Nilipokuwa kijana zaidi,miongoni mwa wanamuziki niliopenda kuwasikiliza alikuwa ni Sade.Niliupenda zaidi wimbo wa Smooth Operator Enzi hizo sikujua kama Sade pia ni jina la bendi anayoiongoza ambayo inabeba jina lake.
Huyu ni mzaliwa wa kule Ibadan,Oyo State nchini Nigeria aliyekulia nchini Uingereza.Wazazi walikutana nchini Uingereza kisha baadaye wakaenda kujaribu kuishi nchini Nigeria.Mambo hayakuwa mambo na hivyo akiwa bado kinda kabisa akarejea Uingereza na mama yake.Jina lake halisi ni Helen Folasade Adu na alizaliwa tarehe 16 Januari mwaka 1959.
Baada ya miaka kadhaa yenye mafanikio makubwa katika muziki,Sade walipotea.Sasa mwaka huu,mwezi wa Februari,wanarudi.Albamu inaitwa Soldier of Love.
Leo tukiwa katika siku ya mwisho ya mwaka 2009 na tukijiandaa kuingia mwaka mpya wa 2010, tumepatwa na habari za msiba wa Kiongozi mwanzilishi wa Taifa letu Simba wa Vita Mzee Rashidi Mfaume Kawawa. Kwa Mtanzania yeyote kifo hiki ni pigo kubwa sana, lakini pia ni fursa ya kukumbuka vyema historia ya Tanganyika na Tanzania. Ni fursa ya kuona Watanzania waliojitoa kuona kuwa kunakuwa na Taifa kutoka miongoni mwa nchi iliyokuwa ni mkusanyo tu wa makabila zaidi ya 120. Watu waliojitoa bila kuwa na uzoefu wowote wa si tu kuongoza serikali bali muhimu zaidi uzoefu wa kukusanya makabila, dini na wasio na dini na kuunda Taifa moja imara na la kujivunia linaloitwa Tanzania. Mzee Rashidi Mfaume Kawawa ni mmoja wa watu hawa waliorithi kutoka kwa mkoloni mwingireza nchi iliyokuwa na wakazi takribani milioni 8, isiyo na chuo kikuu hata kimoja, yenye madaktari wawili tu na isiyo na mfumo kabisa. Uhai wa mzee Kawawa, kuwepo kwake na kupumua kulitupa ahueni kuwa tunapo pa kukimbilia na kujifunza kama lolote lingetokea.
Mzee Kawawa ni mfano wa kuigwa kuhusu maana halisi ya utumishi wa Umma. Alikuwa jemedari wa kutegemewa katika utekelezaji wa Dira na ajenda za kujenga Taifa bila kujali maumivu yake kisiasa. Sisi vijana tuliozaliwa miaka ya sabini mwishoni mpaka themanini hatukuona kwa jicho la kuelewa kipindi kigumu cha ujenzi wa Taifa na ujenzi wa Ujamaa nchini. Hata hivyo tulikuwa tukisikia wakubwa wakizungumza na kummlaumu sana Mzee Kawawa kutokana na utekelezaji wa sera mbalimbali kana kwamba zilikuwa ni zake na sio maamuzi ya vikao vya TANU na Serikali iliyokuwa inaongozwa na TANU. Tukiwa masomoni tumejifunza kuwa (more…)

