
Miezi michache iliyopita, Rais Jakaya Kikwete, alifanya mabadiliko na teuzi kadhaa za mabalozi wetu katika nchi mbalimbali. Miongoni mwa mabadiliko hayo ni pamoja na yale ya kumhamisha Balozi Peter A.Kallaghe kutoka nchini Canada kwenda kuwa Balozi mpya wa Tanzania nchini Uingereza.
Wakati akijiandaa kuondoka nchini Canada kuelekea katika kituo chake kipya cha kazi nchini Uingereza,BC ilipata nafasi ya kufanya naye mahojiano maalum utakayoyasoma hivi punde.
Balozi Peter Kallaghe anaelekea nchini Uingereza kuchukua nafasi iliyoachwa na Balozi Mwanaidi Maajar ambaye amehamishiwa nchini Marekani. Fuatana nasi katika mahojiano haya;
BC: Mheshimiwa Balozi,asante sana kwa kukubali kufanya nami mahojiano haya.Nafahamu kwamba una mambo mengi mengine ya kufanya hususan wakati huu unapojiandaa kuondoka hapa Canada.Kwa hiyo nashukuru sana kwa kunipatia fursa hii.
Kwa kuanzia na kwa sababu wewe ni Balozi wa kwanza kufanya nasi mahojiano,ningependa kukuuliza swali ambalo bila shaka lipo katika vichwa vya wasomaji na wafuatiliaji wetu.Ilikuwaje mpaka ukafikia hatua ya kuteuliwa kuwa Balozi?Katika historia yako ya utumishi wa umma(Public Service) umepitia ngazi zipi,milima na mabonde yapi?Hapa ninamaanisha ulisomea wapi,ukakulia wapi na nini kilikusukuma katika ajira ya serikalini au utumishi wa umma kwa ujumla?
Balozi Peter Kallaghe: Historia yangu kielimu ni kwamba nimehama hama sana shule, kwa sababu baba yangu, Marehemu Balozi Cecil A. Kallaghe, alikuwa mtumishi wa umma na alipata kufanya kazi nje ya nchi kama Balozi.
Kwa ufupi nilisoma elimu ya msingi katika shule za OysterBay na Arusha School katika miaka ya sitini. Na nilipata elimu ya sekondari katika shule ya Pugu Secondary School. Chuo Kikuu nilisomea Kieve State University ambapo nilihitimu na degree ya M.A. in International Relations. Aidha nina Post-Graduate Diploma kwenye Diplomacy, Negotiatiations and Strategic Communications.
Kikazi maisha yangu yote nimefanya kazi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ikulu, hususani kama msaidizi wa Rais kwa kipindi kirefu.
Niliteuliwa Balozi kwa mara ya kwanza mwaka 2004 nikiwa pale Ikulu, na mwaka 2007 niliteuliwa Balozi nchini Canada. Mwaka 2010 nimeteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza (UK).
Kuteuliwa kwangu kuwa balozi nakuchukulia kama fursa ya kipekee niliyopewa ya kutoa mchango wangu katika kulitumikia Taifa letu la Tanzania na watu wake. Na ninafanya hivyo nikitambua uzito wa dhamana hii hasa kwa nchi ambayo bado inakabiliana na changamoto nyingi za kimaendeleo.
BC: Sasa kama sikosei hii ilikuwa ni mara yako ya kwanza kuteuliwa kuwa Balozi kamili. Je,ulikuwa na matarajio gani kabla hujafunga safari kuja Canada? Je, ulichokitarajia ndicho ulichokutana nacho?
Balozi Peter Kallaghe: Asante sana Jeff.Kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuzungumzia kazi nilizofanya hapa Canada kwa kipindi cha miaka mitatu tangu nilipoteuliwa kushika wadhifa huu wa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada.
Labda nianze kwa kusema kwamba nilipoteuliwa kuwa Balozi hapa Canada,ilikuwa ni heshima kubwa sana kwangu.Ni kitu ambacho kilinishtusha lakini bila kusita nilikubali kupewa heshima hiyo kubwa na Rais ili kuja kumwakilisha hapa Canada.
Matarajio niliyokuwa nayo na maagizo niliyopewa wakati nilipoteuliwa ilikuwa kwanza;kuendeleza mahusiano mazuri yaliyokuwepo au yaliyopo baina ya Tanzania na Canada iwe ni kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Pili, nilipewa jukumu la kuja kuzungumza na wawekezaji mbalimbali wa Canada ili waendelee kuwekeza nchini kwetu. Jukumu hilo linaambatana na kuja kuzungumza nao ili waelewe mazingira yetu ya kisera na juu ya yote nilitakiwa kufafanua kwao mazingira ya mabadiliko hayo na sababu zake. Nia ya msingi ya kufanya hivyo ilikuwa ni kuendeleza mahusiano na taswira nzuri ya Tanzania nchini Canada.
