Kwa mtu yeyote ambaye anapenda fani ya utangazaji au mtu yeyote ambaye ni msikilizaji wa radio,hakuna shaka kabisa kwamba jina la Master T sio geni. Lakini Master T sio jina lake halisi. Jina alilopewa na wazazi wake ni Taji Liundi.
Yeye ni miongoni mwa watangazaji na waongoza shughuli(MCs) ambao wamejijengea jina ,kujikusanyia idadi kubwa ya mashabiki na kujijengea heshima ya aina yake katika fani hiyo maarufu. Wiki chache zijazo ndiye atakayekuwa jukwaani kusimamia shughuli nzito ya kumtafuta mrembo mpya wa Tanzania(Miss Tanzania 2009).Atashirikiana na Nancy Sumari(Miss World Africa,2005) katika zoezi hilo.
Ukimsikiliza iwe ni redioni au akiwa msimamizi wa shughuli fulani utafurahi,utajifunza,utaburudika na kisha bila shaka utakubali kwamba jamaa ana kipaji,anaipenda kazi yake,anakuthamini wewe kama binadamu na anakupenda kama msikilizaji wake. Umakini anaouweka katika kazi yake yaweza kuwa ndio siri ya mafanikio yake.
Yeye ni miongoni mwa wale watangazaji ambao licha ya kujaaliwa kuwa na sauti inayofaa kabisa kwa masuala ya utangazaji,pia ni wenye kipaji kikubwa katika masuala ya lugha.Master T anaimudu vyema lugha ya Kiswahili na pia anakipambanua vyema Kiingereza na pia huwezi kumuweka mbali na Kifaransa.Hii inamfanya akamilishe ile preamble inayosema;ukitaka kuwa mtangazaji mzuri,sharti ujitahidi sana katika masuala ya lugha.
Hivi karibuni nilipata nafasi ya kufanya naye mahojiano ambayo utayasoma hivi punde.Katika ufupi na ufasaha wa aina yake,Master T anaweka wazi masuala mbalimbali muhimu kuhusu historia ya maisha yake,heka heka za utotoni,kazi yake kama mtangazaji,harakati zake katika mwanaharakati dhidi ya ugonjwa hatari wa ukimwi,maoni yake kwa vijana na mengineyo mengi.
Je, unajua ni mkasa gani mkubwa wa kimaisha uliowahi kumkumba Master T? Unajua wazazi wake walitaka awe nani,afanye kazi gani badala ya utangazaji?Nini mtazamo wake kuhusiana na mapambano dhidi ya gonjwa la ukimwi?Fuatana nami katika mahojiano yafuatayo na Master T;
BC: Taji,kwanza kabisa asante kwa kukubali ombi langu la kufanya nawe mahojiano haya.Pole na majukumu.Mambo yanakwendaje?
MASTER T: Vyema Kaka, nami nashukuru kwa fursa hii.
BC: Natambua kwamba wengi wana ufahamu mkubwa kuhusu historia binafsi ya maisha yako.Lakini kwa faida ya wale ambao hawana habari,unaweza kuniambia kwa kifupi tu kuhusu maisha yako ya awali;ulizaliwa wapi,ukakulia wapi,ukasoma wapi na mambo kama hayo?
MASTER T: Nimezaliwa Dar, nilisoma shule ya Msingi Kisarawe pale Kariakoo kwa muda mfupi. Nikaelekea Uswiss (Switzerland) mwisho wa miaka ya 70′ ambapo niliendelea na shule ya msingi nikijifunza Kiingereza na Kifaransa. Tukahamia Zambia na dingi, nikamalizia darasa la saba.
Ikafuata Zimbabwe niliposoma form 1-2, nikaomba kurudi Bongo, nikapangiwa Ilboru Arusha, nikapiga mpaka form 3-6, nikafurahia mafunzo ya Oljoro JKT halafu Chuo cha Diplomasia mapema miaka ya 90′.

Mr.and Mrs.Taji Liundi with their daughter Upile.
BC: Kila binaadamu huwa na hadithi au mikasa ya utotoni ambayo huwa haisahauliki.Kwa upande wako,ukikumbuka maisha ya utotoni,kabla ya kufikisha miaka kumi hivi,nini huwa kinakujia kichwani kwako mara moja?Unakumbuka mkasa gani?
