
Nchi yetu imepitia katika awamu nne mpaka sasa katika siasa na uongozi. Kwanza ilikuwa enzi za Mwalimu Nyerere ambazo wengine hupenda kusema enzi za “mchonga”. Kisha ikaja awamu ya pili chini ya Mzee Mwinyi ambaye alikuja kujulikana sana kama “Mzee Ruhksa”. Kisha akaja Mheshimiwa Mkapa ambaye alipewa jina la “ukapa” kwani alipoingia madarakani, na shilingi ikapotea mifukoni mwa watu. Tupo katika enzi za JK. Bado sijajua akimaliza muda wake zitaitwaje enzi zake.Tusubiri.
Wakati sote tunakubaliana kwamba awamu zote ni muhimu kwa maendeleo kamili ya nchi,bila shaka tunakubaliana pia kwamba awamu ya pili,ya Mzee Mwinyi,ilifungua milango mingi sana. Hapo ndipo vitu kama vituo vya televisheni,vituo vya redio vya FM,biashara za nje na ndani,zilikuja kwa kasi.Enzi za mageuzi.
Kufunguka kwa milango hiyo kulitoa pia nafasi kwa vijana kuonyesha vipaji vyao ambavyo hapo nyuma vilikuwa vimejificha bila sehemu ya kufichuliwa. Tukaanza kupata vijana watangazaji.Tukapata vijana wenye vipaji vya kisanii kama vile tunaouita “muziki wa kizazi kipya” hivi sasa. Tukapata wazalishaji muziki (producers). Watangazaji wapya wakaambatana na wale “wakongwe” kutoka vituo kama Radio Tanzania na kutupatia ufanisi na ushindani katika masuala ya utangazaji ambao haukuwepo kabla ya hapo.
Miongoni mwa vijana waliopata fursa ya kuingia katika fani na kuonyesha vipaji vyao ni Sunday Simba Shomari.(pichani). Ghafla maisha yakabadilika,enzi za AM zikazibwa na FM.Soko la muziki wa kizazi kipya likaanza kukua. Majumba ya sinema yakatoweka.Hakuna wateja. Kila mtu yupo nyumbani akikodolea macho luninga yake. Kama kwenu hakuna TV basi unajongea kwa jirani. Muziki wa kimataifa,soka la kimataifa yakiwemo kama mashindano ya kombe la dunia yakawa ni mambo ya kawaida.
Nini kiliwasukuma vijana kama Sunday Shomari kuingia katika fani ya utangazaji wa radio na televisheni? Ilikuwaje enzi hizo ukizingatia kwamba wengi wao walikuwa hawana uzoefu katika masuala hayo? Na je anazungumziaje safari yake kutoka Radio One/ITV mpaka Voice of America alipo hivi sasa? Nilimtafuta Sunday na kufanya naye mahojiano yafuatayo;
BC: Sunday karibu sana ndani ya BC.Tunafurahi kuwa nawe hapa.Mambo yanakwendaje?
SS: Mambo safi tunamshukuru Mungu.
BC: Labda bila kupoteza muda,kwa faida ya wale ambao wanakufahamu kwa sura na jina tu,unaweza kutupatia japo kwa kifupi tu historia ya maisha yako?
SS: Mimi ni mzaliwa wa Dar-es-salaam na mwenyeji wa Tanga. Nimepata elimu ya msingi Arusha School na Muhimbili. Elimu ya sekondari Forodhani na Al-Muntazir.Halafu nimefanya kazi na Dr.Jane Goodall Institute kabla ya kujiunga na ITV na Radio One. Baadaye nikajiunga na Chuo Cha Uandishi wa Habari (TSJ) kwa kozi fupi ya uandishi. Kisha nilikuja hapa Marekani kwa kozi nyingine fupi ya uandishi wa TV kabla ya kurudi tena Tanzania na kuendelea na masomo yangu ya juu ya uandishi hapo TSJ.
