Roma Mkatoliki: Yupo Wapi? Huu Ndio Wimbo Uliomuweka Matatani? (VIDEOS)

Usiku wa jana, kupitia mitandao ya kijamii, taarifa zilianza kuenea mitandaoni. Msanii Roma amekamatwa akiwa ndani ya studio za Tongwe Records. Mtu wa kwanza kuujulisha umma kuhusu habari hizo ni Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule aka Professor Jay kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Habari zilizidi kupasha. Roma ametwalia sambamba na msanii mwingine Moni ambaye hivi karibuni walishirikiana katika wimbo Msimsahau Mchizi. Mbali ya Roma na Moni, waliowachukua waliondoka pia na kijana wa kazi za nyumbani anayejulikana kwa jina la Ima. Mbali ya kuondoka na kina Roma waliondoka pia na vitendea kazi kama computer na camera.

Taarifa hii na hatua za mwanzo zilizochukuliwa, zimethibitishwa na mmiliki wa studio, J Murder alipokuwa akiongea na DJ Tass wa Magic FM katika kipindi cha Kwetu Fleva. Unaweza kusikiliza kipande cha mahojiano hayo hapa chini.

Mbali ya J Murder, mke wa Roma Mkatoliki amethibitisha pia kuhusu kutoweka kwa mumewe. Anaomba msaada wa kujua alipo mumewe. Anakuomba mimi na wewe na yule kumsaidia.

Kutoweka kwa Roma, kunakuja takribani wiki moja tangu msanii mwingine, Ney Wa Mitego, aliposhikiliwa na polisi kwa tuhuma ambazo hazijawahi kuwekwa wazi wala kufafanuliwa. Inahisiwa alikamatwa baada ya kutoa wimbo wa Wapo ambao ulionekana kuwakera baadhi ya watu (wakubwa). Baadae aliachiwa kufuatia “msamaha” wa Rais.

Je, yawezekana kutoweka kwa Roma ni muendelezo wa kinachoonekana kuwa ukandamizaji wa uhuru wa kujielezea hata kupitia sanaa ya muziki?

Nadharia iliyopo ni kwamba Roma amekamatwa kwa sababu beat ya wimbo wake na Moni, imetumiwa na msanii mwingine anayeitwa Sifa Digital. Jina la wimbo wa Sifa Digital ni Tanzagiza. Maudhui ya nyimbo hizi mbili ambazo utasikiliza punde hayafanani. Kinachofanana ni beat. Je, ni kweli kwamba nyimbo hizi au beat hizi ndizo ambazo zimemuweka Roma matatani?

MSIMSAHAU MCHIZI-Roma & Moni

TANZAGIZA-Sifa Digital

 

Comments Closed

Comments are closed.

Copyright © Bongo Celebrity