MASTER T: Sina kumbukumbu nzuri, tena ni ugonjwa wangu. Lakini katika udogo wangu, nakumbuka kidogo na nimehadithiwa jinsi nilivyonusurika baada ya kunywa sumu. Wadogo zangu wakafariki. Ni zamani, maisha yanaendelea.Mungu mkubwa katika mipango yake.
BC: Hivi sasa unafanya kazi wapi, kama nani?
MASTER T: Mkuu wa TBC International Radio, 90.fm Dar es salaam. Naipenda sana kazi yangu. Nafurahi pia kuwepo TBC ama Radio Tanzania ambapo mzee wangu aliwahi naye kutangaza kipindi cha Tuambie mwaka 64′.
BC: Nikikaa mahali nikaanza kukuongelea ni lazima kwanza nianze kukuongelea kama mtangazaji kabla sijarukia kwenye mambo mengine. Je nini kilikushawishi ukaamua kwamba utangazaji ndio kazi unayotaka kuifanya maishani mwako? Nani alikuvutia kuingia katika fani hii? Nini chanzo cha jina “Master T”?
MASTER T: Nilitakiwa kuwa mwanadiplomasia. Mama mzazi ndiye aliyeandika barua ya maombi ya kazi IPP. Nilienda kwenye usaili nikiwa sina wazo lolote, usingizi tu. Nikapita mara moja. Sikujua nina sauti nzuri wala nini! Nilikuwa napenda muziki balaa lakini! Nikiwa Zimbabwe, nilikuwa msikilizaji sana wa Radio 3 na msumbufu kwa madjs nikitaka wanipigie nyimbo. Nadhani dingi ndiye aliyeotesha mizizi ya mimi kuwa mtangazaji kwani aliniruhusu kuwa na radio tu! Katika ujana, nilikosa Tv, baiskeli, gari nk! Unoko wake umesaidia.
Charles Hillary aliona ni vema kunita Master na sio Mister kwani nilikuwa mdogo. Hivyo akaanza kunita Master T. Kilichofuata ni kupotea kabisa kwa jina la Taji Liundi hadi siku hizi…
BC: Tangu uanze kazi yako ya utangazaji ni wazi kwamba umeshawahoji watu wengi. Katika watu wote uliowahi kufanya naye mahojiano yupi hutomsahau kamwe? Kwanini? Na labda ni tukio gani la utangazaji ambalo unalikumbuka zaidi?
MASTER T: Dah, labda niseme Kanda Bongoman, kwani ndiye maarufu wa kwanza kumhoji alipokuja kwa mara ya kwanza Tz! Nakumbuka baada ya kipindi, Charles akaniita na kunipa Tax Invoice. Akaniambia nilipie gharama za matangazo ya kupromote tamasha la Kanda nililokuwa nalizungumzia hewani…eh! Monica Mfumia kuniita mwizi…Rankim kufukuzwa, sikufurahi. Mengi kunirudisha Radio One na kuniambia niache kuendesha vicessna wakati ROne ni Boeing, kumkacha Diallo, kusikitika kuondoka Clouds na kuacha vipindi vyangu kama Apex. Kifo cha Kiiza Kahama mtangazaji mwenzangu, kuendesha kituo cha Times hadi kilipofika, na kuangalia nyuma na kumshukuru Mungu kwa watangazaji kibao niliowapa fursa…na watu niliowagusa na wanaonipenda na wengine kutonielewa lakini kuniongelea kama wananijua fika!!
BC: Ulimwengu wa utangazaji na habari hivi sasa unakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kuingia kwa tekinolojia mpya na mbinu mbalimbali za kupashana habari kama vile blogs,facebook,twitter,myspace nk. Kwa mtizamo wako,unadhani ulimwengu wa habari na mawasiliano tuliouzoea unafaidika au unaangamia kutokana na hizi zana mpya? Unatabiri nini kitatokea katika miaka kama kumi hivi ijayo katika habari na mawasiliano?
