Upo msemo usemao “Biashara au mali bila daftari,hupotea bila habari”.Msemo huo naweza kuufananisha na ugumu wa kuendesha kitu kama nchi bila bajeti.Haiwezekani. Pengine hiyo ndio sababu kubwa kwamba kila mwaka,Waziri wa Fedha,pamoja na majukumu mengine aliyonayo, huwa pia ana jukumu la kuwasilisha bungeni Bajeti ya mwaka unaofuata wa fedha na uchumi.
Tarehe 10 Juni mwaka 2010 ilikuwa ni siku ya kuwasilishwa kwa Bajeti ya nchi yetu kwa mwaka 2010/2011. Pengine umeshapata nafasi ya kuisoma au kuipitia. Nimeona ni jambo jema niiweke hapa BC bajeti hiyo kwa kuzingatia mambo kadhaa yakiwemo; Huu ni Mwaka wa Uchaguzi.Ukitaka kujua tunapoelekea katika miaka kadhaa ijayo,basi huna budi kuisoma kwa makini bajeti hii.
Pili,baada ya kuyumba kwa uchumi wa dunia,ni muhimu kujua nchi zinazoendelea kama yetu ya Tanzania zimejipanga namna gani kukabiliana na hali halisi ya “ahadi za misaada na mikopo” ambazo ni dhahiri zitakuwa ngumu kutekelezeka. Je,tumejiandaaje? Tunalenga kuingiza kiasi gani kama pato la taifa na tunapanga kukopa kiasi gani kutoka kwa wafadhili? Tunapanga kutumia kiasi gani? Mwaka uliopita ulikuwaje? Kwa majibu ya maswali kama hayo na mengineyo mengi,hii hapa ni Bajeti nzima kwa mwaka 2010/2011 kama ilivyowasilishwa Bungeni na Waziri wa Fedha,Mheshimiwa Mustafa H.Mkulo(pichani) hivi karibuni;
HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA UCHUMI, MHE. MUSTAFA HAIDI MKULO (MB.), AKIWASILISHA KATIKA BUNGE MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2010/2011, TAREHE 10 JUNI, 2010
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2010/2011. Pamoja na hotuba hii, vipo vitabu vinne vinavyoelezea kwa kina takwimu mbalimbali za bajeti. Kitabu cha Kwanza kinahusu makisio ya mapato. Kitabu cha Pili na cha Tatu ni vya makisio ya matumizi ya kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kitabu cha Nne kinaelezea makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2010 ambao ni sehemu ya bajeti hii.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote ningependa kuchukua nafasi hii kueleza kuwa, Bajeti ya mwaka wa fedha 2009/2010 unaomalizika mwezi huu, inakamilisha kipindi cha miaka mitano cha Serikali ya Awamu ya Nne iliyoingia madarakani Desemba 2005. Katika kipindi hiki, Bajeti imetumika kama chombo muhimu katika kutekeleza Sera na Malengo ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala cha CCM. Kwa hiyo, bajeti ya mwaka wa fedha 2010/11 inalenga kuendelea na utekelezaji wa sera na malengo ya kiuchumi na kijamii. Katika kipindi hiki, yamekuwepo mafanikio ya kuridhisha katika kutoa huduma bora kwa wananchi na kuimarisha miundombinu ili kuwezesha uchumi kukua na kupunguza umaskini.
3. Mheshimiwa Spika, naomba pia nichukue fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha matayarisho ya Bajeti hii. Maandalizi ya bajeti ya Serikali yanahusisha wadau na vyombo mbalimbali. Kipekee ninaishukuru Kamati ya Fedha na Uchumi chini ya uenyekiti wa Dkt. Abdallah Omari Kigoda, Mbunge wa Handeni, pamoja na kamati nyingine za kisekta kwa ushauri mzuri waliotoa wakati wakichambua mapendekezo ya bajeti hii. Naomba niishukuru kwa namna ya pekee Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2010 na nyaraka mbalimbali za kisheria ambazo ni sehemu ya bajeti hii.
4. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Wizara ya Fedha na Uchumi, nawashukuru Naibu Mawaziri, Mhe. Jeremia H. Sumari (Mb) na Mhe. Omari Y. Mzee (Mb). Namshukuru Katibu Mkuu Ndugu Ramadhani M. Khijjah na Naibu Makatibu Wakuu, Ndugu John M. Haule, Ndugu Laston T. Msongole na Dkt Servacius B. Likwelile, pamoja na Katibu Mtendaji Tume ya Mipango; Dkt. Philip. I. Mpango. Aidha, napenda kuwashukuru Wakuu wa Idara na wafanyakazi wote wa Wizara ya Fedha na Uchumi. Vile vile, namshukuru Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa kuchapisha hotuba hii kwa wakati. Mwisho, nawashukuru wataalamu na wale wote waliotoa mapendekezo kuhusu sera, mikakati na masuala mbalimbali ya kodi ambayo yamezingatiwa katika kuandaa Bajeti hii.
