Upende,usipende,leo hii unapoongelea masuala ya nyanja ya habari na mawasiliano kupitia zana za blog kwa upande wa Tanzania(Tanzanian Blogsphere), huwezi kuepuka kumtaja Muhidin Issa Michuzi a.k.a Ankal,Mzee wa Libeneke.

Mwanzoni alipoanzisha blog yake maudhui yake yalikuwa zaidi ni picha na maelezo kidogo juu ya picha hiyo au picha hizo.Hiyo ilitokana na ukweli kwamba Michuzi ni seasoned professional photographer.

Baada ya muda fulani,na kutokana na mafanikio aliyokuwa ameyapata,ilimlazimu kutanua wigo wa blog yake na hivyo kutoishia katika picha na maelezo mafupi mafupi tu bali kujumuisha maelezo au habari zaidi.Leo hii,blog yake imekuwa kimbilio la wengi pale wanapotafuta habari motomoto kuhusu kinachoendelea nchini Tanzania,maeneo ya jirani na hata sehemu mbalimbali za ulimwengu.

Hivi sasa yupo mbioni(keshazianza mbio zenyewe) kuboresha zaidi kazi ngumu anayoifanya ya kuendeleza “libeneke”.Ameanzisha tovuti/blog mpya inayopatikana kupitia http://michuzipost.com

BC imepata nafasi ya kuongea naye machache kuhusu ujio huo wa MichuziPost na mambo mengine kuhusiana na tasnia ya habari na mawasiliano. Je,”wadau” watarajie nini katika uwanja huo mpya?Nini siri ya mafanikio yake mpaka hivi sasa?Ana ushauri gani kwa bloggers wapya na wale wanaofikiria kuanzisha blog?Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo;

BC: Kwanza nikupe Hongera nyingi kwa kazi nzito unayoifanya.Mambo yanakwendaje?

MICHUZI: Ahsante sana, mambo mswano tu. Libeneke kwa kwenda mbele. Yaani baada ya miaka mitano ya tufanikio kiduchu tulikopatikana, sasa ni wakati muafaka wa kupiga hatua tano mbele, na kusaidia ujenzi wa taifa letu kwa njia ya habari.

Nitakuwa mtovu wa hisani na fadhila endapo kama nitaanza kujieleza bila kwanza kuwashukuru wadau wa Globu ya Jamii popote walipo duniani, kwani bila sapoti yao sidhani kama ningefikia robo tu ya hapa nilipo.

Naomba kwa heshima na taadhima wape AHSANTE SANA wadau. Waambie nawapenda, nawaheshimu na nitandelea kuwa mtumishi wao wakati wa raha na wakati wa shida. Pia naomba ninaowaudhi kwa njia moja ama nyingine wanisamehe kwani mie ni binadamu na si kamilifu. Pia si rahisi kumridhisha kila mdau kwa kila jambo. Napenda sana kutumia ule msemo wa ‘what’s good for the goose, is bad for the hen’. Hivyo naomba uvumilivu na kuelekezana pale palipo na dosari.

BC: Hivi karibuni utatimiza miaka mitano tangu ulipoanza ku-blog pale Helsink,Finland.Umepitia mengi,umeonana na wengi.Waliokuwa hawakujui,bila shaka hivi sasa wanakujua japo kwa sura tu.Unaielezea vipi safari hiyo ndefu tangu ulipoanza kwa maana ya kwamba umekabiliana na changamoto zipi nzito nzito na umejifunza mambo gani ya msingi katika uwanja mpana wa habari na mawasiliano?

MICHUZI: Changamoto nzito kubwa ya kwanza kwangu mimi ni maoni ya wadau. Kwa kweli haya maoni, ambayo ndiyo kiungo muhimu, nayaheshimu sana kiasi hata siruhusu mtu mwingine ayapitie maana yote yameletwa kwa minajili ya kuonekana na kusomeka.

