
Happy New Year! Kheri Ya Mwaka Mpya! Naam ni mwaka 2010,karne ya 21.Binafsi napenda kukupa pongezi kwa kuumaliza mwaka 2009 na kuingia mwaka 2010.
Nakupa hongera nikiwa na sababu nyingi.Baadhi yake ni kwamba,kwa wengi mwaka 2009 ulikuwa ni mgumu kupita kiasi.Hali mbaya ya kiuchumi iliyoikumba dunia,ni sababu tosha ya kuufanya mwaka 2009 kuwa mgumu.
Isitoshe,tumepoteza wapendwa wetu wengi,ndugu,jamaa na marafiki.Mfano ni hivi leo,tunaomboleza kifo cha Mzee wetu,Rashid Mfaume Kawawa. Maradhi mbalimbali,mengine yakiwa mapya kama vile H1N1 (homa ya mafua ya nguruwe),yaliikumba dunia na kuleta mtikisiko wa aina yake.Hofu ikatanda ulimwenguni.Wengi wamepoteza maisha katika vita na mashambulizi ya kigaidi na kujitoa mhanga.
Wakati bado tunatafakari yaliyojiri katika mwaka 2009,naukumbuka msemo wa wahenga wetu.Yaliyopita si ndwele,tugange yajayo.Ni mwaka mpya na ni nafasi nyingine ya kuanza upya,kuweka malengo mapya,kumalizia ya zamani.Ni wakati wa kujipanga upya kuzikabili upya changamoto mbalimbali za maisha na ubinadamu.
Unapouanza mwaka mpya na kama unataka au umeshajiwekea malengo, kumbuka yafuatayo;
- Orodhesha malengo yako. Tafuta mahali penye utulivu.Chukua kalamu na karatasi kisha orodhesha malengo yako.Kisha pembeni ya malengo,orodhesha mambo ambayo unatakiwa kufanya(actions) ili kutimiza malengo uliyoorodhesha.Jaribu kuorodhesha malengo machache.Kumbuka mtaka yote,hukosa yote.
- Weka malengo halisi.Je malengo uliyoorodhesha hapo juu ni halisi? Ninaposema halisi namaanisha weka malengo yanayokabilika.Usiweke malengo yaliyozidi kiwango au yasiyotimia kimsingi.Kwa mfano,ukiweka malengo kwamba mwaka huu unataka kuwa tajiri kupita watu wote duniani wakati hivi leo akiba yako benki ni ya kiwango duni,utakuwa unaweka malengo yasiyo halisi.
- Jiamini kwamba unaweza kutimiza lengo/malengo yeyote uliyojiwekea.Kujiamini kunaenda sambamba na imani.Ukiamini kwamba inawezekana,utaweza.Kama sio leo basi kesho.Piga taswira kichwani kwako jinsi itakavyokuwa ukitimiza malengo yako.
- Fanya tathmini ya mara kwa mara juu ya malengo yako na mwenendo mzima wa kuyatimiza.Ukiona hauelekei kuyatimiza,usiingiwe na hofu ya kuyafanyia marekebisho.Siku hazifanani na mazingira hubadilika.Malengo pia yanaweza kubadilika.
- Mwambie ndugu au rafiki wa karibu kuhusu malengo yako.Naelewa…unataka malengo yako ya mwaka huu yabakie siri.Ninachotaka kukuambia ni kwamba unapomwambia ndugu au rafiki yako wa karibu unayemwamini kuhusu malengo yako,unakuwa umejipatia msaada.Ndugu au rafiki huyo atakuwepo kukukumbusha au kukusaidia,kwa njia moja au nyingine,kutimiza malengo yako.Isitoshe,kwa kumwambia ndugu au rafiki,unakuwa umejitilia chachu ya kutimiza malengo yako.Utaonekanaje kama mwisho wa mwaka utakuwa hujatimiza yale uliyotaka kutimiza? Binadamu tumeumbwa na soni.Itumie.
- Orodhesha watu wa kukusaidia. Kutimiza malengo kunaweza kuwa kitu kigumu.Unaweza kuhitaji msaada ili kutimiza malengo.Usisite kufanya hivyo.Weka mahali orodha ya watu ambao unadhani wanaweza kukusaidia pindi utakapohitaji msaada katika kutimiza malengo yako.Wengine wanaweza kukusaidia kimawazo au kimtazamo(role models).Watumie ipasavyo.
- Jipongeze. Kutimiza lengo au malengo ni jambo la furaha.Linastahili pongezi.Kila unapotimiza lengo au malengo fulani,usisahau kujipongeza.
- Usisahau kumweka Muumba mbele. Hata kama huna imani,huamini wala kuabudu kufuatana na dini au dhehebu lolote,bila shaka tunakubaliana kwamba yupo aliye juu,aliyetuumba.Usimsahau.
Nakutakia kila la kheri katika mwaka mpya wa 2010. Enjoy.
Feedback / Comments
2 Responses to “HAPPY NEW YEAR 2010!!!”
Leave a Reply


sending...
Mkubwa Heri ya Mwaka Mpya!!
HONGERA NAWE PIA, MWAKA HUU UWE WA BARAKA KWAKO