
Ninapoandika ujumbe huu,matokeo mbalimbali ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika hapo jana yanaendelea kuingia. Kama ambavyo umesikia au umeona na kama ambavyo “alama za nyakati” zilishaanza kuonyesha(waliozipuuzia bila shaka wanalia sasa) wananchi wengi walishachoka.Walitaka mabadiliko. Tanzania tunayoijua bila shaka haitokuwa ile ile.
Wakati tukiendelea kusubiri taarifa rasmi kutoka kwa Tume ya Uchaguzi, tunaamini una mengi au machache ya kuwaeleza wengine kuhusu ulichokiona,ulichokisikia wakati zoezi la uchaguzi lilipokuwa linaendelea. Je,uliona nini?Mambo yalikwenda kama ulivyotarajia? Ulitarajia matokeo ya namna hiyo/hii?Uliyetaka ashinde ndiye aliyeshinda? Ukumbi ni wako.Tunasikiliza.Wanasikiliza.Wanasoma.Karibu

Kwa upande wa Tanzania,hadithi ya kuwa wasindikizaji,inaelekea kuendelea.Mrembo wetu,Genevieve, ameshindwa kufua dafu katika fainali za mwaka huu za mrembo wa dunia, Miss World,zilizofanyikia Sanya nchini China.
Katika mashindano hayo ambayo yalikuwa yanafanyika kwa mara ya 60 tangu yaanzishwe, mshindi ameibuka kuwa mrembo kutoka nchini Marekani, Alexandria Mills.Mshindi wa Pili, ni mrembo kutoka Afrika,nchini Botswana, Emma Wareus huku mshindi wa tatu akiwa ni Adriana Vasini kutoka nchini Venezuela.
Alexandria Mills ni binti mwenye umri wa miaka 18 tu kutoka jijini Louisville ndani ya Jimbo la Kentucky. Ana urefu wa mita 1.75(5’9) na tayari kabla ya kushinda taji hilo,ni model aliyemo kwenye orodha ya models wa Elite Models Agency.
Umati uliojitokeza kumsikiliza Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM-Mh.Jakaya Mrisho Kikwete. Hapo ni Mwembeyanga-Temeke jijini Dar-es-salaam.

Umati uliojitokeza kumsikiliza Mgombea Urais kwa tiketi ya CHADEMA.Hapo ni pale pale Mwembeyanga,Temeke jijini Dar-es-salaam.
Kama umekuwa ukifuatilia kwa makini kampeni za wagombea mbalimbali hususani wale wa kiti cha juu kabisa(Urais), bila shaka utakuwa pia umesikia tambo, majivuno na vijembe mbalimbali ambavyo vimekuwa vikitolewa na watu wanaoviunga mkono vyama au mgombea fulani.Wengine wamefikia hata hatua ya kutukanana,kupigana nk. Wengine wameenda hata jela. Sijui ni kwa ajili ya ushabiki tu au la?
Neno “nyomi” kwa maana ya wingi wa watu waliohudhuria mkutano wa kampeni,limetumika mara nyingi. Wingi wa watu waliojitokeza kuhudhuria umekuwa ni mwanya wa kuwashawishi wengine kwamba mgombea fulani au chama fulani kinakubalika zaidi!Bila shaka wingi huo huo ndio ulitumika na baadhi ya waendesha kura za maoni(polls) kupata matokeo yao! Uwanja umeshona vibaya sana leo.Ah mgombea wetu anakubalika sana.Anakubalika au inawezekana watu hao hawana ajira na wametumia muda huo kuja kusikiliza kama angalau una sera ya kuwakomboa kutoka walipo? Just thinking….
Utakuwa umesikia na kuona vichwa vya habari vilivyokwenda kwa staili ya “JK Funika Bovu Kilakala” au “Dr.Slaa Funika Bovu Manzese”.Sina uhakika sana na maana ya neno “funika bovu” lakini natumaini neno hilo lilikuwa linamaanisha kwamba mgombea fulani au chama fulani kupitia mgombea wake,kimeonyesha kuwa na sera zinazoeleweka na kutekelezeka.Kinyume na hivyo,neno hilo litakuwa limetumika visivyo.Limetumika kishabiki tu.
Ninaposema sera zinazoeleweka na kutekelezeka namaanisha sera zilizoundwa kutokana na mazingira halisi ya Tanzania na sio kukopi na kupesti kutoka katika vitabu vya nchi za nje kama ambavyo nimesikia wagombea wengi wakiwasukumia wananchi misemo na maneno ambayo kimsingi haina maana kwao. Eti kasema nini vile?…Info..mesheni.. teki nini? Hata mimi sijamsikia.Tusubiri labda atarudia tena.Imetoka hiyo.
Kumbuka kwamba kama mwananchi haelewi unachokiongelea, hatokuwa tayari kutoa ushirikiano wake katika kuleta maendeleo.Utamlaumu? Sidhani. Ulimfanya mbumbumbu,ukamweka mtu kati kwa mikogo na maneno ya kuazima. Lazima uweke mbwembwe.Watajuaje kwamba umesoma?Alah!
Nimesikia vijana wakibishana kwa misingi ya kwamba muziki uliofungwa kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea wake ulikuwa “sio wa kitoto”.Suala sio sera tena bali ukubwa wa sauti au burudani!Hawa ni vijana ambao wote hawana ajira,hawakusoma na ikitokea mmoja wao akaanguka kutokana na “mishipa ya ubishi” kumpasuka,hakuna gari wala njia ya kumwezesha kuwahishwa hospitalini!
Hapo ndipo ninaposema, nilichokiona mimi wakati wa kampeni ni Ushabiki Vs Utashi. Muda mwingi umetumika au umetumiwa katika kurushiana “makombora”. Sera zimekuwa sisi waungwana wao majangili.Muziki mnene, dhidi ya helikopta ile ya kisasa zaidi. Tumlaumu mwananchi? Kivipi.Mbona akifungua blog au kusoma gazeti,habari ndio hizo hizo?Maneno ndio yale yale?
Matumaini yangu ni kwamba Ushabiki utaishia siku ya Jumamosi.Jumapili ni siku ya Utashi.Ninaposema utashi namaanisha ile nguvu au ari ya kuona nchi yetu inasonga mbele,kuendelea kuwa na amani na utulivu. Siku ya kuweka kando matarumbeta,khanga,kofia,nk na kupiga kura inayofaa. GO VOTE.NENDA KAPIGE KURA.

