
Mafanikio maishani yana sura nyingi. Tunatofautiana katika maana nzima ya mafanikio.Unachokiona wewe kuwa ni cha mafanikio yawezekana jirani yako akakiona si mali kitu.
Pamoja na tofauti hizo za maana au matinki ya mafanikio,wengi tunakubaliana kwamba furaha na amani maishani ni miongoni mwa mafanikio au malengo muhimu sana ya binadamu. Kila mtu anataka kuishi maisha yaliyojaa furaha na amani.Ndio maana tunapokumbwa na vitu ambavyo kibinadamu havikaribii kabisa maana ya furaha na Amani,wengi wetu huangua vilio,kujuta,kulaumiana,kufarakana nk.Kila mtu anatamani kutokuwa na huzuni au masononeko mbalimbali moyoni.
Tunatofautiana pia katika mbinu za kujenga maisha yenye furaha na amani. Kwa wengine,kuwa na pesa nyingi ndio furaha.Ndio kipimo chao cha furaha.Kwa mwingine kuendesha gari ya thamani kubwa ndio kipimo cha furaha yake.Mifano ipo mingi.
Pamoja na tofauti za kimantiki na mbinu za kuwa na furaha na amani,yapo mambo mbalimbali madogo madogo(kwa wengine yanaweza kuwa makubwa) ambayo binadamu anaweza kuyafanya ili kujiongezea furaha maishani na kuwa na amani zaidi.Haya ni mambo ambayo sote tunaweza kuyafanya bila kuzingatia sana jinsia wala hali za vipato vyetu. Ni mambo gani hayo? Leo tutaangalia baadhi ya mambo hayo.
-
Piga marufuku mawazo hasi(negative thoughts): Furaha ya kweli huanzia kwenye akili yako na mawazo yako. Ukijipa mawazo hasi,ni wazi kwamba kitu kinachoitwa furaha utakuwa unakipiga kikumbo kwenda nje.
Bahati nzuri ni kwamba kama binadamu,tumepewa uwezo mkubwa wa kuchagua. Unaweza kuchagua kuilisha akili yako mawazo hasi,yasiyojenga,yasiyo leta maendeleo yoyote au unaweza kuamua kuilisha akili yako mawazo chanya(positive thoughts),ya kimaendeleo na yanayojenga.Chaguo ni lako.
Nimeshawahi kusikia watu mbalimbali wakilalamika kwamba hawana furaha maishani. Cha ajabu ni kwamba watu hao hao ukiwasikiliza sana katika maongezi yao,wamejaa mawazo hasi.Kila kitu kwao ni kibaya,kila mtu ni mbaya. Mahali pa kuanzia ni kichwani,akilini mwako.Jijengee tabia ya kuhifadhi mawazo mazuri. Mabaya achana nayo.Hayakufai na huna muda nayo.
-
Angalia mazuri ya kila jambo: Hili halitofautiani sana na hilo hapo juu. Tofauti inakuja katika utekelezaji. Wakati kupiga marufuku mawazo hasi kunatokea au kunatakiwa kutokea kabla ya tukio au matukio fulani, hili la kuangalia mazuri katika kila jambo hutokea baada ya kitu fulani. Kwa mfano:Una mtoto ambaye hakusikilizi? Badala ya kuzidi kumfokea na kulaani bahati yako ya kumzaa,kwanini usitumie nafasi hiyo kumfundisha jinsi na faida ya maelewano miongoni mwa binadamu. Kwanini usichukulie hali hiyo kama mojawapo tu ya mambo ambayo wewe kama mzazi ni lazima uyapitie? Kwanini usimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukupa mtoto kwani unajua kabisa kwamba wapo wengine wengi ambao wanaomba kupata mtoto/watoto?
Ushauri wangu ni kwamba angalia mazuri ya kila jambo. Unapokabiliwa na majaribu ambayo yangeweza kukudidimiza katika mawazo hasi,chagua upande mzuri.Jiulize naweza kujifunza nini kutokana na jambo hili? Je kuna lolote zuri?
-
Fanya mazoezi: Naelewa kwamba sio kila mtu ni mshabiki au mpenzi wa mazoezi. Nimeshawahi kuongea na binti mmoja ambaye alidiriki kabisa kuniambia kwamba yeye hakuumbwa afanye mazoezi. Anasema mazoezi sio sehemu ya maisha yake na wala haitokaa iwe.
Kwa ufupi binti yule anakosea. Hajazingatia analolisema na kuliamini.Naomba nikuambie kitu kimoja; tabia ya kufanya mazoezi inaweza kukuletea muujiza wa furaha maishani mwako.Ingawa watu wengi hufanya mazoezi kwa nia ya kuboresha muonekano wao, mazoezi ni njia nzuri sana ya kuondoa mawazo mabaya,maradhi mbalimbali ambayo husababisha ukosefu wa furaha na amani.
