIKUHUSU KUKIUKWA KWA HAKI ZA BINADAMU NA HAKI ZA RAIA KATIKA WILAYA YA NGORONGORO KWA MASLAHI YA MWEKEZAJI; KAMPUNI YA ORTELLO BUSINESS CORPORATION (OBC)
Sisi Muungano wa Asasi za Kiraia zinazotetea Usawa wa jinsia, haki za binadamu na maendeleo na ukombozi wa wanawake kimapinduzi (FemAct) kwa pamoja na Mitandao ya Wafugaji mkoa wa Arusha tumeguswa na kusikitishwa na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, haki za raia na uvujaji wa sheria katika kutekeleza oparesheni ya kuhamisha wafugaji wakaazi wa jamii za Kimaasai unaoendelea katika wilaya ya Ngorongoro, Tarafa ya Loliondo inayofanywa na vyombo vya dola kwa maslahi ya mwekezaji kutoka Uarabuni, Kampuni ya Ortello Business Corporation (OBC).
Baada ya taarifa za kushitua za watendaji wa serikali kukiuka haki za binadamu dhidi ya jamii za kimasaai kutangazwa katika vyombo vya habari kadhaa ndani na nje ya nchini, FemAct na Mitandao ya Wafugaji, tuliamua kufuatilia kwa karibu ili kubaini usahihi wa taarifa hizo. Kati ya Agosti 19 na 23 2009, viongozi wa mashirika wanachama wa FemAct walifanya ziara maalum katika vijiji vya Ololosokwan, Soitsambu, Olorien – Magaiduru na Arash, pamoja na kutembelea kambi ya Oterloo Business Corporation (OBC) na uongozi wa wilaya ya Ngorongoro kwa lengo la kubaini na kuthibitisha kiwango na namna watendaji wa serikali wanavyoshirikiana na mwekezaji wa OBC kunyanyasa na kutesa raia wakaazi wa vijiji vilivyotajwa hapo juu.
FemAct na Mitandao ya Wafugaji wamebaini kuwa kampuni ya OBC ilipewa kitalu cha uwindaji mwaka 1992 na serikali kupitia wizara ya maliasili. Hatua hii ilipingwa kwa nguvu zote na kuibua mjadala wa kitaifa ulioitwa “Loliondogate scandal”. Kitalu hiki kiko katika eneo linalomilikiwa kisheria na vijiji vya Loliondo, hivyo wafugaji wanaishi kihalali katika eneo hilo. Aidha, imebainika kuwa serikali kwa kutumia jeshi la polisi, hususan kikosi cha kutuliza ghasia cha FFU, wakishirikiana na askari wa OBC, kuanzia mwanzoni mwa mwezi julai, wamekuwa wakihamisha kwa nguvu, raia wenyeji na wakaazi wa jamii za kimaasai kwa kisingizio cha kudhibiti uharibifu wa mazingira, bila kujali uhalali wao wa ukaazi kisheria. Kuwaondoa kwa nguvu wafugaji na wakaazi wa jamii za kimasaai katika vijiji vyao vya asili, pasipo kuzingatia uhalali wa uwepo wao, ni ukiukwaji mkubwa wa haki za raia, haki za binadamu na ukiukwaji wa sheria na katiba ya nchi.
Wakati wa ziara ya kikazi ya viongozi wa FemAct na Mitandao ya Wafugaji tumebaini na kuthibitisha yafuatayo: -
1. Kwamba oparesheni za serikali na OBC zinafanyika katika maeneo ya wakaazi ambao wanayamiliki kihalali kwa mujibu wa sheria ya Ardhi ya Vijiji ya 1999 hivyo Wamaasai siyo wavamizi kama inavyodaiwa na serikali na kampuni ya OBC;
2. Kwamba kuna ukiukwaji uliokithiri wa haki za binadamu, haki za raia na sheria ikiwa ni pamoja na kuchoma maboma (nyumba za kiasili za Kimaasai) pasipo kuwapa makazi mbadala; ubakaji na udhalilishaji wa wanawake ikiwa ni pamoja na vitendo vilivyopelekea baadhi ya wanawake wajawazito kutoka mimba, watu kukamatwa na kuteswa, chakula kuharibiwa, na mchakato nzima kutofuata sheria na taratibu;
3. Kwamba madai ya serikali na mwekezaji kuwa wananchi wa jamii za wafugaji za kimaasai wanaharibu mazingira ni madai ya uongo. Isipokuwa, uharibifu wa mazingira uliopo katika eneo la mgogoro ni ule unaosababishwa na kampuni ya OBC, kama vile kujenga kiwanja cha ndege katika mapito na mazalio ya wanyama pori, kelele zinazosababishwa na kutua na kuruka kwa ndege, kujenga majengo ya kudumu katika maeneo ya hifadhi ya wanyama, na uchukuaji wa maji kutoka katika vyanzo vya maji vya mbugani; na
4. Kwamba kuna mapungufu mengi ya taratibu za ki-sheria ikiwa ni pamoja:-
a) Uingiaji wa mikataba kati ya OBC na Serikali za Vijiji, mikataba ambao inaonyesha serikali imesaini mikataba na vijiji kwa niaba ya OBC iliyosaini kama shahidi katika mikataba hiyo.