Wakati huo huo nikiendelea na kazi hatimaye nilitoka kwenye uandishi nikaingia Shirika la Ndege la Alliance kabla ya kuja tena Marekani kujiendeleza kielimu na kutafuta maisha mengine. Na hivi sasa naendelea na shahada ya mawasiliano katika Chuo Kikuu Cha Maryland.
BC: Ilikuwaje ukaingia kwenye fani ya utangazaji? Nini kilikushawishi au nani alikuvutia katika fani ya utangazaji?
SS: Nilikuwa napenda kuwaona watangazaji wengine wa wakati huo hasa Tumaini Meshack ambae nilisoma nae sekondari na alikuwa ITV kwa wakati huo akifanya kipindi cha watoto. Mzee wa Macharanga Charles Hillary, Mikidadi Mahmud a.k.a Brother Micky Uncle J Nyainsangah, Suzan Mungi na wengine lakini niliingia baada ya kumaliza kidato cha sita na wakati huo IPP MEDIA walitangaza nafasi za kazi basi nikajaribu na kufanikiwa kuingia siku moja na Mike “Magic” Muhagama na Peace Kuyamba a.k.a Peace K.
BC: Turudishe nyuma kidogo.Miaka ileee…kipindi unaanza kutangaza.Unakumbuka ilikuwaje siku ya kwanza uliporusha matangazo kwa mara ya kwanza kabisa.Ulijisikiaje ulipoambiwa kwamba 1,2,3 go.You are now “live”?
SS: Nilikuwa na hamasa kubwa sana na moyo ulikuwa ukipiga kwa kasi na wakti huo huo nilisikia raha moyoni ambayo siwezi kuielezea na sitasahau Aboubakar Liongo alinipa moyo sana na ushauri bila kumsahau Master T .
BC: Kwa watu wengi,kuanza kazi mpya huwa inakuwa kazi ya ziada.Kuzoea mazingira mapya,watu wapya,taratibu mpya za kazi nk huweza kuwa mambo magumu kwa baadhi ya watu.Kwa upande wako ilikuwaje hususani ulipoanza kazi pale ITV na Radio One miaka ile ambapo kila mtu alikuwa anapatizama? Ulikumbana na “kasheshe” zozote?
SS: Nyingi tu kama ulivyosema kila kazi ina kasheshe zake hasa kubwa ilikuwa kipindi kinaitwa kumepambazuka inabidi uamke alfajiri saa 11 ili uweze kuwahi kufungua kituo,mengine ni mambo ya utendaji kuelewana na wenzako kazini na kutofanya makosa lakini nashukuru watu niliofanya nao kazi walikuwa na usaidizi na upendo wa hali ya juu na nilikuwa tayari kujifunza kwao kama vile Blandina Muongezi a.k.a Anti Ndina.
BC: Kazi ya utangazaji huendana na umaarufu mara nyingi.Kama ujuavyo,umaarufu sio lelemama.Una raha na karaha zake na kimsingi ni mabadiliko makali ya kimaisha.Unatoka kuwa mtu asiyejulikana na yeyote na kuwa mtu unayejulikana na wengi.Kwa upande wako mabadiliko hayo yalikuja vipi na ulikabiliana vipi na changamoto za kuwa mtu maarufu?
Ni nzito sana na inatahitaji umakini wa hali ya juu nilikutana na mengi kila nililokuwa nafanya ni hadithi kwa wengine wakati mengine si ya kweli na wakati huo huo tukienda kwenye madansi nasikia jina linaimbwa na maband kwa mfano “Diamond Sound” kwahiyo unajikuta huwezi kuwepo mahali bila watu kukuzungumzia wakati mwingine inakera au usifanye jambo lolote ni hadithi mtaani. Na wakati mwingine unapata maadui ambao hawapendi tu kukuona bila sababu yeyote.