Kazi ya tatu niliyokabidhiwa, Ilikuwa ni kukaa karibu na watanzania waliopo Canada kwa lengo la kuwashauri wakae kwenye jumuiya za watanzania na kujadiliana nao jinsi wanavyoweza kutoa mchango wao katika maendeleo ya Tanzania. Hayo ndio yalikuwa malengo makubwa niliyokuwa nayo ukiondolea mengine ya kawaida ya kazi za kila siku za balozi.
Sasa kuhusu kama tulipata mafanikio kwa kipindi hiki cha miaka mitatu, nadhani kwa kiasi kikubwa tumetimiza malengo yetu. Kwanza kama unavyofahamu,Canada ilipunguza nchi ambazo inashirikiana nazo katika Bara la Afrika hadi kufikia sasa inaposhirikiana na nchi 6 tu za Africa. Nafurahi kusema kati ya hizo nchi 6 mojawapo ni Tanzania.Kwa hiyo tunashukuru kwa hilo.Hatusemi kwamba hiyo imetokana na kazi yetu tu hapa Ubalozini, bali imechangiwa na kazi nzuri ya kujenga mahusiano mazuri ya muda mrefu baina ya Canada na Tanzania.
La pili wawekezaji; Kama unavyofahamu,Canada ndio mwekezaji mkuu nchini Tanzania, hasa kwenye sekta ya uchimbaji wa madini. Hivi majuzi Canada wametoa takwimu kwamba makampuni ya Canada wamewekeza takribani Dollar Billioni 2 nchini Tanzania kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Hii ni kuonyesha kwamba sera zetu nyumbani wamezielewa na bila shaka wataendelea kuwekeza zaidi.
Kwenye sekta ya utalii; idadi ya watalii kutoka Canada inazidi kuongezeka.Kwa hiyo tunashukuru kwa hilo.Pia tumeweza kukutana na watanzania wengi wanaoishi hapa Canada na kuendelea kuwahamasisha ili waendelee kujiunga kwenye vikundi au jumuiya mbalimbali za watanzania.
Kwa hiyo kwa ujumla naweza kusema kwamba nimeridhika kwamba na mimi nimetoa mchango wangu katika kuendeleza mahusiano mema baina ya Tanzania na Canada.
BC: Labda sasa tuzungumzie changamoto ambazo umekabiliana nazo tangu umefika hapa Canada au kwa miaka mitatu ambayo umekuwa hapa Canada. Unaweza kusema ni changamoto zipi ambazo umekabiliana nazo wewe kama Balozi na ninyi wote kama Ubalozi kwa ujumla na mmefanya juhudi gani kuzitatua?
Balozi Peter Kallaghe: Kama unavyojua changamoto kubwa ni kwamba kila nchi ya kiafrika yenye ubalozi Canada inajaribu kujieleza kwa serikali ya watu wa Canada kwamba nchi zao ndizo zinazofanya kazi nzuri zaidi na hivyo zinastahili kusaidiwa zaidi.
Kwa hiyo inategemea sasa nchi gani ina sera nzuri ambazo zinaeleweka.Sisi kwa bahati nzuri, mpango wa MKUKUTA, unatusaidia au kuwa nyenzo nzuri ya kuelezea jinsi tunavyopanga kutumia misaada mbalimbali tunayopata na jinsi inavyotumika. Tunawaeleza kwamba misaada tunayoipata tunaielekeza katika uboreshaji wa huduma za elimu na afya ama katika maeneo ya kusaidia sekta ya sheria na utawala bora.
Mpango wa MKUKUTA unatupa nyenzo dhabiti ya kuelezea mafanikio yetu pamoja na changamoto zinazoendela kutukabili.Hiki nadhani ni kitu ambacho nchi nyingi za kiafrika hazina. Wakati huo huo, kuna suala zima la kuhakikisha kwamba wenzetu wanazielewa vizuri sera na mipango yetu. Tunafanya hivyo kwa kuwa-engage wa-Canada kupitia mazungumzo mbalimbali katika ngazi ya kibalozi au kitaifa.
Pili kwenye suala la kuvutia watalii. Kama unavyofahamu,bado kuna watu wanaogopa sana kwenda kutalii barani Afrika.Wanadhani Afrika ni nchi moja. Kwa hiyo tuna jukumu la kuitofautisha Tanzania na maeneo mengine ya Afrika huku tukisisiza kwamba Tanzania ni salama.
Changamoto nyingine inatokana na ukubwa wa eneo la Canada. Canada ni nchi kubwa sana. Ni kitu ambacho hata mimi nimekuja kukielewa zaidi nilipokaa hapa. Nilipoambiwa nakuja Canada nilidhani nakuja Ottawa. Canada ni kama bara. Kwa mfano kusafiri kutoka Ottawa kwenda Vancouver inachukua kama masaa 7.Ni kama kutoka Dar-es-salaam kwenda mpaka Ivory Coast. Ottawa kwenda Winnipeg inawezekana ni kama kutoka Dar-es-salaam mpaka Johanesburg.