Sina hakika kama mambo haya mawili,kwa kuzingatia umuhimu wake,yanafanana. Lakini kwa sababu ni “matukio”, basi kwa namna moja au nyingine, naamini tunaweza kuyaweka kwa pamoja. La kwanza lina umuhimu wa aina yake. Ni Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania kwa mwaka 2010.
Jumapili hii,Tarehe 31 October 2010, mamilioni ya watanzania watapanga foleni ndefu ndefu ili kutimiza miongoni mwa wajibu wa msingi wa raia;Kuchagua viongozi. La,sio viongozi tu bali viongozi bora na sio bora viongozi.
Kama “Polls” ni jambo la kuaminika, uwezekano wa Tanzania kujitengenezea historia ya aina yake ni mkubwa. Kuna mwamko ambao haukuwepo miaka mitano iliyopita. Kuna hali ya wananchi kutaka mabadiliko fulani. Business as usual inaelekea kuwa kauli ambayo inaanza kutoingia vichwani mwa watu. Kinachoombwa ni kutawala kwa amani,haki na kuzingatia msemo wa Asiyekubali Kushindwa Si Mshindani. Ikitokea wapiga kura wakakataa kumpa mtu fulani ridhaa ya kuwaongoza,jazba ziwekwe kando.We pray for peace!
La pili ni mashindano ya kumsaka mrembo wa dunia,Miss World 2010.Kulinganisha na hilo la hapo juu,naweza kabisa kuthubutu kusema kwamba hili halina maana sana. Lakini lina maana yake na nafasi yake.
Bendera ya Tanzania itakuwa inapepea huko Sanya nchini China wakati Miss Tanzania 2010,Genevieve Mpangala, atakapokuwa anawania taji la Dunia la Urembo/Ulimbwende. Ukitaka kusoma kidogo kumhusu Genevieve kwamba anapenda nini, ana mafanikio gani maishani mwake mpaka hivi sasa,bonyeza hapa. Tunamtakia kila la kheri.

Miss Tanzania 2010, Genevieve Mpangala
Naam,wikiendi ya aina yake hiyo inakuja.Kama unavyo vigezo vyote vya kupiga kura,tafadhali NENDA KAPIGE KURA,GO VOTE!!!

Kila mashindano Kombe la Dunia la Soka(FIFA) huwa na vituko au vitu fulani ambavyo huwekwa katika kumbukumbu ya kudumu vichwani mwa wapenzi wa soka na hata wale ambao sio wapenzi.
Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu zitakumbukwa kwa mambo mawili makubwa.Kwanza ni zile tarumbeta za Vuvuzela na Pili ni Paulo,yule Pweza wa nchini Ujerumani aliyetabiri matokeo ya mechi mbalimbali na kuwa sahihi kwa asilimia 100%.
Bahati mbaya ni kwamba wakati Vuvuzela bado zinadunda na kuzidi kusambaa ulimwenguni kote, Paulo Pweza amefariki. Paulo Pweza amefariki akiwa nyumbani huko Oberhausen, nchini Ujerumani akiwa na miaka miwili.