Kwahiyo nilijikuta kila ninapoenda nina maswali ya kujibu si kwa watoto au wazee na hasa wengi wao wakitaka kujua mimi na Monica tuna nini kinachoendelea lakini nikiwaambia uhusiano wetu ni wa kazi tu imekuwa ngumu watu wengi kuamini mpaka leo lakini nilijitahidi kuwa makini na maisha yangu. Na nawashukuru wazazi wangu kwa kunipa msingi bora wa maisha na Mungu awalaze pahali pema peponi Amen.

Sunday Shomari akiwa na mwanamuziki maarufu kutoka nchini Marekani,Avant.
BC: Na je huwa inatokea ikafikia mahali ukakubaliana na hali halisi kwamba mimi ni maarufu na hivyo mengi yanaweza kusemwa juu yangu,ya uongo na ya ukweli? Na pia je huwa unajisikiaje hivi leo ukiona picha yako kwenye gazeti fulani,televisheni nk?Big deal?
SS: Hapana si hivyo hata kidogo kwa sababu kwa kweli ni mambo ya kawaida mi ni mwandishi kwahiyo najua kila chombo kinatafuta habari na najitahidi kutojali nini kimezungumzwa mradi najua maisha yangu yanakwendaje.
BC: Hivi sasa upo nchini Marekani,Voice of America.Ilikuwaje mpaka ukafika hapo?Na unaonaje mabadiliko ya kiutendaji kazi hapo nchini Marekani ukilinganisha na nyumbani Tanzania?Kuna yepi ambayo unaweza kusema kule nyumbani tunaweza kujifunza ili kuboresha utendaji kazi?
Nimepitia sehemu nyingi tu za kazi kabla ya kufikia hapa na kutokana na uzoefu na masomo yangu nikapata nafasi ya kuingia hapa nashukuru lakini nikilanganisha na nyumbani hapa nimejifunza mengi sana kama mtangazaji unatakiwa kuwa na uwezo wa kufanya vitu vingi ikiwa ni pamoja na kuandika habari, kutafsiri, kufanya usaili, kuhariri , kusoma kwa Kiswahili fasaha na pia kutumia teknolojia mpya katika vyombo vya habri ikiwa ni kompyuta, mtandao , vifaa vya kisasa n.k. Nyumbani tulivyokuwa tukitangaza kwa wakati huo ukiwa mtangazaji basi ni hivyo tu huandiki habari wala kwenda kutafuta habari mitaani au ukiwa mpiga picha ni hilo tu kwani wapo watu wa kuandika wewe ni kusoma tu, na pia ukija kwenye masuala ya studio si lazima ufanye uhariri lakini hiyo ni wakati huo najua sasa kuna mabadiliko ambayo siwezi kuyachanganua. Kwa hiyo kwa ujumla utangazaji wa hapa unahitaji uwe muandishi kwasababu hii ni radio ya kimataifa.
BC: Na kwa wale ambao hawajui ratiba ya matangazo ya Voice of America kwa wakazi wa Afrika Mashariki,wanaweza kuyasikiliza wapi,katika vituo gani,muda gani na mara ngapi kwa siku?
Matangazo yapo kwenye vituo mbali mbali Afrika mashariki ikiwa ni pamoja na Radio Tumaini Daressalaam Tanzania na Radio Free Afrika katika eneo zima la maziwa makuu, Citizen Radio kote nchini Kenya, Radio yetu ya VOA 107.5 FM Nairobi, Baraka FM Mombasa, Radio Ngoma Afrika Bujumbura Burundi, Raga FM DRC na Coconut 100.9 FM Zanzibar. Matangazo yapo ya alfajiri na jioni saa moja na nusu saa za Afrika Mashariki na saa kumi na mbili na nusu jioni saa za Afrika ya kati. Wakati asubuhi ni saa kumi na moja alfajiri na kumi na mbili. Na wale walioko hapa Marekani na sehemu nyingine duniani wanaweza kuingia kwenye mtandao www.voanews.com/swahili masaa 24 na pia tupo kwenye face book Voaswahili unaweza kutoa maoni na kutuma maswali pia.
