“SUMU YA MAPENZI”-MAQUIS ORCHESTRA (ZILIPENDWA)

Miongoni mwa vitu ambavyo tangu mwanzo wa ulimwengu(na bila shaka mpaka mwisho) vimeendelea kukuna vichwa vya wanasayansi, wasomi, watafiti mbalimbali na hususani wanasaikolojia, ni pamoja na kitu kinachoitwa “Mapenzi”. Nimeshawahi kumuuliza mdada mmoja hivi kwamba unajuaje kwamba unachokiwaza au unachokifanya kinatokana na mapenzi?Unawezaje kutofautisha kati ya mapenzi,tamaa za muda mfupi au mfano wa mapenzi?

Kama ambavyo maswali hayo hapo juu ni magumu kwangu(naamini hata wewe) basi ndivyo hivyo hivyo jinsi gani mapenzi yanabakia kuwa somo lisiloisha. Tukianzisha darasa hata saa hizi, wewe pale utakuwa na tafsiri yako na yule kule kona atakuwa na tafsiri yake. Mapenzi ni matamu na pia mapenzi ni machungu. Inakuwaje kitu kitamu kiwe pia kichungu? Ni katika wakati gani kinakuwa kitamu na katika wakati gani kinakuwa kichungu? Maswali yanaweza kuwa lukuki na wala majibu ya moja kwa moja yasipatikane…

Sasa mbali na wanasayansi, wasomi na watafiti mbalimbali, kundi mojawapo la watu ambalo limekuwa mstari wa mbele katika kutafuta maana na mantiki ya mapenzi ni lile la wasanii.Wasanii, kwa kutumia vipaji vyao, wameelezea dhana ya mapenzi na bado wanaendelea kuelezea. Wao wanatizama jamii zaidi.Wanaona mtu anafurahia mapenzi na pia wanaona mtu analia kutokana na kutendwa na mapenzi. Msanii akiona vile anawaza na kutunga sentensi mbalimbali zinazohusiana na kile anachokiona au kukisikia. Tunaziita nyimbo za mapenzi.

Kati ya nyimbo nyingi za mapenzi, mojawapo ni hii ya leo katika kipengele cha Zilipendwa kutoka kwao Maquis. Hii ni mojawapo ya kazi zilizopendwa sana kunako mapenzi.Kinara hapa(nipo tayari kusahihishwa na historians wa muziki wa dansi) ni Nguza Viking (pichani) ambaye sote tunajua kwamba bado yupo ndani(gerezani) na wenzake kama vile Vumbi Dekule na wengineo.Usikilize hapa chini na uwe na weekend njema.

Audio clip: Adobe Flash Player (version 9 or above) is required to play this audio clip. Download the latest version here. You also need to have JavaScript enabled in your browser.

Comments Closed

Comments are closed.

Copyright © Bongo Celebrity