Imeandikwa na Na Angela Semaya wa Habari Leo

MAISHA yake sasa yamebadilika, amelazimika kuwa mtumwa wa kujificha kwa kuvaa vazi aina la Hijab ambalo anasema kwake limegeuka kuwa vazi analoliheshimu na kulithamini kwa kuwa ndio msiri wake mkubwa siku hizi, hii yote ni gharama inayotokana na moyo wake wa ujasiri na ushupavu uliotokana na kutumia kalamu yake kufichua uovu na unyanyasaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa kuuawa kwa imani za kishirikina.

Kwa walio wengi ndani na nje ya Tanzania, jina la Vicky Ntetema sio geni masikioni mwao kwani ni mwandishi mahiri wa Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Ntetema aliyezaliwa miaka 51 iliyopita ameibuka kuwa mwandishi mahiri, jasiri na shupavu baada ya kufichua siri ya kutisha kutokana na uchunguzi wa mauaji ya albino na familia zao akitaka kujua kwa undani sababu hasa za mauaji na ukatili dhidi ya albino. Hatimaye kazi yake hiyo imemuwezesha kupata Tuzo ya Ujasiri katika fani ya Uandishi wa Habari inayotolewa na International Women’s Media Foundation.

HABARI LEO Jumapili iliamua kumtafuta Vicky baada kutaka kufahamu kwa undani wa kilichomsukuma kufuatilia habari hiyo na kwa kiwango gani amefanikiwa, maisha yake kwa ujumla na kuhusiana na tuzo hiyo.

Ntetema ambaye alifanya uchunguzi wake kwa siri bila woga anasema Novemba, 2007 alipokea ujumbe wa maneno ukimuelezea kuhusu matukio ya kuuawa albino na kukatwa viungo vyao kwa imani za kishirikina, lakini awali naye hakuamini kama hicho kitu kinawezekana.

Na baada ya kufuatilia kwa muda na kujithibitishia habari hizo, alianza kuishawishi BBC, lakini walionekana kusitika wakiwa na mashaka kwamba kweli inawezekana kuwepo kwa matukio hayo? Hata hivyo anasema hakukata tamaa aliwasiliana na waandishi wengine walioko katika maeneo husika nao walimsaidia kuchunguza na kumpa taarifa zaidi.

Wakati akiendelea na uchunguzi wake aligundua kuwa waganga wa kienyeji ndio waliokuwa wakisababisha mauaji ya albino kwa kuwaambia wateja kuwa wanaweza kupata utajiri kwa kutumia viungo vya walemavu hao, ndipo alipoamua kuishawishi tena BBC huku akiendelea na uchunguzi wake kwa njia ya simu kwa kuwasiliana na watu wa Kanda ya Ziwa.

Kile alichokuwa amekusudia kukifanya na kukifichua, kilithibitishwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye Mwezi Machi, 2008 alikemea vitendo hivyo vya kikatili dhidi ya albino na kuweka wazi kuwa tayari watu 19 walishauawa.

“Baada ya Rais kutangaza hivyo, nikasema kama kiongozi wa nchi amekemea kiasi hili na ametaja hadi maeneo yanayohusika na matukio hayo…kwa sababu ya kuwa na uhusiano mzuri na wahariri nilipeleka maombi yangu bila kusita wanisaidie ili niweze kwenda kabisa eneo husika ingawa waliniambia kwa kipindi hicho hawakuwa na bajeti,” anasema.

Dhamira yake ilimsukuma Ntetema kuchukua fedha zake za mshahara na kuamua kwenda Mwanza kwa ajili ya kuendelea na uchunguzi wake. Anasema kazi hiyo ilimlazimu kuzunguka sehemu mbalimbali hadi akajikuta ameishiwa fedha na kulazimika kuomba kwa mama yake.

Akiwa Mwanza, alilazimika kutumia jina lingine kwa ajili ya usalama alifika Kituo Kikuu cha Polisi mkoani humo na kuonana na Kamanda wa Polisi wakati huo, Zelothe Stephen na Mkuu wa Mkoa wakati huo, James Nsekela na walimueleza kwa undani kuhusiana na matukio hayo na kuthibitisha kuwapo.

