Baraza Jipya La Mawaziri: Mvinyo Mpya Kwenye Chupa Ile Ile?

Mwishoni mwa juma lililopita, Rais John Pombe Magufuli ambaye vyombo vingi vya habari vya nje ya nchi hupenda kumuita “Bulldozer” kwa maana ya Tingatinga, alitangaza mabadiliko kwenye Baraza Lake La Mawaziri. Akiwa anaelekea kutimiza miaka miwili madarakani, hii ni mara ya pili kulifanyia marekebisho baraza lake.

Kama kumbukumbu zangu zipo sahihi, mabadiliko madogo yalitokea baada ya Mheshimiwa Nnape Nnauye kufungashiwa virago kutoka Wizara Ya Habari,Utamaduni na Michezo. Mikoba yake ikachukuliwa na Mheshimiwa Harrison Mwakyembe.

Tofauti ya mabadiliko yaliyopita ambayo yaliitwa “mabadiliko madogo”, haya ya sasa yamelipa baraza lake sura mpya. Idadi ya wizara na mawaziri zimeongezeka kutoka 19 hadi 21. Kubwa katika mabadiliko haya ni kuipasua iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini na kuwa wizara mbili yaani Wizara Ya Nishati na Wizara Ya Madini.

Katika Baraza La Mawaziri lililopita, “kigogo” mmoja aliyeng’oka ni Prof. Jumanne Maghembe, Mbunge wa Wilaya Ya Mwanga (CCM) ambaye alikuwa Waziri Wa Maliasili na Utalii.Nafasi yake imechukuliwa na kijana Dk.Hamisi Kigwangwala ambaye ameiacha nafasi ya Unaibu Waziri Wa Afya. Huko amemuachia Mbunge wa Kigamboni kijana mwingine Dr.Faustine Ndugulile.

Kawaida mabadiliko katika Baraza La Mawaziri huwa hayaji hivi hivi. Huwa ni njia ya Rais kujipambanua kwamba mambo hayaendi sawa. Huwa ni ahadi ya ndani kwa ndani kwamba changamoto zipo,ninaziona na najaribu kukabiliana nazo. Njia rahisi huwa ni kubadilisha watendaji. Ni patashika nguo kuchanika ya kujaribu “kuweka mambo sawa”.

Sasa endapo maneno na maoni ya wanaoonekana kuwa wengi ni jambo la kutiliwa maanani, mambo mengi yanaonekana kwenda kombo. Kuna imani. Lakini imani pekee haiwezi kuweka chakula mezani. Yapo matatizo ambayo yanahitaji ufumbuzi wa haraka. Hayawezi kusubiri. Sera lazima zitoe majibu yanayotarajiwa. Hakuna jibu rahisi na sahihi zaidi ya maisha bora. Hakuna jibu zaidi ya ongezeko la kipato na udhibiti wa mfumko wa bei wa bidhaa hususani za kila siku mfano vyakula.

Hivi sasa ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana unaendelea kuwa “changamoto”.Wapinzani wanaliita “bomu” linalosubiri kulipuka. Ni rahisi kujua kwanini.  Huduma za kijamii, japo kuna mipango mingi na ahadi nyingi, kimsingi bado hali ni tete. Mfano, upatikanaji wa maji safi na salama, nishati kama umeme, huduma za tiba, elimu (ikiwemo mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu) nk. Biashara zinaendelea kufungwa na au kupunguza nguvumali. Zinaitwa changamoto. Ndio wanavyosema.

Turudi kwenye baraza. Kwa kutizama “sura”, hili sio Baraza jipya. Sio mabadiliko “makubwa”. Ingawa ni wazi upokeaji wa hali kama hii hujawa na matumaini mapya hususani kutoka kwa wananchi, kuna haja ya kuangalia kwa kina kama kuna muelekeo mpya.

Hivi sasa, changamoto zinazidi kuonekana wazi. Pengine ni kutokana na mtizamo wa jumla. Kuna mitizamo ya kufuata mkumbo. Yawezekana. Pengine ni kweli na ni hali halisi isiyokwepeka. Kila palipo na mabadiliko makubwa ya sera, huwa kuna mtikisiko mkubwa kwenye nyanja mbalimbali hususani uchumi. Kwa bahati mbaya, uchumi wa kisasa unatepeta au kulendemka kama mlenda. Na ukiubomoa, kuuweka sawa tena ni jambo la majaaliwa ya Mwenyezi Mungu. Hili linatia hofu.

Ingawa kwa muda serikali ya Rais Magufuli imekuwa ngumu kueleweka hususani kutokana na mkanganyiko wa kinachosemwa majukwaani na kinachofanyika, hivi sasa taswira inaanza kujiunda kwamba urais wake unataka kuja kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kama urais uliosimamia malighafi za nchi.

Kitu ambacho bado kinasuasua ni kuwateka wananchi wote kuamini katika ndoto hii ya Tanzania mpya. Kuna upinzani. Dawa ya upinzani sio kuwatwanga risasi. Ni kuwa na mijadala yenye sura ya kitaifa badala ya vyama na hoja za kwenye majukwaa ya kisiasa. Isitoshe, kwenye siasa za vyama vingi, upinzani ndivyo unavyokuwa siku zote. Wapo.Watakuwepo. Wataendelea kuwepo.