MASTER T: Knowledge is Power, power is corrupting. Ni jinsi mtu unavyoelewa ama kutafsiri habari. Teknolojia inasogeza uwezo wa mtu kuwa na habari azitakazo kiganjani! Pia inawezesha watu kutengeneza habari na maelezo watakavyo. Inawezekana hata leo Serikali kuiangusha kutokana na maendeleo haya. Matabaka ya wenye uwezo wa kufahamu na wajinga litapanuka, siri zitanyanyasa watu na uongo utawagawanya watu. Habari ndio mfumo ujao wa maisha yetu, jiandae kuwa muelewa vinginevyo….
BC: Hivi karibuni wewe mwenyewe uliamua kuingia kwenye ulimwengu wa “blogs”.Ukaanzisha blog ambayo imelenga zaidi kwenye masuala ya urembo.Ni kwanini umeanza kublog na kwanini labda umeamua kuwa na “niche” ya masuala ya urembo?
MASTER T: Inaitwa UMODO kwenye modotz.blogspot.com. Napenda sana urembo. Sio fashion haswa. Mimi nilikuwa mchoraji, nilikuwa napenda sana kuchora maumbile. Naona uzuri katika kucha, nyusi, vidole, tumbo, makalio, goti nk. Lakini pia, naamini kwamba nchi yetu ipo katika wakati muafaka wa kibiashara kuruhusu umodo kuwa sehemu ya ajira kwa vijana wengi Tanzania. Nashauri tu kwamba tujenge upeo mkubwa zaidi wa maana ya umodo, isije ikiwa ya maumbile vimbaumbau kama wanavyopenda magharibi. Tutafsiri kivyetu, kimitindo na “malighafi zetu”. Hivi karibuni nitatafsiri maana yangu kwa onyesho/shindano langu la kwanza litakaloitwa UNIQ MODO. Tega macho na masikio…
BC: Suala la uhuru wa vyombo vya habari,uhuru binafsi wa mtu kujielezea ni miongoni mwa mambo ambayo bila shaka yatazidi kuwa gumzo kutokana na maendeleo haya ya tekinolojia na upashanaji wa habari. Unapoangalia kuhusu masuala hayo hapa nchini Tanzania; unadhani tunao uhuru wa kutosha katika vyombo vya habari?
MASTER T: Jeff, mimi sio mwandishi wa habari.I am not a journalist. Nasema ukweli na huwa natamka hivyo, nimeweza kufanya kazi katika vyombo vya habari lakini sijasomea hata chembe. Ni mbunifu tu na kwa kweli ni rahisi mno. Kwahiyo najibu kwa mtazamo wangu.
Uhuru wa habari? Uhuru wa aina gani haswa? Wa kumfichua kwa uhakika na taarifa sahihi Fisadi? Kukosoa Chama tawala kwa kukiuka itikadi? Kuainisha kiueledi matatizo ya kimkakati yanayokabili maendeleo ya jamii? Je, tunahitaji uhuru wa namna hiyo? Nani anataka kutunyima uhuru huo? Sio yule yule anayewajibika na ukweli na uwazi unaoendana na demokrasia ya kweli na utawala bora? Uhuru wa habari unaendana na ueledi wa uandishi na wajibu wa dhamana ya uongozi wa wananchi waliyoitoa kwa mtawala. Uwiano ukiwepo. Uhuru upo. Tafakari.
BC: Pamoja na utangazaji, Master T ni msimamizi mzuri wa shughuli . Je ni jambo gani ambalo unaweza kusema huwa unalihofia zaidi unapokuwa unasimamia shughuli au kwa maneno ya kigeni unapokuwa Master of Ceremony?
MASTER T: Sihofii kitu, nakuwa nimesoma na kujianda kwa shughuli kama vile muhusika mkuu! Huwezi kuendesha shughuli ya Rais Kikwete kiblah blah tu, atakuumbua! Unaweza kujenga ama kuporomosha muonekano wa mteja kwa kuboronga. Hivyo ni heshima kubwa na fahari pia kuwakilisha wateja wengi wakubwa wanaonipa fursa ya kuendesha shughuli zao.

Master T akiwa kazini.MC
BC: Kwa muda mrefu sana, wewe umekuwa miongoni mwa watu muhimu waliosimama kidete kuhakikisha kwamba muziki wa bongo fleva unakua,kuheshimika na kuchangia kwa dhati katika maendeleo ya kijamii nk. Nini hasa kilikufanya ukaingia katika harakati za kusaidia maendeleo ya Bongo Fleva?