Happy New Year! Kheri Ya Mwaka Mpya! Naam ni mwaka 2010,karne ya 21.Binafsi napenda kukupa pongezi kwa kuumaliza mwaka 2009 na kuingia mwaka 2010.
Nakupa hongera nikiwa na sababu nyingi.Baadhi yake ni kwamba,kwa wengi mwaka 2009 ulikuwa ni mgumu kupita kiasi.Hali mbaya ya kiuchumi iliyoikumba dunia,ni sababu tosha ya kuufanya mwaka 2009 kuwa mgumu.
Isitoshe,tumepoteza wapendwa wetu wengi,ndugu,jamaa na marafiki.Mfano ni hivi leo,tunaomboleza kifo cha Mzee wetu,Rashid Mfaume Kawawa. Maradhi mbalimbali,mengine yakiwa mapya kama vile H1N1 (homa ya mafua ya nguruwe),yaliikumba dunia na kuleta mtikisiko wa aina yake.Hofu ikatanda ulimwenguni.Wengi wamepoteza maisha katika vita na mashambulizi ya kigaidi na kujitoa mhanga.
Wakati bado tunatafakari yaliyojiri katika mwaka 2009,naukumbuka msemo wa wahenga wetu.Yaliyopita si ndwele,tugange yajayo.Ni mwaka mpya na ni nafasi nyingine ya kuanza upya,kuweka malengo mapya,kumalizia ya zamani.Ni wakati wa kujipanga upya kuzikabili upya changamoto mbalimbali za maisha na ubinadamu.
Unapouanza mwaka mpya na kama unataka au umeshajiwekea malengo, kumbuka yafuatayo;
- Orodhesha malengo yako. Tafuta mahali penye utulivu.Chukua kalamu na karatasi kisha orodhesha malengo yako.Kisha pembeni ya malengo,orodhesha mambo ambayo unatakiwa kufanya(actions) ili kutimiza malengo uliyoorodhesha.Jaribu kuorodhesha malengo machache.Kumbuka mtaka yote,hukosa yote.
- Weka malengo halisi.Je malengo uliyoorodhesha hapo juu ni halisi? Ninaposema halisi namaanisha weka malengo yanayokabilika.Usiweke malengo yaliyozidi kiwango au yasiyotimia kimsingi.Kwa mfano,ukiweka malengo kwamba mwaka huu unataka kuwa tajiri kupita watu wote duniani wakati hivi leo akiba yako benki ni ya kiwango duni,utakuwa unaweka malengo yasiyo halisi.
- Jiamini kwamba unaweza kutimiza lengo/malengo yeyote uliyojiwekea.Kujiamini kunaenda sambamba na imani.Ukiamini kwamba inawezekana,utaweza.Kama sio leo basi kesho.Piga taswira kichwani kwako jinsi itakavyokuwa ukitimiza malengo yako.
- Fanya tathmini ya mara kwa mara juu ya malengo yako na mwenendo mzima wa kuyatimiza.Ukiona hauelekei kuyatimiza,usiingiwe na hofu ya kuyafanyia marekebisho.Siku hazifanani na mazingira hubadilika.Malengo pia yanaweza kubadilika.
- Mwambie ndugu au rafiki wa karibu kuhusu malengo yako.Naelewa…unataka malengo yako ya mwaka huu yabakie siri.Ninachotaka kukuambia ni kwamba unapomwambia ndugu au rafiki yako wa karibu unayemwamini kuhusu malengo yako,unakuwa umejipatia msaada.Ndugu au rafiki huyo atakuwepo kukukumbusha au kukusaidia,kwa njia moja au nyingine,kutimiza malengo yako.Isitoshe,kwa kumwambia ndugu au rafiki,unakuwa umejitilia chachu ya kutimiza malengo yako.Utaonekanaje kama mwisho wa mwaka utakuwa hujatimiza yale uliyotaka kutimiza? Binadamu tumeumbwa na soni.Itumie.
- Orodhesha watu wa kukusaidia. Kutimiza malengo kunaweza kuwa kitu kigumu.Unaweza kuhitaji msaada ili kutimiza malengo.Usisite kufanya hivyo.Weka mahali orodha ya watu ambao unadhani wanaweza kukusaidia pindi utakapohitaji msaada katika kutimiza malengo yako.Wengine wanaweza kukusaidia kimawazo au kimtazamo(role models).Watumie ipasavyo.
- Jipongeze. Kutimiza lengo au malengo ni jambo la furaha.Linastahili pongezi.Kila unapotimiza lengo au malengo fulani,usisahau kujipongeza.
- Usisahau kumweka Muumba mbele. Hata kama huna imani,huamini wala kuabudu kufuatana na dini au dhehebu lolote,bila shaka tunakubaliana kwamba yupo aliye juu,aliyetuumba.Usimsahau.
Nakutakia kila la kheri katika mwaka mpya wa 2010. Enjoy.

