“UTANGAZAJI NI KAMA KAZI ZINGINE ZOZOTE,PEOPLE SHOULDN’T JUDGE US”-SAUDA MWILIMA

Jina la Sauda Mwilima (pichani)sio geni miongoni mwa watanzania wengi hususani wapenzi wa vipindi mbalimbali vya televisheni.Yeye ni mtangazaji kupitia Kituo Cha Televisheni cha Star kinachomilikiwa na kampuni ya Sahara Communications sambamba na vituo vya radio vya Kiss FM na Radio Free Africa.Vipindi anavyoruka navyo hewani ni Bongo Beats na Mcheza Kwao.

Hivi karibuni BC ilipata nafasi ya kufanya naye mahojiano utakayoyasoma hivi punde.Je unajua Sauda anapendelea kuvaa namna gani anapotoka?Kuna mahali maalumu anapopenda kununulia “viwalo” vyake? Ana ushauri gani kwa vijana wengine ambao wangependa kuja kufanya kazi ya utangazaji kama yeye? Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo;

BC: Sauda,asante sana kwa kukubali kufanya nami mahojiano haya…mambo vipi?

SM: Mambo fresh tu.Nashukuru Mungu,siku zinakwenda.

BC: Kwa kuanza na kwa faida ya wasomaji wetu,unaweza kuniambia ulizaliwa lini,wapi,ukakulia wapi na mambo kama hayo?

SM: Nilizaliwa miaka 30 iliyopita,hapa hapa jijini Dar-es-salaam katika hospitali ya Rufaa ya Muhimbili.Baadaye tulihamia Dodoma ambapo niliishi mpaka nilipomaliza elimu ya msingi ambapo nilirudi jijini Dar-es-salaam.Mpaka sasa maisha yanaendelea hapa hapa jijini Dar.

BC: Ilikuwaje ukaamua kufanya kazi ya utangazaji wa televisheni?Unaweza kukumbuka siku yako ya kwanza uliporekodi au kurusha kipindi cha televisheni “live”?

SM: Wakati nipo sekondari, ndoto yangu kubwa ilikuwa nikimaliza shule niwe Mwanasheria au Mwandishi wa Habari.Lakini baada ya kumaliza shule nikaangukia kwenye mambo ya habari. Na kikubwa zaidi nilivutiwa katika kazi ya utangazaji na dada yangu, Saida Mwilima, ambaye alikuwa mtangazaj TVT(Televisheni ya Taifa) ambayo kwa sasa inajulikana kama Tanzania Broadcasting Corporation (TBC). Nilivutiwa sana na kazi aliyokuwa akiifanya sister kwa sababu ni mtu ambaye nilikuwa naishi naye kipindi nasoma.Wakati huo yeye tayari alikuwa mtangazaji.

Yeah nakumbuka kipindi cha kwanza kwenda hewani ilikuwa mwishoni mwa mwaka 2004.Katika kipindi hicho niliwahoji AY,Ray C,Stara Thomas,Banana Zorro na Ruge Mutahaba. Hicho kilikuwa kipindi kimoja ambacho tulikuwa tunajadili kuhusu wasanii wa Kiume kuwapa support wa kike.Ruge nilimhoji katika nafasi ya Promoter anayechangia kukua kwa muziki.Hicho ndicho kilikuwa kipindi changu cha kwanza.

BC: Tuambie kidogo kuhusu kipindi chako pale Star TV.Maandalizi ya kipindi huwa yakoje na kwa mtu ambaye hajawahi kuangalia kipindi chako,nini maudhui ya kipindi?

SM: Star Tv nina vipindi viwili ambavyo nafanya kwa sasa. Cha kwanza kinaitwa Bongo Beats na cha pili kinaitwa Mcheza Kwao. Miaka miwili iliyopita niliwahi kufanya kipindi cha Afya.

Maandalizi ya kipindi ni kwamba kabla sijakutana na msanii husika kwanza huwa nafanya research(utafiti) kumhusu yeye kwa kutumia vyanzo mbalimbali. Kutokana na ninachokuwa nimepata kutoka kwenye utafiti,ndio naandaa maswali yangu. Kinachofuata baada ya hapo ni miadi ya kukutana katika location kwa ajili ya mahojiano. Kipindi cha Bongo Beats kinaruka hewani kila siku kasoro Jumapili tu.

Kuhusu kipindi cha Mcheza Kwao,maandalizi yake huwa hayatofautiani sana nay ale ya kipindi cha Bongo Beats isipokuwa katika kipindi hiki huwa zaidi nafanya mahojiano na watu maarufu. Hapa nakutakana na wacheza filamu,warembo,wadau wa sanaa tofauti tofauti na mtu yeyote ambaye kwa namna moja au nyingine ana mchango katika jamii inayotuzunguka. Kipindi hiki huwa kinaruka hewani mara moja kwa wiki,siku ya Jumamosi Saa Nne na Robo usiku na kisha marudio yake hurushwa siku ya Ijumaa Saa Nne asubuhi.

Maudhui ya kipindi cha Bongo Beats ni kumuwezesha msanii kufahamika zaidi kwa mashabiki wake na vile vile kujielezea zaidi kuhusiana na nyimbo zake na mwisho kabisa kuwaburudisha watazamaji.

BC: Mpaka hivi sasa kuna kipindi chochote ambacho ulishakirusha hewani ambacho unaweza kusema ndicho ulichokipenda zaidi kuliko vingine vyote?