Hata hivyo polisi walikataa kumsindikiza katika vijiji vinavyotajwa kuwa na waganga wa kienyeji wanaofanya biashara ya viungo vya albino kwa hofu ya kulogwa na badala yake walimuonya kuwa akifika huko asile, asinywe wala kulala ama sivyo anaweza kupotea.

“Kwa kweli nilipata hadithi za kutisha hasa kuhusu kijiji kinachoitwa Gambush, lakini nilisema nakwenda na walikuwa wakiniona mbishi sana…niliamua kununua biblia na rozari, nilimpigia mama, alinitia moyo nimtegemee Mungu,” anasema.

Akiwa Sengerema alikokwenda kufuatilia habari za wavuvi haramu alipigiwa simu na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kuwa mchawi amekwenda kutubu baada ya kufanya kazi hiyo muda mrefu tangu akiwa na miaka mitatu na kuua watu 40.

Ntetema anasema walimkuta mchawi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Daniel Shilinde akiwa ametapika sana yakiwa madonge ya damu na mwisho alilazimika kulazwa hospitali baada ya kuishiwa damu, lakini kila aliyeombwa kumsaidia alikataa kwa hofu ya kurogwa.

“Mimi nilitaka mtu huyu aishi ili anieleze vizuri mambo ninayoyataka kikiwemo hicho kijiji cha Gambush, nikajitolea damu na aliweza kupona na kuniwezesha kunipa taarifa nyingine nilizokuwa nahitaji,” anasema.

Uchunguzi wake ulimwezesha kupita wilaya mbalimbali na akiwa wilayani Magu, alikutana na Mwenyekiti wa Waganga wa Tiba za Asili ambaye alimfafanulia kuwa kuna waganga wa tiba za asili ambao hutumia miti shamba kutibu na kuna waganga wa kienyeji ndio wanaohusika na ushirikina.

Anasema alikwenda Gambush na dereva teksi mmoja ambaye amekuwa akipeleka wafanyabiashara na hata viongozi wa serikali kwa waganga. Alipofika mwandishi mwenzake na dereva teksi waliegesha gari mbali na yeye alienda kwa mganga mmoja maarufu.

“Wakati nikiwa kwa mganga wakati wote kidole kilikuwa kwenye simu ndani ya nguo ili kikitokea chochote niwataarifu wenzangu…sasa nilipofika nikaambiwa nitafute kuku ikabidi nitoe fedha ili akanunuliwe, haya alipoletwa kuku nikaambiwa nimshike kuku na kumueleza shida zangu zote.

“Jamani waganga ni waongo kuku hata sikumueleza chochote, baadaye mganga alivyofika nikamueleza mimi nataka kupata utajiri, lakini cha ajabu nilipokuwa nikimuuliza kuku kasemaje mganga anashindwa kusema mara ooh! lazima usafishe kwanza, nikagundua aha! Hiki ndio nilichoonywa na wenyeji,” anasema na kuongeza kuwa mganga huyo alimtaka alale ili apewe dawa, lakini Ntetema alikataa na matokeo yake mganga huyo aliwaelekeza njia ya kurudia ambayo haipitiki na walikwama hadi waliposukumwa na watu wengine.

Katika uchunguzi wake wote, Ntetema alifika kwa waganga 12 na wawili kati ya hao walithibitisha kwa vinywa vyao kuwa wanaweza kumuuzia viungo vya albino na anaongeza kuwa mara nyingine, lazima ukifanya habari za uchunguzi uwe mjinga ili upate unachotaka.

“Mmh! nakumbuka wakati nikiwa kwa mganga mwisho wakati nataka kutoa fedha kutoka kwenye pochi, kiredio kidogo cha kurekodia kilidondoka ikabidi nifanye kama ni simu.

Akaniuliza unatembea na simu mbili nikamwambia ndio si unajua mara nyingine moja inaweza isipatikane, akaniambia hebu nipe namba nikupigie, nikamwambia namba yake siijui sana mpaka niiangalie, akaridhika ingawa alinitazama sana,”anasema.

Akiwa kwa mganga huyo wa mwisho huko Magu, Ntetema anasema alipigiwa na mganga ambaye alishawahi kwenda kwake awali ambaye alimwambia amemshitukia kuwa si mfanyabiashara, bali mwandishi. Akaenda mbali zaidi na kusema alidokezwa na askari polisi mmoja aliyekuwa ampigia simu mganga huyo.

