
Msanii maarufu wa vipindi vya redio,maarufu kama Mzee Pwagu(jina lake halisi ni Rajab Kibwana Hatia),amefariki dunia hivi leo katika Hospitali ya Amana jijini Dar-es-salaam alipokuwa amelazwa kwa muda,akisumbuliwa na ugonjwa wa kwikwi(hiccups) pamoja na matatizo mengine yatokanayo na uzee.
Kama utakumbuka, kabla ya ujio wa televisheni au luninga nchini Tanzania kila mtu alikuwa akitegemea Radio Tanzania Dar-es-salaam(RTD) katika kupata habari,burudani na elimu kupitia sanaa ya kuigiza kupitia kitu kilichojulikana kama “michezo ya redio”. Hapo ndipo vipindi kama vya Pwagu na Pwaguzi vilipotamba.
Kipindi cha Pwagu na Pwaguzi kilikuwa kinarushwa hewani hewani kila Jumamosi kuanzia saa 11:45 hadi 12;00 jioni na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) tangu mwaka 1966 mpaka miaka ya 1980.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kikundi cha Sanaa cha Kaole ambapo marehemu alikuwa mwanachama(kama mshauri) mpaka alipofariki, mazishi yanaweza yakafanyika kesho. Shughuli zote za msiba zinafanyikia nyumbani kwake maeneo ya Kigogo Mbuyuni jijini Dar-es-salaam.
Mzee Pwagu alizaliwa mwaka 1923 mjini Tabora. Ameacha mke na watoto wawili. Mmoja kati ya watoto wake ndiye mama mzazi wa msanii chipukizi Abdul Ahmad Salum maarufu kwa jina la Mr Benny wa kundi la Sanaa la Kaole.
Mwenzake,Pwaguzi, ambaye jina lake kamili ni Ali Said Keto,naye alishafariki dunia miaka kadhaa iliyopita.
MWENYEZI MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU MAHALA PEMA PEPONI,AMINA.
Picha na sehemu za habari/Habari Leo Ukitaka kujikumbusha kidogo mchezo wa Pwagu na Pwaguzi,Bonyeza hapa.
Page 1 of 3 | Next page