SM: Kwa kweli vipindi ambavyo nimeshafanya mpaka sasa ni vingi sana na kila kipindi kina utofauti wake maana unaambiwa safari moja huanzisha nyingine.

Vipo vipindi vingi sana ambavyo nimevipenda sana lakini kipindi ambacho naweza kusema nilikipenda sana ni cha binti aitwaye Zena Salehe. Huyu binti alianza muziki akiwa bado mdogo sana.Hivi sasa amekua.Nilimfanyia mahojiano ndani ya Bongo Beats akiwa darasa la pili.

Wakati akinijibu maswali, mwili wangu ulikuwa unanisisimka kutokana na majibu aliyokuwa ananipa. Yalikuwa hayafanani na umri wake kabisa.Alikuwa anajiamini kushinda hata wasanii wakubwa.Nilikipenda sana na pia nilipongezwa na watu wengi sana kutokana na kipindi kile.

BC: Bila shaka kuna watangazaji wengine wa televisheni duniani ambao unawafuatilia na ambao unapenda kazi zao.Unaweza kuniambia kidogo kuhusu mtangazaji au watangazaji hao na kwanini unapenda zaidi kazi zao?

SM: Nampenda sana Mwanamama Oprah Winfrey. Sijui hata nielezee vipi hisia zangu maana napenda sana utendaji wake wa kazi.Napenda jinsi anavyojiamini na jinsi anavyouliza maswali. Nina uhakika yule ni mmoja miongoni mwa watangazaji hodari sana duniani.

BC: Kazi ya utangazaji wa televisheni inakwenda sambamba kabisa na kuwa maarufu.Je,kuna nyakati umaarufu huo unakusumbua?Kivipi?

SM: Siwezi kusema kama nasumbuka sana ila ndio hali halisi.Kikubwa zaidi watu wanatakiwa waelewe kwamba utangazaji ni kazi tu kama kazi zingine zozote.Tofauti pekee iliyopo ni kwamba sisi tunaonekana na kujulikana kwa watu wengi.Mara nyingi watu wanatu-judge vibaya kitu ambacho kinakera kupita kiasi.

BC: Nikikupa nafasi ya kujifafanua au kujielezea wewe mwenyewe kwa kutumia maneno matano(5),ungetaja maneno gani?

SM: NAJIHESHIMU SANA PIA MPENDA WATU.

BC: Kazi ya utangazaji inakwenda sambamba na suala zima la style na fashion.Unaweza kuniambia kwa kidogo kuhusu style yako.Unapendelea zaidi kuonekana au kutoka namna gani na unapendelea duka au maduka gani ya nguo na vitu vingine vya urembo ili kukidhi mahitaji yako?

SM: Kuhusu style napenda zinazokwenda na wakati lakini zenye heshima.Kama ni nguo napenda kuvaa kutokana na sehemu ninayokwenda maana kila sehemu ina aina yake ya nguo. Kuhusu viatu napenda sana viatu virefu.Kama ni vifupi basi iwe raba.Kuhusu maduka sina duka maalumu.Ntaingia popote pale ili mradi pawe na kitu kizuri ntakachopendezewa nacho.

BC: Akitokea kijana akakwambia “Sauda,napenda sana kuja kufanya kazi ya utangazaji wa televisheni kama unavyofanya wewe” ungempa ushauri gani?

SM: Cha kwanza kabisa nitamuulza klichomvutia.Pili nitampa ushauri unaohitajika katika utendaji wa kazi na kisha ntamkaribisha kwa moyo mkunjufu.

BC: Nini mipango yako katika miaka mitano ijayo?

SM: Kikubwa zaidi ni kujiendeleza zaidi kmasomo. Hivi sasa ninayo Advanced Certificate in Journalism.Nahitaji kujiendeleza zaidi ya hapa nilipofikia.Pia napenda kuwa mfanyabiashara na pia kuendelea na kazi. Kingine ni kuwa na familia yangu mwenyewe.Panapo majaaliwa kuwa na watoto japo wawili.

BC: Asante sana Sauda.Nakutakia kila la kheri katika kazi zako.

SM:Asante na wewe pia.Kila la kheri.


 1. eliza, 17 August, 2010

  jaman napenda kuwa mtangazaji mimi uta nishauri vp npo 4m4 sasa iv

 2. chiku, 23 June, 2011

  Jamani nampenda sana huyu dada Saida Mwilima
  Namjua siku nyingi sana ila,sijui imekuwaje, kwa nini ajichibue kiasi hicho, mbona alikuwa bomba tu japo vichunusi kwa mbali , ambapo angeweza kutumia njia nyingine ya kutoa chunusi na si kujichubua kiasi hicho
  Naomba kumshauri kwamba aachana na hayo mambo ya mkorogo

 3. consolata, 03 January, 2012

  Kwanza npenda kumpongeza sana dada Sauda kwa kazi yake ya utangazaji anayoifanya, vilevile hata vipindi vyake anavyovifanya mana vinanivutia sana kwa ilo.hongera kwa ilo dada.
  Pia mie napenda sana hii kazi ya utangazaji sababu ipo ndan ya damu na pia kwa sasa ndo naisomea katika chuo cha TUMAINI-IRINGA. Hivyo nilikuwa naomba sana ushauri wake nifanyaje ili nami siku moja niwe kama yeye jamani?

Copyright © Bongo Celebrity