Sasa linapokuja swala la kuchuja hapo ndipo kunakuwa na kazi kubwa kupita zote. Na hapo sijataja wingi wake (saa ingine hufika hadi 2000 kwa siku) wala urefu wake, katika kupitia ambapo inabidi upitie yote neno kwa neno.

Kaka Ndesanjo Macha alipokuwa ananiingiza rasmi kwenye tasnia ya Blog hiyo September 8, 2005 kule Helsinki, onyo la kwanza alilonipa ni kuwa makini sana na michango ya wadau. Awali nilikuwa naachia ‘Fungulia Mbwa’ ikaelekea wadau kutumia uhuru huo isivyofaa na kuanza kuchafua hali ya hewa na kujeruhi watu.

Changamoto ingine ni gharama za uendeshaji kwani inabidi utumie pesa nyingi sio tu kwenye intaneti bali pia vifuta jasho kwa wasaidizi.Nashukuru kwamba hivi karibuni michuzipost.com itakuwa kampuni kamili na kuanza kuajiri wafanyakazi wa kada zote. Tuombe mungu tu.

Cha msingi nilichojifunza katika safari yangu hii ni kwamba Watanzania tunapendana, hatusiti kusaidiana na pia ni wacheshi na wapenda utani sana. Kama huna haiba hiyo unaweza kujikuta unakuja juu na kukasirika kwa kucharurwa kidogo tu, na watu walio na nia njema tu kwako.

Mfano nilikuwa natuhumiwa kwamba napendelea CCM katika kuposti, ila hawakutaka kujua kwamba CCM wana njia nzuri ya kufikisha habari kila kona. Hatimaye vyama vingine kama CHADEMA na CUF vilipoanza kuleta habari nami kuchapisha, nikaanza kucharurwa – ati nimewagwaya CHADEMA na CUF kwa kuwa wamenipiga mkwara, wakati ukweli ni kuwa habari zao sasa zinapatikana kirahisi. Hizo ndizo changamoto nilizozipata nami nashukuru nimeshazoea, na kujua fika kwamba ubinadamu kazi.



BC: Blog yako ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya habari.Leo hii watu wengi,hususani waliopo nje ya nchi,wakitaka kujua kinachoendelea nchini,hukimbilia kwenye blog yako.Nini siri ya mafanikio hayo?

MICHUZI: Hakuna siri ya mafanikio zaidi ya kumuomba Mungu, kufanya kazi kwa mapenzi (passion), kujua nini wadau wanataka na sio nini wewe unataka. Uendelevu usiokoma (unflagging consistency), kupenda utani na matani na kuelezea kitu kwa lugha nyepesi iliyo katika anga kwa wakati husika.

Vile vile kuwa na lengo la kupasha habari chap chap, na sio kungoja taarifa ya habari ya saa mbili ama gazeti la kesho. Mambo ya leo lazima wadau wayajue leo leo. Nafurahi kuona vyombo kibao vya habari vimebuni tovuti na kuweka habari zao humo. Nawasikitikia wenye vyombo vya habari ambao hawana mitandao ya magazeti, redio, TV na kadhalika. Ni mawazo hasi kudhani kuwa kwa kuweka habari kwenye tovuti ni kudumaza usomaji ama usikilizaji.  Tovuti hujenga heshima kwa chombo husika na kuaminika. Pia ni muhimu kwa waandishi wa vyombo kuwa na blog kila mmoja. Yaani baada ya kuandika habari kwa chombo chake, anatumia blog kuchambua tukio kwa muono wake.

Wenzetu ughaibuni wanafanya hivyo na hupelekea wingi wa wasikilizaji ama wasomaji kuongezeka. Mwandishi wa habari aliye na blog ambayo kijuujuu inaonekana anashindana na mwajiri wake si adui bali ni rasilimali ambayo ikitumiwa vyema inaweza kupandisha chati chombo husika. Hapo ni kujipanga na kumtaka mwandishi awe anaelekeza wasomaji ama wasikilizaji kwenye chombo hicho. Mfano kukiwa na Breaking News mwandishi kwenye blog yake anaweza akatoa dondoo ya tukio ama habari hiyo kwa ufupi, kisha kumwelekeza msomaji apate habari nzima kwenye chombo husika. Hapo atakuwa amewezesha idadi ya wasomaji kuwa wengi na hakuna kitu ambacho watangazaji (advertisers) wanapenda kama wingi wa wasomaji katika chombo husika.