5. Mheshimiwa Spika, huu ni mkutano wa mwisho wa Bajeti kwa Bunge hili baada ya miaka mitano ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Nne. Wengi wetu tutarudi kwa wananchi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi yetu, kuomba ridhaa yao ya kurudi tena katika ukumbi huu. Nina matumaini makubwa kuwa, wananchi hawatasahau kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Awamu hii.
6. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mkakati wa Taifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA); Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs); na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005. Napenda kulipongeza Bunge lako Tukufu chini ya uongozi wako, kwa mchango mkubwa ambao umeiwezesha Serikali kupata mafanikio makubwa katika kipindi hiki.
Mafanikio ya utekelezaji wa Sera za Bajeti na changamoto zilizojitokeza katika kipindi cha Awamu ya Nne
7. Mheshimiwa Spika, yafuatayo ni baadhi ya mafanikio ya Serikali katika kipindi cha kwanza cha Awamu ya nne:
(i) Mapato ya ndani ya Serikali yameongezeka kwa asilimia 121 kutoka shilingi 2,124.8 bilioni mwaka 2005/06 hadi shilingi 4,688.3 bilioni ambazo zinatarajiwa kukusanywa kwa mwaka 2009/10. Mapato ya ndani yamefikia zaidi ya wastani wa shilingi 390 bilioni kwa mwezi ikilinganishwa na wastani wa shilingi 177 bilioni mwaka 2005/06, sawa na ongezeko la zaidi ya mara mbili katika kipindi hicho. Aidha, mapato ya ndani kama asilimia ya Pato la Taifa yaliongezeka kutoka asilimia 12.5 mwaka 2005/06 hadi asilimia 16.4 mwaka 2009/10. Hii imesababishwa na jitihada za Serikali katika kuboresha sera za kodi na usimamizi wa ukusanyaji wa mapato;
(ii) Jumla ya misaada na mikopo ya Bajeti (GBS) iliongezeka kutoka shilingi 588.702 bilioni mwaka 2005/2006 hadi shilingi 1,307.707 bilioni zinazotarajiwa kupatikana kwa mwaka 2009/10. Aidha, misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo iliongezeka kutoka shilingi 1,047.266 bilioni mwaka 2005/06 hadi kufikia shilingi 2,825.431 bilioni ambazo zinatarajiwa kupatikana kwa mwaka 2009/10. Hii imetokana hasa na utekelezaji wa Mkakati wa Pamoja wa kusimamia Misaada (MPAMITA) pamoja na uhusiano mzuri uliopo baina yetu na washirika wa maendeleo;
(iii) Jumla ya matumizi ya serikali yaliongezeka kutoka shilingi 4,131.946 bilioni mwaka 2005/2006 na matarajio ni kwamba hadi Juni 2010 matumizi yote yatakuwa shilingi 9,238.801 bilioni. Katika kipindi hicho matumizi yalizingatia katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, MKUKUTA, Malengo ya Milenia 2015 na katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005;
(iv) Mikopo iliyotolewa na mabenki kwa sekta binafsi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi iliongezeka kutoka shilingi 1,571.0 bilioni mwezi Desemba 2005 hadi shilingi 4,836.0 bilioni mwezi Oktoba 2009. Sera sahihi za fedha (prudent monetary policy) zimechangia ongezeko hilo;
(v) Deni la Taifa limepungua kutoka Dola za Kimarekani 10.01 bilioni mwaka 2005/06 hadi kufikia Dola za Kimarekani 8.25 bilioni mwaka 2008/09 sawa na upungufu wa asilimia 18. Kwa mujibu wa mwenendo wa viwango vya deni kuwa himilivu, Deni la Taifa linaonesha kuwa linadhibitiwa na linahimilika;
(vi) Miundombinu ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na barabara, nishati na umwagiliaji imejengwa na kukarabatiwa. Sekta ya elimu imeimarishwa ikiwa ni pamoja na kujenga shule za sekondari za Kata, Chuo Kikuu cha Dodoma na kuvipa hadhi baadhi ya vyuo kuwa vyuo vikuu;
Page 1 of 11 | Next page