Kuanzia hapo, simu na ujumbe wa vitisho havikukoma, akalazimika kuwahi Mwanza ambako alishauriwa na mwenyekiti wa waganga wa tiba asilia asirudi hotelini na BBC walimtaka aondoke haraka Mwanza.

“Nikiwa uwanja wa ndege watu wawili walinifuata wakiniambia wao ni maofisa wa usalama wa taifa hivyo wanataka kitambulisho changu na pasi ya kusafiria, lakini niliwataka waonyeshe vya kwao walikataa,” anasema na kuongeza kuwa ilipofika ndege ya Precision na hivyo alipanda na kukimbilia Kenya.

Kutokana na uzoefu wake mwandishi huyu anasema waganga ni watu hatari kwa sababu wana nafasi kubwa katika jamii za kitamaduni za Kiafrika na wanatumia wauaji wa kukodi na wanalindwa na polisi wa kawaida.

Tangu alipoanza kuripoti habari hiyo Ntetema amepokea vitisho na watu wengine walijaribu kumfuata hadi ofisi za BBC Dar es Salaam na kumkosa, hali iliyomlazimu kuondoka nchini mara mbili kwa ajili ya usalama wake ingawa mwenyewe anasema kamwe hawezi kukimbia nchi yake kwa sababu ya waovu.

Katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu anaishi maisha ya kuhamahama huku akitembea amevaa hijab, vazi ambalo anasema analiheshimu sana kwa kuwa linamsaidia kujificha na sio hivyo tu analazimika pia kutembea na mlinzi wake binafsi.

Je, Uandishi wa habari ni kitu alichotamani tangu zamani? Vicky anasema; “Ndiyo.” Na anakiri kwamba, tamaa ya uandishi wa vitabu au magazeti ilimjengea umakini wa kusoma kwa bidii shule ya msingi na sekondari na alipomaliza kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari Jangwani alitakiwa kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), lakini alifanyiwa operesheni ya kongosho.

Hata hivyo serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa lilimtaka kujiunga na JKT na kufanya kazi za kuandika hivyo jukumu lake lilikuwa kuandika majina ya makuruta wapya na kumbukumbu za makuruta waliomaliza mafunzo.

Ntetema anasema akiwa na umri wa miaka 16 baba yake alifariki akiwa shule na kwamba aliona kama ndoto zake zimepotea maana lengo lake ilikuwa kusoma uandishi kisha aje kumuonesha baba yake na pia aliona ana jukumu la kuangalia wadogo zake na mama yake ingawa alikuwa na ndugu zake waliomtangulia.

Hata hivyo, akiwa JKT rafiki yake wa sekondari alimletea gazeti la DailyNews ambalo lilikuwa na tangazo kuwa kuna nafasi za kwenda kusoma Urusi na moja ya kozi ni uandishi wa habari wakati huo ikiwa ni mwaka 1979, aliomba nafasi hiyo na alichaguliwa na wasichana wengine 22 kwa sababu ilitaka wasichana ndio waombe na kati ya hao ni yeye peke yake ndio alikwenda kuchukua masomo ya uandishi wa habari.

Ntetema alisoma miaka saba Urusi na akisomea lugha, upigaji picha, sinema, uandishi wa habari wa magazeti, redio na televisheni na kati ya hiyo miaka miwili alisomea uandishi wa habari za radio. Lakini alipomaliza chuo alipotaka kurudi nyumbani Tanzania kufanyakazi serikali ilimwambia amepata elimu ya juu sana, yaani Shahada ya Pili wakati wahariri nyumbani (Tanzania) hakuwa na elimu kama hiyo hivyo hakuna nafasi ya kazi.

“Unajua wakati tunaondoka tuliingia mkataba na serikali kuwa ukirudi unatakiwa kutumikia kwanza Watanzania kabla ya kufanya mambo mengine, lakini walishindwa kunipa kazi…bahati niliona tangazo la Shirika la Afro International Theatre la Uingereza ambalo walihitaji mwalimu wa Kiswahili na mtu wa kuanzisha jarida,” anasema na kuongeza kuwa alibahatika kupata nafasi hiyo na hivyo mwaka 1987 alitoka Urusi na kuhamia Uingereza.