BC: Hivi sasa upo katika soft launching ya mtandao mpya ambao bila shaka katika siku kadhaa zijazo unatarajiwa kuumeza mtandao wa sasa.Naongelea http://michuzipost.com ambayo tayari ipo hewani.Unawaambia nini wasomaji wako na watanzania kwa ujumla kuhusu uwanja huu mpya?Umejiandaa vipi kuhakikisha kwamba unaendeleza “libeneke” kwa namna ile ile ambayo watu wengi wameshaizoea?

MICHUZI: Ama hakika kama ni ndoto, basi imetimia. Siku zote katika miaka hii mitano ya ku-Blog nimekuwa nikiota kuwa na mtandao kama huu http://michuzipost.com na kama utakumbuka kuna wakati nilijaribu kuja na aina nyingine ya mtandao ila ukashindikana kwani sikuwa nimejiandaa. Sasa hivi nimejiandaa kikamilifu kwa kuwa na nyenzo kibao ikiwa ni pamoja na kuwa na dedicated server yangu mwenyewe ambapo wasomaji 100,000 wanaweza kuwa ndani ya wavuti kwa wakati mmoja bila kuleta kwikwi ya spidi ama nini.

Pia kuna viunganishi katika social networks zingine maarufu kama vile facebook, twitter na YouTube pamoja na RSS feeds ili kuweza kufikia kila mtu katika kile kona.

Jipya katika libeneke hili la http://michuzipost.com ni Michuzi TV ambayo kwa kupitia ‘Live Streaming’, na mambo yakishakaa sawa kabisa, wadau watakuwa na fursa ya kuangalia matangazo ya moja kwa moja ya TV kwenye kompyuta zao. Yaani kutakuwa na matangazo ya TV  ya taarifa za habari, upembuzi wa magazetini leo, muziki na matukio kama zilivyo TV zingine. Mfano wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu ujao wadau watapata fursa ya kuona na kusikia kinachoendelea moja kwa moja toka sehemu ya tukio na wakati ule ule kupitia Michuzi TV. Mipango ya kuwa na Michuzi Radio ndani ya tovuti hii pia iko mbioni.

Uwanja huu mpya pia utajikita katika kutoa taarifa muhimu kama vile nyumba (real estate & property) zilizo sokoni kwa kuuzwa ama kupangishwa, tenda zilizopo serikalini ama kwa watu binafsi, manunuzi (procurement) na kadhalika. Pia kutakuwa na uwanja wa wadau kuleta Hoja Binafsi zijadiliwe. Hali kadhalika mfumo mzima unaompa msomaji fursa rahisi ya kufunua ukurasa autakao, tofauti na blog ya kawaida ambapo kila kitu kipo katika ukurasa mmoja na hutoweka ukurasani baada ya muda. Hivyo kama utataka habari za michezo unabofya penye ‘Sport’ nawe utapata mlolongo wote wa mambo ya michezo yaliyopo hewani katika ukurasa husika. Ukiangalia kwa makini utakuta kurasa zote ni rafiki wa matumizi (user friendly) na haihitaji mtu kuwa mtaalamu wa TEKNOHAMA kuweza kuperuzi na kudadisi.

Vile vile sehemu ya maoni ipo wazi kwa kila post, na hakuna jambo linalochangamsha mtandao kama kuruhusu ushiriki wa wasomaji (interaction), badala ya habari kuwa ya upande mmoja tu. Yaani hivi sasa msomaji naye ana uhuru wa kuchangia mawazo ama upande mbadala wa lililoandikwa ama kutangazwa.