Kutokana na ukubwa huo, uwezo wa kuizunguka au kutembelea sehemu zote ni mdogo, kitu ambacho kinasababisha tuchague maeneo machache ambayo tunajaribu kuyafanyia kazi kwa nguvu zaidi.
Changamoto nyingine ilikuwa ni jinsi ya kukutana na watanzania na kuzungumza nao jinsi gani tunaweza kushirikiana katika kuleta maendeleo.Lakini naomba niseme wazi kwamba hii haikuwa changamoto kubwa sana kwani kwa bahati nzuri watanzania waliopo huku ni waelewa na tumekaa nao na kuanza kufanya maandalizi rasmi ya kufikira nini cha kufanya.
Kwa ufupi changamoto zilizo nikabili kama hizo. Hakukuwa na changamoto kubwa sana.
BC: Kwa namna moja au nyingine umeshagusia kazi za ubalozi.Lakini kwa mujibu wa uchunguzi kidogo tulioufanya, watu wengi inaonekana bado hawaelewi vizuri kuhusu kazi au majukumu ya balozi zetu nchi za nje.Unaweza kuwafafanulia kidogo kwamba zipi hasa ni kazi au majukumu ya balozi zetu zilizopo katika nchi mbalimbali ulimwenguni?
Balozi Peter Kallaghe: Jeff nakushukuru sana kwa swali hilo. Kusema kweli, kazi za balozi nchi za nje ni jambo ambalo halifahamiki vizuri. Inawezekana na sisi hatujalifanyia kazi sana suala hili. Kwa bahati nzuri, natambua kwamba hivi sasa tupo katika mkakati wa kujaribu kuelezea zaidi shughuli na majukumu ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje, majukumu ya mabalozi ni yepi, wanafanya nini nk. Hili ni jambo jipya serikalini.
Pengine nifafanue hii dhana na kusema kwamba, serikali yote ina majukumu ya kimsingi kwa wananchi wao nchini. Hayo ni kama vile kutoa huduma mbalimbali kama vile huduma za Polisi, elimu, afya, utawala, huduma za mahakama na huduma zingine mbalimbali zinazotolewa kupitia wizara mbalimbali zilizopo.
Huduma nyingine ni kujipanga jinsi itakavyoshirikiana na mataifa mengine ulimwenguni kwa sababu hatuishi au hatuwezi kuishi kama kisiwa.Tanzania ni miongoni mwa nchi za bara la Afrika na miongoni mwa nchi za ulimwenguni.
Kwa hiyo kazi au jukumu mojawapo ambalo serikali inapewa chini ya uongozi wa Rais, kama ilivyo kwetu kwa Rais Jakaya Kikwete, ni jinsi gani itakavyojipanga katika kushirikiana na mataifa mengine kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania.
Sasa kazi hiyo inafanywa siku hadi siku na wanadiplomasia. Nadhani katika mazungumzo yetu ya awali nilikwambia kwamba katika mfumo wetu mwanadiplomasia au diplomat wa kwanza ni Rais mwenyewe.Yeye ndio ana jukumu la kwanza la kujenga mahusiano kati ya Tanzania na mataifa mbalimbali na ndio maana anasafiri nje, anaalikwa katika vikao mbalimbali nk.Kama yeye hawezi kwenda atamtuma makamu wake, Rais wa Zanzibar ama Waziri Mkuu kumwakilisha.
Diplomat namba mbili ni Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje. Yeye pia anakwenda akiwa na jukumu hilo hilo la kufanya hizo kazi za kuiwakilisha nchi na kuendelea kushawishi mataifa mbalimbali ama yatusaidie ama tushirikiane nayo katika maswala mbalimbali. Hawa wawili wanakwenda na kurudi nchini. Sasa kwa jinsi ambavyo serikali itaona inafaa,katika sehemu ambazo inadhani itahitaji ofisi ili kuendeleza yale mahusiano kwa karibu zaidi, ndio serikali inajaribu,kutokana na uwezo wake,kufungua ofisi ya ubalozi.
Kwa hiyo kazi ya ubalozi ni kama vile ofisi ya serikali iliyofunguliwa katika nchi fulani kwa lengo la kuendeleza mahusiano baina ya ile nchi kwa karibu zaidi.Na ile ofisi ndio inaongozwa na mtu ambaye anaitwa Balozi. Na katika taratibu za kimataifa, tunasaidiana katika kumpa yule balozi uwezo wote ili aweze kuendeleza yale mahusiano. Kwa hiyo jukumu kubwa la ubalozi ni kujenga mahusiano baina ya ile nchi husika na Tanzania katika nyanja zote za kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Lakini pia dunia inabadilika na kwa maana hiyo watendaji wa kidiplomasia hubadilika pia. Siku hizi wabunge pia wanatoa mchango wa kukuza diplomasia ya nchi. Wafanyabiashara na sekta nyigine nyinginezo pia zinachangia. Wote hawa wanachangia katika kujenga mahusiano baina ya nchi husika na nchi yetu.