b) Kutekwa kwa mawasiliano ya makampuni ya simu ya Tanzania katika maeneo yaliyo karibu na kitalu cha OBC ambacho hakina mipaka inayoonekana. Mfano, ukiwa eneo hilo unapata ujumbe mfupi was simu (sms) kutoka kampuni ya ETISALAT unaokukaribisha na kusema, “karibu katika Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu”.
c) Kujenga kiwanja cha ndege na kuwepo kwa mawasiliano ya Anga ya moja kwa moja kutoka eneo la kitalu kwenda nchi za nje. Kiwanja hicho hutua ndege kubwa zenye uwezo wa kubeba takribani watu mia nne na magari kadhaa.
d) Kutokueleweka utaratibu wa ukusanyaji wa kodi mbalimbali kwa sababu hakuna taarifa zinazoonyesha iwapo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yanakusanya mapato kutokana na magari yanayoingizwa na kutumika nchini yakiwa na namba za usajili wa Nchi za Falme za Kiarabu pamoja na rasilimali zinazochukuliwa moja kwa moja kupitia uwanja huo.
e) Kampuni ya OBC inapewa hadhi ya kidiplomasia na wakati ni kampuni iliyosajiliwa kama kampuni nyingine. Mfano, kambi ya kampuni hiyo inalindwa na FFU, jeshi la polisi na chombo cha dola! Aidha kuna vikundi-kazi vya serikali katika ngazi za wilaya hadi taifa vilivyoundwa kuratibu shughuli za kitalu hicho. Viongozi wa FemAct pamoja na Mitandao ya Wafugaji walikataliwa kuingia ndani ya kambi ya kampuni husika ila, badala yake, waliondoshwa kwa kusindikizwa na FFU na baadaye kusimamishwa na kuhojiwa na FFU walioagizwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Ngorongoro.
5. Kwa matukio haya FemAct inarejerea na kuthibitisha kauli yake ya Mei 22 mwaka huu kuwa dola ya Tanzania imetekwa na hivyo kuwatumikia wachache; wawekezaji wenye mitaji na hata mafisadi kwa gharama ya wananchi waliowengi wanaoteseka.
Kutokana na hayo tuliyoyabaini na kuthibitisha, FemAct na Mitandao ya Wafugaji, wanadai:
1) Serikali isimamishe mara moja oparesheni zinazoendelea kuamisha wafugaji katika Wilaya ya Loliondo na sehemu nyingine , ambazo zinakiuka kwa kiwango kikubwa haki za binadamu na za kiraia na taratibu za ki-sheria;
2) Serikali iwajibike kuchukua hatua za ki-sheria dhidi ya watendaji wake wote watakaobainika kuhusika na ukiukwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa sheria na katiba ya nchi dhidi ya wananchi wakaazi katika wilaya ya Ngorongoro;
3) Wahanga wa operasheni katika wilaya ya Ngorongoro wapelekewe misaada ya ya dharura ya kibinaadamu haraka sana iwezekanavyo, hususan maji na huduma za matibabu kwa akina mama, chakula na mahema;
4) Wahanga wote wa operesheni walipwe fidia kutokana na kuharibiwa na kupotelewa kwa mali zao;
5) Serikali iwajibike kufafanua sababu za kuipa kampuni ya OBC hadhi ya kidiplomasia;
6) Serikali itoe maelezo ya kina juu ya usimamizi na ufuatiliaji wa mapato (TRA), uendeshaji wa shughuli za mawasiliano ya simu (TCRA) na matumizi ya anga ya Tanzania (TCAA), na hadhi ya ukaazi wa wageni (IDARA YA UHAMIAJI) wanoendesha kampuni ya OBC;
7) Serikali itoe tamko rasmi kuhusu hatma ya wafugaji Tanzania; na
Serikali kutoa ufafanuzi wa kina wa mgongano wa ki-sheria kati ya Sheria za ardhi na Sheria za wanyapori, hususani Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya 1999 na Sheria ya Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro ya 1959.
9) Wanaharakati na wananchi wote katika ujumla wetu tujitokeze waziwazi kupinga vitendo vinavyofanywa na serikali dhidi ya wananchi wa jamii za wafugaji na wakaazi wengine katika wilaya ya Ngorongoro.
Page 1 of 4 | Next page