BC: Natambua kwamba wewe ni mpenzi wa muziki ukiwemo ule wa kizazi kipya au Bongo Fleva.Ni wasanii gani wanaokuvutia zaidi?
SS: Wengi mno maana wamebadilika kweli sisi tuliiona Bongo Flava tangu ilipoanza na kina sugu a.k.a Mr II, Diplomatz na kina Sindira, na hivi sasa wasanii wanazidi kuibuka kwa hiyo ninavutiwa na wengi ila baadhi tu ni kama Ali Kiba, Marlow, K-Lynn, Banana Zoro, Mwana FA na Ay.
BC: Ungetoa ushauri gani kwa wasanii wa kitanzania kwa ujumla katika kuboresha kazi zao na kutizama kwa mapana na marefu masoko ya mbali ikiwemo nchi za Ulaya na Marekani kama ambavyo wasanii wengi wa Afrika Magharibi wamekuwa wakifanya?
SS: Wajitahidi kutumia nafasi za kukutana na wasanii wa hapa Marekani hasa wanapozuru Tanzania na kupata kuongea nao na kuwapa mawasiliano yao na kujaribu kuwa na menejimenti inayoeleweka mameneja na mawakili ili wasiibiwe wala kudanganywa kwasababu ili ufanye kazi na watu wa nje ya nchi yako inatakiwa ujue nini unakifanya. Na pia wasanii wa Marekani hawapendi biashara uchwara kama msanii unaonekana huna mipangilio itakuwa ngumu kushirikiana na wewe.
BC: Sunday,kama unavyojua ulimwengu umekuwa ukishuhudia mabadiliko makubwa,kisiasa,kijamii na kiuchumi.Kwa upande wa siasa,mtu mweusi hivi leo ndio yupo katika “jumba jeupe” hapo hapo Washington DC ulipo.Unaongeleaje uongozi wa Barack Obama kwa muda mfupi ambao ameshakuwa madarakani?
SS: Ni mtu anayejituma sana na anajua nini anataka kwa muda mfupi ameshaonyesha uwezo wa kufanya mengi na wakati huo huo ana upinzani mkali kutoka kwa wa-republikan kwenye Uchumi na Afya ndio masuala makuu yanayoangaliwa na wananchi wa Marekani mpaka hivi sasa anapigania ajenda ya kuwapa watu wote uwezo wa matibabu wa gharama nafuu ambapo serikali itashindana na mashirika binafsi ya Bima kuwapa wale wasio na uwezo nafasi ya kupata huduma za afya.
Lakini mpaka hivi sasa kuna kasheshe nzito bungeni kwani wa-Republican wanamshutumu kwamba anataka kuleta Ujamaa au kuingiza mfumo wa Afya wa Canada na yeye anawaambia la hasha ila kwa kiasi kikubwa anakaribia mno kufanya mageuzi ya kweli katika afya huduma za jamii elimu, sera za biashara, kodi kila jambo amesema atalifuatilia kwa makini kiasi kwamba wanamwambia anajaribu kufanya kila kitu kwa wakati mmoja atashindwa lakini la hasha huyu bwana ana nguvu za kufanya kazi kama Simba, anasafiri anakutana na watu wake hasa Gavana na kamati ya fedha kila siku Jumba jeupe kupata ripoti za maendeleo ya uchumi na pia ana wahudumia wananchi kwa mtandao ameitwa ni rais wa Teknolojia haongei tu kwenye Televisheni bali pia kwenye mtandao wa Jumba jeupe na pia kwenye You Tube nk .Itakumbukwa kampeni zake zilishika moto kwenye mtandao na hivyo moto huo hajauzima amewaruhusu watu kutuma maswali kwenye mtandao wakati akizungumzia masuala muhimu ya taifa hili.
