Natumaini kwamba hujambo na unaendelea na mapambano ya maisha kwa ujasiri,bila woga wala dalili za kukata tama.Hivyo ndivyo inavyotakiwa.Kumbuka kwamba penye nia pana njia.Jifunze jambo jipya kila siku.Usipoteze muda bure.

Uchumi wa dunia bado haujatengemaa.Bado habari za makampuni kufungwa,kupunguza wafanyakazi,kufilisika na mambo kama hayo,tunazisikia na tutaendelea kuzisikia.Hatujui lini uchumi utarudia hali yake ya kawaida au tuseme ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita.Hakuna anayejua kwa hakika.Hata Rais Obama hajui. Kilichobakia hivi sasa ni imani tu kwamba huenda kesho ikawa bora kuliko jana.Imani.

Kwa sababu ya kuyumba huko kwa uchumi,wengi wameshapoteza kazi zao na wengi zaidi wapo mbioni kupoteza.Lakini kupoteza kazi sio mwisho wa maisha.Kwa ufupi ukipoteza kazi uliyonayo hivi leo,huo ni mwanzo wa mbio za kutafuta kazi nyingine.

Kwa maana hiyo wengi wanaopoteza,kuachishwa au kuanza kutafuta kazi hivi leo,wanahitaji mbinu za kushinda mtihani wa usaili(interview). Leo nitaongelea jinsi ya kujiandaa kwa ajili ya usaili,jinsi ya kujiongoza wakati wa usaili nk.

Kabla sijakuambia ninachotaka kukuambia,naomba nikwambie jambo moja la msingi.Ushindi katika jambo lolote hutokana na jinsi unavyojiamini.Kujiamini hata wakati wa usaili ni jambo la msingi na ambalo lazima ulizingatie.Lakini kumbuka kujiamini hakumaanishi kiburi,majivuno au maringo.Ninaposema kujiamini ninamaanisha kuwa na uhakika na unachokisema na kuonyesha kwamba una uhakika bila majigambo wala kiburi.

Umepata barua au simu kuhusu usaili.Zingatia yafuatayo;

  • Hakikisha umepata taarifa za kutosha: Mara nyingi upatapo barua au simu inayokuita kwenye usaili,mtu yeyote hujawa na furaha au msisimko wa ajabu.Ni ruksa kufurahi lakini kumbuka kuchukua taarifa muhimu(hususani kama habari hii inakujia kwa njia ya simu) kuhusu mahali utakapofanyiwa usaili(anuani,namba ya chumba,gorofa ya ngapi nk),muda na kama usaili huo utakuwa na watu zaidi ya mmoja au la.Taarifa kama hizo zitakusaidia katika kujiandaa.
  • Fanya uchunguzi kuhusu shirika/kampuni husika: Kabla ya kwenda kwenye usaili hakikisha kwamba umefanya uchunguzi wa kutosha kuhusu kampuni au shirika husika(research).Wanashughulika na nini,wateja wao ni kina nani,linamilikiwa na nani,lilianzishwa lini na kwa malengo gani.

    Kama unamjua mtu au rafiki ambaye aliwahi kufanya kazi katika shirika au kampuni hiyo,mtumie ili kupata taarifa za ndani zaidi.Ufahamu wako kuhusu kampuni au shirika utawaonyesha wanaokufanyia usaili shauku uliyonayo kuhusu kampuni/shirika. Kumbuka tu kutojifanya unajua kupita kiasi.Bakia kwenye kiwango kinachostahili.

  • Mavazi na muda: Jambo mojawapo gumu linalomkabili mtu anayejiandaa kwa usaili ni uamuzi wa nguo gani za kuvaa.Jambo zuri ni kwamba una muda wa kujiandaa na pia kuchunguza. Cha kwanza unachotakiwa kufanya ni kuchunguza kuhusu utamaduni wa mavazi wa kampuni au shirika husika.Wanavaaje wafanyakazi wake?Kama ni kampuni ambayo kila mtu anavalia suti,basi jitahidi kwamba siku ya usaili na wewe uvae suti(hata kama ni ya kuazima).Lakini ukishindwa kupata suti usihofu; unachotakiwa kufanya ni kuvaa nadhifu.Jaribu kuepuka nguo zenye rangi kali au za kuwakawaka.