Hili, kimsingi, ni jambo zuri. Hakuna mtu mwenye akili timamu atakayekubali kuona almasi aliyoshika mkononi inaondoka na yeye kuachwa na kipande cha chupa kisicho na thamani. Hata hivyo, ni wazi kwamba panapo mikataba inayolindwa na sheria za kimataifa na ambazo tumeziridhia, mwendo wa kasi ya umeme unaweza kuwa na madhara. Na atakayeumia zaidi ni mwananchi anayeitwa wa kawaida kama vile wengine sio wa kawaida.

Kwa kuipasua katikati iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini, bila shaka Rais amelenga kwenye uwajibikaji zaidi na kuondoa mkanganyiko wa sera na sheria husika. Lakini labda niseme kitu, madini pekee hayawezi kuwa suluhisho la kila tatizo linalotukabili. Ni rahisi sana kusema kwa madini haya tutatatua kila tatizo. Ni wimbo mzuri wa kisiasa. Ukitaka kujua zaidi jiulize ziko wapi pesa zote za misaada ambazo tumewahi kupewa na wafadhili na kusamehewa?

Tatizo letu, hivyo basi, halijawahi kuwa ukosefu wa fedha per se. Tatizo letu ni vipaumbele na tabia ya kukabidhi bucha kwa fisi. Isitoshe bado watu wengi wakiongelea “mabadiliko” bado wanagusia miji mikubwa pekee. Wanamsahau bibi na babu kule Itingoko.

Ipo imani kwamba hizo ni zama zilizopita na sasa tunasonga mbele. Kama nilivyosema hapo juu, kwa kulinganisha maneno ya majukwaani na yanayotokea, ukakasi mkubwa bado upo. Matumizi bado ni makubwa kushinda uwezo. Posho za wabunge, magari ya kifahari, gharama za ulinzi, matumizi yasiyofuata bajeti ni baadhi tu ya mambo ambayo yanaweza kukuonyesha ni kwa kiasi gani tumeamua “kubadilika”.

Jibu la swali kwenye kichwa cha habari hapo juu naomba nikuachie wewe msomaji…

Hii hapa orodha nzima ya Baraza La Mawaziri.

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. I. Waziri – George Huruma Mkuchika

Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI ). I. Waziri – Selemani Said Jafo
II. Naibu Waziri – Joseph Sinkamba Kandege
III. Naibu Wazri – George Joseph Kakunda

Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. I. Waziri – January Yusuf Makamba
II. Naibu Waziri – Kangi Alphaxard Lugola

Ofisi ya Waziri Mkuu: Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu. I. Waziri – Jenista Joackim Mhagama
II. Naibu Waziri – Anthony Peter Mavunde ( Kazi, Vijana na Ajira)
III. Naibu Waziri – Stella Alex Ikupa ( Walemavu )

Wizara ya Kilimo. I. Waziri – Dkt. Charles John Tizeba
II. Naibu Waziri – Dkt. Mary Machuche Mwanjelwa

Wizara ya Mifugo na Uvuvi. I. Waziri – Luhaga Joelson Mpina
II. Naibu Waziri – Abdallah Hamis Ulega

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. I. Waziri – Prof. Makame Mbarawa Mnyaa
II. Naibu Waziri – Mhandisi Atashasta Justus Nditiye
III. Naibu Waziri – Elias John Kwandikwa

Wizara ya Fedha na Mipango. I. Waziri – Dkt. Philip Isdor Mpango
II. Naibu Waziri – Dkt. Ashatu Kijaji

Wizara ya Nishati. I. Waziri – Dkt. Medard Matogoro Kalemani
II. Naibu Waziri – Subira Hamis Mgalu

10. Wizara ya Madini.
I. Waziri – Angellah Kairuki
II. Naibu Waziri – Stanslaus Haroon Nyongo

11. Wizara ya Katiba na Sheria. I. Waziri – Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko
Kabudi.

12. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
I. Waziri – Dkt. Augustine Philip Mahiga
II. Naibu Waziri – Dkt. Susan Alphonce Kolimba

13. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga ( JKT ).
I. Waziri – Dkt. Hussein Ali Mwinyi

14. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
I. Waziri – Mwigulu Lameck Nchemba
II. Naibu Waziri – Mhandisi Hamad Yusuf Masauni

15. Wizara ya Maliasili na Utalii.
I. Waziri – Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla
II. Naibu Waziri – Josephat Ngailonga Hasunga

16. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
I. Waziri – William Vangimembe Lukuvi
II. Naibu Waziri – Angelina Sylivester Mabula

17. Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
I. Waziri – Charles Paul Mwijage
II. Naibu Waziri – Mhandisi Stella Martin Manyanya

18. Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi.
I. Waziri – Prof. Joyce Lazaro Ndalichako
II. Naibu Waziri – William Tate Ole Nasha

19. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
I. Waziri – Ummy Ally Mwalimu
II. Naibu Waziri – Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile

20. Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
I. Waziri – Dkt. Harrison George Mwakyembe
II. Naibu Waziri – Juliana Daniel Shonza

21. Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
I. Waziri – Mhandisi Isack Aloyce Kamwelwe
II. Naibu Waziri – Jumaa Hamidu Aweso

 

Comments Closed

Comments are closed.

Copyright © Bongo Celebrity