Mzee Rashid Mfaume Kawawa,amefariki! Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari zikiwemo blogs,Mzee Kawawa amefikwa na mauti katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili ambako alikuwa amelazwa.
Rashid Mfaume Kawawa alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza nchini Tanzania na baadaye kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi.Alizaliwa mwaka 1926 katika kijiji cha Matepwende Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Tanzania. Alianza elimu ya Msingi huko Liwale -Lindi mnamo 1941 – 1942 na kuendelea na masomo ya sekondari katika shule ya Dar es Salaam Secondary School.
Ni hivi karibuni tu Mzee Kawawa alizindua kitabu kinachoelezea maisha yake.
Majuzi Rais Kikwete na mkewe Salma Kikwete,walikwenda Muhimbili kumuona Mzee Kawawa.Laiti wangelijua kwamba hawatomuona tena Mzee Kawawa akiwa hai!
Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi ambayo imetolewa,Mzee Rashid Mfaume Kawawa anatarajia kuzikwa Jumamosi nyumbani kwake Madale nje kidogo ya jiji la Dar-es-salaam.
Mwili wa marehemu Mzee Rashid Mfaume Kawawa ukitolewa katika hospitali ya rufaa ya Muhimbili kwenda kuhifadhiwa katika hospitali ya jeshi ya Lugalo.Anayesikika akilia kwa uchungu ni mkewe Asina Kawawa.

Rashid Mfaume Kawawa enzi za ujana wake.
Utumishi wa Mzee Rashid Mfaume Kawawa kwa taifa letu ni wa siku nyingi.Pichani kulia anaonekana akishuhudia Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akichanganya michanga ya ardhi ya Tanganyika na Zanzibar kuashiria Muungano.Hiyo ilikuwa ni mwaka 1964

Mwanamuziki Ambwene Yessayah au maarufu kama AY,anakusalimia na kukutakia Kheri ya Mwaka Mpya! Ametuagiza tufikishe ujumbe na sisi bila kinyongo na kwa sababu ni wajibu wetu kukupa habari tunawasilisha.
Yeye mwenyewe yuko wapi? AY yupo nchini Rwanda katika jiji la Kigali.Hapo ndipo atakapoukaribishia mwaka mpya. Anasema show ya kwanza anaifanya usiku wa leo,yaani mkesha wa mwaka mpya ndani ya Top Tower Hotel na kesho anatarajia kuuanza mwaka mpya pale katika Uwanja wa Amahoro.
Katika maonyesho hayo,AY ataperform na wasanii wengine kutoka Afrika Mashariki kama vile Farias(Burundi),Amani(Kenya),HB Toxic(Uganda),K8(Rwanda) na wengine wengi.Nchini Rwanda,AY ameongozana na Producer wake Hermy B.
Kila la kheri AY.