MASTER T: Mmmh, nilijiengua kwenye muziki huo miaka kama 5 iliyopita baada ya kuona vijana hawasikilizi wala hawaambiwi, soko linapenda rushwa na dhuluma. Nafahamu kwamba nina uwezo mkubwa sana wa kuwasaidia vijana kwani nimeona mengi na nimeishi na kutembela sehemu nyingi duniani. Hivyo nilipogombana na wakuu wangu wa kazi Radio One ili wakina Jaydee waimbe hewani, nilikuwa najitoa wao wapate fursa. Nikawa nafukuzwa kazi na kuhamahama najaribu kueneza injili ya flava zao. Leo mimi naishi kama shujaa masikini wao wanatoa rushwa na kukumbatia soko hewa! Nimechoka.
BC: Hivi karibuni nilifanya mahojiano na Mr.II ambaye kama tunavyojua ni miongoni mwa wasanii wa mwanzo mwanzo kuifanya Bongo Fleva ikubalike katika jamii. Katika mahojiano hayo,Mr.II alisema kwamba muziki wa B-Fleva unahitaji “total overhaul” akimaanisha kwamba hivi sasa muziki umepoteza muelekeo. Je unakubaliana na hoja hiyo? Kama ndio,unadhani nini kinaweza kufanyika ili kurekebisha mambo?
MASTER T: Duh, baada ya maelezo yangu hapo juu, sasa nitapimwa uzalendo! Muziki sio mbaya jamani! Wabane pua au makoo, mbona Marekani wanabana na auto-tune! Ha ha ha ha! Tatizo ni SOKO. Mr 2 alinialika kuzungumza kwenye Hip Hop Summit yake, wasanii sijui walinisikia nikielezea kuhusu SOKO? Nakumbuka siku moja katika uzinduzi wa filamu fulani, nilipata fursa ya kuzungumza mbele ya Waziri wa Utamaduni, nikamwambia, afungue milango yake tuende tukashauriane kuhusu nini kifanywe juu ya SOKO. Hakujibu. Kimya hicho ndicho kitanzi cha muziki huu wa vijana wetu hadi leo. Ukijumuisha na teknolojia ya kushusha muziki kwenye mtandao, nashindwa hata jinsi ya kushauri tufanyeje!
BC: Kwa mapana na marefu umejihusisha na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi.Umewahi kuwa Kamishna wa Tume,Mwanaharakati asiyechoka katika mapambano. Ukiangalia tangu ulipojitosa katika mapambano haya,kumekuwepo na maendeleo gani? Tunaelekea kuishinda vita hii au safari bado ni ngumu?
MASTER T: Jitihada na fedha tele. Nahisi hatushindi lakini pia najua wapo wanaookoka kwa kuwa wasikilizaji na watekelezaji wa ujumbe sahihi zinazotolewa. Mabadiliko ya tabia ni muhimu sana! Sio rahisi lakini nilazima tuwe wajasiri wa kupinga hisia zetu na kutumia njia bora za kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU. Kupima ni njia moja madhubuti. Mh. Rais anatakiwa kuendelea na kampeni yake kwa KASI na ARI. Hakurudi kupima baada ya miezi mitatu! Kwa kweli, na humu ningeweza kuendelea kufanya kazi ya kuelimisha kitaifa. Lipo jeshi la vijana wengi mahiri waelimishaji rika nchi nzima, wawezeshwe.
Naamini utegemezi wa wahisani ni muhimu katika maeneo nyeti lakini kama ni kufikia wananchi, ni jukumu letu wenyewe. Vyama vya siasa, mashirika, makampuni na asasi ziongeze bidii. Tuwe na mpango kabambe wa kupambana vijijini. Mkakati wa kupunguza maambukizi mijini. Kuna vijana wengi ambao hawakunisikia nikielimisha Ukimwi redioni miaka 7 iliyopita, leo wanahitaji kuelimishwa, vipindi vya nguvu havipo hewani. Siri ni elimu. Wala sio magunia ya pesa! Ugumu wa mapambano ni mafisadi wa raslimali za mapambano dhidi ya UKIMWI!