Lakini pamoja na hayo yote, centre ya mahusiano bado inakuwa ni Ubalozi.Kwa hiyo jukumu kubwa ambalo tunapewa tukija kama hapa Canada ni kwamba viongozi wa serikali ya Canada wafahamu nini Tanzania inafanya na kwamba wanaelewa kile tunachofanya nyumbani kinatokea katika mazingira gani na mtazamo wa serikali ni upi.
Kutokana na hayo, mara nyingi tunaitwa ili kubadilishana mawazo na kuombwa kutoa ufafanuzi kwa yale yanayotokea nyumbani.
Lakini pia kama nilivyosema tunalo pia jukumu la kutafuta wawekezaji, kuzungumza nao na kuwashawishi wawekeze nchini kwa lengo la kukuza uchumi wetu.Hili ni jukumu kubwa la kimsingi la ubalozi na linakwenda sambamba na sera yetu ya “Diplomasia ya Uchumi” (Economic Diplomacy).
Pia jukumu kubwa ambalo siku hizi linatiliwa maanani sana, ni kushirikiana na watanzania waliopo katika nje ya nchi.Hili inatokana na ukweli kwamba sura nzima ya watanzania waliopo nje ya nchi siku hizi imebadilika sana.
Siku hizi watanzania wengi waliopo katika nchi za nje ni wanataaluma,wana shughuli na kazi zao.Isitoshe uwezo wao wa kifedha na mapenzi yao kwa taifa ni makubwa.Kwa hiyo tumepewa jukumu la kukaa nao,kushirikiana nao na kuangalia jinsi watakavyoweza kuchangia maendeleo ya nyumbani.
Kwa hiyo hizo ndio kazi za kimsingi za Ubalozi tukiondoa kazi zingine za kawaida kama vile kutoa Viza, kusimamia maombi ya pasi za kusafiria,kutoa huduma za ki-Counsellor nk.Hayo ndio majukumu ya kimsingi ya balozi zetu.
BC: Katika suala hilo hilo la majukumu au kazi za balozi zetu;ni mambo gani ambayo watu wengi hususani watanzania wanaoishi nchi za nje kwa mfano hapa Canada,wamekuwa wakidhani ni majukumu au kazi za ubalozi wakati kimsingi hazipo katika orodha rasmi ya kazi au majukumu hayo?
Balozi Peter Kallaghe: Kusema ukweli sisi hapa ubalozini,tunapokea kila kitu.Mtanzania akija pale na kuuliza chochote,tuna jukumu la kumsikiliza kwa sababu anakuwa amekuja “nyumbani”.Anakuja kwenye ofisi ambayo inatakiwa imsikilize.
Kwa hiyo tuna wajibu wa kumsikiliza na kumshauri.Ila ni kweli pia kwamba kuna wakati mwingine labda mtu ametoka nyumbani na kwa bahati mbaya,vyeti vyake au karatasi zake hazijakaa vizuri.Anakuja katika hizi nchi bila kufuata utaratibu kamili uliowekwa nk.Kutokana na hilo inawezekana kutokea akakwama kwa njia moja au nyingine. Sasa kukimbilia ubalozini akiwa na mategemeo kwamba sisi tutatatua tatizo lake ,hapo panakuwa pagumu wakati mwingine.
Inapojitokeza hali kama hiyo,tunaelimishana nini cha kufanya. Tunapenda kushauri kwamba ni vizuri watu wakija huku waje kwa kutumia njia ambazo ni halali ili iwe rahisi kwetu kuwapa huduma zetu.Kama anakuwa amekuja katika njia ambazo ni ngumu, mara nyingine inakuwa ngumu kumsaidia. Hata hivyo tunajaribu kadiri ya uwezo wetu kusaidia.
Scenario nyingine ni pale mtu analeta bidhaa mbalimbali akataka tumsaidie kuziuza. katika mazigira ya Canada,kama mtu huyo hakufuata taratibu tunakwama katika kumsaidia.Kwa bahati nzuri,kesi za namna hiyo siyo nyingi Canada,labda ni kutokana na umbali,hatuzipati sana.Lakini pale ambapo tunaweza kumsaidia mtanzania huyo huwa tupo tayari kufanya hivyo.
BC: Umezungumzia kidogo kuhusu suala la kuboresha sekta ya utalii.Baadhi ya watu wamekuwa wakisema au kulaumu kwamba balozi zetu hazifanyi kazi ya kutosha katika kutangaza sekta ya utalii au nafasi za uwekezaji zilizopo nchini mwetu. Unasemaje kuhusu lawama hizo?
Balozi Peter Kallaghe: Nadhani kama nilivyokwambia huko nyuma siasa zetu za mambo ya nje zilikuwa zimeegemea sana kisiasa.Jukumu kubwa lilikuwa kama vile ukombozi wa Kusini mwa Afrika na kujenga mahusiano ya kisiasa zaidi na nchi mbalimbali ulimwenguni.
Lakini sasa hivi tunatilia mkazo “sera ya kidiplomasia ya kiuchumi” ambayo lengo lake ni kutilia mkazo kutafuta wawekezaji na watalii, vitu ambavyo vinaweza vikachangia kukua kwa uchumi wa Tanzania na kupunguza umasikini.