Mwaka 1991 Ntetema aliona tangazo la BBC, Idhaa ya Kiswahili likitaka mwandishi na hivyo aliomba na alipata nafasi hiyo ingawa kituo kilikuwa, Uingereza lakini alikuwa akisafiri nchi mbalimbali kutafuta habari.

Mwaka 1992 vyombo binafsi vya habari vilianzishwa na aliona tangazo la kituo cha televisheni cha ITV na Radio One aliomba kazi, lakini walipata hofu namna ya kumlipa maana alikuwa ni mwandishi wa kiwango cha juu. Basi alikuwa na kipindi chake maarufu kilichojulikana kama Rekodi Bora maarufu ambacho kilimpa fursa ya kufahamu aina ya muziki na wasanii mbalimbali.

“Nilipenda kuwa mwandishi wa habari zaidi, si DJ. Sikupenda pia kukaa ofisini kutafsiri kazi zinazofanywa na watu wengine nilitaka niende kwenye kazi mwenyewe badala ya kusoma kazi za watu wengine…niliona kama akili yangu inadumaa,” anasema na kufafanua kuwa, kuanzia hapo alianza kutoka nje kwa kazi mbalimbali.

Ntetema anasema aliweza kutembelea nchi za Senegal, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Uganda, Malawi na Zimbabwe ambapo aliweza kupata habari za Waafrika wengine na kuziripoti na kujulikana na watu wengine duniani.

Moja ya kazi zake ambazo pia ni kumbukumbu nzuri katika kazi yake ya uandishi wa habari ni kwenda nchi takatifu ya Israeli kipindi cha mapambo ya mara ya pili ya Palestina kudai maeneo yao kipindi hicho ikiwa ni mwaka 2002.

Ntetema anasema hiyo ni safari ambayo hataisahau hasa akizingatia kwamba alikuwa anakwenda katika nchi takatifu ambayo alikuwa akiisikia kwa kusimuliwa na baba yake kutoka kwenye biblia, aliufikiria mji wa Yerusalemu na Bethlehemu.

“Nilipata faraja, tena hata sikuamini kwamba nakwenda huko. Lakini zaidi nilitaka kujua kwa nini pande hizi mbili zilikuwa zikipigana katika nchi takatifu, nilipofika nilijifunza mambo ya Kiyahudi, Kiislamu na Kikristo.

Nilizungumza na viongozi wao yaani wa Wayahudi Rabi Mkuu, Waislamu Sheikh Mkuu ambaye alikuwa Yassin Arafat na Kiongozi wa Wakristo wa Kanisa Katoliki,” anasema mtoto huyo wa tano kuzaliwa katika familia ya watoto kumi.

Cha ajabu! Alichobaini makundi hayo hayagombani kwa sababu ya dini la hasha! Wanachogombania ni ardhi yaani kila mmoja anataka Nabii Issa Bin Mariam kwa waislamu akija awakute katika eneo hilo takatifu, wakati Wakrito wanataka mtoto wa Mungu akija awakute katika eneo takatifu na Wayahudi wanataka akija Masiha awakute katika eneo hilo takatifu, kimsingi wote walitaka Bwana Yesu akirudi awakute katika nchi takatifu, hivyo hawagombei suala la dini ila ardhi takatifu.

Ntetema anasema alipofanya mahojiano na Hayati Yasser Arafat, kiongozi huyo alimwambia Muislamu wa dhati hawezi kudharau kuzaliwa Bwana Yesu na atamheshimu Bikira Mariakwa hiyo ni lazima aelewane na mkristo. Anasimulia zaidi anasema hawezi kusahau maishani safari hiyo ilimwezesha kufahamu mambo mengi.

Hata hivyo, anakumbuka alilazimika kuondoka Israeli baada ya BBC kumtaka kukimbia haraka maana saa chache zilizopita bomu lililipuliwa mjini Tel Aviv karibu na ofisi za BBC, wakati huo akiwa katika ofisi za Waziri Mkuu wa Israel wakati huo Ariel Sharon, kwani alikuwa na miadi naye ya kufanya mahojiano.

Anakumbuka pia kuumwa na hadi kufariki dunia kwa Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere anasema alifanya habari hiyo akiwa katika wakati mgumu, kwani hakutaka mwalimu afariki dunia. Ntetema, mama wa watoto wawili wa kiume Douglas na Thomas, anasema ujasiri na uhodari wa kufanya habari za uchunguzi umechangiwa na kusoma vitabu vya upelelezi na filamu.