BC: Maendeleo ya tekinolojia yanamaanisha kupatikana kwa urahisi habari ambazo hapo awali ilikuwa ngumu kuzipata.Hivi leo,kwa mfano,kupitia mitandao, vijana wengi wanaweza kuona vitu kama pornography nk.Unadhani nini kifanyike ili kukabiliana vyema na maendeleo haya ya kitekinolojia hususani katika uhusiano wake na mapambano dhidi ya ukimwi?
MASTER T: Hakuna sehemu duniani ambapo wanashinda vita dhidi ya pornography. Kupigana na moto kwa moto ni kuukuza moto. Kwanini tusiwaelimishe vijana madhara ya kisaikolojia yanayoweza kutokea kwa kujikita kwenye mitandao ya ngono? Tusiwatishe. Kila kijana anataka kuona au kuchungulia utupu akifikia umri fulani, ni natural. Mimi niliangalia na naangalia, lakini hainiathiri kwa vile nimeiweka kwenye kabati maalumu kwenye ubongo wangu la kujiliwaza kingono. Tena sipendi ngono ya moja kwa moja, bora ile inayonifundisha jinsi ya kufurahia tendo zuri la ngono na mke wangu! Sawa?!! Dingi alikomea sehemu tu katika maelezo yake…nani angenifunda zaidi?

To be able to love people,you have to love nature first.People are products of nature.
BC: Mara nyingine katika mapambano makali kama haya dhidi ya Ukimwi,huwa inaweza kutokea kukawa kuna jambo ambalo umelifanyia utafiti binafsi na kuamini kwamba linaweza kuwa suluhisho lakini kila unapojaribu kulisema hakuna anayeelekea kusikia. Je kwako wewe hiyo imeshawahi kutokea? Ni jambo gani?
MASTER T: Nchi yetu iwekeze kwa vijana. Elimu ni swala nyeti. Elimu rasmi, elimu ya vitendo na maarifa ili vijana waweze kujishughulisha na kazi mbalimbali. Fursa za maendeleo katika michezo na kazi za sanaa zizingatiwe. Vijana wengi wanaweza kuvumbua vipawa na vipaji vyao. Tukuze utamaduni wetu ili vijana waitangaze nchi, kwa sanaa za maonyesho, sinema, uchoraji, uchongaji na uundaji samani. Naamini pia kwamba sekta ya hudumua ni muhimu sana na vijana wengi wanaweza kuajiriwa, vijana wa Kenya na Uganda(hata Malawi) wanatupiku mf. mahotelini.
Kaka, hapa naweza gombania urais kwa hoja mbalimbali…nadhani naeleweka kiasi.
BC: Taji anapokuwa hayupo hewani,anapokuwa hayupo katika shughuli yeyote ya ki-uanaharakati ni mtu wa aina gani? Au nikiwauliza rafiki zako wa karibu kuhusu wewe unadhani watasema nini?
MASTER T: Naishi a very private life, inatisha na pia ni faraja kujulikana kwa kiwango changu, huwa najishtukia nikiwa katikati ya watu wengi, nakuwa huru ninapokuwa jukwaani! Napenda sana kucheza soka hivyo nipo uwanjani ofisini ama Kiwanja cha Garden Kino, au Leaders weekend na timu ya Mango. Jumapili naenda Ocean Road kucheza kikapu. Ama nipo sehemu na mamodo tunapiga picha kwa ajili ya blog. Sometimes nazuka kiwanja chochote kile uzunguni ama uswahilini!
Napenda pia kutumia muda na familia ikiwa Mamsup hayuko busy na mwana naye hana mitikasi yake. Vinginevyo, naangalia filamu kwa sana, soka la Arsenal na video za muziki ama nawasha laptop na kurambaza mtandao! Niko simple sana.
BC: Watu wengi wanaweza kusema wewe umeshatimiza ndoto zako kwa kiasi kikubwa. Lakini bila shaka wewe mwenyewe unaweza kuwa na ndoto ambayo bado haijatimia na ungependa itimie siku moja. Ipo?Unaweza kuniambia ni ndoto gani hiyo?
MASTER T: Yes, now I wanna make money!
