Saudia Arabia Kuruhusu Wanawake Kuendesha Magari Kuanzia Mwakani!

Kama hujazunguka duniani, kujisomea au kusikia, unaweza ukasema unaongopewa. Lakini ni kweli. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Saudi Arabia, nchi hiyo imetangaza kwamba kuanzia mwakani wanawake wataruhusiwa kuendesha magari.

Hatua hiyo ambayo inaelezewa kama hatua kubwa katika vita au juhudi za kumkomboa mwanamke ni mabadiliko makubwa katika utawala wa kifalme wa Saudia Arabia. Tangazo la mabadiliko haya ya kisera na kisheria yametangazwa kupitia muswada uliotolewa na Mfalme wa Saudia Arabia, Salman bin Abdulaziz Al Saud.

Tangu mwanzo wa miaka ya 90s wanawake duniani kote(ikiwemo Saudi Arabia) walianzisha vuguvugu la kudai haki zao zikiwemo haki za kurithi mali, kupiga kura, kuwa na sauti katika familia zao, kuwa na maamuzi kamili kuhusiana na afya au miili yao na hata jambo ambalo linaonekana kuwa la kimantiki kama kuendesha gari.

Tangazo au mabadiliko hayo, yamekuja wakati Saudi Arabia inaonekana kupitia mlolongo mpya wa kisiasa na kiutawala. Mwezi Juni mwaka huu mtoto wa mfalme Mohammed Bin Salman ambaye ana umri wa miaka 32 tu alipandishwa ngazi ghafla na hivyo kuwa mrithi wa kiti cha ufalme katika miaka ijayo.

Wengi wanamchukulia Salman kama kijana mwenye mtizamo tofauti ya wa utawala wa ufalme ambao umedumu tangu miaka ya 30s. Mbali na kuonekana kuwa na nia ya kubadili masuala ya kijamii, Salman anatizamwa kama mrithi wa kiti cha ufalme ambaye ataleta mapinduzi makubwa katika uchumi. Pamoja na kuwa na mrengo wa kimabadiliko, Salman analaumiwa pia kwa kutokuwa na ustahimilivu kwa yeyote anayepingana naye.

Mpaka hapo mwakani sheria hizi mpya zitakaporuhusu , Saudi Arabia ndio nchi pekee duniani ambayo imekuwa hairuhusu wanawake kuendesha  magari. Kwa miaka kadhaa Saudi Arabia imekuwa ikikabiliana na wanawake ambao wamekuwa wakidai haki yao na pia viongozi wa dini wenye msimamo mkali ambao wamekuwa wakipinga ufalme wa nchi hiyo kulegeza masharti katika mambo kadhaa ya kijamii.

 

Comments Closed

Comments are closed.

Copyright © Bongo Celebrity