BC: Kila kukicha watanzania mbalimbali wanaanzisha blogs.Pamoja na hayo blog nyingi zinakuwa active kwa muda mfupi sana kisha zinatokomea.Una ushauri gani kwa watu wanaoanzisha blogs kuhusu jinsi ya kuhakikisha kwamba blog zao zinakua na kubakia active?

MICHUZI: Ni kweli kila kukicha blog mpya huanzishwa nami huwa nafurahi sana. Aidha, huwa sisiti kumtangazia mtu blog yake akiomba nifanye hivyo. Lakini si uwongo kwamba wakati mwingine inaboa, hasa pale blog uliyoipromoti inapododa baada ya muda mfupi.

Lakini nadhani kuna mambo kadhaa yanayochangia hilo, na si vyema kutuma lawama za jumla. Tuangalie sababu ambazo nadhani ndizo chanzo cha kudoda kwa blog nyingi.

Mtu kuanzisha blog bila kuwa na lengo mahususi la kufanya hivyo. Mtu anakurupuka kuanzisha blog na kutaka kuwa kama BongoCelebrity ama Michuzi kwa usiku mmoja. Hajui ama kasahau kwamba wenzie sio tu wameanza muda mrefu na wameumia sana kufika hapo walipo kwa kazi za usiku na mchana (mfano mie muda wa kulala nimeshasahau ni wakati gani kwa wingi wa kazi, hasa za kupitia maoni ambayo kuna wakati hufikia hata 2000 kwa siku! Na lazima uyapitie yote ili yasijepenya ya kuchafua hali ya hewa ama kujeruhi nafsi ya mtu ama za watu). Hivyo utakuta mtu asiye na malengo anadhani blog ni habari za kila siku tu, kwa vile Michuzi na wenzie wanafanya hivyo na kupata wasomaji kibao. Anasahau kuwa wakina Michuzi ni wanahabari wenye vibali vya kuingia kila mahali na kusaka habari.

Ushauri wangu ni kwamba sio lazima kila blog iwe ya habari za siku. Tafuta mada ambayo utaivalia njuga na kucheza nayo kila siku. Mfano rahisi ni kama kina Jane John ambaye anashambulia mambo ya michezo na wachezaji. Shamim Zeze anaendeleza libeneke la mitindo na mavazi. Kuna Jiang Alipo anayekupa habari za mama na mwana (malezi na uzazi), ama Ernest Makulillo jr anayecheza mna libeneke na vyuo vikuu na nafasi za masomo ughaibuni. Hivyo utakuta hawa hawahangaiki sana, kwani mada zao zipo kila pembe na haina kazi kuzipata. Nashauri kila mtu aanzishe blog lakini iwe na mada anayoifahamu, anayoimudu na ambayo haina ukomo.

BC: Kila la kheri kaka katika kazi zako.

MICHUZI: Nashukuru sana BC

Feedback / Comments

6 Responses to “MAHOJIANO NA ISSA MICHUZI JUU YA UJIO WA MICHUZIPOST.COM”

  1. Comment by Mickey Jones Amos on August 19th, 2010 12:53 pm

    HONGERA:MAHOJIANO YENYE MTAZAMO WA MAENDELEO

    Kwanza ningependa kuwashukuru wote BC na Uncle Michuzi kwa kuweza kupata nafasi ya mahojiano ya pamoja,imetupa imani kuna ushirikiano wa wanahabari wetu wa Tanzania.
    michuzipost.com imepokelewa na wadau wote ulimwenguni kwa furaha na mafanikio mazuri,
    haya ni maendeleo ambayo tunaweza kuyaita
    “TANZANIAN DREAM” mafanikio yaliyowezekana kwa kipindi kifupi cha miaka mitano,sawa na mkulima kuangalia mmea/mti ulioupandwa unaanza kutoa matawi kwa kuleta matumaini ya kuyaona matunda katika kipindi kifupi kijacho.
    Nini cha kuwapongeza hapa wana-blogu wetu wa kitanzania zaidi ya kusema mmekuwa na moyo wa kujituma kwa manufaa ya watanzania