Anatoa mfano wa vitabu vya mwandishi James Hardley Chase, Ian Flemming na Agatha Christine ambavyo anasema vilimsaidia kumpa mbinu za kufuatilia habari za uchunguzi. Vile vile kusoma mtandao na kusikiliza radio.

Mwandishi huo ambaye pia ana Shahada ya Uzamili katika Uhandisi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kutoka Chuo cha Uchumi London, anasema aliamua kusomea taaluma hiyo iwapo siku sauti yake itakauka. “Waandishi pia waangalie na taaluma nyingine ili unapoona unataka mabadiliko unacho kitu kingine cha kufanya.”

Akizungumzia kuhusu Tuzo ya Ujasiri ambayo atakwenda kupokea mwezi Oktoba mwaka huu katika sherehe itakayofanyika katika miji mitatu ya Los Angeles, NewYork na Washington anasema hawezi kufurahia Tuzo hiyo mpaka mauaji ya albino yatakapokoma na watu wenye ulemavu wa ngozi kuthaminiwa.

Wito wake kwa wanawake ni kuwa waachane na fikra kuwa hawawezi kufanya kitu na kutoa mfano wa mtangazaji wa habari wa kwanza mwanamke kutoka Afrika kutangaza BBC, Zeyana Seif (marehemu) kuwa alimhamasisha na kumfanya ajiamini kuwa naye aweza kufanya vizuri kama mtangazaji huyo.

Huyo ndiye Vicky Mtetema, mwanahabari aliyegeuka mkimbizi ndani ya nchi yake.

Pichani Vicky Ntetema akiwa na Mariamu.Picha  na habari kwa hisani ya Habari Leo. Tafadhali usinakili bila ruhusa kutoka Habari Leo.

Feedback / Comments

11 Responses to “VICKY NTETEMA:MWANDISHI MAHIRI “ANAYETESWA” KWA KUFICHUA MAUAJI YA ALBINO”

  1. Comment by Gasper Materu on May 19th, 2010 8:50 am

    Dear dada vicky,

    Taifa hili litakombolewa na watu wenye misimamo na juhudi kama zako…yako mengi tusiyoyajua yanayokwamisha maendeleo na ustawi katika nchi hii lakini hatupati fursa ya kuyajua kwani yamefanywa ni siri kubwa…

    Habari za uchunguzi zinapaswa kuwa chachu kubwa kwa wadau wa habari katika kuuhabarisha umma changamoto mbalimbali zinazowakabili na wao wachukue hatua.. Mimi binafsi nimechoshwa na habari za UDAKU zilizojikita katika muelekeo wa kusifu au kuelezea mambo aliyosikia kwenye vijiwe…

    Wakati tunaendelea kupigania mchakato wa kuifanya tasnia ya habari itambulike kama mhimili wa nne wa dola hatuna budi kuuthibitishia umma kwa unagaubaga kuwa tunaweza kubeba jukumu hilo zito

    God bless you.
    Regards
    Gasper.

  2. Comment by SALIM on May 19th, 2010 8:54 am

    …..MTENDA MEMA HULIPWA MEMA……
    TUNAFURAHISHWA SANA NA KAZI YAKO MUNGU NDIYE ATAKULIPA,NA DAIMA UTAKUWA MOYONI MWA WATENDA MEMA………..

  3. Comment by ritta on May 19th, 2010 3:33 pm

    mimi niliwahi kuona habari zake nimefurahi sana habari hii tungepata watu kama vick mia moja ktk nchi tungepona na magojwa yanayotusumbua ikiwemo rushwa

  4. Comment by BLACKMANNEN on May 20th, 2010 12:05 am

    Dada Vicky Ntetema,

    Hongera sana kwa kupewa tuzo unayostahili kutokana na kazi yako ya uandishi wa habari ambayo umeyaepusha maisha ya Watanzania wengi kupotea kutoka kwa wenzetu wachache wenye uchu wa utajiri.

    Wewe mwenyewe ulikuwa umeyaweka maisha yako rehani kwa ajili ya kutusaidia Watanzania wenzako katika kutafuta kiini na kwa undani wa mauaji yaliyokuwa yakiendelea, kama vile hakukuwa na chombo cha serikali cha kuyalinda maisha ya Watanzania.

