MY TANZANIA   |   PLACES TO GO   |   MEDIA   |   ONLINE ENTERTAINMENT    

Kabwe12Leo tukiwa katika siku ya mwisho ya mwaka 2009 na tukijiandaa kuingia mwaka mpya wa 2010, tumepatwa na habari za msiba wa Kiongozi mwanzilishi wa Taifa letu Simba wa Vita Mzee Rashidi Mfaume Kawawa. Kwa Mtanzania yeyote kifo hiki ni pigo kubwa sana, lakini pia ni fursa ya kukumbuka vyema historia ya Tanganyika na Tanzania. Ni fursa ya kuona Watanzania waliojitoa kuona kuwa kunakuwa na Taifa kutoka miongoni mwa nchi iliyokuwa ni mkusanyo tu wa makabila zaidi ya 120. Watu waliojitoa bila kuwa na uzoefu wowote wa si tu kuongoza serikali bali muhimu zaidi uzoefu wa kukusanya makabila, dini na wasio na dini na kuunda Taifa moja imara na la kujivunia linaloitwa Tanzania. Mzee Rashidi Mfaume Kawawa ni mmoja wa watu hawa waliorithi kutoka kwa mkoloni mwingireza nchi iliyokuwa na wakazi takribani milioni 8, isiyo na chuo kikuu hata kimoja, yenye madaktari wawili tu na isiyo na mfumo kabisa. Uhai wa mzee Kawawa, kuwepo kwake na kupumua kulitupa ahueni kuwa tunapo pa kukimbilia na kujifunza kama lolote lingetokea.

Mzee Kawawa ni mfano wa kuigwa kuhusu maana halisi ya utumishi wa Umma. Alikuwa jemedari wa kutegemewa katika utekelezaji wa Dira na ajenda za kujenga Taifa bila kujali maumivu yake kisiasa. Sisi vijana tuliozaliwa miaka ya sabini mwishoni mpaka themanini hatukuona kwa jicho la kuelewa kipindi kigumu cha ujenzi wa Taifa na ujenzi wa Ujamaa nchini. Hata hivyo tulikuwa tukisikia wakubwa wakizungumza na kummlaumu sana Mzee Kawawa kutokana na utekelezaji wa sera mbalimbali kana kwamba zilikuwa ni zake na sio maamuzi ya vikao vya TANU na Serikali iliyokuwa inaongozwa na TANU. Tukiwa masomoni tumejifunza kuwa yeye ndiye alikuwa mtekelezaji mkuu wa maamuzi magumu chini ya Mwalimu Nyerere. Katika kutekeleza huku alibeba lawama za kisiasa, hakujali. Hakutikisika. Muhimu zaidi alimkinga Mwalimu Nyerere kwa yeye kubeba lawama zote za utekelezaji wa maamuzi yote ya chama. Aliweka Taifa mbele ya maslahi yake ya kisiasa. Simba wa Vita alichukulia uongozi katika mantiki ya utumishi haswa na sio katika mantiki ya sasa ya uheshimiwa. Hili ni jambo kubwa la kujifunza.

Maisha ya Mzee Kawawa Kisiasa na Kiuongozi yanawakilisha taathira ya Utanzania kwa maana ya Utu na Usawa bila ya kutumia madaraka yake kujikweza kitabaka. Watoto wa Mzee Kawawa wamesoma katika shule ambazo watoto wa Watanzania wengine wamesoma. Mimi binafsi nimesoma na binti yake anayeitwa Zainab na tulikuwa naye katika harakati za wanafunzi pale Mlimani kama mwanafunzi mwingine yeyote. Hii iliwezekana tu kwa sababu waasisi hawa wa Taifa walihakikisha kuwa shule za Umma ni bora kuweza kuelimisha Watanzania. Hivi sasa hali ni tofauti kwani viongozi tunashindana aina za shule ambazo watoto wetu wanasoma. Hii ni kwa sababu tumedidimiza shule za Umma, na kwa kuwa hazituumi ni rahisi sana kuzipuuza. Sera za kiliberali zimefanya elimu kuwa bidhaa inayouzwa katika soko. Wasisi wa Taifa hawakutaka hili kwani kama wangekuwa na fikra hizi toka mwanzoni mwa uhuru watoto wengi wa masikini ambao ndio viongozi wetu leo wasingepata elimu. Utekelezaji wa Azimio la Arusha ambalo lilitekelezwa kwa ujasiri mkubwa na Mzee Kawawa ulifungua fursa kwa watoto wote wa Tanzania bila kujali hali za wazazi wao kupata elimu na huduma nyingine za jamii. Hali ni tofauti kabisa katika nchi nyingine za Kiafrika ambapo mwenye mali ndio anapata huduma bora.