Mazoezi huleta dhana ya kujiamini na pia ni njia nzuri ya kupata marafiki wapya maishani. Anza taratibu tu.Unaweza kuanza kwa kufanya mazoezi japo kwa dakika kumi tu kwa siku. Tembea badala ya kupanda gari,kimbia, nenda gym,cheza muziki nk.Sina shaka kabisa kwamba utaona jinsi gani maisha yako yatabadilika. Kama tayari wewe ni mtu wa mazoezi,usiache hata kidogo.Endelea.
-
Chukua likizo/mapumziko: Pamoja na juhudi zote za kuyafurahia maisha hakuna jambo jema maishani kama mapumziko.Miili na akili zetu za kibinadamu hufikia mahali vikachoka. Unapojipa muda wa kupumzika unajipa nafasi ya kujipatia nguvu mpya,mawazo mapya.
Labda hii naweza kuifananisha na kauli mbiu ya kampeni iliyopita ya uraisi ambayo ilikuwa ni kasi mpya,ari mpya na nguvu mpya. Kila inapowezekana pata muda wa mapumziko.Pata muda wa kuachana na ratiba yako ya kawaida.Kama wewe ni mkulima basi hebu jaribu kuachana na kilimo japo kwa mwezi mmoja.Pumzisha mwili,pumzisha akili.
-
Jitolee/Saidia wenzako: Utamaduni wa kujitolea bado hauna umaarufu mkubwa hapa nchini kwetu ukilinganisha na mataifa yaliyoendelea. Hali duni za kiuchumi, zinasababisha watu wengi wasifanye shughuli za kujitolea kwa kisingizio cha ukosefu wa muda,ukosefu wa vitendea kazi nk.
Lakini hakuna jambo ambalo linaleta furaha ya kweli maishani kama kufanya shughuli za kujitolea(volunteer) au kumsaidia mtu mwingine katika jambo lolote lile. Ni kweli kwamba wengi wetu tuna hali duni. Ni kweli kwamba muda kwa wengine inaweza kuwa tatizo. Lakini jiulize,ni muda kiasi gani unautumia pale baa kwenye kiti kirefu au pale kibarazani ukipiga soga na rafiki zako? Unaonaje kama muda huo ungeutumia kwenye shughuli za kujitolea? Badala ya kushinda kijiweni, kwanini usijiunge na wenzako mkaenda kumsaidia mzee mmoja asiyejiweza kufanya usafi wa mazingira ya nyumbani kwake?
Kujitolea na kusaidia wengine sio tu msingi wa kujenga jamii iliyo bora bali pia ni njia muhimu ya kuleta furaha na amani maishani mwako. Anza leo,jitolee/saidia wengine. Tumia ujuzi,afya njema na uwezo wowote uliopewa na Mungu kusaidia wenzako na kusaidia jamii yako.
Kumbuka kwamba orodha ya mambo ya kufanya yaweza kuwa ndefu zaidi. Chochote kile unachoweza kukifanya bila kumbughudhi mwenzako au wanajamii wenzako na ukaona kinakuletea furaha na amani maishani mwako, nakushauri uendelee kukifanya.Hivyo ndivyo utakavyoweza kufanya ili kujiongezea furaha na amani maishani mwako na pia kuwaongezea wengine furaha na amani. Tuonane wiki ijayo.
Jeff Msangi ni mhariri wa mtandao wa www.bongocelebrity.com. Kwa maswali,ushauri na majadiliano mbalimbali,unaweza kuwasiliana naye kwa kutumia e-mail; makala at bongocelebrity.com au bongocelebrity at gmail dot com.
Feedback / Comments
9 Responses to “UNATAKA KUWA NA FURAHA NA AMANI ZAIDI? JARIBU MAMBO HAYA MATANO(5)”
Leave a Reply


sending...
ubarikiwe ndugu hapo nimekuelewa.nitumie nyingine kama hizo.
Jeff,
Asante sana kwa haya maarifa.Mungu akubariki
Great material Jeff.Simple and Clear.I wish all bloggers were writing something as meaningful as this.
Imetulia kaza buti kusaidia raia nimeifurahi
tanks nadhani nita kuwa na furaha den mhh! tuma nyingine
hongera kwa kubadilisha watu kifikira, nakusihi uendelee hivyo2
Asante Edmund na asante kwa mchango wako.
uko juu mkubwa, nitafuatwa,its is very interesting 2 hav guys like u,may god b with u
You are welcome Alfa.Keep following BC Maarifa Posts.A lot more to come.Thanks for visiting and supporting us.