BC: Kwa ujumla una ushauri gani kwa vijana kuhusiana na suala zima la maisha na mafanikio?
MASTER T: “Acha kufanya yale ambayo yanakuvutia sana sasa, ili utekeleze yale ambayo yataongeza tija na faraja katika maisha yako!”
BC: Ni watangazaji gani ambao unapenda kazi zao hapa duniani? Kwanini?
MASTER T: Duh, Kaka, huwa sina hizo sana. Larry King ni yeye, Oprah ni pekee, Mike Embley, Muhagama, Seba, Nyaisanga, GG, PJ, Joan, Fredwaa, Kipozi, Tido, Sanga, Amanpour, Ducet, Degeneres, Zee A, Gardner, Salama nk,mimi, wote tunatakiwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa vipaji vinavyogusa mamilioni ya watu. Ni nadra na baraka tele!!
Sifa kuu ni muono wa mbali, ubunifu, umahiri na ustadi mkubwa kila siku!
BC: Asante sana kwa muda wako Taji.Nakutakia kila la kheri katika shughuli zako.
MASTER T: Amen! Ahsante tena kwa fursa hii na natumaini majibu yangu ni stahili.
Feedback / Comments
23 Responses to “AN OPEN CHITCHAT WITH MASTER T”
Leave a Reply


sending...
One of a kind.He is my mentor and my brother.Thanks “Master T” for everything! I hope we will get a chance to team up again and do our thing man as we used to.
Regards to Upile & Lily.
Mike Mhagama../LA.
Huyu ni kati ya watangazaji WACHACHE wenye kufikirisha na kufikiri saana.
Master T ni kati ya wachache wanaoweza kufanya mahojiano ukaona undani wa uelewa wao.
Kama anavyosema, Master anajiandaa na ndio maana anaonekana kuwa na UPEO WA JUU katika kuongea na kuhoji.
Huyu NAMHESHIMU SAANA KATI YA WATANGAZAJI WA KIZAZI CHAKE. Kuna wasiogusika kama kina Mr Charles Hillary.
Big Up Master na elimu na msaada wako kwetu utaendelea kuheshimika milele.
Blessings
HI MASTER T,
HUYU JAMAA HUWA YUKO JUU SANA, YAANI MSHKAJI ANAKIPAJI FURANI HIVI NA UELEWA WA HALI YA JUU, EMBU ANGALIA MTU ANAVYOJIBU MASWALI ANAYOULIZWA NA BC, YAANI HUYU JAMAA YUKO SERIOUS. MIMI KWASASA NINA ELIMU ZA CHUO KIKUU LKN NAKUMBUKA HUYU JAMAA NIMEANZA KUMUONA TOKEA NIKO O LEVEL, KIPINDI KILE ANAANDAA MATAMASHA YA MUZIKI WA GWM (GANG STARS WITH MATATIZO) PALE JITEGEMEE, KIPINDI AMBACHO KINA JUMA NATURE KIROBOTO NDIO KWANZA MAKINDA, LKN JAMAA ALIKUWA KICHWA MNO MIAKA HIYO AMBAYO KINA FID Q BADO WAKO BUSH HATA HAWAJULIKANI WALIKO, LKN HAUWEZI AMINI MPAKA LEO JAMAA BADO YUKO NONDO MBAYA. KWELI HUU UTANGAZAJI NA UWANAHABARI NI KIPAJI, SIO LEO KUNA WATANGAZAJI WANAIBUKA TU FROM NO WHERE HATA WANACHOKIFANYA HAKIJULIKANI WAMEKALIA MAJUNGU TU NA KUHARIBU JAMII, MTANGAZAJI ANAITWA DIDA SIJUI, MAIMATHA SIJUI, YAANI KILA KUKICHA WAO NI SKENDO TU, MALA LEO KAFUMANIWA, MALA ATOE PESA KWA WAANDISHI WA HABARI WAMUNDIKE, YAANI FULL MATATIZO, LKN HUYU JAMAA TOKEA ZAMANI MNO YUKO NA SIFA ZAKE ZILEZILE NA KAMWE HAUMKUTI NA SKENDO ZA KINA DINA MARIOS.