Kifo cha Mzee Kawawa ni fursa. Ni fursa ya kutafakari na kujadiliana kuhusu misingi na Dira ya Taifa letu kama ambavyo walifikiri na kuijenga wakati walipokuwa wakipigania uhuru na hata baada ya kupata Uhuru. Ni jukumu la Vijana wa sasa kuona kuwa Wazee hawa waasisi ambao ndio wanakwisha hivyo na kutangulia mbele ya haki walifanya wajibu wao – kuleta Uhuru na kujenga Taifa. Vijana wanapaswa kuhakikisha kuwa tunahodhi jukumu la kuirejesha, kuilinda na kuienzi misingi ya Taifa ya Umoja, Utu na Uzalendo kwa Taifa.

Historia inatuambia kitu kimoja kuhusu Mzee Rashidi Mfaume Kawawa. Kwamba, Kama Mwalimu Nyerere alikuwa Wino ulioandika TANZANIA, Mzee Kawawa alikuwa Kalamu. Nenda Simba wa Vita, msalimu rafikiyo kipenzi Mwalimu.

BY ZITTO KABWE

Share and Enjoy:
  • Digg
  • Sphinn
  • del.icio.us
  • Facebook
  • Mixx
  • Google Bookmarks
  • email
  • LinkedIn
  • Live
  • Spurl
  • Technorati
  • Yahoo! Buzz
  • YahooMyWeb