    Watanzania watawakumbuka vipi mkitoweka, ni wazi kutakuwa na kumbukumbu ya kazi kubwa mliyotufanyia katika mazingara ya shida na matatizo ukiondoa “kwikwi” za ukosefu wa umeme wa hapa na pale kwa kuwa zipo kila nchi katika bara letu la Africa,mmeweza kufikia hatua kubwa ya kimaendeleo katika mtandao wa technologia ya kisasa kitaifa na kimataifa mpaka kutufikisha hapo tulipofika sasa na kuyaona matawi yanayoanza kujitokeza, wazi baada ya kuajiriwa wataalamu zaidi kuwakilisha kama kampuni maalumu na ya kudumu kama asemavyo uncle Michuzi,tutajionea matunda ya mti aliyoupanda uncle Michuzi unatoa matunda.

    Sina zaidi ya kuwapa pongezi na shukrani zidi ya kukuombea maisha marefu na afya njema,bila ya ninyi wengi tunaoishi mbali na nyumbani tungekuwa bado tupo kizani,kazi zenu zinaturudisha nyumbani siku hadi siku.

    Mdau wa DENMARK

  2. Comment by bongocelebrity on August 19th, 2010 1:52 pm

    Mickey,
    Kwa niaba ya timu nzima ya BC,shukrani kwa kuthamini mchango kidogo tunaotoa katika ulimwengu wa habari na mawasiliano.Shukrani pia kwa support yako.Asante

  3. Comment by SN on August 19th, 2010 3:04 pm

    Kwanza kabisa, hongera sana Michuzi kwa hatua uliyofikia. Kusema ukweli mimi nilishindwa kusubiri kukuona na tovuti yako mwenyewe ambayo ni endelevu! Na mambo sasa yamejipa…

    Najua fika kuwa kazi sio mchezo; hasa kwenye wiki za kwanza ambapo unakutana na kwikwi ambazo hujawahi kufikiria. Lakini jinsi unavyohama taratibu, itapunguza matatizo.

    Sasa, mimi binafsi ni mpenzi mkubwa wa makala zinazoletwa pale kijiweni, na ningependa hizi zipewe kipaumbele. Najua hilo ni jukumu la waandishi au watu wanaojitolea kuandika, lakini kwa mfano itakuwa sio vibaya kila wiki tuwe na makala mbili za maana.

    Kuna suala lingine la lugha inayotumiwa kwenye hizi makala, ingawa kutumia ‘lugha ya malkia’ sio tatizo, nadhani itakuwa jambo la busara kama ukiwasukuma waandishi kuandika kwa Kiswahili — kwasababu sio wasomaji wote ni wasomi (kwenye uchumi kuna misamiati mizito!). Na ninaamini kila Mtanzania ambaye anajifunza matumizi ya mtandao kwa mara ya kwanza, basi anaoneshwa Michuzi. Lakini kwa wale ambao bado hawajiamini kuandika kwa Kiswahili kwa ufasaha, hamna tatizo.. Waendelee tu.

    Shukrani kwa haya mahojiano na nawatakia wote kila la kheri!

    Oh, almanusura nisahau.. Shikamoo, Ankal na Jeff!

  4. Comment by bongocelebrity on August 19th, 2010 5:12 pm

    SN,
    Shukrani kwa mchango wako makini kabisa.Bila shaka Michuzi amesikia ushauri wangu kuhusu masuala ya lugha.Ni muhimu kukipa Kiswahili chetu nafasi.Kinyume cha hapo tunaweza kuonekana kama “tumekariri” tu.

    Kazi nzuri sana mnafanya hapo vijana.fm Hakuna kulala

  5. Comment by Namys on August 20th, 2010 11:58 am

    Hongera sana BC na MICHUZI kwa mahojiano mazuri

  6. Comment by Mwanamke wa Shoka (UK) on September 29th, 2010 2:16 pm

    …..libeneke kwa kwenda mbele…hapo umenena Kaka Michuzi….!!..Mungu akupe heri kaza buti…

Leave a Reply