    Dada Vicky, pole sana kwa kujikuta ukiishi maisha ya aina ambayo wewe mwenyewe hukupenda uyaishi. Mwenyezi Mungu atakulinda na atakupa nguvu zaidi za kuwashinda hao maadui wetu wote.

    Mtu huwezi kuamini kuwa ni Polisi aliyewapigia simu waganga kuwaambia kuwa wewe ulikuwa ni Mwandishi wa Habari za Upelelezi kwao. Je, watu tukimbilie wapi sasa kuokoa maisha yetu kama sio Polisi?

    Dada Vicky, kazi uliyoifanya ni kubwa kuliko hata huyo Waziri aliyepewa dhamana ya kuwalinda Watanzania. Umeokoa maisha ya Watanzania wengi, si maalbino tu. Tangu ulipouanika nje uozo mzima wa mauaji ya maalbino, mauaji ya vizee pia ilipungua.

    Dada Vicky, najisikia “sifa” sana ninapokumbuka kuwa, mimi katika maisha yangu nilishawahi kukutana na kuongea na wewe Vicky, LIVE huko Voronezh mwaka 1981.

    Wakina mama wa Kitanzania kote duniani, Vicky ni Mwana Mama wa kujivunia. Kuliko mnavyoshabikia wakina Mama wa nchi za nje. Mwana Mama Vicky, ni jasiri mwenye kudiriki hadi kutoa damu yake kwa ajili ya kuokoa Watanzania wenzake. Hakuna mwanaume wa Kitanzania aliyefanya vitu kama hivi. I Salute You Vicky!!!

    It’s Great To Be Black=Blackmannen

  5. Comment by Anita on May 20th, 2010 1:24 am

    Kwanza kabisa napenda kukupa hongera dada Vicky, kwa moyo wa upendo na ushujaa katika kutetea suala hili mauaji ya albinos.umeweza kutufungua hata sisi tuliopo nje ya nchi jinsi gani tunaweza kusaidia hawa ndugu zetu albinos, na unyanyasaji huu ukomeshwe ni aibu iliyooje.please ntakutafuta dada vick.
    Mungu akubariki
    Anita

  6. Comment by aminatha on May 21st, 2010 5:24 am

    congratulations,

    may the blood of jesus should always protect you.

  7. Comment by Samuel on May 21st, 2010 5:57 pm

    Dada Vicky Mungu akubarikie na kwa kujitolea kwako na akutie nguvu uzidi kuwa na moyo huo maneno ya kiswahili pekee hayatoshi kuonyesha jinsi nilivyoguswa,Ubarikiwe.

    Kwa wale wanao mwaga damu isio na hati akwa tamaa zao wenyewe wajue Mungu yupo na anaona,damu y andugu zetu hawa inalia kwenye ardhi yetu Tanzania,jamani kwanini mtu afanye kitu cha kikatili namna hii??? Mungu ataja jilipia kisasi. ni aibu ambayo haina mfano kwa taifa letu,Mungu tusaidie hurumia taifa letu, Mataifa mengine yasio na amani sio kwamba walipenda,”Baadhi” ni kukithiri kwa uovu na mengin eni ukaidi,hebu ndugu zagu Watanzania tumuogope Mungu,si lazim atufanye waganga wanachotuambia na hakuna ulazima wa kwenda kwao.

  8. Comment by paul joseph on May 21st, 2010 9:04 pm

    Hi, dada vicky pole sana kwa kuishi bila amani pili kuwa kama mkimbizi wa nchini mwako ,vicky swala la kuawa albino lipo hata mimi linaniuma sana lakini ankosa uwezo wa kuwapigania albino kwani ninae msichana albino ambaye niliamua kuwa namtunza kutokana na ndugu yake ambaye alitakaga kumuuza kwa watu ambao ni wachimba madini msichana huyo aligundua baadae alikimbilia dar es salaam na yupo mpaka sasa viki albino wana uawa mno hasa kasikazini mwa tanzania hili suara kama upo tayari naomba tuungane pamoja kuwapigani albino nitakuwa msitari wa mbele wengi wamekatwa mikono kutokana na tamaa ya watu kutaka utajiri vicky .hata baba au ndugu kuamua kumuza mtoto wake ambaye ni albino sababu ya utajiri vicky ukiwa kama mwandishi wa habari dunia nzima ijue swala hili kwani unapomwambia mtu kuwa africa wanaua albino anashangaa tafadhali tushirikiane ili tutokomeze hili balaaa ,wengine wanachukua sehemu zao za siri kwa ajiri ya matambiko vicky mimi nipo tayari kuwa na wewe msitari wa mbele na hata picha za albino wanao uawa
    Nb, vicky mimi nakaa america na hiyo ndio email yangu plse tuwasiliane
    Bye