BROTHER MASTER T MI SINA LAZIADA ILA KAZA BUTI TENA NAKUOMBA SANA KAMA HAUKO BUSY EMBU ULUDIE MZIKI WA BONGO FLEVA KWANI VIJANA WAMECHOKA MBAYA, YAANI HAWANA MUONGOZO KABISA, SIO KAMA KIPINDI KILEE WEWE NA WADAU WA UKWELI MPO KTK GEMU. LEO HII DUDUBAYA AKISHATOA MZIKI MMOJA TU MZURI ANATAKA KUNUNU BAROON BILA HATA YA KUJUA PESA YA MAFUTA ATATOA WAPI, SASA UTAMUONA ANATESA MUDA MFUPI TU KISHA ANARUDI KWENYE MSOTO, KINA MR. NICE YAANI NI CHOKA MBAYA, EMBU WADAU KAMA WEWE RUDINI JAMANI ILI HAWA MADOGO NAO WAWE NAMAISHA MAZURI KAMA SISI WENZAO. HATUWAAMBII WARUDI SHURE WAKACHUKUE DEGREE LKN BADO WAKIWA NA UELEWA KAMA WENZAO KINA MR.II MBONA KITAELEWEKA TU, LEO ANGALIA KINA MR.II AMBAO WEWE ULIANZA NAO TOKEA KIPINDI KILE MPAKA LEO WANAMAISHA YANAYOELEWEKA INAMAANA NYINYI MLIKUWA MNAWAPA MISINGI MIZURI, LEO HII KILA MTANGAZAJI WA REDIO ANATAKA AWAMILIKI WANAMUZIKI NA AWE MENEJA WAO, JAMANI UMENEJA NI KAZI TENA WATU WAMEZISOMEA, JAMANI ACHENI NJAA ZENU HIZO. WEWE UTAKUWAJE MENEJA WAKATI HATA KUJIMANGE MWENYEWE HAUWEZIIII, JAMANI HIZO NI FANI JAMANI. BROTHER MASTER T WACHANI HASIRA RUDINI KUWASIADIA HAWA VIJANA KWANI WANAZIDI KUFURIA SIKU BAADA YA SIKU.
OK ROTHER KEEP IT UP
IS ME YOUR YOUNG BROTHER MUDDY.
jamani huyu master t mimi nilianza kumsikia toka niko mdogo habari za kunywa sumu nilisikia toka kwa kaka zangu waliokuwa wakisoma kisarawe nikakua nikapataa nafasi ya kumjua kwa kweli ni kichwa, kaka nakupa hongera sana kwa bidii zako kwa kuwa kila unapotangaza unanigusa sana na mapoint ya maana maana huongei pumba hata siku moja big up!!!!!!!!.
Hiyo inaitwa “citizen journalism”—usisema online journalism, haitakuwa inatosha. Nakupngeza sana sana kwa kuanzisha blog hiyo.
ONYO:
Kuna changamoto kubwa ya ku-maintain blogs. Please hakikisha haiishii kuwa archive.
Make sure inakuwa up-dated na improved daily.
Otherwise,bravo.
Mpe hi Bw. Mike Mhagama…hivi yuko wapi huyo jamaa…??
Kivamwo, AS
kivamwo@yahoo.com
Ni kweli anaipenda kazi yake, , mimi nimeanza kumskiliza kipindi kirefu sana , wakati ule akiwa mwanza, ninakutakia kazi njema
Mungu akubariki sana
Your are the best MC i have ever known! Congrats!
Jamaa mkali sana, yani ukusikia jina lake kwa wale wanaoijua vizuri fani lazima utataka kujua zaidi.Nilianza kumsikia jamaa nilipokuwa secondary long time sasa niko mbali lakini namheshimu sana huyu mtu kwa kazi yake na jinsi alivyo makini.Hongera sana Bro.
Mh pole sana na tukio la kunywa sumu nilijua hilo baada ya kuwa MC katika mahafali yangu ya kumaliza chuo kukuu Mlimani, nilisoma case yenye jina la Liundi then nikahiji mbona majina yanafanana ndipo nilipojua kumbe ndio yeye. Pole sana ndugu yangu mungu alipenda ubakie duniani ili ukuze kipaji chako. Congrats
I like the guy…lo0ng time in the game…what a wonderful consistent!!..God bless u pal
hongera sana
Taji Liundi.Nimefurahi kusoma mahojiano haya. Hongera kwa majibu mazuri na kwa kuwa Mkuu wa TBC Radio, unastahili.