    Epuka manukato makali au yanayonukia kupita kiasi.Kumbuka kuna watu wengine hawapatani na manukato makali.Usiwatibue.

    Pili ni suala la muda.Hakikisha unafika sehemu ya usaili mapema.Napendekeza ufike japo dakika kumi hivi kabla ya usaili.Hiyo itakupa muda wa kupumua,kuyasoma mazingira na kutuliza mawazo na akili yako.

  • Salamu,bashasha na tabasamu: Tofauti na wengi tunavyodhani,usaili huanza mara tu unapoingia kwenye ofisi husika. Katibu Muhtasi(secretary) au mtu wa mapokezi(receptionist) unayekutana naye kwanza huwa ni mtu muhimu wa kwanza unayekutana naye.Msalimie kwa heshima na tabasamu inayostahili. Mara nyingi yeye huwa ndiye anayesimamia zoezi lote la usaili.Pendekezo lake ni muhimu wakati wa kufanya uchaguzi.Heshima hiyo na tabasamu mpe kila mtu utakayekutana naye katika ofisi hiyo.Kwa sababu huwajui,usifanye makosa.Usipomsalimia mtu na kisha ukakutana naye kwenye chumba cha usaili ni wazi kwamba utakuwa umeshaanza kujuta.

  • Sikiliza / Jiongoze kwa makini: Wakati wa usaili ndio umewadia. Huu ni muda wa maswali na majibu. Jambo la kwanza la kuzingatia ni kitu ambacho wenzetu wa magharibi wanakiita “body language”.Mwili wako huongea hata bila ya wewe kutamka neno.Hakikisha kwamba body language yako inaonyesha kwamba una nguvu za kutosha,una shauku na kampuni/shirika husika,upo tayari,unajiamini na upo makini. Keti kiheshima.

    Siri muhimu ya kuweza kujibu maswali vizuri ni kusikiliza kwa makini.Lisikilize swali vizuri.Usipoelewa usisite kusema kwamba hujaelewa au ungeomba ufafanuzi zaidi kabla hujajibu.

    Usisahau kutabasamu inapobidi na usione haya sana kuwaangalia wasaili wako machoni. Pamoja na kwamba kuna mila na desturi ambazo zinakataza wadogo kuwaangalia wakubwa moja kwa moja machoni,zipo nyakati ambazo mila hizo zinaweza kukuangusha au kukufanya uonekane kama mtu unayeficha kitu fulani wakati wewe unachofanya ni kitendo cha heshima!Kuwa makini ili kutofautisha mazingira.

  • Uliza maswali: Kutegemea na mtu au watu wanaokufanyia usaili,huwa inatokea(mara nyingi mwisho mwisho wa masaili) ukapewa nafasi ya kuuliza swali au maswali kama unayo. Ikitokea hivyo basi uwe tayari. Maswali kama vile ni lini watafanya uamuzi wao wa mwisho wa kuajiri,lini utegemee kusikia kutoka kwao ni muhimu.Unaweza pia kuuliza kama ukiajiriwa utakuwa unafanya kazi chini ya nani na katika kitengo chenye watu wangapi nk.Kwa ufupi usisite kuuliza maswali kama utapewa nafasi hiyo.
  • Shukrani na hitimisho: Hatimaye usaili umefikia mwisho.Washukuru wasaili wako. Omba business card zao na kisha baadaye waandikie(barua ya kawaida au hata barua-pepe) ukiwashukuru kwa muda wao na kuwahakikishia kama kuna kitu hakikueleweka wakati wa usaili basi wasisite kuwasiliana nawe kwa ufafanuzi zaidi.