Feedback / Comments

2 Responses to ““NENDA KWA AMANI SIMBA WA VITA”-ZITTO KABWE”

  1. Comment by kimito on January 1st, 2010 1:51 am

    Nimekuwa nikisema haya maneno kila siku hata kabla muumba hajamchukua simba wa vita.
    Leo nayaandika tena. Laiti kama Nyerere na Kawawa wangekuwa ni hawa viongozi wa sasa basi tusingekuwa na mkoa wala wilaya. Nyerere na Kawawa wangeweza kugawana mikoa na kuiuza bila ya sisi kujua. Wakati wao nani alijua hata kitu kinaitwa hazina.
    Wangechimba madini na leo tungekuwa na mabwawa yenye kina kirefu katika kila mgodi.
    Wasingetuachia mashirika 450 na leo hatuna zaidi ya 10.
    Kawawa hatujasikia hata siku moja mtu akidai wewe uliiba au ulifisadi hata senti moja.
    Hatujasikia mtu akisema wewe umenyang’anya wananchi Mashamba na unamiliki ekari 400 au 600 songea,Lushoto au Morogoro.
    Umeishi maisha ya kawaida na hata ulinzi ulipewa tu kwa heshima kwasababu ungeweza kuishi mtaa wowote bila shida.
    Watoto wako wamecheza chandimu na Nage. Hawa wa sikuhizi wanazaliwa Agakhan hatuwaoni tena wakirudi wanaajiriwa BoT kwasababu wanajua kiingereza zaidi kuliko kiswahili.
    Tukiuliza tunaaambiwa uchunguzi unaendelea.
    Kawawa wewe uliheshimu nafasi ya kazi na sio cheo,umefanyakazi na hata ”watoto” wako kisiasa wakawa mabosi wako. Hukujali bali uvumilivu wa kisiasa ndio msimamo wako.
    Wewe na Nyerere mkaunganisha makabila 120 na sasa tuna taifa. Eti wasomi sikuhizi wanatumia kitu kinaitwa BLOG kuchunguza waziri ni dini gani na kabila gani,mngekuwa wajinga kama hawa wasomi wa blog za jamii zetu siku hizi msingefanikiwa kumuondoa mwingereza. Kawawa tulidhani elimu ni ukombozi lakini ukisoma maoni ya wehu ndani ya blog kuhusu udini na ukabila utajua mumeacha kizazi cha mafisadi na wasomi wasiojua usomi zaidi ya kompyuta na key board. Wewe na wenzako hamkumjua mtu kwa dini wala kabila,la siku hizi ndio mada kwenye hivi vitu vinaitwa blog.
    Kawawa msalimie swahiba wako Mwalimu na mwambie watoto wake kisiasa hawatakiwi kusema eti wakisema wanahatarisha usalama. Hata ile taasisi yake sasa inasakamwa na wenye nazo. Wananunua kila kitu na kifuatacho ni roho zetu.
    Mwambie mwalimu watoto wake wawili kisiasa wameasi,baada ya yeye kuondoka wamegawana migodi na vituo vya maegesho,wakafungua kale kabenki kako kakubwa wakakomba wao na mafisadi. Mhakikishie mwalimu kuwa hawajakamatwa na tumekubaliana tuwaache wapunzike baada ya kazi nzuri ya kuuza kila kitu na kujigawia kilichobaki.
    Mwambie mwalimu bado watoto wake wa kisiasa wachache wapo na ndio tunawategemea.
    Kawawa mwambie mwalimu Uadilifu ni ujinga siku hizi. cheo si dhamana ni mtaji.
    Tumepiga hatua hadi gavana anaishi kwenye jumba la bilioni na nusu, na kule kigoma na singida watoto wanasoma chini ya mti.
    Naibu gavana ana nyumba ya bilioni moja na jirani tu hapa Dar kuna kituo cha afya hakina solar system mwaka sasa kwasababu matengenezo yake ni sh lakini tano na serikali haina fedha.
    Mwambie mwalimu nchi imeendelea viongozi kama hawana VX hawana heshima,wewe na swahiba wako mlitumia Landrover eti wanasema ni ujima.
    Jumamosi watakuja kukuaga watanzania,lakini pia mafisadi watakuja kushuhudia kwisha kwa enzi za Tanganyika huru. Huenda wakafanya tafrija!!!.

    Msalimie Mwalimu, chediel mgonja,Amir Jamal,Dr Sterling,Kinjekitile,Mshume kiyante, Azizi Dosa,Dr Kleruu,mzee Mwapachu, Mzee Rupia, mzee Max Mbwana, Bibi TITI, Mzee Karume,mzee kombo jecha,Mzee Takadir,mzee Tambaza,akina Sewa haji,akina Abdulwahid,Mzee Bomani na wote mliomenyeka kwa ajili yetu.
    TANGULIA SIMBA WA VITA NA UAMINIFU. TANGULIA UKAPUNZIKE KWA AMANI.BURIANI KAWAWA.

  2. Comment by Mwanamke wa Shoka (UK) on January 2nd, 2010 10:07 pm

    Oh what a touching obituary to Our very own Mzee Kawawa….We are already missing you!!

    Kimito keep it up…you are really a proud Tanzanian….nchi inakuuma…but what can we do…hao wanaoajiriwa bOT eti wanajuwa kiingereza,…kiingereza chenyewe cha upupu mtupu…ni sawa na wanaoiuza Bongo kwa Wakenya eti kwa kuwa wanajuwa kiingereza….I am pissed off….

    R. I. P. Mzee Kawawa…you were among the very few ones….and I can see no more…you all have departed now….We miss you.

Leave a Reply