Hata hivyo, kama unavyofahamu,kutangaza kunahitaji uwezo mkubwa wa kifedha.
Pamoja na hayo,ubalozi wetu hapa Canada,unajitahidi kutangaza masuala ya utalii kwa kadiri ya uwezo wetu.Kwa mfano, kila mwaka mwezi Octoba tunashiriki kwenye maonyesho ya utalii ambayo yanafanyikia Montreal.Haya ni maonyesho ya shughuli za utalii yenye heshima kubwa.Mpaka hivi leo tunaweza kusema ushiriki wetu katika maonyesho hayo umetusaidia kwani takwimu zinaonyesha kwamba watalii wengi ambao wanakwenda Tanzania wanatoka jimbo la Quebec.Pia tunashiriki katika maonyesho ya utalii ambayo yanafanyika Toronto na Ottawa.
Zaidi ya hapo, lengo letu lilikuwa ni kujipanga kushiriki katika maonyesho ya Calgary na Vancouver ambako kama unavyojua ni majimbo ambayo yana watu wenye uwezo mkubwa kifedha.
Pia ningependa kuongezea kwamba Wacanada wengi siku hizi wanapenda kwenda kupanda Mlima Kilimanjaro.Imetokea kwamba watu wengi hawapendi utalii wa kivivu.Wanataka utalii wenye fitness.Hiyo ni habari njema kwetu na kwa kweli hili ni eneo jipya ambalo tunalipa kipaumbele.
Kwa hiyo kwa ujumla naweza kusema tunajitahidi, na nadhani balozi nyingine zinajitahidi kuitangaza sekta ya utalii ingawa uwezo wetu bado ni mdogo. Lakini pale tunapoweza,tunafanya sana.
BC: Hivi karibuni tumesikia kwamba serikali, kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje,Mheshimiwa Membe, imekubali kwamba zipo faida nyingi kuliko hasara katika suala la kuruhusu au kutoruhusu uraia wa nchi mbili(dual citizenship). Hizo ni habari ambazo zimepokelewa vizuri na watanzania wengi waliopo nje ya nchi hususani wale ambao wameshachukua uraia wa nchi wanazoishi. Pamoja na hayo, unadhani Watanzania,wanaweza kushiriki namna gani katika maendeleo ya kijamii,kisiasa na kiuchumi kabla hata ya kumalizika kwa mchakato wa uraia wa nchi mbili?
Balozi Peter Kallaghe: Kwanza Jeff niseme kwamba ni kweli kabisa kwamba hata hapa Canada kila ninapozunguka ninaulizwa sana kuhusu suala la uraia wa nchi mbili.
Ni suala ambalo hata Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje,Mheshimiwa Membe, alipokuja kwenye ziara hapa Canada lilijitokeza sana.Waziri ameshalizungumzia sana na kwa bahati nzuri viongozi wetu wakuu wamesikiliza kwa makini na wanaelewa umuhimu wake.Lakini kama ambavyo Waziri amekuwa akisema mara kwa mara,ni jambo ambalo bado linatafutiwa muafaka na ninaamini likishapata muafaka,litatimizwa.
Sasa kabla ya masuala yote kuwekwa sawa,jambo ambalo tumekuwa tunajaribu kufanya ni kuandaa hii mikutano ya Diaspora ambapo tunakutanisha watanzania na viongozi mbalimbali kutoka katika sekta mbalimbali nchini ili kwa pamoja tuangalie tunawezaje, katika kipindi hiki cha mpito ,kuwawekea utaratibu watanzania waliokuwa nje ili waweze kushiriki katika sera na mabadiliko ambayo yanatokea nchini.
Nadhani utakuwa umesikia kwamba Uingereza wamefanya hivyo pamoja na wenzetu wa Washington.Ilikuwa nia yangu kwamba na sisi hapa Canada pengine mwaka ujao tungeweza kufanya kitu kama hicho kwa sababu hapa Canada lipo kundi la watu wenye uelewa mkubwa wenye profession mbalimbali na kama nilivyosema wenye uwezo na wenye uzalendo na ambao wanataka kuwekeza na kushiriki kwa namna mbalimbali katika maendeleo ya kiuchumi nyumbani Tanzania.Nina uhakika kwamba wenzangu ambao watabaki kwenye ubalozi wataliendeleza hili.
BC: Kama Balozi wa Tanzania hapa Canada bila shaka umepata nafasi ya kukutana na watu wengi,kuona mengi na pia kujifunza mengi. Miongoni mwa hayo,unadhani ni yapi ambayo sisi kama watanzania tunaweza kuyaiga ili kuongeza chachu ya juhudi za kuleta maendeleo nchini mwetu?
Balozi Peter Kallaghe: Asante Jeff.Kwanza niseme kabla ya kuja huku Canada nilianza kwa kukutana na mabalozi wa zamani/wastaafu ambao walishafanya kazi hapa Canada.