Kwa kumalizia labda nikukumbushe kwamba unapofanya maandalizi kwa ajili ya usaili yafanye kawaida tu na sio kwa shauku inayovuka mipaka. Kumbuka kuwa wewe.Usiige wala kujaribu kujifanya kuwa mtu mwingine.Ni muhimu pia kukumbuka kwamba pamoja na maandalizi yote,yaweza kutokea usipate hiyo kazi.Hilo likitokea,usikate tamaa. Endelea kutafuta,endelea kujiboresha zaidi.Roma haikujengwa kwa siku moja.

Jeff Msangi ni Mhariri na mwendeshaji wa mtandao wa www.bongocelebrity.com. Unaweza kuwasiliana naye kwa e-mail: makala at bongocelebrity dot com

Feedback / Comments

15 Responses to “JINSI YA KUSHINDA USAILI(INTERVIEW) YA KAZI”

  1. Comment by Mussa Mjumi on January 29th, 2010 3:40 pm

    Asante sana kaka Jeff kwa haya maarifa.

  2. Comment by Mwalo Gabriel on January 30th, 2010 5:54 am

    Ina tija san Nashukuru

    Just keep it up bro!

  3. Comment by Mwalo Gabriel on January 30th, 2010 5:54 am

    Ina tija sana Nashukuru

    Just keep it up bro!

  4. Comment by Mohamed on February 1st, 2010 9:20 am

    nimeipenda sana vp unaweza kunitumia?

  5. Comment by judith henry on March 22nd, 2010 1:50 am

    nashukuru sana kwa maelezo yako mazuri yanaeleweka endelea na moyo huu.

  6. Comment by omarah on June 7th, 2010 1:52 am

    Nashukuru sana kwa muda wako ulitumia kutuelemisha kuhusu usaili.Endelea kutoa msahada MUNGU akubariki.

  7. Comment by james yaundey on September 9th, 2010 5:59 am

    good for tz graduates.keep it up bro.

  8. Comment by Joseph kawogo on September 16th, 2010 12:56 pm

    Ahsante sana!kuna vitabu vyovyote,tukanunua?

  9. Comment by Joseph kawogo on September 16th, 2010 1:01 pm

    Kuna vitabu vyovyote na tutavipataje?

  10. Comment by bongocelebrity on September 16th, 2010 7:37 pm

    Joseph,
    Asante kwa mchango wako.Ukweli ni kwamba vipo vitabu vingi sana vinavyoelezea jinsi ya kushinda usaili.Hata hivyo,nachelea kusema kwamba vingi miongoni mwa vitabu hivyo,havijaandikwa kulingana na mazingira,mila na tamaduni zetu.Ndio maana mpango madhubuti upo mbioni kuandaa vitabu vya namna hiyo,kwa lugha yetu na vitakavyokidhi haja kufuatana na mazingira yetu.Utapewa taarifa zoezi hilo likikamilika.

  11. Comment by Bahati Ngowi on December 21st, 2010 12:22 pm

    Nimeipenda hii kaka, i will be facing interview just kesho, ni imani yangu kubwa kuwa nimepata vingi vya kunifanya nipate the chance i’m fighting for..
    God bless you!

  12. Comment by bongocelebrity on December 21st, 2010 1:34 pm

    Karibu Bahati,
    Nafurahi kusikia kwamba umepata mawili matatu hapo.Ntaendelea kuandika maarifa ya namna hii.

  13. Comment by Solomon Shangali on January 21st, 2011 8:49 am

    Hii kweli imenipa picha ya namna ya kupambana na kujiandaa na usaili. Asante sana Mr Jeff Mungu akubariki sana.

  14. Comment by Solomon Shangali on January 21st, 2011 8:50 am

    Thanks a lot

  15. Comment by Renatus Kalamata on September 14th, 2011 10:58 am

    bro nashukuru sana kwa kutuelimisha. unajua maswali mengine ni papo kwa papo, hivyo ufahamu wa kuface hiyo hali unahitajika.

Leave a Reply