Alipokwenda Ghana aliruhusu watu wa Afrika kutuma maswali kwenye mtandao na wakati alipoongelea vichocheo vya uchumi na mfumo wa afya alizunguka karibu nchi nzima na kufanya mikutano midogo midogo (town hall meetings) na huko pia aliruhusu watu kutuma maswali kwenye mtandao kwa hiyo kwa kweli anafanya si kazi nzuri tu bali ni ya ziada. Amewapa wanajeshi nafasi ya kusoma vyuo bure na pia wachumi wanaeleza masoko ya fedha yamepata ahueni kubwa lakini ni mapema mno kusema kama uchumi ndio umeduta ila nafikiri anafanya kazi nzuri kwa muda mfupi aliokuwa madarakani.
BC: Yapi mapya ambayo yanatokea hivi sasa kwenye maisha yako kwa ujumla?
Ni mengi tu namshukuru Mungu baadhi ni mambo ya kublog na ninawaalika wadau wakipata fursa kutembelea na kujiunga nami kwenye blog yangu www.sundayshomari.blogspot.com tuendeleze libeneke.
BC: Katika masuala ya u- MC unaendelea na unalionaje kwa ujumla?
SS: Hilo suala linaendelea kama kawa nafanya hiyo shughuli kwa wakati wangu binafsi na nimeshazunguka karibu majimbo yote ya Marekani kufanya shughuli hiyo hasa kwenye maharusi na kwa kweli napata nafasi ya kukutana na watu mbali mbali na linanipa faraja kubwa kuwatumikia watu.
BC: Nimeona uliwahi kupata tuzo miaka ya nyuma na pia hivi karibuni unaweza kutuelezea zaidi?
SS: Naam hivi karibuni nilipewa tuzo ya Ubalozi Bora na Jumuiya ya Wanawake na kina Dada wa Afrika waishio Columbus, Ohio wakati wa maadhimisho ya sherehe za Uhuru wa Tanzania kwa sababu ya uwakilishi wangu kwa jumuiya ya watanzania wa Ohio.
Kwahiyo nawashukuru kwa hilo.Pia niliwahi kupata tuzo nyingine huko huko Ohio mwaka 2004 ya Mwl.Nyerere kwa ajili ya huduma na kujitolea katika mambo mbali mbali kwenye jumuiya ya Waafrika huko Ohio na tuzo hiyo nilipewa na gazeti liitwalo African Weekender linalotoka kila mwezi huko Ohio.

Sunday akikabidhiwa tuzo ya Ubalozi au uwakilishi Bora aliyopewa na Jumuiya ya wanawake na kina dada wa huko Columbus,Ohio hivi karibuni.
BC: Asante kwa muda wako Sunday.Tunakutakia kila la kheri katika kazi zako.
SS: Shukran.
Feedback / Comments
5 Responses to “SUNDAY SHOMARI:KUTOKA IPP MEDIA MPAKA VOICE OF AMERICA”
Leave a Reply


Go brother.
PamoJAH
Hongera sana ndg yangu kwa Sunday kwa kuitumikia vema tasnia ya habari na mawasiliano kwa umma.Naomba uendelee kwa balozi mwema wa lugha ya kiswali na bidhaa zake huko ughaibuni.
Angalizo:
“JASIRI HAACHI ASILI NA MUACHA ASILI NI HASIDI.”
kaka,hongera sana,
enzi hizoo nipo azania nakula old skul skul zako from radio one, kwenye kipindi chako na yule dada (monica) …ukisaidiana na kina misanya bingi.dj rankim ramadhan…we real appreciate…kwa mapinduzi mliyofanya..hapa bongo miaka ya 1990……..
sunday shomary wapi monica mfumia??????????????????
Sunday,
Down to earth. Mvumilivu, a genuine, warm, handsome smile! Mchapa kazi. Nakupongeza saaaana kwa kila hatua unayochukua, kila mara umerejea kuomba ushauri, au kujalia hali tu!
Mungu akusaidie, akuongoze na wewe weka jitihada zaidi maana bado ni kijana na dunia ni yako!
Nipo nawe pamoja, daima!
Master T