Kwa bahati nzuri walinisihi kwamba watanzania waliopo hapa Canada ni watulivu na professionals sana.Nashukuru kusema kwamba na mimi nakubaliana kabisa na hiyo tathmini kwamba watanzania wanaoishi Canada,kama nilivyosema na nitarudia, wengi wao ni wanataaluma,wanafanya shughuli zao. Hawana matatizo ambayo yanawasumbua ki-uraia.
Pia nafurahi kusema kwamba ni wazalendo.Wanaipenda nchi yao.Tumekaa tumebadilishana mawazo mara nyingi.Hatukukubaliana kila mara lakini hata pale tulipotofautiana,tulitofautiana kistaarabu.Nadhani mimi ninaondoka nikielimika kuhusu mawazo yao na pengine na wao wamejifunza jambo moja au lingine kutoka kwangu.
Isitoshe nimewakuta na wao wana shauku kubwa ya kuelewa zaidi jinsi ambavyo wanaweza kushiriki katika mabadiliko mbalimbali yanayotokea na kuendelea kutokea nchini mwetu.Kuna kiu kubwa ya kushiriki mijadala ya kisiasa,kutoa michango katika sera mbalimbali,kushiriki katika maendeleo ya kiuchumi,kijamii nk.Sasa kama nilivyosema hapo awali,hiki ni kitu kipya na sisi tunajiandaa na kujipanga kuji-organize ni jinsi gani tunaweza tukasaidiana nao katika kutekeleza mambo hayo.Bila shaka shauku hiyo inachangiwa na zama hizi za uwazi hususani kupitia vyombo mbalimbali vya habari na njia zinginezo za kupashana habari.Kwa upande mwingine,nadhani tumeonyesha mifano mzuri katika suala hili la kuwashirikisha au kushirikiana nao kupitia balozi zetu za Uingereza na Marekani.
BC: Umegusia kidogo kuhusu uwazi katika maendeleo ya vyombo vya habari.Siku hizi kuna vitu kama blogs,kuna mitandao ya kijamii kama Facebook,Twitter,YouTube na vitu kama hivyo.Kwa uzoefu wako au ushauri wako unadhani watanzania tunawezaje kuzitumia nyanja hizi mpya za mawasiliano ili kuongeza ufanisi katika masuala ya utendaji na suala zima la kushiriki katika maendeleo ya nchi yetu?
Balozi Peter Kallaghe: Nianze kwa kuwapongeza watanzania wengi wanahabari au sijui tuwaite wanatekinolojia ambao sasa wamechangia sana katika kupanua mijadala ya masuala mbalimbali ya nyumbani hasa kwenye blogs mbalimbali na pia kwenye forums mbalimbali. Wengine tunapenda sana kuzisoma.
Leo hii popote unapokwenda duniani,huna haja tena ya kuwaeleza nini kilitokea Tanzania kwa sababu kila mtu anakifahamu.Inafikia mahali watu wanafuatilia moja kwa moja matukio mengine “live”sio tu ya kisiasa,kijamii na kiuchumi.Leo hii likitokea tu jambo kubwa nyumbani,kila mtu anafahamu.Hii imetoa changamoto sana kwa sisi viongozi kwa sababu lazima uwe na kitu kipya cha kuzungumza.Ni faraja kuwa watu wanajua nini kinatokea nyumbani,wanaona.Kwa hiyo upeo wa watu kuelewa nini kinatokea nyumbani umekuwa ni mkubwa zaidi.Ingawa mara nyingine kunakuwa na upotoshaji katika mijadala hiyo,kwa ujumla mijadala ni mizuri.
Mimi napenda sana kukupongeza wewe Jeff na wenzako wengi ambao mnafanya kazi hii.Naomba muendelee kuelimisha na kuendeleza hali hii ya kuwa na uhuru zaidi.Naamini hili ni jambo jema kwa “afya” ya taifa kwamba tuna uwazi na uhuru wa kujadili mambo mbalimbali yanayohusu nchi yetu.Tuitumie vizuri nafasi hii.
Kwa upande mwingine,pengine na sisi serikalini imefika wakati tuangalie ni jinsi gani tunaweza tukaanzisha vyombo kama hivi kwa faida ya watu kuelewa balozi zinafanya nini,majukumu yao ya kimsingi ni nini.Kwa hali ilivyo hivi sasa,nadhani bado kuna gap kati ya vitu tunavyofanya na jinsi watu wanavyoelewa kazi zetu.Kwa hiyo ni suala ambalo linatoa changamoto maalumu kwa sisi tuliopo serikalini.
BC: Una ushauri gani au ujumbe gani kwa watanzania unaowaacha Canada hususan katika suala zima la kudumisha Umoja, undugu na ujamaa?
Balozi Peter Kallaghe: Kwa watanzania waliopo hapa Canada,nataka tu kuendelea kuwapongeza kwa moyo wao wa kizalendo kwa nchi yetu na wanavyoendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo yetu.