Mungu akulinde.
Master T.
Kuna vitu vingi sana ambavyo naweza kuvikumbuka kuhusu ufanisi na maono ya Taji hasa kwa kulenga vijana ila hivi viwili sitavisahau, Moja. Kuanzisha kipindi cha Apex Pale Clouds FM, hiki kilifungu platform ya vijana kuongelea masuala yanayowahusu hasa ya mahusiano na VVU/UKIMWI, leo tunakisikiliza kile kipindi kama njia panda, kazi ilikuwa kubwa sana nakumbuka. Pili, zile talent show za FM Club Kino pale, Jamaa alizihangaikia sana, nakumbuka bongo superstar mmoja wa leo, TID, alikuwa anapanga vijana ili wafanye free style yeye akiwa kama lead MC bila ujuzi sana ila leo ni big time performing artist na wengine wengi. Jamaa ameitendea haki fani ya muziki wa kizazi kipya na sacrifice yake kazini alikopitia, leo imewapa vijana wa kibongo nafasi ya kuishi kwa muziki, jamaa ni mwanaharakati makini
Best Man, You are the best. DD
That’s a fantastic interview, well, i’v known Taji Liundi as one of the best radio presenter in the country, always on the front_line campaigning against the spread of HIV as well as educating youth abt AIDS preventation, also his contribution toward recognition of BONGO FLEVA, has a very big impact in its successiful scenario, bt i believe, that was his call frm GOD, and he achieved it 2 a greater extent. GOD bless u ma brother.
Hi Master T..
Mahojiano ni mazuri hongera kwa kua mkubwa wa radio tz…nimemshangaa sana bint yako jamani amekua mkubwa namkumbuka alikua anasoma na mwanangu pale hekima mikocheni…congrats sana!
You the meaning of citizen journalism, firt and foremost, a person is called a citizen journalist not journalism. KWA KISWAHILI INA MAANA NI KWA MTU NI MWANDISHI RAIA, KIFAN NI UANDISHI WA KIRAIA, INA MAANA NI MTU TU WA MTAANI AMBAYE HAJASOMEA UANDISHI WA HABARI NA WALA AFANYA KAZI ZINAZOHUSIANA NA MASWALA YA HABARI LAKINI HUWA ANACHANGIA AMA KUTOA HABARI AU KUPELEKA HABARI KATIKA VYOMBO VYA HABARI BILA MALIPO YAANI BURE KAMA HOBBU HIVI. MTU ANAYEFANYA KAZI KATIKA CHOMBO CHA HABARI HUWEZI KUMUITA CITIZEN JOURNALIST AS HHIS OR HER JOB AND BEING PAID FROM THAT
Jmaaa yupo juu sana kwa kipaji. mimi nimeanza kumfahamu nikiwa nasoma Kibaha High School akiwa Times fm kuanzia mida ya saa nne kama na robo hivi usiku nikishatoka “Prepo” alikuwa na kipindi chake cha Pillow talk….dah huyu jamaa ni noma jamani…hilo tu ndilo linalonifanya nisimsahau kamwe…muwazi sana.
Siku moja litoa assignment ya mtu kutafuta G-Spot kwenye va***a…dah watu walimbwelambwela sana
Big up MASTER
Mr T Big Up unafanya kazi nzuri sana nakumbukia enzi zetu ITV KEEP IT UP!
you are doing good man! wish you lucky in everything you do
big up masta p yo shows n chats on radio gives me encouragement n ope 4 better things in ma life ,kaka am tryin to get ma self movies(acting n scriptwriting) but ma weakness is i don’t undastands wat producer look 4 during auduitions .pliz bro u been thro this stuff help me some guidlines asante….. te^darlin
Taji.. umekuwa mwanga kwa vijana wa Kitanzania ndani na nje ya nchi… Uongozi wako wa kimawazo na vitendo daima utakumbukwa….Mungu aendelee kukuongoza katika maisha yako….akulinde na kukujalia neema teleeeeeee!!!
ur shem jay..
uko juu sana bro since nakusoma keep it up