MY TANZANIA   |   PLACES TO GO   |   MEDIA   |   ONLINE ENTERTAINMENT    

Posti hii nilitakiwa kuipandisha jana lakini sikufanikiwa maana jana nilifunga kiroho na kifikra ili kumkumbuka Malcom X, mpigania haki za watu weusi kule Marikani. Malcom X alizaliwa na kupewa jina la Malcom Little kisha akaamua kubadili “Little” na kuweka “X” kwa kile alichodai kuwa jina la awali lilikuwa ni la kikoloni na lenye nia ya kuiba utu wake. “X” inasimama kama “Aliyepotea/Asiye na Jina” ikimaanisha Mwafrika aliyepoteza utambulisho wake baada ya kutekwa na kupelekwa utumwani kule Marikani.

Nimeona niweke posti hii ili tuelewe kwamba isingekuwa Malcom X na wengine waliotangulia kama Martin Luther King Jr., Mama Rosa Parks, au mapambano ya kuwakomboa watumwa ya Reli ya Ardhini” (Undeground Railroad) yaliyoongozwa na mwanamke mweusi Harieth Turbman, pengine Marekani ya leo isingekuwa na Rais Mweusi tunayemfahamu na kumshabikia, Barack Obama.

Malcom X alizaliwa katika familia yenye maisha duni na akiwa na umri wa miaka 13, baba yake ambaye alikuwa mpigania haki za watu weusi pia aliuawa na wazungu wabaguzi waliojulikana kama Ku Klux Klan (KKK), na mama yake alikuwa amefungiwa katika hospitali ya wagonjwa wa akili. Hivyo Malcom akaanza maisha ya kujitegemea akitumia wizi wa mifukoni kama njia ya kujipatia kipato.

Mwaka 1946 Malcom alifungwa jela kutokana na wizi. Akiwa Jela, Malcom ambaye hakuwahi kusoma vitabu akajikuta akiwa msomaji mkubwa wa vitabu ambavyo vilimwongezea maarifa aliyokuja kuyatumia baadae katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa watu weupe kwa watu weusi.

Malcom X aliwahi kusema, “Ukitaka kumshinda adui yako, jifunze lugha yake”. Hivyo akiwa jela Malcom X mbali ya kusoma vitabu vingi changamoto aliyojiwekea ilikuwa ni kukariri Kamusi ya Kiingereza ya Oksfodi, changamoto ambayo aliweza kuivuka. Malcom aliweza kujieleza vyema katika mahakama na vyombo vya habari juu ya mapambano yake, kitu ambacho kiliwaudhi sana wazungu waliokuwa wakitaka kupindisha ujumbe wake.

Ukisoma kitabu chake cha “The Autobiography of Malcolm X” kuna wakati Maclom alikutana na dada wa kizungu aliyetamani kufanya kazi ya ukombozi na Malcom lakini Malcom akamwambia, “Mzungu ni mzungu tu hata kama roho yako ni nzuri lakini bado wewe ni mzungu, hatukuamini!” Dada yule akaondoka amefadhaika.

Lakini mwaka 1964 akapata bahati ya kwenda kuhiji Mecca, huko akakutana na Wazungu, Weusi, na Waasia ambao waliketi pamoja, wakila pamoja na kulala pamoja. Kufikia hatua hii Malcom X akagundua jambo moja na akasema katika barua yake iliyopewa jina la ‘A Letter from Mecca’, “Nimegundua kwamba tatizo sio wazungu (watu weupe) bali ni mfumo wa Kibepari wa Kimarekani”. Baadae aliwahi kusema, alipokuwa akimzungumzia yule dada wa Kizungu, “Siku zote nimekuwa nikiomba Mungu anisaidie nikutane tena na dada yule ili nimwombe msamaha lakini sijafanikiwa, natumaini dada huyu asomapo kitabu changu (The Autobiography of Malcolm X) atanisamehe kwa ujinga wangu”.