Pamoja na kwamba Ottawa iko mbali sana na labda Edmonton,Halifax,Vancouver nk , tutaendelea kwa kadiri ya uwezo wetu kuwatembelea,kubadilishana nao mawazo na nashukuru kwamba kwa kipindi changu chote hapa halijawahi kutokea vaga lolote la watanzania ambalo limetuabisha.
Hilo ni suala ambalo ninajivunia sana.Na kila nikienda katika vyuo vikuu mbalimbali na sehemu nyingine wanakofanyia kazi watanzania,napewa sifa nzuri kuhusu taaluma na utendaji wao wa kazi. Mambo kama hayo yanafanya wa-Canada wapende kwenda Tanzania.Nimeshawahi kuwauliza watalii kwamba kwanini wanapenda kwenda Tanzania wakasema kwamba sisi tumeshaambizana kwamba ukitaka kwenda nchi ambayo ni salama yenye amani na ukarimu basi nchi hiyo si nyingine bali ni Tanzania.
Kwa hiyo naomba watanzania waendelee kudumisha ushirikiano huo,mapenzi yao kwa Tanzania na wasisite au kuwa waoga wa kutoa maoni yao kuhusu kinachotokea kule nyumbani.
BC: Natambua kwamba kama Balozi wa Tanzania Canada,pia unazo nchi zingine ambako unawakilisha nchi yetu, mfano mmojawapo ni Cuba. Unaweza kuzungumziaje uhusiano wetu na Cuba hivi sasa tangu tumejiweka mbali kidogo na siasa zisizofungamana na upande wowote na mabadiliko mengine yanayoendelea duniani.Uhusiano wetu na Cuba ukoje?
Balozi Peter Kallaghe: Ni kweli kati ya moja ya nchi ambazo tunawakilisha tukiwa hapa Ottawa ni Cuba.Na kama unavyofahamu,hilo linatokana na sababu za kihistoria.Hata kama Cuba ipo karibu na Marekani lakini Canada imekuwa na mahusiano mazuri zaidi na Cuba kwa hivyo wanapenda wawakilishi wa zile nchi ambazo hazijafungua ubalozi Havana wawe wanakaa katika nchi ambazo wanadhani hawatakuwa wanashawishiwa na wapinga mapinduzi ya Cuba(Cuban anti-Revolutionaries).Kwa hiyo Canada imekuwa ni sehemu ambapo mabalozi wengi wa kiafrika ambao hawana ofisi pale,wanawakilisha.
Kwa kipindi cha miaka hii mitatu,naweza kusema kwamba mahusiano kati ya Tanzania na Cuba yamekuwa mazuri.Wa-Cuba kama unavyojua wametengwa na nchi nyingi duniani.Kwa hiyo ni vizuri tukaonyesha mshikamano nao,pamoja na matatizo yao.
Nafurahi kusema kwenye kipindi hiki ambapo nimekuwa mwakilishi nchini Cuba kumekuwa na mabadilishano ya ziara za viongozi wa nchi zetu.Rais Kikwete amefanya ziara rasmi ya kiserikali.Makamu wa Rais,Dr.Mohamed Ali Shein,amefanya ziara.Makamu wa Rais wa Cuba ametembelea Tanzania.Kwa hiyo kwa kweli kisiasa wameridhika kwamba kisiasa bado tunaendelea kushikamana nao.
Pia katika nyanja ya elimu, kumekuwepo na ongezeko zuri la wanafunzi wa kitanzania wanaosoma Cuba.Nilipoanza uwakilishi,tulikuwa na wanafunzi chini ya 20.Sasa hivi tuna wanafunzi karibu 45. Kati ya hao 20 wanasomea udaktari.Hayo ni matunda ya hizi ziara za viongozi na mahusiano kati yetu.
Sasa hivi tunashirikiana nao katika programu ya kutokomeza malaria Tanzania na Tanzania na Cuba tumeshatiiliana mkataba wa kuanzisha kiwanda cha kisasa cha teknologia mpya ya kutokomeza Malaria nchini.Wanatusaidia katika elimu ya msingi kwani kama unavyofahamu wao wamepata mafanikio makubwa sana katika kufuta ujinga. Kule Zanzibar wameanzisha programu ya kufundisha madaktari kule kule Zanzibar kutokana na mazingira ya Zanzibar.Kwa hiyo pamoja na uwezo mdogo,tunajitahidi pale tunapoweza kusaidiana tunasaidiana.Walikumbwa na kimbunga ambacho kilisababisha uharibifu mkubwa wa mali. Serikali ya Tanzania nayo ilijikusanya kusanya ikatoa mchango ambao kwa kweli waliguswa nao sana.Kwa hivyo,mahusiano yetu na Cuba naondoka nikiwa nimeridhika kwamba niliyaendeleza vizuri na wenzangu watayaendeleza.
BC: Sasa unaelekea Uingereza ambapo ndiko kutakuwa kituo chako kipya cha kazi. Umejiandaa vipi kukabiliana na changamoto ambazo bila shaka zitakuwa tofauti na za hapa Canada kutokana na mazingira ya Uingereza na Canada kuwa tofauti?