Mke wa Rais wa Zimbabwe,Robert Mugabe,kwa mara nyingine tena amejaza kurasa za mbele za magazeti na vyombo vya habari huko kusini na kati mwa Afrika baada ya kuenea kwa uvumi kwamba amekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtu ambaye ni miongoni wa marafiki wa karibu wa mumewe.
Kwa mujibu wa Gazeti la Times Live la nchini Afrika Kusini,Mugabe aliambiwa siri hiyo nzito na dada yake,Sabina, alipokuwa mahtuti kitandani kabla hajafariki baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Grace Mugabe,ambaye ni kiumri ni mdogo kwa Rais Mugabe kwa miaka 41,mara kwa mara amekuwa akihusishwa na kashfa za kimapenzi nje ya ndoa.Miaka kadhaa iliyopita alisemekana kuwa na uhusiano na jamaa aliyeitwa Peter Pamire kabla jamaa huyo hajafariki katika ajali ya gari ambayo ilitokea katika mazingira ya kutatanisha. Jamaa mwingine anayeitwa James Makamba,ilibidi akimbie nchi baada ya kuenea kwa tuhuma hizo.
Mtu ambaye anahusishwa katika uvumi ulioenea hivi sasa ni Gideon Gono,ni Gavana wa Benki Kuu ya nchi hiyo,mshauri wa karibu wa Mugabe na pia mfuasi mzuri wa chama anachokiongoza Mugabe cha ZANU-PF.
Hii inaweza kuwa hadithi ya what comes around,goes around,kwani uhusiano wa Mugabe na mkewe Grace pia ulianza katika wigo wa mapenzi ya nje ya ndoa.Wawili hao walianza mapenzi yao wakati Grace alipokuwa Katibu Muhtasi(Secretary) wa “Jongwe”.Watatu miongoni mwa watoto wao,walipatikana katika kipindi hicho huku Mugabe akiwa ndani ya ndoa halali na mkewe Sally ambaye alikuwa akiugua kabla ya kufariki dunia mwaka 1992

Mwanamuziki maarufu wa mtindo wa Reggae ulimwenguni, mzaliwa wa Jamaica, Gregory Isaacs, amefariki dunia hivi leo nyumbani kwake jijini London nchini Uingereza. Gregory Isaacs alizaliwa jijini Kingston nchini Jamaica mwaka 1951.Amefariki akiwa na umri wa miaka 59.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na meneja wake, Copeland Forbes,Gregory Isaacs amefariki kutokana na ugonjwa wa kansa ya mapafu(Lung Cancer) ambayo aligunduliwa kuwa nayo mwaka mmoja uliopita ingawa aliendelea kuwa jukwaani mpaka wiki chache zilizopita.
Gregory ambaye wapenzi wa muziki walimpa jina la “Cool Ruler” kutokana na aina yake ya muziki wa reggae iliyokuwa imejaa nyimbo zenye dhana za mapenzi au mahaba,alianza kazi za muziki tangu akiwa kijana mdogo kabisa.
Baadhi ya nyimbo zake zilizowahi kutamba ni kama vile “Love is Overdue”, “All I Have is Love”,”Soon Forward” and What Feeling bila kusahau kibao chake kilichompatia umaarufu ulimwenguni kote cha “Night Nurse” kilichomo katika albamu yake ya mwaka 1982 iliyobeba jina hilo.
Maisha yake katika muziki yaliingia dosari,pale alipojiingiza katika utumiaji wa madawa ya kulevya kitu ambacho kilipelekea kuswekwa lupango mara kadhaa. Mwaka 2007 aliwahi kusema kwamba yeye amepitia “Cocaine High School”, shule bora kupita zote lakini pia ya bei mbaya kupindukia!
Utumiaji wa madawa ya kulevya ulisababisha kupotea kiasi kwa sauti yake iliyokuwa imezoeleka ingawa hali hiyo haikuathiri sana mauzo ya albamu yake ya mwisho aliyoitoa mwaka 2008 na kwenda kwa jina “Brand New Me”