Ni mabadiliko ya falsafa ya Malcom X toka kwenye falsafa ya ‘Jino kwa Jino’ au Militant Philosophy kwenda falsafa ya ‘Ukipigwa Shavu la Kulia Geuza na lile Lingine’ ndio iliyomjengea uadui mkubwa zaidi na shirika la kijasusi la CIA na lile la kikachero la FBI ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakituhumiwa kuwa ndio waliopanga mauji ya Mtume huyu. Mashirika haya yaliogopa kwa sababu yaliona Malcom yuko njiani kuunganisha watu wa rangi zote kufikia lengo lake.

Februari 21, 1965 Malcom akihutubia mbele ya wafuasi wake 400, kati yao akiwemo mkewe na binti zake wanne, aliuawa kwa kupigwa risasi, mbaya zaidi ni kwamba waliofyatua risasi hizo walikuwa ni watu weusi wenzake. Zipo tetesi kwamba wauaji wake walikuwa ni wafuasi wa jumuiya ya Nation of Islam, ambao Maclom aliamua kuachana nao kutokana na kiongozi wa Jumuiya hiyo kwenda kinyume na mafundisho yake. Kila nikikumbuka mauaji haya ujumbe toka kwa Mtume mwingine, Bob Marley, huwa unarindima masikioni mwangu. Marley anauliza kwenye wimbo wake wa Redemption Song, “Mpaka lini wataendelea kuwaangamiza Mitume wetu nasi tukiwa tumesimama na kuangalia tu?/How long will they kill our prophets while we stand aside and look.”

Tumia dakika tano kila unapoamka asubuhi kabla ya kupiga mswaki kufikiria mashujaa/manabii wako waliofanya uweze kuishi unavyoishi leo. Tumia dakika nyingine tano kufikiria ungependa watoto wako waishi vipi miaka michache tangu sasa.

Pia ukumbuke kwamba Mungu ametutumia Mitume mingi tu baada ya Yesu na Muhamad (Amani iwe juu yao), na bado anatutumia mitume mingi zaidi tatizo letu huwa hatuelewi wanachotufundisha, na tukielewa tunawaua ili kuwanyamazisha. Ukweli huu umefunikwa miaka mingi lakini sasa haufichiki tena.

Makala hii imeandikwa na Babukadja Sankofa. Yeye ni mwendeshaji wa mtandao wa www.fotobaraza.ning.com

Share and Enjoy:
  • Digg
  • Sphinn
  • del.icio.us
  • Facebook
  • Mixx
  • Google Bookmarks
  • email
  • LinkedIn
  • Live
  • Spurl
  • Technorati
  • Yahoo! Buzz
  • YahooMyWeb

Feedback / Comments

10 Responses to “MIAKA 45 TANGU ALIPOFARIKI MALCOM X”

  1. Comment by jackline on February 23rd, 2010 6:02 am

    ubaguzi wa rangi auto isha ikiwa sisi wenyewe ni wepesi sana wa kukaribisha wageni nchini kwetu na atutweza kamwe kutetea nchi yetu ikiwa sisi wote ni wanyonge wa nchi tawala inabidi tuwe wamoja ili tuweze kutokomeza itifaki hii.

  2. Comment by mr. Degree on February 24th, 2010 5:23 am

    Jackline tatizo si rangi, tatizo ni mfumo! Malcom alipoenda kuhiji mecca alikuta watu wa rangi tofauti wakila na kunywa pamoja na hapo ndipo alipogundua kuwa watu wa rangi tofauti wanaweza kukaa na kuishi pamoja bila tatizo! si vizuri kujenga chuki kwa watu wa rangi tofauti na ndio maana hata Malcom alijuta alipokumbuka kukataa kushirikiana na mzungu katika harakati za ukombozi. watanzania pia ifike mahali tutafakari na kujiuliza hivi tatizo letu ni wahindi au mfumo wetu unaowaruhusu wao kuneemeka? sio vizuri kujenga chuki na binadamu mwenzio kwani yeye ameumbwa kama wewe na mungu hakufanya kosa kumuumba! tunatakiwa kujenga chuki na mifumo yetu ya kinyonyaji inayoruhusu matabaka. bila shaka hicho ndio kilikua kilio cha malcom X! hata mwalimu nyerere hakuwahi kuwachukia wazungu kwa rangi yao bali kwa mifumo yao na ndio maana hata katika baraza lake la mawaziri la kwanza lilikua na wazungu na wahindi.mhindi alikua Amil Jamal na mmoja wa wazungu simkumbuki jina ila alikua Waziri wa afya!

