Miezi 3 Tangu Kufariki Kiongozi Wa Upinzani Nchini DRC, Étienne Tshisekedi, Bado Hajazikwa.Sababu Ni Hii Hapa

Kwa zaidi ya miongo minne, Étienne Tshisekedi, alikuwa sauti kuu kutoka upande wa upinzani nchini DRC ambalo ni miongoni mwa mataifa ya barani Afrika yaliyobarikiwa kuwa na utajiri wa kustaajabisha ingawa wananchi wake ni miongoni mwa masikini wa kutupwa ulimwenguni.

Hata hivyo, kama ilivyo kwetu sote, mwezi wa pili mwaka huu, nafsi yake ilirejea kwa Muumba. Cha kustaajabisha ni kwamba tofauti na mila za watu wa DRC ambapo wafu hupumzishwa kwenye nyumba zao za milele ndani ya siku chache tu toka wafariki, kiongozi huyo wa upinzani bado hajazikwa. Mwili wake bado upo ndani ya majokofu ya baridi nchini Ubelgiji tangu afariki tarehe 1 Februari mwaka huu.

Kinachosababisha ucheleweshwaji wa mazishi ni mgogoro mkali ulioibuka baina ya familia yake na serikali kuhusu mahali anapostahili kuzikwa.

Kwa mujibu wa New York Times, kinachohisiwa kuwa chanzo cha mgogoro unaoendelea ni hofu (na mchango wa serikali ya Rais Joseph Kabila kwamba mazishi ya kiongozi huyo wa upinzani, yanaweza kuibua chachu ya upinzani ambayo kila siku inazidi kukua.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya New York Times kura za maoni zinaonyesha kwamba Rais Kabila anakubalika na idadi chache sana ya wananchi kufikia asilimia 7.8 pekee. Kuporomoka kwa uungwaji mkono wa Rais Kabila ambaye alichukua madaraka mwaka 2001 kufuatia kuuawa kwa baba yake ambaye alikuwa Rais (Kabila) kunatokana na imani kwamba Rais Joseph Kabila amezidi kujilimbikizia mali zinazotokana na utajiri mkubwa wa madini nchini humo huku wananchi wakiendelea kuishi kwenye ufukara.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo hiyo ya New York Times, mwili wa Tshisekedi ulikuwa uwasilini nchini Kongo Ijumaa ya wiki iliyopita tayari kwa mazishi yaliyokuwa yafanyike katika Makao Makuu ya chama chake cha Muungano Kwa Ajili ya Demokrasia na Maendeleo Ya Jamii jijini Kinshasa lakini mwili huo haukuwasili.

Taarifa inazidi kupasha kwamba kutowasili kwa mwili kwa mwili huo ni mwendelezo wa muingilio wa kisiasa unaofanywa na serikali ya Joseph Kabila kwa nia za kisiasa.  Mapema wiki iliyopita gari la polisi na kituo cha polisi kilichopo mbele ya ofisi za chama hicho cha upinzani viliwashwa moto na watu wasiojulikana. Zaidi ya polisi 100 walilizunguka eneo hilo. Baada ya hapo polisi wamewazuia wapinzani kuingia kwenye ofisi zao au wanaporuhusiwa ni kuingia chini ya ulinzi mkali wa polisi kitendo ambacho kinatafsiriwa kama njia mojawapo inayotumika kuwadhibiti wapinzani nchini humo.

Hata hivyo  Roger Ilunga ambaye ni miongoni mwa watoto wa Tshisekedi, amenukuliwa akisema mwili wa baba yao utawasili nchini DRC ndani ya siku 12 na tayari wao na serikali wamekubaliana kwamba mwili wake hautozikwa tena katika viwanja vya makao makuu ya chama hicho bali sehemu nyingine.

 

Comments Closed

Comments are closed.

Copyright © Bongo Celebrity