Tizama: “Atabadilika”-Lameck Ditto (Video Rasmi)

Lameck Ditto-Atabadilika

Kama umewahi kupenda, unajua maana ya “kubadilika”. Alivyoanza sivyo alivyo. Alichosema ukikikumbuka unashikwa na butwaa. Akili inapwaya kama vazi lisilo lako. Lakini bila shaka unajua pia kwamba kwenye mapenzi kuna kukingiana kifua. Unatetea. Unamtetea japo unajua sio kweli. Unafanya hivyo ukiamini atabadilika. Unaamini atakuja kuketi na kubadili mwelekeo.

Lakini utamtetea mpaka lini? Mara ngapi? Nahisi inategemea na upana wa penzi. Kuna jembamba la kushikiwa na uzi. Kuna nene kama kamba ya Power Mabula. Mapenzi ni siri. Ni safari ambayo mwisho wake ukiujua hutoianza. Yakubidi ujifunze huku ukiicheza ngoma.

Lameck Ditto hajawahi kuniangusha. Mashairi yake hunifanya niwaze. Alipoimba hivi karibuni kuhusu kazi ya moyo niliwaza. Unaumiaje moyo kunako mapenzi? Unaumaje? Kivipi? Hapa Ditto anasema “atabadilika”. Subira huvuta heri. Naam!

Comments Closed

Comments are closed.

Copyright © Bongo Celebrity