  3. Comment by Mwanamke wa Shoka (UK) on February 25th, 2010 2:22 pm

    Mr Degree nakupa five….!! Nimekusoma.

  4. Comment by Ezijumwi on February 26th, 2010 2:52 am

    Nafikiri watu wa aina ya Kina Malcom X, Harrieth Tubman, Martin Luther King Jr, Black Panthers na kina Mwalimu Nyerere, Didan Kimathi wanahitajika sana kwa sasa ambapo mfumo wa ukandamizaji dhidi ya watu weusi na watu wa dunia ya tatu umerahisishwa bila kiboko chini ya mwavuli wa utandawazi na uwekezaji. Mfumo wa kibeberu na kibepari haswa katika Afrika utaendelea kuwepo ikiwa hatuchuki juhudi za kuwafundisha vizazi vya sasa juu ya mashujaa wetu hawa ambao walidiriki kujitoa muhanga kukomboa nchi zao. Wachache waliopo kama ni Mugabe wakijaribu kutetea Ardhi ya Wanyonge wanawekewa vikwazo na mashirika ya kibeberu kama WB na IMF ambayo yameundwa makusudi kufanikisha modern colonialism.
    Walale pema wapigania haki za mtu mweusi popote walipo.

  5. Comment by EDWARD on February 27th, 2010 8:19 pm

    Ttatizo ni rangi pia, kuna kitu kinaitwa WHITE SUPREMACY nI kwamba mtu yoyote mwenye rangi ambayo si nyeusi ni mbaguzi wanahisi mtu mwenye rangi black ni mjinga na ni mtu wa jungle/pori hawezi kufanya lolote, hao weupe wachache ni mitizamo yao ya kifikra tu ndiyo inatushawishi kuwa si wabaguzi bali mifumo ndiyo baguzi si kweli kwani kuna watu ambao si weupe wanamifumo ya kibebari na si wabaguzi, kiini cha ubaguzi ni rangi na hii ni colonial mentality of White Supremacy wanajiona bora kuliko race ingine yoyote ile hata kama wangetumia mifumo tofauti na wanayotumia sasa ni bado wanguluwa wabaguzi, utakuja huku Ulaya utakutana na mzungu masikini kabisa wa kutupwa hana kazi, hajuwi kusoma wala kuandika omba omba bado atakuwa mbaguzi, so it not about the system of the economy, it is about race superiority. They think colour it has to do with knowing to much, hata watu wa Asia wenye rangi tofauti na nyeusi pia wanajionasecond to white race na wanatubagua pia, MALCOM X alibadilisha msimamo wake baada ya kuona force haitamsaidia kushindi kitu anacho kisimamia so it was brave thing to change and give that a weak arguement.

  6. Comment by MANI on February 28th, 2010 8:24 am

    tatizo serikali zetu na mifumo yake ndio inaruhusu mpka leo eti mchina anathubutu kumchapa vibao binti wakitanzania na kumtumisha kadri atakavyo au maisha bora kwa mhindi na sikwamzalendo.ukweli nikwamba wenzetu ktk chi zao zimempa nafasi kubwa mzalendo kupata mafanikio ktk kusaka maisha kuliko mgeni.system otomatikali inakubana wewe mgeni na kuona huna jinsi zaidi ya kubeba boksi na kuendelea kumnyeyekea yeye na system hiohio ndio inampa fursa hata akija nchini mwako wewe na viongozi wako mtaendelea kumnyenyekea na kumuona bora.INAUMA SANA UKITEMBEA NDIO UNAONA MENGI SANA.VIONGOZI WAPO KWAAJILI YA MASLAHI YA UMMA LAKINI KWETU VIONGOZI WAPO KWA MASLAHI YAO BINAFSI NA FAMILIA ZAO.NIBORA NCHI IUZWE TUPANGE FOLENI TUPEWE CHETU TUJUE MOJA KUTAWALIWA MPAKA MWISHO WADUNIA KULIKO KUFANYWA WAJINGA ILHALI AKILI TUNAZO,WASOMI TUNAO,MALIGHAFI TUNAZO AH MACHO YENU