Endapo unataka kufaidi kibao kinachosindikiza wikiendi hii hapo chini,nina shauri kitu kimoja;Bonyeza player,ongeza sauti kidogo,sio sana.Kisha fumba macho.Sikiliza kwa makini huku ukiwaza na kutafakari ujumbe unaokujia.Dr.Remmy Ongala akiwa na bendi yake ya Matimila anaongelea Maisha kwa mtindo wa aina yake.
Maisha ni nini? Inakuwaje mmoja anazo nyingi mpaka kusaza wakati mwingine hata ya kununulia mhogo inapiga chenga?Inakuwaje huyu anaonekana bora kuliko yule wakati wote ni binadamu na wana mahitaji sawa? Au ni kweli kwamba aliyesema Binadamu wote ni sawa lakini wengine ni sawa kuliko wengine hakukosea?
Majibu kwa maswali hayo hapo juu na mengine ni mengi.Yana tofautiana kutegemea na mambo chungu mbovu.Lakini kama kuna jambo ambalo tunaweza kukubaliana na pengine ndio ujumbe uliokusudiwa na Dr.Remmy Ongala ni kwamba sote hatuna budi kufanya kazi kwa bidii. Habari ya kuketi kijiweni na kusubiri neema ya Dr.Slaa au Kikwete,ni kama ndoto mbaya.Si unajua kwamba kampeni zikiisha tour ya nchi nzima ndio nazo zinafikia kikomo?Mwendo unakuwa kutambaa kwa Obama,David Cameron na kina Sarkozy.Tunaenda kutafuta wawekezaji.Kwanini usiwapigie simu tu? Ah hapana…wakiniona ndio safi.Na pia mimi na Mama wa kwanza tunahitaji mapumziko!Alah..kijana mbona una maswali namna hiyo?
Pamoja na kufanya kazi kwa bidii,Dr.Remmy anakumbusha “kwenda taratibu”.Wenzetu ughaibuni wanapenda kusema Taking it Easy.Bidii ya kazi isikufanye ukasahau kupumzika,kujumuika na wana jamii,ndugu na marafiki kila mara inapobidi na inapowezekana.Hayo ndio Maisha.After all,pesa ni za nini kama siku moja moja huwezi kupata muda wa kuzifurahia na wenzako hususani wanaostahili na unaowapenda? Pata Burudani.Msikilize Dr.Remmy Ongala & Orchestra Super Matimila katika wimbo Maisha.Wikiendi Njema.
Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.

Majuzi shindano maarufu la Big Brother Africa limemalizika huku Afrika ikishuhudia ushindi,kwa mara ya pili mfulululizo,ukienda nchini Nigeria.Mshindi wa safari hii akiwa ni Uti Nwachukwu,ambaye amejizolea kitita cha dola za kimarekani laki mbili ($ 200,000)
Wakati tukimpongeza mshindi,yapo mambo kadhaa ambayo yamejitokeza hususani kupitia katika maoni ya wengi katika mitandao ya kijamii(Social Networks). Fikra tofauti tofauti zimekuwa zikitolewa kuhusiana na ushindi wa Uti na pia kushindwa kwa Mwisho Mwampamba ambaye ndiye alikuwa akiiwakilisha Tanzania ndani ya jumba la Big Brother.
Kumekuwepo na maoni kwamba Mwisho hakushinda kwa sababu watanzania wengi,hususani wale waliokuwa na uwezo wa kupiga kura,hawakufanya hivyo na badala yake kuishia kumtakia kheri bila kutimiza kitendo muhimu cha kupiga kura za kuwatoa wengine ili Mwisho abakie na hatimaye kuibuka mshindi.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation la nchini Kenya, nchi zilizopiga kura ili kumuokoa Uti zilikuwa ni Angola, Ethiopia, Ghana, Kenya, Mozambique, Nigeria na Uganda wakati mshindi wa pili, Munya, kutoka Zimbabwe, alikingiwa kifua na Botswana, Malawi, Namibia, South Africa, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.

Mwisho Mwampamba.
Kama takwimu hizo ni za kuaminika, lipo jambo ambalo watanzania inabidi tujifunze.Ushindi hauletwi na maneno peke yake.Ni sharti maneno yaambatane na vitendo.Ushabiki bila vitendo ni kazi bure.
Hivi sasa, kupitia mitandao mbalimbali, tunashuhudia kampeni za nguvu za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 nchini mwetu.Kuna mwamko wa aina yake ambao haujapata kutokea. Hakuna anayezembea.Ndio maana tunaona kila mtu yuko “busy”.Wananchi wengi wanatoa maoni yao.Kuna wanaotaka mabadiliko na kuna ambao bado wanasema “Jini likujualo,halikuli likakwisha”.
Hali niliyoieleza hapo juu inatia moyo.Binafsi naamini kwenye mseto wa kiserikali ambapo hakuna chama kinachoweza kupitisha kila kitu bungeni ati kwa sababu tu, kufuatana na demokrasia, basi “mwenye nyingi mpe”.Naamini kwenye check and balance yenye kufanya kazi kivitendo na sio maneno ya kwenye kamusi na katiba.
Basi ushabiki wa kampeni za kisiasa,usiishie kwenye maneno tu.Kama una uwezo wa kupiga kura,basi tarehe 31 Octoba,damka nenda katimize wajibu.Tujifunze kutokana na tulichokiona majuzi katika Big Brother Africa.Ushabiki na kutakiana kheri bila vitendo ni kazi bure.
Pichani juu:Uti(mwenye rasta) akifurahia ushindi wake.


sending...