Balozi Peter Kallaghe: Kwanza niseme ni heshima nyingine ambayo nimepewa na Rais Kikwete na taifa kwenda kuwakilisha nchi yetu Uingereza nchi ambayo ina historia ndefu sana na taifa letu.Lakini sio tu kwamba ni nchi yenye historia ndefu na taifa letu lakini ndio mshiriki wetu mkubwa wa maendeleo.Uingereza ndio nchi ambayo tunashirikiana sana kibiashara ukiondoa labda nchi za jirani kama vile Kenya.Kibiashara ndio nchi ambayo tunaiuzia mazao yetu mengi.Lakini pia nadhani idadi ya watanzania wanaoishi Uingereza ni kubwa zaidi.Kwa hiyo ni heshima kwenda kuendeleza mahusiano mazuri baina ya nchi zetu.Nitajitahidi kadri ya uwezo wangu wote kufanya hivyo.
Lakini nataka niseme pia kwamba katika kipindi cha hivi karibuni tumeshuhudia kazi kubwa waliyofanya watanzania kwa kushirikiana na ubalozi kwa kukaa pamoja na mwenzangu Balozi Mwanaidi Maajar anayeondoka.Wamefanya kazi kubwa.Wamekuwa na mikutano mikubwa miwili ya Diaspora. Ninawapongeza sana kwa hatua hii kubwa waliyofanya.
Napenda tu kuwaahidi kwamba na mimi nitaendeleza yale yote ambayo mwenzangu alifanya.Ningependa nikifika tu nikae nao chini ili tupange mikakati jinsi tunavyoweza kuendeleza hayo mahusiano.Tanzania ni nchi yetu wote.Haitajengwa na mtu mwingine.Itajengwa na sisi. Mwalimu Nyerere na wenzake walituacha taifa likiwa moja ,likiwa tulivu, na salama sasa ni wakati ambapo vizazi vipya vionyeshe vinaweza kutoa mchango gani katika kuliendeleza taifa katika misingi imara tuliyoachiwa na waasisi wa taifa letu.Bahati nzuri viongozi wa sasa hivi ni wasikivu,ni waelewa wa mambo ya ulimwengu.Kwa hiyo ninasubiri kwa hamu kukutana na hao wenzangu ili tuangalie tunaweza kushirikiana kwa namna gani.
BC: Asante sana Balozi Kallaghe,nakutakia kila la kheri katika kazi zako za uwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huko nchini Uingereza.
Balozi Peter Kallaghe: Karibu.Asante sana.
Feedback / Comments
8 Responses to “BC EXCLUSIVE: AN INTERVIEW WITH AMBASSADOR PETER KALLAGHE”
Leave a Reply


sending...
hongeramkuu kwa kutuwakilisha watanzania vema
Mungu akulinde na kukubariki
Nimefurahishwa sana na mazungumzo baina ya Balozi na ndg.Jeff, haswa suala la uwezwkano wa uraia wa nchi mbili Tz, uwekezaji wa mitaji nyumbani, na mahusiano mazuri baina ya Tz na Canada na Cuba.
Zuri zaidi la kujivunia ni sifa aliyoitoa Balozi kwa Watanzania waishio hapa Canada kwamba hawajiingizi kwenye majanga hapa ugenini,na sifa alizopewa na Wacanada wenyewe kwamba Watanzania waishio hapa ni wachapa kazi wazuri na wanajiheshimu ! Pia ni kweli kwamba tunaipenda nchi yetu ya Tz,na wananchi wake. Tutaendeleza heshima hiyo na kuuendeleza uhusiano mzuri baina ya mataifa haya mawili.Tunamtakia afya na kazi njema Balozi Kallaghe na familia yake huko UK.
Mahojiano mazuri sana Jeff.Balozi Kallaghe asante kwa utumishi wako hapa Canada.Nakutakia kila la kheri huko Uingereza.
hongera sana Mheshimiwa Balozi Kallaghe. kwa mazungumzo yako mazuri na JEFF.SISI WATU WA edmonton tuna sema asante kwa kazi yako nzuri uliyo ifanya kwa kipindi cha miaka 3.na tunakutakia kazi njema uendako.
Balozi tunaomba uwe Mbunge wetu huku Kigoma.
Karibu UK Mheshimiwa Balozi.Bila shaka,kama ulivyosema,utaendeleza yote mazuri aliyofanya Balozi Maajar.
Good interview Jeff.I wish waandishi wa bongo nao wangekuwa wanajituma na kufanya vitu out of the ordinary.Sio kila siku tusikie habari za kina Makamba na Kikwete tu.
Swali moja tu la ziada kwa balozi;una mpango wowote wa kugombea nafasi za kisiasa nchini Tanzania pindi labda utakapomaliza muda wako hapo Uingereza?
hongera mkuu bado tunakuhitaji uendelee na kazi ya kujenga taifa, mungu akuzidishie nguvu.