  7. Comment by mr. Degree on March 1st, 2010 4:10 am

    Weupe ni wabaguzi, so what? na sisi tuwabague? yaani tutangaze ubaguzi dhidi yao nao watangaze ubaguzi dhidi yetu,hebu tafakari hapo! tukibadilisha mifumo naamini tutaendelea na kupewa heshima yetu kama ambavyo sasa tunawaheshimu wao kwa maendeleo yao! nafikiri ubaguzi wao tuuchukulie kama ni ujinga wao na isiwe ishu kubwa kwetu! tujipange tutafute mfumo utakao tufikisha pale ambapo wao wamefika! najua rasilimali zinazowapa kiburi zinatoka kwetu sasa tunashindwaje kuendelea? ni kujipanga tu bwana Edward! rangi sio ishu!

  8. Comment by mr tele on March 4th, 2010 12:04 pm

    nimefurahi sana kuona coment zenu wote nakuona jinsi gani wa AFRICA tunauchungu na continent ye2 kwa kutoa mifano kama ya malcom,nyererena mpendwa mugabe kwa upande wng nashangaa kuona wa AFRICA wanaomchukia mugabe hao niwa2 wanaojiangalia wenyewe bali c kwa janga le2 na hataa wengine kusema nyerere hakutusaidia TANZANIA, hukitaka kuangalia hawa w2 wanaongea hivi nawa2 ambao tunaweza kusema hali kwa c mbaya ila hawangalii taifa kwa ujumla WHITE r alwayz gonna remain ze same.zey come 2 africa take land thy pretend they invest n after zey get what zey want wanaondoka zao.kuupinga ubaguzi nilazima viongozi,wanasiasa na wananchi kwa ujumla AFRICA kuwa ki2 kimoja co kujinufaisha binafsi na ss wenyewe tujibadilishe co tunawababaikia wazungu

  9. Comment by mwanaharakati on March 4th, 2010 12:19 pm

    kwa upande wng mm naamini ata uchumi waliyo nao leo WHITE people unatokana na wa AFRICA,mfano ni hili swala hisa kuuzwa london nasio kwa wazalendo hiki niki2 cha kushangaza kweli na selikali kupata asilimia 10 kweli waacheni hawa wa2 watunyasenyase

  10. Comment by Guka,Hassan Rajabu CBE DOM on March 10th, 2010 6:07 am

    Nakushukuru sana muandaaji wa Makala hii ya Kumbukumbu Ya Miaka 45 tangu Kifo cha MALCOM X.Binafsi napenda kuchangia kwa kusema kwamba,Watanzania na Waafrika wenzangu hatutaweza kujikwamua kutoka katika manyanyaso kama sisi wenyewe hatujui haki zetu.Tuko nyuma sana kielimu,kiuchumi na kisiasa.Tujielimishe na tuelimishe vizazi vyetu vya sasa na vijavyo ili kwayo tuweze kujua haki zetu,wajibu wetu.Haitawezekana kudai haki bila kutimiza wajibu.Tuwe na tabia ya kujielimisha,elimu inaanzia pale ulipo zaliwa mpaka pale utakapo kufa.Mimi nimezaliwa kijiji huko MRIJO CHINI,katika wilaya ya Kondoa.Miundo mbinu kwasasa ipo ya Mawasiliano,kipato kinaridhisha kwa wastani.Lakini kwakuwa ndugu zangu waliko kule walikosa Msingi wa Elimu hususan ya Sekondari,na wakachagua Style ya Maisha ni kutafuta Fedha,hivyo Fedha wanazo lakini kujiendeleza kwao kielimu sasa nivigumu kwasababu wanamajukumu ya kifamilia.Mimi ninawashauri sasa wabadilike na waweke nguvu zao kusomesha watoto.

Leave a Reply