Zimebaki siku chache tuumalize mwaka 2009 na kuingia mwaka 2010 ambao kwa mujibu wa katiba ya nchi yetu,ni mwaka wa kupiga kura ili kumchagua tena mtu atayeongoza jahazi la nchi yetu kwa miaka mingine mitano.Tunauita mchakato huo “demokrasia”.
Tunapoelekea kwenye mwaka wa uchaguzi,tayari vibweka vya wanasiasa vimeshaanza kujitokeza.Nimesahau sio wanasiasa tu,hata wanajimu kama kina Sheikh Yahya.Wanasiasa wameanza kujitokeza na kumkingia kifua Rais aliyepo madarakani,Jakaya Mrisho Kikwete. Hawataki aguswe.Hawataki kusikia mtu anasema Kikwete alitoa “ahadi hewa” aliponadi sera ya maisha bora kwa kila mtanzania. Alijua haiwezekani lakini hakujali.Akajivika ngozi ya ukweli ya uanasiasa.Longolongo.Mageuzi huhitaji muda ati!
Miongoni mwa wanasiasa waliojitokeza ni Augustine Lyatonga Mrema. Anasema kama watu wanataka kumpinga JK basi waanzishe vyama vya siasa ili wawe wapinzani.Huna haki ya kumpinga Rais kama hujavaa kofia ya upinzani! Kuwa mwananchi,mzalendo,msema kweli na mpenda maendeleo haitoshi.Anzisha chama.
Mrema anatumia mbinu ya utaratibu.Anasema kama upo ndani ya CCM na unataka kumkosoa Rais,basi fuata utaratibu wa vikao vya chama na sio hadharani.Vikao vya chama huwa vinafanyika in closed doors! Kwa Mrema,hiyo ndio demokrasia ya kweli.Hajali kitu kinachoitwa Uhuru wa Habari na Uhuru wa Kujielezea.
Huyu ndie mpinzani ambaye huenda akawania Urais hapo mwakani!Ni Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Tanzania Labor Party(TLP).Watabiri wa masuala ya siasa wanasema Mrema keshakwisha kisiasa.Sasa anatapatapa.Ujumbe wangu kwa Mrema ni kwamba Mzee hatuendi hivyo.Wacha watu waseme,wajielezee.Kama JK kakosea,lazima aambiwe.

Kwa niaba ya timu nzima ya BC,napenda kuchukua nafasi hii kukutakia kila la kheri katika wakati huu wa kusherekea sikukuu ya Christmas.Utumie wakati huu kuwa karibu na wale uwapendao na pia kupumzika kidogo kama inawezekana.
Pia ni wajibu wetu kukumbushana; Usiendeshe gari kama umekunywa.Ni hatari kwako binafsi,abiria wako na watumiaji wengine wa barabara.
Jizuie.Ikishindikana kabisa,tumia kinga.Tunakupenda.
Christmas Njema.
MTABIRI maarufu wa Afrika Mashariki, Shehe Yahya Hussein ametabiri kuwa Rais Jakaya Kikwete atashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao na atakayempinga ndani ya chama chake atakufa ghafla.
Sambamba na hilo, atakayeonekana kumshinda nje ya chama chake pia atapoteza maisha vivyo hivyo.
Akitoa utabiri wake jana Dar es Salaam, juu ya uchaguzi mkuu mwakani, Shehe Yahya alisema ushindi wa Rais Kikwete unatokana kurithishwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1995 ilipodaiwa kuwa Rais Kikwete alishinda kwenye kura za maoni lakini akamsihi amwachie Benjamin Mkapa.Kwa undani wa habari hii bonyeza hapa.
Je huu unaweza kuuita “utabiri” au ni…Unakubaliana naye ?Kwanini ?
Pichani juu ni Sheikh Yahya akiwa nyumbani kwake mapema mwaka huu.Ubavuni mwake ni mkewe Bi.Fetty

Mapenzi kati ya wanamuziki mashuhuri,wanandoa, Beyonce Knowles na Jay-Z yanazidi kukolea. Katika kuthibitisha hilo,wapenzi hao wameamua kubadilisha au tuseme kubadilishana mpaka majina sasa!
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Star la nchini Uingereza,hivi punde Jay-Z ambaye jina lake halisi ni Shawn Carter atakuwa anajulikana kama Shawn Knowles-Carter huku Beyonce atakuwa akijulikana kama Beyonce Knowles-Carter.
Wakati Beyonce na Jay-Z wanaendelea kukoleza penzi,mambo hayaendi vizuri kwa wazazi wa Beyonce,Tina na Mathew Knowles kwani hivi karibuni mama yake Beyonce ameomba talaka kutoka kwa mume wake huyo kwa miaka 29 iliyopita.Kisa na mkasa? Baba yake Beyonce inasemekana “amechapa nje” na kwamba anatarajiwa kuwa baba kwa mtoto wa nje ambaye bado hajazaliwa. Mwanamke anayemshtaki baba yake Beyonce anaitwa Alexandra Wright.