  9. Comment by solomon on June 2nd, 2010 7:14 am

    Hongera sana dada,wala wasikukatishe tamaa,nipo radhi kukusaidia mpaka the end point ili tupate solution ya mambo madogo yanayoangamiza jamii,usitishike na hao wajinga wachache kama ni uchawi mungu wetu naye hajatuacha,wakimwaga mboga tunamwaga ugali.

  10. Comment by felix mallya on December 3rd, 2010 10:06 am

    Ndugu yangu Vicky Ntetema, hongera sana kwa maisha ya kujitoa sadaka kwa ajili ya watu wengine wenye kuteseka bila sababu.
    Hili ni somo umetoa kwa watu wengine ambao hatujafanya lolote la namna hiyo. Sina maan ya kufanya kitu kama hicho tu bali jambo lolote muhimu kuondoa japo kero moja kati ya nying ambazo zimeikabili jamii ya Afrika na hasa nchi yetu Tanzania.Umefungua barabara, naamini tutaifuata kwa namna nyingina kwa manufaa ya watu wetu katika nchi, bara na dunia hii. Mungu aliyeanzisha ujasiri huu ndani yako na kukutumia kukomboa wenzetu albino, atakusimamia na hakuna atakayeweza kufanikiwa kuyadhuru maisha yako. Jipe moyo na songa mbele, siku moja watafahamu unachofanya na watakuheshimu badala ya kuyawinda maisha yako. Kwa sasa, jitahidi sana kuwa mpole kama njiwa lakini mwerevu kama nyoka. Kwa watanzania wenzangu, tumlinde Vicky na tujifunze kitu kwake.
    Kama jumuiya ya kimataifa imemtambua, sisi tuansubiri nini wakati yeye ni ndugu yetu hapa na amefanya kazi miongoni mwetu na kwa manufaa ya nchi yetu? Nadhani tumeshapata aibu kubwa. Mtu wetu anafanya kazi nzuri hapa nyumbani hatujaitambua kazi yake mahiri badala yake tunahatarisha maisha yake! Mambo gani haya ndugu zangu watanzania na hasa wenye nafasi za kuweza kutoa tamko la kubadili hali halisi kwa vitendo? Tunakwenda wapi? Tnasubiri wazungu wamtunuku mtu kwa kazi aliyoifanya kwetu? Kwa nini tusianze sisi? Bado hatujachelewa, tuamke sasa tutaweza kurejesha heshima yetu na nchi yetu kwa kuyadhamini maisha ya watu wetu wote bila ubaguzi wa namna yoyote ile.

  11. Comment by Mubaarak on March 20th, 2011 4:43 pm

    Hello….Kwanza kabisa natoa shukrani zangu kwa dada Vicky Ntetema, kwa kweli kazi anaifanya ni kubwa sana na sio ya kawaida na kila mtu anatakiwa kuikubali, a few days ago…nilikuwa na dada Vicky katika office yetu na yuko tofauti sana na jinsi tunavyomuona katika vyombo vya habari, Dada Vicky yeye ni mtu wa watu na rafiki wa kila mtu na wala haringi wala kujidai nimeshuhuduia hata watoto wadogo sana amezunguza nao na aliweza hata kukaa chini mahali ambapo mtu yeyote alieko juu kama yeye hawezi kukaa. kwa kifupi dunia imehitaji mtu mwenye upendo, akili, busara wa kuweza kushulikia suala zima la watu wenye ulemavu wa ngozi na sasa tumempata dada Vicky Ntetema. Hongera sana na karibu tena IZAAS MEDICAL PROJECT

    Mubaarak Abdullah

Leave a Reply